JUMAMOSI WIKI YA 2 YA KWARESMA
Somo:
Mik 7:14-15; 18-20
Zab:
103:1-2, 3-4, 9-10, 11-12
Injili:
Lk 15:1-3; 11-32
Nukuu:
“Ni nani aliye Mungu
kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuachilia kosa la watu wa urithi wake
waliosalia? Hashiki hasira yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema,” Mik
7:18
“Baba, nimekosa juu ya
mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa
watumishi wako,” Lk 15:18-19
TAFAKARI:
“Toba
ya kweli; Upendo na Msamaha wa Mungu.”
Wapendwa wana wana
Mungu, kwa pamoja tutafakari kwa undani “toba ya kweli; Upendo na Msamaha wa
Mungu.” Somo la kwanza linatuelezea uhalisia wa Mungu. Mungu kwa asili ni
Upendo, Huruma, na Msamaha. Ni Mungu anayetutakia mema muda wote sisi viumbe na
wana wake. Ni Mungu anayejifunua kwetu kwa njia mbali mbali, ikiwa ni kwa njia
ya historia na vile alivyoviumba. Ni Mungu ambaye yupo na alikuwepo nyakati
zote hata kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu. Tulikuwa daima ndani ya mawazo yake.
Kwa upande wetu, tuna kazi moja tu, yaani, kumtafuta kwa maana
anapatika. Nabii Isaya anatuambia hivi, “Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana,
Mwiteni, maadamu yu baribu; Mtu mbaya na aache njia yake, na mtu asiye haki
aache mawazo yake; na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu,
Naye atamsamehe kabisa.” Isa 55:6-7.
Ndugu yangu, kumwasi
Mungu ni tendo ambalo lipo chini ya uwezo wetu. Kumrudia Mungu ni tendo la toba
na kufanya maamuzi sahihi na ya msingi. Tunapofanya maamuzi haya ni wazi kabisa
kwamba yatupasa kuachilia mengi ambayo kwayo yalitupa furaha na hata kujulikana
na kujikweza. Ila tukitambua umuhimu wa umilele wa maisha yetu, hatuna budi
kuachilia yote haya ambayo ni ya kupita na ya muda mfupi.
Tunapofanya toba ya
kweli na kumrudia Mungu, hutupokea kama tulivyo. Mungu katika mapokezi haya
hatazamani historia yetu. Mungu huanza mradi mpya nasi na kutufanya wapya tena
katika yale mazuri anayotufikiria. “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi,
asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku
zenu za mwisho,” Yer 29:11. Ndugu yangu, kwa nini hubadiliki? Waitaji malaika
washuke na kukuambia jambo hili? Kwa nini unakuwa kero kwa ndugu na jirani
zako? Kwa nini unakuwa kero kwa wanajumuiya zako na viongozi wako? Je, unapenda
kuishi hivyo hadi lini?
Injili yetu ya leo
inatupa kisa na simulizi la mwana mpotevu. Wahusika wakuu katika kisa hiki ni
Baba mzazi, Mwana mpotevu, na Kaka ya mwana mpotevu. Wengine ni watumishi au
watumwa wa Baba mzazi wa Mwana mpotevu, na marafiki wa mwana mpotevu. Mwana
mpotevu, tena aliye mdogo katika familia hii, anafanya kitu ambacho si cha
kawaida katika jamii na hasa mila na desturi kama zilivyokuwa. Kitendo cha
kuomba urithi au sehemu ya mali yake kabla ya kifo cha baba yake, kulimaanisha
kumtakia baba yake mabaya. Ni kutokumtambua baba yake. Ni kumchukulia baba yake
kama marehemu.
Kwa upande wa baba
yake, na kutokana na upendo aliokuwa nao kwa wana wake na familia, anakubali
aibu hiyo, na kufanya kadiri ya matakwa ya mwanaye. Baba anampa sehemu ya
urithi wake. Yaliyompata kijana huyu wote tunafahamu simulizi hili. Ndugu
yangu, kutenda makosa ni hali yetu sote wanadamu. Ila tofauti ipo hapa;
unapotambua umefanya kosa na kuchukua hatua kwa uliyoyafanya ndiko
kunapoturejeshea hadhi na heshima yetu tena. Mwana mpotevu analiona kosa lake
na anakiri kwa matendo na maneno, “Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na
kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana
wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako,” Lk 15:18-19. Ndugu yangu,
haya ndiyo majuto ya kweli. Tunachoangalia si aibu tutakayopata, bali huruma,
neema, na stahili tunayoyapata kwa kufanya toba ya kweli.
Ndugu yangu, unapodondoka
kwa sababu ya dhambi, usione aibu kuamka na kuomba msamaha kwa muumba wako.
Yeye Mungu anasema, “mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana
Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.” Ufu 1:8. Je, kuna
mwingine wa kumkimbilia zaidi ya Mungu wetu? Mungu aliye Upendo hana mipaka
wala masharti ya pekee unapomrudia. Mungu anasema, “nawapenda wale wanipendao,
na wale wanitafutao kwa bidii wataniona,” Mit 8:17.
Upendo wa Baba hauna
mfano. Katika simulizi hili la mwana mpotevu, Baba huyu anapomwona mtoto wake,
hapendi na wala haitaji kujua historia ya yale maovu aliyofanya. Furaha yake ni
kumwona mwanaye kama alivyo, na anajua kurudi kwake ni toba ya kweli. Anachofanya
Baba ni kumrudishia stahili yake kama mwana na mmoja wa familia. Ni kumwesabia
haki tena kama mwana familia. Lakini jambo la kushangaza ni kwamba tendo hili
la Baba, linakuwa sononeko la Kaka ya mwana mpotevu. Haoni maana ya furaha hii
na sababu ya kuwa hai mdogo wake. Ndugu yangu, katika safari ya wokovu,
tusipende kujitazama wenyewe. Wokovu ni kwa wote na nifuraha ya Mungu. Katika
mfano huu, Yesu anawakemea Waisraeli na hasa Mafarisayo ambao wanahuzunika kwa
yale anayofanya Yesu ambao ndio upendo wa Mungu Baba.
Yatupasa mimi na wewe kutiana
moyo na kufurahia pale mwenzetu au wenzetu wanapomwongokea Mungu na kuishi
maisha ya kumpendeza Mungu. Mara nyingi hatuachi kuwasema vibaya wale
wanaojitahidi kuishi njia impendezayo Mungu. Tunawapachika majina mengi, na
kuwakatisha tamaa kabisa. Kwa upande wetu, mwenzetu anapojitahidi kuishi
vizuri, basi iwe changamoto ya sisi kufanya vizuri.
Ndugu yangu, wakati
ndiyo sasa! Kaa na tafakari namna utendavyo. Je, unafanya kadiri ya mapenzi ya
Mungu? Urithi wako ni fursa uliyonayo sasa katika utendaji. Je, unatumia fursa
hiyo vizuri kwa Sifa na Utukufu wa Mungu? Je, baada ya kuishi ovyo kwa muda
wote huo, upo tayari kufanya toba ya kweli na kuacha njia hiyo mbaya? Basi nielewe
nafasi niliyo nayo ni leo na sasa tu. Ni vyema nikachukua hatua sasa na
kuutafuta uso wa Bwana. “Mtafuteni Bwana, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa
dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake; itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu;
huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya Bwana,” Sef 2:3
Tumsifu Yesu Kristu!
“Baba, nimekosa juu ya mbingu na
mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi
wako,” Lk 15:18-19
Tusali:-Ee
Yesu, niongoze katika kweli yako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario