IJUMAA WIKI YA 1 YA KWARESMA
Somo:
Eze 18:21-28
Zab:
130:1-2, 3-4, 5-7a, 7bc-8
Injili:
Mt 5:20-26
Nukuu:
“Lakini mtu mbaya akighairi, na kuacha
dhambi zake zote alizozitenda, na kuzishika amri zangu zote, na kutenda yaliyo
halali na haki, hakika ataishi, hatakufa,” Eze 18:21
“Mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda
uovu, akafa katika uovu huo; katika uovu wake alioutenda atakufa,” Eze 18:26
"Tena, mtu mwovu
atakapoghairi, na kuuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo halali na
haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai," Eze 18:27
“Kwa sababu atafakari, na kughairi, na
kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda, hakika ataishi, hatakufa,” Eze 18:28
“Maana
nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo,
hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 5:20
"Basi mimi
nawaambia, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea
ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehenam ya moto,"
Mt 5:22.
“Basi ukileta sadaka yako madhabahuni,
na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya
madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka
yako,” Mt 5:23-24
TAFAKARI:
“Tunaponywa na kuwa hai kwa kusamehe na kusamehewa.”
Wapendwa wana wa Mungu,
karibuni tutafakari pamoja "uponyaji na uhai tuupatao kwa kusamehe na
kusamehewa." Hili ndilo wazo kuu la Masomo yetu ya leo. Naomba tusafiri
pamoja katika tafakari hii. Usiwe na haraka ya kumaliza kusoma. Usipopaelewa rudia
tena kwa utulivu. Sasa tuanze safari yetu.
Ndugu
yangu, swali la kujiuliza ni hili; Je, uponyaji na uhai huo tunaupataje? Kwa
upande wa uhai, somo la kwanza limeeleza vizuri sana. Uhasili wa Mungu ni UHAI.
Uhai ni zawadi kwetu na ni mali ya Mungu. Kama ni mali yake, Mungu hasingependa
uhai huo ufifishwe kwa jambo lolote lile au kukatizwa kwa vyovyote vile.
Uhai tuliopewa na Mungu
tuna uharibu na hata kuufifisha na kuua na kuutokomeza kabisa kwa dhambi na
uovu. Njia moja na ya pekee kuupata na kuustawisha uhai huo ni kughairi njia
mbovu na kumrudia mwenye uhai huo ambaye ndiye Mungu mwenyewe. Mungu anasema,
"Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? Asema Bwana Mungu; si afadhali
kwamba aghairi, na kuiacha njia yake, akaishi?" Eze 18:23.
Ndugu yangu, wachagua
kuishi au kufa? Wapo watu ambao leo tunaishi nao, sala yao kubwa kila siku ni
kumwomba Mungu awape uhai ili waendelea kujiboofusha kwa maisha ya anasa na
starehe. Pia wapo watu wengi leo wanaishi maisha ya taabu na mateso makubwa.
Kauli mbiu yao ni "aheri ya jana kuliko leo." Je, Mungu halioni hilo?
Je, Mungu mwenye kuhodhi uhai huu kwa nini yupo mbali na wanaoteseka?
Ndugu yangu, ni ukweli
usiotia shaka kwamba sisi na vyote tulivyonavyo na kile tulicho ni mali ya
Mungu. Swali ni kwamba, "Je! Tupate mema mikononi mwa Mungu, nasi tusipate
na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa mikono yake"
Ayu 2:10b. Wapo wengi wanaokumbwa na majaribu kama Ayubu. Ila kabla Mungu
hajakujaribu na kuipima imani yako anajua kabisa jaribu hilo utalishinda na
hasa pale utakapomwelekea Yeye tu. “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo
kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita
mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze
kustahimili,” 1Kor 10:13. Mungu hawezi kuliumba jiwe kubwa akashindwa kulibeba.
Huyo siye Mungu muumba mbingu na dunia. Huyo siye Mungu mweza wa yote. Hicho
kitakuwa ni kitu kingine kabisa na ovyo kutokea!
Kwa upande mwingine
Yesu anatupa angalizo kwa wale tunajiboofusha kwa anasa na starehe, na anasema,
"Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au
kujipoteza mwenyewe?" Lk 9:25.
Ndugu yangu, uponyaji
na uhai unapatikana kwa Mungu na kupitia mwanawe mpenzi Yesu Kristo tu. Kwa
kuwa, "Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka;
nami nitamfufua siku ya mwisho." Yoh 6:44
Ndugu yangu, hasa
ninayesafiri nawe kwenye tafakari hii, jeuri yako ya kutokughairi njia zako
mbovu na ovu zinatoka wapi? Bila Yesu
utaitoboa kweli mbingu? Yatupasa kutafakari sana juu ya maisha yetu na yenye
kumpendeza Mungu. Majaribu yapo kila kona. Uhai huu tumekopeshwa tu kwa muda.
Na hapa duniani tulipo ni mahali tu pa maandalizi ya maisha ya umilele. Kila
mmoja wetu ajihesabie kwamba kengele ifuatayo kupigwa ni zamu yake. Je,
umejiandaa? Au unapoteza muda kwa kuwaangalia wenzako na kuhesabu waliokufa,
unaowazika na walikuwa mautiuti? Je, waona jambo hilo kwako haliwezi kutokea?
Au lipo mbali? Ukweli ni kwamba nami pia nipo miongoni mwao. Ukweli huu hautoshi
nisipozighairi njia zangu ovu na kuukumbatia uhai.
Wapendwa katika Kristo,
Injili yetu ya leo yatufafanulia uponyaji kwa njia ya kusamehe na kusamehewa.
Yesu katika hili anatoa angalizo kubwa na kusema, "haki yenu isipozidi
hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa
mbinguni," Mt 5:20. Mafarisayo na waandishi walijihesabia haki kuwa ni
watu wema, na ndiyo kipimo cha kweli. Ndugu yangu, Mungu pekee ndiye
hutuhesabia haki, tena si kwa matakwa yetu, bali kwa matakwa yake kwa sababu Yeye
tu ndiye HAKI. Sisi binadamu tunashiriki tu ukamilifu wa Mungu kwa kuwezeshwa
naye. Mafarisayo na waandishi walijihesabia haki na kuwa miungu watu. Huu ni
upofu uliopitiliza. Kuwajua vizuri Mafarisayo na Waandishi nakualika usome sura
yote ya 23 ya mwinjili Mathayo. Ni kwa sababu hiyo Yesu anatoa angalizo kwanza
kama kweli tunataka uponyaji lazima kusamehe, kama hatua mahususi na kusamehewa
ikiwa ndilo tokeo la tendo mahususi.
Kusamehe ni amri kama
kweli na sisi tunataka kusamehewa. Sala ya ‘Baba yetu’ imeliweka jambo hili
wazi kama sharti la upatanisho na Mungu. Cha ajabu sala hii tunaisali wengine
kila siku na kila mara kwa siku, ila bado kusamehe ni shiiida! Je, utaponywaje
kama tatizo lako ni kuvunjika mguu, ila "P.O.P" umefunga shingoni?
Mbona kila siku unatibu ugonjwa usioumwa kwa dawa tofauti? Kwa nini inakuwiya
vigumu kusamehe na kupatana na ndugu yako? Je, wewe ni mkamilifu sana?
Unatofauti gani na mafarisayo na waandishi wanachukuwa nafasi ya Mungu kwa
kujihesabia haki?
Agizo la Yesu ni
kwamba, "patana na ndugu yako uwapo naye njiani," Mt 5:25. Maana yake
ni nini? Ndugu yangu, maana yake yakupasa upatane na ndugu yako angali hai, na
mungali mnaishi, ukiwa na ufahamu wa kutosha. Msivute muda pasipo sababu.
Kengele ikishagongwa hakuna tena pa kujitetea. Maapizo na laana hazikusaidii
chochote. Unazidi jizibia riziki zako bure kutoka kwa mwenyezi Mungu.
Unaposamehe unajiponya na kumponya mwenzako pia. "Hivyo watu wote
watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa
ninyi," Yoh 13:35.
Wapendwa wana wa Mungu,
ibada na sadaka zetu kwa Mungu huwa safi na za kumpendeza Mungu pale tunapokuwa
na amani ya kweli na ndugu zetu. “Basi
ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno
juu yako, iache sadaka yako
mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe
sadaka yako,” Mt 5:23-24. Amani hii ni pale unapokuwa tayari kupatana na
kusamehe bila kipimo.
Tumsifu Yesu Kristo!
"Tena, mtu mwovu
atakapoghairi, na kuuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo halali na
haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai," Eze 18:27
Tusali:-Ee
Yesu, nijalie Neema ya kughairi yasiyokupendeza. Nipe Neema ya kusamehe hata
pale itakaponibidi kufanya sadaka kubwa. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario