IJUMAA WIKI YA 2 YA KWARESMA
Somo: Mwa 37:3-4,
12-13a, 17b-28
Zab:
105:16-17, 18-19, 20-21
Injili: Mt 21:33-34, 45-46
Nukuu:
“Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko
ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani,” Mwa 37:4
“Atawaangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la
mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake,”
Mt 21:41
TAFAKARI: “Wivu na kutokuona mazuri ya wenzetu, na mwisho kupeleka
katika umauti.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo tutafakari kwa undani
kuhusu “wivu na chuki ya kutokuona mazuri ya wenzetu, na mwisho wake kutupeleka
katika umauti. Somo letu leo la kwanza ikiwa ni pamoja na Injili kwa namna moja
yanaongelea hathari za wivu, na tokeo lake, yaani umauti.
Bila shaka ndugu yangu unajua vizuri kisa cha Yusufu
na ndugu zake. Yusufu akiwa ni mtoto wa mwisho, alitokea kupendwa sana na baba
yake. Kupendwa kwa mtoto wa mwisho si jambo ya ajabu katika makuzi na hata katika
mila na desturi zetu. Ni kweli iliyo wazi kwamba aliye wa mwisho hutupiwa jicho
na wengi. Kwa wazazi ni wakati wa kujitazama na kujiona kupitia mtoto wao huyu
wa mwisho. Mtoto huyu wa mwisho ujeuka kuwa kama kioo kwa wazazi wao. Hili si
jambo baya. Hali hii pia huwa kivutio kwa ndugu zake, na kupendwa na wote.
Ila cha kushangaza kwa familia hii ya Israeli, tendo
la kupendwa sana Yusufu na baba yake, linakuwa kero kwa ndugu zake, na hata
kupanga mpango wa kumwua. Hii ni chuki ya hali ya juu.
Kujaribu kumwaga damu ya ndugu yako kwa sababu tu anapendwa, tena na baba yako,
ni jambo la kushangaza sana.
Ndugu yangu, swali la
kujiuliza ni hili, kwa nini unachukia wakati mwenzako anafanikiwa? Kwa nini
ukose usingizi kwa mafanikio ya mwenzako? Sisemi tusiwe na wivi, ila wivu huo
uwe wivu wa maendeleo. Kama mwenzako kajenga nyumba akatumia bati kuezeka, basi
wewe jitahidi uezeke kwa vigae. Huu ni wivu wa maendeleo usiokuwa na madhara
kwa mwingine.
Yanayomtokea Yusufu, yanamulika
pia maisha ya Yesu na hatma ya kifo chake. Ndugu za Yusufu baada ya kuguswa na
dhamiri zao, wanaamua kumuuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande ishirini tu vya
fedha. Yesu pia anauzwa na mwanafunzi wake, Yuda Eskariote kwa vipande
thalathini tu vya fedha. Mbele ya safari, Yusufu anakuwa mwokozi kwa ndugu na
familia yake wakati wa njaa. Yesu pia ni kielelezo chetu na mwokozi wetu kwa
njia ya mateso, kifo, na ufufuko wake.
Wivu usio wa kujenga ni
chanzo cha mateso na hata kifo kwa wengine. Katika Injili, Yesu nafundisha kwa
mfano na kuwakumbusha waandishi na mafarisayo safari nzima ya wokovu na
makusudi ya Mungu katika kumkomboa mwanadamu. Ila kwa mioyo yao migumu iliyojaa
wivu na chuki hawapotayari kuupokea ukweli huo na kubadilika. Kwa tendo hili, Ufalme
wa Mungu unaondolewa kwao na kupewa taifa lingine.
Je, hili la Yusufu na
Yesu linasema nini kuhusu Ukristo wako? Ndugu yangu, ni ukweli ulio wazi
kwamba, kuishi maisha ya kweli na ufuasi thabiti kwa Kristo, ndani ya Kristo,
na kwa ajili ya Kristo, ni kutangaza vita vya kudumu dhidi ya utawala wa giza.
Ni kutangaza vita pia dhidi ya ndugu, jamaa na marafiki, na matamanio yako
binafsi. Mashambulio haya ni mtihani kwa ye yote yule aliye mwaminifu katika
ufuasi wa Yesu Kristo. Katika hili Yesu anasema, “Nanyi mtakuwa mkichukiwa na
watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumila hata mwisho, ndiye
atakayeokoka,” Mt 10:22.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ndugu zake wakaona ya kuwa baba
yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye
kwa amani,” Mwa 37:4
Tusali:-Ee
Yesu tujalie ujasiri wa kuvishinda vita dhidi ya imani yetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario