JUMAMOSI WIKI YA 3 YA PASAKA
Somo: Mdo 9:31-42
Zab: 116:12-13, 14-15,
16-17
Injili: Yoh 6:60-70
Nukuu:
“Basi
kanisa likapata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa,
likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu,”
Mdo 9:31
“Roho ndiyo itiayo
uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima,”
Yoh 6:63
“Akasema, Kwa sababu hiyo
nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na
Baba yangu,” Yoh 6:65
“Basi Simoni Petro
akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe
ndiwe Mtakatifu wa Mungu,” Yoh 6:68-69
TAFAKARI:
“Jambo lolote lile lenye kuakisi Utukufu wa Mungu lililo chini ya Kristo na
ndani yake linausalama. Kristo ndiye neno la uzima wa milele na Mtakatifu wa
Mungu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
‘jambo lolote lile lenye kuakisi utukufu wa Mungu na lililo chini ya Kristo na
ndani yake linausalama. Kristo ndiye neno la uzima wa milele na Mtakatifu wa
Mungu.’ Baada ya Ufufuko wake Yesu Kristo, jumuiya ya kwanza ya Wakristo
ilijawa hofu na hawakuwa na usalama wa maisha yao hasa hujuma ya wazi iliyokuwa
inafanywa na Wayahudi ambao hawakuamini wala kuifuata njia hii. Hali ilikuwa
mbaya zaidi pale Sauli ambaye baada ya kuongoka kwake anajualikana kama Paulo,
alivyolitesa Kanisa hili la mwanzo. Pauli sasa akiwa ndani na katika Kristo
anakiri na kusema, “mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume,
kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu. Lakini
kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si
bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni
neema ya Mungu pamoja nami,” 1Kor 15:9-10
Ndugu yangu, kile
ulicho na ukifanyacho ndani na katika Kristo, ni baraka na neema za Mungu.
Mungu kamwe hawezi kukutupa unapokiri kwenda kinyume na mpango na mawazo yake.
Mpango na mawazo ya Mungu kwa kila mmoja wetu ni ya amani na yenye tumaini siku
ya mwisho ya kila mmoja. “Maana nayajua mawazo
ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa
ninyi tumaini siku zenu za mwisho,” Yer 29:11. Kuishi katika mpango na mawazo
ya Mungu ni kujisalimisha kwake, na hii ndiyo njia sahihi ya kuishi.
Wakristo
wa mwanzo kwa kutambua ukweli huu-‘kujisalimisa’ na njia sahihi ya kuishi,
wanawajibika kikamilifu kwa Mungu Baba, Mungu Mwana na Roho Mtakatifu. Ndani ya
Utatu huu Mtakatifu na Umoja huu usiogawanyika, unabii wa Yeremia
unajidhihirisha wazi kwamba, “Nanyi
mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza,” Yer 29:12. Baada ya kuongoka
kwake Paulo ikiwa ni ishara ya wazi ya Kristo kulisimamia Kanisa lake, amani na
utulivu kwa wafuasi wa Kristo vinarejea. “Basi
Kanisa likapata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa,
likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu,”
Mdo 9:31. Hali hii ya Kanisa ni uthibitisho pia wa maneno ya Kristo
mwenyewe kwamba, “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye
ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi
kufanya neno lo lote,” Yoh 15:5. Hakika bila Kristo hatuwezi kufanya lo lote
lile liwe dogo au kubwa!
Ni katika amani hii,
utulivu, na matumaini ndani na katika Kristo na Roho Mtakatifu ishara nyingi
zinafanyika katika jumuiya hii ya kwanza ya Wakristo. Hapa tukumbuke jambo hili
muhimu; Ishara hizi siyo kielelezo cha Imani, bali ni kikoleza cha Imani hasa
kwa wale ambao bado hayajakomaa Kiroho. Hivyo tunaona Mtume Petro akiwa Lida
anamponya Ainea, mtu aliyekuwa amelala
kitandani miaka minane; maana alikuwa amepooza, Mdo 9:33. “Petro akamwambia, Ainea, Yesu Kristo
akuponya; ondoka, ujitandikie. Mara akaondoka,” Mdo 9: 34. Ni huko Lida pia tunaona ishara nyingine
akiifanya Mtume Petro kwa njina la Yesu anaurudishia tena uhai wake mwanamke
yule Mjane Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke ambaye
alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa, Mdo 9:36. “Petro akawatoa nje
wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha,
ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi,” Mdo
9:40.
Matendo
haya ya uponyaji yanasadifu na kuitimisha unabii wa Yeremia kwamba, “Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu
wote,” Yer 29:13. Kristo anaonekana katika maisha ya kila moja kwenye jumuiya hii
ya kwanza ya Wakristo iliyomridhia kwa Imani. Jumuiya inakuwa kitu kimoja
katika shida na raha ndani na katika Kristo Yesu. Umoja huu wa kupendana na
kutaabikiana unazaa utume na uinjilishaji kwa wale wote wasiolifahamu jina hili
yenye nguvu na la ajabu-Yesu wa Nazareti. Mtindo huu wa maisha unakamilisha pia
unabii wa Yeremia, “Nami nitaonekana kwenu, asema Bwana, nami nitawarudisha
watu wenu waliofungwa, nami nitawakusanya ninyi, nikiwatoa katika mataifa yote,
na katika mahali pote, nilikowafukuza, asema Bwana,” Yer 29:14a. Ndani na
katika Kristo si watumwa tena wa hali yoyote ile, bali tu huru.
Wapendwa
wana wa Mungu, hayo yote tuliyoyatafakari yanauzima yakiwa ndani na katika
Kristo. Ni katika roho na siyo mwili yote upata uzima. “Roho ndiyo itiayo
uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima,”
Yoh 6:63. Ni kwa njia ya Mungu Baba na Mungu Mwana-Kristo, tunapewa Roho huyu
wa Mungu kuyaishi yale yote kila mtu kadiri ya hali na wito wake. “Kwa sababu
hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa
na Baba yangu,” Yoh 6:65. ‘Kristo ndiye njia, kweli, na uzima,’ Yoh 14:6.
Miongoni mwetu na tulio Wakristo, yaani wafuasi wake Kristo kwa Sakramenti ya
Ubatizo, wapo ambao maisha yao ya kila siku yametawaliwa na ujanja-ujanja tu. Ndugu
yangu, fanya yote ufikiriyo kuyafanya, ila kumbuka maneno haya ya Yesu, “pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote,” Yoh 15:5
Mafundisho
haya ya Yesu kuhusu kujiachia kwake kunakoendana na wito wa kila mmoja wetu,
yanakuwa mafundisho magumu sana kwani yanatuhitaji kujiachilia kwake kabisa. Asilimia
98% hazitoshi! Yatupasa kuushinda ubinadamu wetu kila siku. “Basi
Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka?” Yoh 6:67. Katika hali hii ya kukata tamaa kwa wanafunzi (kundi
lile kubwa lililokuwa likimfuata) juu ya fundisho hili la kujiachia bila
kujibakiza, na hivyo kurudi nyuma, Simoni Petro anajibu, “Bwana! Twende kwa
nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi
tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu,” Yoh 6:68-69. Wapendwa wana wa Mungu, Kristo anayo maneno ya
uzima. Je, uzima wako unaupata wapi? Ni kwa hila na ujanja-ujanja wako? Embu
itazame vizuri filamu ya maisha yako. Yatazame vizuri matukio yale ambayo
hukuwa Ufunuo wa Utukufu na Uzuri wa Mungu. Hata kama matukio hayo yanauzunisha
na ukajiona kutokuwa na thamani mbele ya Mungu, kamwe usiyafanye ukuta wa
kutokuona neema na huruma ya Mungu. Tambua ukweli huu: ‘Neema na Huruma ya
Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu.’
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi Simoni Petro
akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa
wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu,” Yoh 6:68-69
Tusali:-Ee Yesu Mwema, ni
kwako tu kuna usalama na uzima wa milele. Tuongoze kila mmoja wetu kufahamu
ukweli huu na kuuishi. Liongoze Kanisa lako ili siku zote liwe kielelezo kamili
cha uwepo wako. Amina