jueves, 31 de diciembre de 2015

TAFAKARI: SIKUKUU YA BIKIRA MARIA MAMA WA MUNGU

SIKUKUU YA BIKIRA MARIA MAMA WA MUNGU
1/1/2016
Somo I: Hes 6:22-27
Zab: 67:2-3, 5, 6, 8
Somo II: Gal 4:4-7
Injili: Lk 2:16-21
Nukuu:
Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa Israeli; nami nitawabarikia,” Hes 6:27
Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,” Gal 4:4

 Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu,” Gal 4:7

Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini,” Lk 2:16

Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake,” Lk 2:19 

Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa,” Lk 2:20 

Hata zilipotumia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba,” Lk 2:21 

TAFAKARI:Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake.”
Wapendwa wana wa Mungu, Leo ni mwaka Mpya. Tulio hai tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa yale yote aliyotujalia na hasa yale tuliyokutana nayo kwa mwaka tuliouaga, tukijua kwamba kila jambo lilikuwa na sababu yake na mapenzi ya Mungu ndani yake. Leo tunapouanza mwaka kwa namna ya pekee Mama Kanisa anaadhimisha siku hii kwa Heshima ya Mama Bikira Maria Mama wa Mungu. Kuuanza mwaka Mpya twahitaji baraka za Mungu, tukisafiri pamoja na Mama Bikira Maria Mama wa Mungu kama mfano hai wa kuiga na kufuata.

Kadiri ya somo letu la kwanza, wana wa Israeli iliwapasa kuliweka jina la Bwana juu ya mambo yote na ndivyo walivyobarikiwa. Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa Israeli; nami nitawabarikia,” Hes 6:27. Wana wa Israeli walilishika na kulibeba jina la Mungu kama ilivyo uhusiano kati ya mke na mume. Jina hili la Bwana liliathiri kwa kiasi kikubwa mafanikio yao, wakati mwingine ilikuwa balaa walipoliasi jina hili. Hivyo hatima ya maisha yao ilitegemea namna walivyolichukulia jina hili la Mungu aliye hai. Ndivyo hivyo basi wakati wana wa Israeli walipokuwa uhamishoni na katika unyonge wao, jina la Mungu lilinajisiwa katika mataifa, Eze 36. Ni kwa namna hiyo hiyo tunaona kwamba wana wa Israeli walipowekwa huru kwa maajabu makubwa ya Mungu, jina la Mungu lilitakatifuzwa, liliinuliwa juu kabisa kutoka unyonge na kudhalilishwa, na kutakatifuzwa, Eze 36. Ni kutoka katika mtazamo huu kulitaja jina la Mungu na watu wake ni chanzo cha baraka na dhana ya ukarimu. Hivyo kuuanza mwaka na kuumaliza yatupasa kuweka vipauwa mbele muhimu na hasa kwa maisha ya kiroho.

Kipauwa mbele namba moja ni kukaa ndani ya jina la Mungu na neno lake. Huko ndiko kwenye uzima wa kweli. Kristo ni Mzabibu nasi ni matawi. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote,” Yoh 15:5. Uzima huu twaupata pia kwa kulishika neno lake; kulisoma, kulipokea, kulitafakari, kulitafiti, na kulikumbuka kusiko kikomo. Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani,” Yoh 5:24.

Kipauwa mbele namba mbili ni kulishwa na kuhuishwa kila mara kwa kupokea Masakramenti katika hali iliyo safi, hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Ndani ya Sakramenti hii ya Ekaristi Takatifu, tunakaa ndani na katika Kristo, na kupata uzima wa milele. Mwili na damu ya Kristo ni chakula na kinywaji cha kweli.  Naye Yesu anasema, Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake,” Yoh 6:54-56. Pamoja na makuu tuyachotayo kutoka Sakramenti hii, neema na baraka zake, Mtume Paulo anatupa angalizo juu ya Mwili huu na Damu hii ya Kristo. Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana,” 1Kor 11:27. Ndugu yangu, kabla ya kuijongea meza hii ya Bwana jihoji kwanza nafsini mwako. Je, nastahili kwa hali niliyo nayo? Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe,” 1Kor 11:28.  Tusiogope macho ya watu, na wala tusipende kushiriki Sakramenti hii na Karamu hii ya Upendo kwa mazoea. 

Kipauwa mbele namba tatu tusiache kwamwe kupatanishwa kwanza na Mungu kwa Sakramamenti ya Upatanisho au Kitubi          o. Kwa namna ya pekee Mama Kanisa ameutenga mwaka huu kama mwaka pekee wa Huruma ya Mungu. Jambo la kusikitisha leo Sakramenti hii ya Upatanishao imekuwa kama ‘kituo cha polisi.’ Walio wengi leo wanataka kuhalalisha dhambi. Sakramenti hii ya Upatanisho imewekwa rasmi na Kristo mwenyewe katika Kanisa, na wahudumu wake ni wale walioteuliwa {kuhesabiwa haki na Mama Kanisa}, kupakwa mafuta,  na kuwekwa wakfu, {Mapandre na Maaskofu} na kwa ajili hiyo huadhimisha Sakramenti hiyo. Hapa tunakutana na Huruma ya Mungu, Msamaha wa Mungu, na Kupatanishwa na Mungu. Naye Yesu anasema,Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa,” Yoh 20:23. Ndugu yangu tuijongee Huruma ya Mungu, Msamaha wa Mungu, na Kupatanishwa naye {nafsi, jirani, na mazingira}. Mwaka huu tunaouanza unatudai kuishi katika ukweli huu kama kweli twautaka uzima ndani yetu.

Somo letu la pili na Injili linafafanua fumbo zima la kumwilishwa, Neno akafanyika mwili akakaa kwetu, Yoh 1:14. Na hapa ndipo tunapoona nafasi ya Mama Bikira Maria Mama wa Mungu tunaye msherehekea leo katika tendo hili zima. Tendo hili limetokea katika utimilifu wa wakati, baada ya muda mrefu wa kusubiri. Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,” Gal 4:4. Tendo hili limebeba sehemu kuu mbili kwa wakati mmoja; kwanza linawapa watu uwana wa Mungu kwa kuwafungua kutoka sheria ya Musa.  Wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu,” Gal 4:7.  Sehemu ya pili, kumwilishwa kwa neno kumefanyika katika hali ya kibinadamu na kwa sheria, yaani,  kwa Kristo kuzaliwa na mwanamke chini ya sheria ili kumkomboa huyo mwanadamu aliye katika sheria. Sheria inamweka Kristo katika historia ya wokovu, yaani katika historia ya watu wake. Mwanamke ni kati ya watu, yaani, ndugu zake Kristo aliokuja kuwaweka huru na kuwakomboa kwa kuwafanya kama yeye, yaani, wana wa Baba. Kwa maana hiyo, Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu,” Rum 8:15-16.

Katika hali hii ya kumwilishwa, tunaona katika Injili yetu ya leo kwamba waamini wa kwanza wa tukio hili ni wachungaji ambao wapo karibu ya Maria Mama yake Yesu  na Mtoto Yesu, walio jiachia wazi kwa Mungu. Hapa Bikira Maria ni Mama kwa utayari na NDIYO yake kwa Neno la Mungu, kwa uamini wake na ukimya ambao unamfanya kupokea fumbo hili: Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:1,14. Mapaswa na ubora wa wana wa Israeli ulikuwa ‘kusikiliza Neno la Mungu.’ Katika tendo hili, Bikira Maria ndiyo kielelezo cha ukamilifu na utimilifu wa Neno hili la kumwilishwa kwa NDIYO yake. “Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema,” Lk 1:38a. Fumbo hili ndilo linalomwinua Bikira Maria katika nafasi hii ya juu kabisa Binadamu kuwekwa. Hivyo katika shina la Daudi limetoka chipukizi ambalo ndilo tumaini na jibu la Mungu kwa watu wake.

Nafasi ya Maria katika tendo hili la utayari wake, yaani Neno kumwilishwa ni uchungu na mateso na furaha. Yusufu mumewe katika sintofahamu hii anataka kumwacha kwa siri. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri,” Mt 1:19. Ndiyo ya Bikira Maria kwa Mungu inakuwa mwanzo wa aibu, ugumu wa kueleweka na mumewe, na maumivu. Hata pamoja na hali hii Bikira Maria hakuwa sababu ya kuzuia mapenzi ya Mungu yasitendeke kwa sifa na Utukufu wa Mungu na watu wake aliowaridhia. Sauti ya Mungu ilimfikia Mama Maria kupitia mwanaye Yesu Kristo aliyemzaa, Simeoni, na wachungaji. Maria aliyaweka yote haya na kuyatafakari  moyoni mwake. U Mama wa Bikira Maria na upana wa kifua chake wa kuyabeba mambo makuu na mazito haukuishia pale horini tu, bali aliendelea kuubeba U Mama huo wa Mungu na hali hiyo hadi Msalabani. Hapa ndipo aliposhuhudia kifo katili dhidi ya mwanaye mpenzi ambaye hakuwa na kosa lolote zaidi ya wema aliyotutendea.

Hakika Mama Bikira Maria aliyastahimili na kuyashiriki kikamilifu mateso ya mwanaye Yesu Kristo. Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene,” Yoh 19:25. Pamoja na huzuni na uchungu aliokuwa nao Mama Bikira Maria na Yesu ambaye kwa sasa alikuwa tayari kesha wambwa juu msalabani, Yesu analikabidhi Kanisa (kwa mitume) na jumuiya yote ya waamini kwa Mama yake. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake,” Yoh 19:26-27. Huyu ndiye Mama Bikira Maria Mama wa Mungu tunaye msheherekea leo. Huyu ndiye tunayetaka kuanza naye mwaka huu mpya tukiwa na imani pasipo shaka kwamba tutamaliza naye mwaka huu salama kama iliyokuwa NDIYO yake wakati ulipotimia pale horini, na kuendelea na NDIYO yake hadi mwisho pale msalabani ulipotundikwa wakovu  wetu na UTUKUFU wa Kristo na wetu. Hakika yatupasa kumshangilia Mama Yetu Bikira Maria, Mama wa Mungu.

Mwaka huu nilipokuwa likizo nyumbani mwezi wa saba hadi wa tisa mwanzoni, nilikumbuka tukio la miaka 23 iliyopita mara baada ya kumaliza mwaka wa Malezi huko Mahanje Songea. Nilikuwa na furaha kubwa sana ya kuchaguliwa na kuendelea na masomo ya sekondari katika Seminari ya watawa wa Mt. Fransisco wa Assis huko Maua Seminary-Moshi.

Nikiwa nyumbani Arusha-Njiro najiandaa kwa kuanza masomo hayo ya kidato cha kwanza, niliugua homa ya miguu na kuhisi kupooza na kutoweza kutembea tena. Niliona kama vile ndoto yangu ya kuwa siku moja Mtawa na Padre kuanza kutoweka. Mama yangu Mzazi alinihudumia kwa upendo mkubwa; kuniogesha na kunisaidia hudumu nyingine nilizohitaji kwa hali ile niliyokuwa nayo. Nakumbuka alinibeba mgongoni mwake umbali usiopungua zaidi kilomita 15 hivi kwenda na kurudi, kwani wakati ule hapakuwa na usafiri wa daladala na bodaboda kama ilivyo sasa. Safari hii tulikuwa tunaelekea hospitali ya KCMC-Moshi kwa vipimo zaidi. Hakika Mama yangu alitaabika sana nami. Jambo la ajabu sikuona kukerwa na hali ile niliyokuwa nampatia.

Nilipata vipimo na kurejea nyumbani Arusha-Njiro. Mungu alivyomwema kwa watu wote na nyakati zote, baada ya wiki kama mbili hivi nilianza kupata hauweni. Tarehe za kufungua Seminari zilipowadia nilikuwa tayari kwa masomo na mwenye afya ya kutosha.

Hivyo mwaka huu baada ya miaka hiyo 23 kupita, Mama yangu Mzazi naye alipatwa na homa ya miguu kama ilivyokuwa kwangu ila kwa tatizo tofauti. Nikiwa likizo ilinipasa kumuhudumia, hasa kumwinua kitandani na kumkominisha kila siku mara baada ya kuadhimisha Misa kigangoni kwetu St. Josephina Bakhita Korona-Njiro. Ilinipasa pia kumpikia kwani karibu ndugu zangu wote wameolewa na kuoa hivyo wanamiji yao. Wajukuu aliokuwa anaishi nao Mama yangu nyumbani asubuhi hadi jioni iliwapasa kuwa shuleni {shule ya upili}. Hivyo muda mwingi nilikuwa naye. Nilimbeba ingawa siyo mgongoni hadi KCMC kwa matibabu. Nilitumia muda mwingi kumfurahisha kwa kumchezea gitaa na kuimba. Kwa kweli nilijaribu kurudisha shukrani zangu japo kwa uchache aliyonitendea miaka 23 iliyopita.

Leo ninamshukuru Mungu Mama yangu anaendelea vizuri licha kwamba hajapona kabisa. Huu upendo ni sehemu tu ya upendo niliouonja kwa Mama kwa namna alivyotesema na kutaabika nami bila kuchukizwa na karaha nilizompatia. Hakika kama nikiambiwa leo nilipe alichonitendea sintoweza kufanya hivyo hata nikipewa miaka 1000 na Mungu ya kuishi nikiwa nafanya kazi usiku na mchana. Sintoweza kulipa kwa sababu kadiri nitakavyoishi na kuwa hai, ni kwa kipimo hicho hicho deni hili litakavyoongezeka hata kama yeye atakuwa kesha kufa.

Wapendwa wana wa Mungu, kwa sadaka na matojitoleo ya Mama Maria, Mama wa Mungu na hasa kwa NDIYO yake katika fumbo hili la kumwilishwa, mimi na wewe tuna deni kubwa sana la lipa licha ya kwamba Mwanaye Yesu Kristo kesha tulipia deni letu, dhambi zetu kwa sadaka yake pale msalabani. Kwa upande wa kwanza, deni hili ni kuishi upendo wa kweli na haki kwa kila aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni kwa sababu ya upendo huu Kristo alikubali kuyatoa maisha yake kwa ajili yako na yangu. “Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:12-13.  Ni kwa kumkomboa huyu aliyeumbwa kwa sura na mfano wake, Mungu anaruhusu mwanaye ateseke kwa ajili yangu na yako, na Mama Bikira Maria kushiriki mateso haya ya mwanaye. Na sehemu ya pili ya deni hili ni kuwa watakatifu kama Baba yetu wa Mbinguni alivyo Mtakatifu. Utakatifu huu tunaupata kwa kuishi vyema na kuzitumia vyema karama zetu kila mmoja kadiri ya wito wake, kwa kutimiza utume wake vyema.

Tumsifu Yesu Kristo!

Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,”

Mt 5:48

TAFAKARI: ALHAMISI, SIKU YA SABA YA OKTAVA YA NOELI

ALHAMISI, SIKU YA SABA YA OKTAVA YA NOELI
31/12/2015
Somo: 1Yoh 2:18-21
Zab: 95:1-2, 11-12, 13
Injili: Yoh 1:1-18
Nukuu:
Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho,” 1Yoh 2:18 

Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote,” 1Yoh 2:20
Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu,” Yoh 1:1

Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:3

Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu,” Yoh 1:4

Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza,” Yoh 1:5

Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua,” Yoh 1:10

Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea,” Yoh 1:11

Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu,” Yoh 1:12-13

Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:14

Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema,” Yoh 1:16

Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo,” Yoh 1:17

Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua,” Yoh 1:18

TAFAKARI:Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu.”

Wapendwa wana wa Mungu, tunaishi katika siku za mwisho. Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho,” 1Yoh 2:18. Hata hivyo si wakati wa kujawa hofu na wasiwasi. Wanafunzi wa Yesu pia walitaka kujua hasa siku hiyo itakuwa lini. Yesu Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe,” Mdo 1:7. Kwa muda tulibaki nao kila mmoja wetu atimize vyema utume wake kadiri ya wito na karama alizojaliwa na mwenyezi Mungu. Matokeo ya utume wake yatadumu milele kuliko matokeo ya kazi zako. Hivyo Yesu anawaambia wafuasi wake, Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi,” Mdo 1:8. Hili ndilo tunalopaswa kufanya sote tulio mpokea Roho huyu Mtakatifu kwa Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara.

Kwa maana nyingine siku ya mwisho ni mpaka pale dunia yote itakapofikiwa na habari njema ya wokovu. Hivyo kuharakisha siku hii ya mwisho ni sawa na kusema kila mmoja wetu atimize utume wake vyema na habari hiyo ifike kila kona ya dunia. La sivyo ni kupoteza muda buru kubashiri siku ya mwisho. Hakuna ajuaye siku hiyo. Naye Yesu anasema, Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake,” Mt 24:36. Neno, yaani, Yesu kesha fanyika mwili na kesha ushinda ulimwengu, ila tunatembea katika siku zetu za mwisho. Hata hivyo udhihirisho ulio wazi na kamili wa ushindi wa Yesu upo unakuja. Katika safari hii kuelekea udhihirisho huo wazi na kamili kati yetu wapo mbwa mwitu waliovaa ngozi ya kondoo. Katika mtazamo huu, kuishi ni vita. Wapinga Kristo sio wale wazushi tu, bali ni mtindo pia wa kuishi.

Sote tu wapinga Kristo katika maana ya kwamba maisha yetu yasipo akisi ukweli na upendo wa Kristo. Haya ndiyo ayasemayo Mtume Paulo, Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli,” 1Tim 4:1-3. Leo si jambo la ajabu kusikia dini za waabudu mashetani, wajenzi huru-free-masons.

Kristo kesha shinda ila vita inaendelea dhidi wa wema na uovu. Wale watakaokuwa katika kweli watakuwa katika hatua ya ukomavu na utakaso. Kuzaliwa kuliko kwa kweli kunatoka juu, ambako ndiko kupakwa mafuta kwetu kupitia Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara. Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote,” 1Yoh 2:20. Hivyo kuishi Ukristo ni vita dhidi ya mpinga Kristo. Utaielewa vizuri vita hii unapofanya tafiti moyo.

Injili ya leo mada kuu ni hii, Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua,” Yoh 1:18. Yesu, mwana, ni dhihirisho la Baba. Kwa hiyo kwa maneno haya, Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu,” Yoh 1:1, kati yetu uwazi wa utufuku wake unawezesha uelewa wetu wa maneno haya, Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:14.

Ni kwa mantiki hilo kwamba katika mwili Mungu ni kama Baba, Yoh 1:1-3. Ye yote yule amtazamaye mwana, Yesu Kristo, amwona Baba. “Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?” Yoh 14:9. Ni katika tendo hili la “kuona,” upewa tu yule asikiaye neno, ni yule kwa imani kupitia mwili anaona utukufu wa Baba. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu,” Yoh 1:12-13.

Kwa hiyo ujio wa Kristo ni mgogoro katika maana ya mtengano wa wanaoishi katika mwanga na wale waishio katika giza, Kristo akiwa ndiye mwanga wa ulimwengu. Watakao upokea mwanga huu, watapokea kwa imani zawadi zilizo kubwa atakazo kuja nazo. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu,” Yoh 1:12-13

Wapendwa katika Kristo, pona yetu katika siku hizi za mwisho ni kuishi katika mwanga wa Kristo. Sote tuliobatizwa yatupasa kuziishi ahadi zetu za ubatizo kwa uaminifu. Pia tuwe makini kwa mafundisho ya uongo juu ya kweli na haki ya Kristo, kwani wengi watakuja kwa jina lake.

Tumsifu Yesu Kristo!


Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani,” 1Yoh 4:1

martes, 29 de diciembre de 2015

TAFAKARI: JUMATANO, SIKU YA SITA YA OKTAVA YA NOELI

JUMATANO, SIKU YA SITA YA OKTAVA YA NOELI
30/12/2015
Somo: 1Yoh 2:12-17
Zab: 95:7-8a, 8b-9, 10
Injili: Lk 2:36-40
Nukuu:
Nawaandikia ninyi, watoto wadogo, kwa sababu mmesamehewa dhambi zenu,” 1Yoh 2:12
Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake,” 1 Yoh 2:15

Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia,” 1Yoh 2:16

Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele,” 1Yoh 2:17 

Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake,” Lk 2:36 

Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba,” Lk 2:37

Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake,” Lk 2:38 

Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake,” Lk 2:40

TAFAKARI:Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia.”

Wapendwa wana wa Mungu, kadiri ya masomo yetu ya leo, uhuru wa kweli kutoka utumwa wa dhambi umewezekana kupitia Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa yeye Kristo tumemjua Baba Yetu wa Mbinguni, na hivyo kuushinda ulimwengu. Barua hii ya Mtume Yohane kwa watu wote, anatambua wazi nafasi ya Yesu katika maisha yetu, na kile alichokijia kukikomboa. Hivyo Mtume Yohane anasema, Nawaandikia ninyi, watoto wadogo, kwa sababu mmesamehewa dhambi zenu,” 1Yoh 2:12. Ni Yesu Kristo tu awezaye kutuoka kwa sababu upendo wake hauna kipimo na alitupenda upeo. Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo,” Yoh 13:1. Hivyo niwapo hapa duniani nina nyajibu kuu mbili; mosi, kuishi upendo huu kwa waamini wenzangu, na pili, kuishi upendo huu kwa wale wasiomwamini Kristo. Kwa wale wasiomwamini Kristo yanapasa kuishi ushuhuda wa ukimya kwa kuwapenda na kutenda kama alivyofanya Kristo Yesu. Hivyo, “yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu,” Yoh 3:21. Ni “katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu,” 1Yoh 3:16. Upendo huu unatuwajibisha kumpenda Mungu na jirani.

Kadiri ya mtazamo wa Yohane, ulimwengu ni ufalme wa dhambi. Kwa mantiki hiyo tuwapo hapa duniani hatuwezi kuwatumikia mabwana wawili tukabaki salama. Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali,” Mt 6:24. Ndugu yangu, kwa maana hii, huwezi kula keki na wakati huo huo wataka ibaki kama ilivyo. Ama uile na isibaki au ibaki na usiile. Hivyo kumpenda Baba kweli ni kuichukia dunia katika kuikoa nafsi yako. Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake,” 1 Yoh 2:15. Matendo ya mwili, Gal 5:19-21, yote hupatikana katika dunia hii. Na katika hayo hakuna Mbingu. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia,” 1Yoh 2:16. Niwapo hapa duniani yanipasa kuelewa kwamba ni mahali tu pa kujiandaa na kupita kuelekea umilele.

Yote tuyaonayo hapa duniani hayana umilele kwa sababu ni vivuli vyo uhalisia ambao unapatikana ulimwengu wa mafaa, yaani mbinguni alipo Mungu mwenyewe, kadiri ya mtazamo wa falsafa ya Plato. Kwa maana nyingine ni kupoteza nguvu bure tunapowekeza kiroho hapa duniani. Ukweli ni kwamba, dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele,” 1Yoh 2:17. Kuyafanya mapenzi ya Baba ni kujitambua kwamba haupo ulimwenguni hapa kwa bahati mbaya. Upo hapa duniani kwa shughuli maalum, yaani, kufanya kile alichokijia Kristo katika kuukomboa ulimwengu. Yesu anasema, Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho,” Yoh 6:39. Wapo wengi miongoni mwetu wanafikiri kwamba uwepo wao hapa duniani ni kuishi kwa ujanja ujanja katika hila, fitina, ufisadi, ukatili na dhuluma. Haya siyo uliyoitiwa katika ulimwengu huu ndugu yangu.

Kuyafanya mapenzi ya Mungu wakati mwingine hakuhakisi kabisa miono na mitazamo ya kibinadamu. Mitazamo yetu ni kwamba tuwapo karibu sana na Mungu na kufanya mapenzi yake, ndiyo miminiko ya baraka na neema. Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii, hatutendi mema wala kuwa waaminifu mbele ya Mungu ili tununue baraka na neema zake, bali tunayafanya hayo yote kwa sababu ndiyo hali na uwepo wa Mungu, na ndivyo impendezavyo sisi kufanya. Uwepo wetu hapa duniani ni moja ya uzuri na utukufu wa Mungu. Mfano wa wale waliyafanya yote vyema ila hayakuendana na miono na mitazamo ya kibinadamu ni Ana binti Fanueli. Tunambiwa Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake,” Lk 2:36. Bila shaka Ana kama Mwanamke na Mama, kuwa na familia kamili katika maana ya Yeye, Mumewe na mtoto au watoto ilikuwa moja ya  furaha yake kubwa hapa duniani. Pamoja na kukosa hilo, hakuwa na nafasi ya kumlaumu Mungu wala kuasi Imani yake. Aliishi kwa matumaini makubwa ingawa umri wake ulisogea. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba,” Lk 2:37. Wangapi kati yetu tunaujasiri huu tunapoona mbele yetu ni giza tupu?

Furaha ya Ana binti Fanueli inakamilika anapokutana na Yesu. Ni kama asemavyo Mt. Agustino kwamba ‘mioyo yetu haitulii mpaka itakapotulia kwako Ee Bwana.’ Ndivyo ilivyokuwa kwa Ana binti Fanueli alipokutana na Yesu. “Huyu (Ana binti Fanueli) alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake,” Lk 2:38. Alichokua akikitazamia amekiona kwa macho yake.

Na Yule mtoto (Yesu) akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake,” Lk 2:40. Maana yake aliyaishi maisha yetu, furaha zetu, mahangaiko yetu, na kuyashiriki yote bila kutenda dhambi hadi kikomo chake pale Msalabani kwa kutuweka huru. Hivyo Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Je, una chochote chenye thamani  katika ulimwengu huu ambacho waweza kulinganisha na wokovu aliyokupatia Kristo Yesu?

Tumsifu Yesu Kristo!


Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14

lunes, 28 de diciembre de 2015

TAFAKARI: JUMANNE, SIKU YA TANO YA OKTAVA YA NEOEL

JUMANNE, SIKU YA TANO YA OKTAVA YA NOELI
29/12/2015
Somo: 1Yoh 2:3-11
Zab: 95:1-2A, 2b-3, 5a-6
Injili: Lk 2: 22-35
Nukuu:
Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake,” 1Yoh 2:3 
Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake,” 1Yoh 2:4 

Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake,” 1Yoh 2:5 

Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe,” 1Yoh 2:5

Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani,” 1 Yoh 2:9

Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana),” Lk 2:22-23

wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili,” Lk 2:24

Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake,” Lk 2:25

Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli,” Lk 2:32 

Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa,” Lk 2:34

Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi,” Lk 2:35

TAFAKARI: “Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi.”

Wapendwa wana wa Mungu, kuishi katika Nuru ya kweli ni kuishi katika KWELI na HAKI. Hii ndiyo mizania au kipimo halisi ndani na katika Kristo. Mizania hii hutuongoza katika kuzishika amri zake kwa sababu tunajua kweli juu ya amri hizo na sababu yake kuelekea umilele. Mizania hii hutupeleka zaidi kwa Kristo, kwani tu huru katika kweli, Yoh 8:32. Na nuru hii ambayo ndiyo uwepo wa Kristo ndani yetu, ni vita isiyo na kikomo dhidi ya giza. Mkristo amfuataye Kristo Yesu katika kweli na haki ni mtangaza vita dhidi ya mwanga na giza, wema na uovu. Mtihani mkubwa ambapo tunaopambana nao katika hali hii ni pale ninapoishi upendo kati  yangu na Mungu, kati yangu na jirani, na kati yangu na Mazingira yanayonizunguka. Hivyo huu ndio mwaliko wa kila mmoja wetu kwamba tu chumvi na nuru katika ulimwengu huu; Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima,” Mt 5:13-14. Wote wale walio chumvi na nuru katika ulimwengu huu kamwe Mungu hatovunja ahadi na mategemeo yao.

Hivyo somo letu la kwanza na Injili, yanatutafakarisha juu ya maisha ya nuru ambayo msingi wake ni kuishi katika kweli na haki. Kweli na haki hutuongoza kuzishika amri za Mungu kwa uaminifu.Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake,” 1Yoh 2:3. Asiyeishi katika kweli na haki ni vigumu kumwelewa Kristo aliye Haki na kweli. Hakika tutakuwa waongo wakubwa. Hivyo, Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake,” 1Yoh 2:4. Kweli na haki hutuongoza kwenye neno lake ambalo ndilo uzima. Huku ndiko kukamilika ndani na katika Kristo Yesu. Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake,” 1Yoh 2:5.

Kukaa ndani na katika Kristo ni ukomavu wa kiroho. Hatuendi kwake kwa shuruti  wala kulazimishwa  mara tunapoutambua ukweli na nafasi ya Kristo ndani ya maisha yetu. Tunaenda kwake kwa hiari yetu kwa sababu tunajua yeye ndiye kweli, njia na uzima, Yoh 14:6. Hivyo, Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe,” 1Yoh 2:5. Ukomavu wa wa Imani ambao ni nuru chini ya msingi wa kweli na haki utuweka karibu sana na Kristo Yesu. Hivyo kila tunayekutana naye twamwona Kristo ndani yake. Hivyo hatuwezi kamwe kuishi katika chuki na yeyote yule kwa sababu twaishi katika nuru ya kweli. Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani,” 1 Yoh 2:9. Kuishi katika chuki yamaanisha kwamba bado hatujakutana na Kristo na hivyo bado tu gizani.

 Matumaini yetu ingawa kama binadamu hatujui ni lini yatakuwa kweli, Mungu hawezi kuyasahau kwani twaishi kile tunachokiamini katika kweli na haki. Injili ya leo inatupa mfano ulio hai wa yule aliyeishi katika nuru ya kweli chini ya msingi wa kweli na haki. Huyu ndiye Simeoni. Simeoni anakutana na nuru hii ya kweli na haki wakati Yesu anapotolewa hekaluni kama ilivyo desturi ya Wayahudi kwa kila mzaliwa wa kwanza wa kiume. Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana),” Lk 2:22-23. Hata hivyo, kumkomboa huyu mzaliwa wa kwanza kutoka hekaluni iliwapasa wazazi wake kumtolea Bwana sadaka kama shukrani. Wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili,” Lk 2:24. Sadaka hii inaonyesha umasikini wa Familia hii Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Ni katika tendo hili pale Hekaluni, Simeoni mtu wa kweli na haki ahadi yake inatimizwa na Mungu. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake,” Lk 2:25. Yesu Kristo hapa ndiye nuru halisi na uhuru wa kweli wa wana wa Taifa la Mungu. Kristo ndiye  ile nuru aliyokuwa ikisubiriwa, Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli,” Lk 2:32. Mungu anaifunua nuru ya Yesu ndani ya moyo wa Simeoni naye anayaona makuu ndani ya Yesu: Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa,” Lk 2:34. Kristo ndiye sababu ya kuanguka na kuinuka wengi, kwa sababu ulimwenguni hapa ni vita dhidi ya mwanga ambaye ndiye Kristo, na giza ambayo ndiye yule mwovu shetani. Watainuliwa wale watakaoambatana na mwanga na wataangushwa wale waambatanao na giza, yaani yule mwovu.

Katika vita hii Mama Bikira Maria hatakuwa salama katika maana ya kufurahia tu uwepo wa mwanaye. Ni katika uchungu na kushiriki mateso ya mwanaye nuru ya kweli na haki itafunuliwa ndani yake. Hivyo ni katika msalaba ambao mwanaye anauendea ndipo utakapokuwepo utukufu wake. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi,” Lk 2:35. Kwenye Msalaba Mtakatifu na wenye ushindi wa Bwana Yetu Yesu Kristo ndipo penye utukufu, kufunguliwa kwa mioyo yetu kutoka utumwa wa dhambi, na kuuelekea uzima wa milele. Hivyo kwa Mkristo na Mfuasi wa Kristo, hakuna UTUKUFU pasipo MSALABA.

Tumsifu Yesu Kristo!


Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki; Bali shahidi wa uongo hutamka hila. Nuru ya mwenye haki yang'aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika,” Mit 12:7, 13:9