JUMAPILI
YA 2 YA KWARESMA-A
Somo I: Mwa 12:1-4a
Zab: 33:4-5, 18-19, 20, 22
Somo II: 2Tim 1:8b-10
Injili: Mt 17:1-9
Nukuu
“Nami nitakufanya
wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka,”
Mwa 12:2
“Nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na
katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa,” Mwa 12:3
“bali
uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu;
ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu
sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa
katika Kristo Yesu tangu milele,” 2Tim 1:8-9
“na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi
wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa
ile Injili,” 2Tim 1:10
“Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na
Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani,” Mt 17:1
“akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama
jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru,” Mt 17:2
“Alipokuwa
katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka
katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa
naye; msikieni yeye,” Mt 17:5
TAFAKARI:
“Imani ya kweli ndiyo
msingi wa ufahamu wote.”
Wapendwa wana wa Mungu, kuaminiana ni
jambo la kawaida na la muhimu kwa maisha ya kawaida kabisa tunapoishi zaidi ya
mtu mmoja. Tendo hili la kuaminiana ni matokeo ya imani tulinayo juu ya yule au
wale tunaoishi nao. Mfano, ninaposafiri na kuingia duka lolote au hoteli yoyote
na kununua maji, ninayoimani maji yale ni salama. Kitu cha kwanza kabisa ni
Imani niliyonayo. Hatua ya pili ni ufahamu kama tokeo la imani ile, yaani,
ninapokuwa salama au kutokuwa salama baada ya kunywa maji yale. Hatua hii ndiyo
tunayoiita ufahamu wa jambo lile.
Abramu ni mfano thabiti wa Imani ya
kweli. Abramu ukiwa umri umeenda, yapata miaka 70, anapata ujumbe wa kutoka
mazingira aliyoyazoea na kwenda asipokujua. “Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa
zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha,” Mwa 12:1. Embu fikiria inavyotuwia vigumu
kuondoka mazingira tunayoyajua na kwenda mazingira tusiyo yajua inavyokuwa
vigumu. Pili, Abramu anaondoka na mali zake zote kwenda katika nchi ya ahadi
asiyoijua, bali kwa kuonyeshwa kuwa ni nchi ya kanaan. “Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa nduguye, na
vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani,
wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya Kanaan,” Mwa
12:5. Hili ni tendo la ujasiri mkubwa sana
kwa binadamu kufanya. Abramu anaishinda hofu ya sintofahau kuhusu kesho.
Ingawa Abramu
anahaidiwa kubarikiwa na kupata ulinzi wa kutosha, jambo hili si rahisi
kuliamini kwa kirahisi. “Nami
nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote
za dunia watabarikiwa,” Mwa 12:3. Tunakuwa
salama zaidi kwa mazingira tunayoyajua kuliko yale tusiyoyajua. Hapa ndipo
penye ugumu kwa binadamu kufanya maamuzi ya kina kuhusu maisha yake. Abramu
anashinda mtihani huu mgumu. Ni ukweli usiotia shaka kwamba kwa binadamu hakuna
mtihani mgumu kama kufanya maamuzi msingi ya maisha yake, yaani, kuacha njia
aliyoizoea na kuanza njia nyingine au kuacha maisha aliyoyazoea na kuanza
maisha mapya na mazingira mapya. Jambo la msingi hapa kuhusu Abramu ni uhusiano
wake na wakaribu na Mungu aliyemwamini na kuyaweka yote kwake. Mimi na wewe leo
kielelezo chetu Kristo aliye kila kitu kwetu. Kwake Yesu kuna Njia, Kweli, na
Uhai, Yoh 14:6.
Hivyo wapendwa katika
Kristo, lnjili ya leo inauweka sawa ukweli huu kwa mambo makuu matatu; Dira
yetu ya kufuata kama Wakristo, Utumilifu wa nyakati, na Hatma yetu iliyojengeka
katika agano la umilele. Haya yote yanafanyika katika tukio hili la kung’ara
kwa Bwana wetu Yesu Kristo kadiri ya simulizi la Injili ya leo.
Kwanza, ni dira yetu ya
kufuata kama Wakristo. Heshima na cheo chako kama Mkristo ni utakatifu wako.
Hivyo maisha yetu kama Wakristo kuelekea umilele yatafikika na kuwezekana kama
ni tokeo la utakatifu wetu kwa kuyaona maisha kama ni jukumu la muda fupi hapa
duniani na kama pia sehemu pekee ya maandalizi. Udhihirisho wa utakatifu huu
kama dira yetu ya maisha ni tendo lile la kung’ara Kristo Yesu. “Na baada ya siku
sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima
mrefu faraghani, akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua,
mavazi yake yakawa meupe kama nuru,” Mt 17:1-2.
Kristo anavikwa Utukufu
wake ambao ataunyakua rasmi mara baada ya mateso, kifo na ufufuko huko
Yerusalemu. Hivyo Utukufu wa Kristo hautenganishwi na msalaba/mateso. Kwa maana
nyingine hakuna Utukufu pasipo msalaba. Kama Kristo ndiye njia, kweli na uzima,
Yoh 14:6, nasi wafuasi wake itatupasa kupita njia hiyo ya
msalaba, ukweli huu anaotufundisha, ili tuufikie uzima ule, yaani, maisha ya
milele. Kristo ni masiha wa Msalaba, nasi twamfuata Masiha wa Msalaba ili
tuifikie taji ile ya Utukufu baada ya kuhesabiwa haki.
Pili, ni ukamilifu wa
nyakati. Katika tendo hili la kung’ara, tunaelezwa tokeo la watu wawili, yaani,
Musa na Eliya katika mazungumzano na Yesu. “Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza
naye,” Mt 17:3. Katika tendo hili, Musa anawakilisha Torati, na Eliya
Unabii. Hivyo leo Yesu anaikamilisha Torati. Naye Yesu anatuambia, “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au
manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin,
nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya
torati haitaoondoka, hata yote yatimie,” Mt 5:17-18. Torati inatimilizwa kwa
amri ya upendo kwa Mungu na jirani. “Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu,
nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii,” Mt 7:12. Ni
ndani na katika Kristo Yesu tunapata neema na kweli kwa mkono wake. “Kwa kuwa
torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu
Kristo,” Yoh 1:17. Na huku ndiko kutimilika kwa sheria na kutamalaki kwa
upendo, kweli, na neema.
Leo pia unabii wote
ulionenwa juu ya Kristo na historia nzima ya wokovu wetu unakamilika. Unabii
huu unafika ukomo wake kwa uwepo wa Kristo ambaye ni UPENDO WA MUNGU kwetu.
Mtume Paulo anasema, “Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii
utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika,” 1Kor
13:8. Huyu ndiye Kristo Yesu! Kung’ara kwake Bwana wetu Yesu Kristo
kulikoonyesha Ufukufu wake, kunaamsha furaha ya ndani ya Mtume Petro na
kuyasema ya moyoni mwake. “Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa
vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya,” Mt
17:4. Hata hivyo hilo halikuwa kusudi la Yesu kubaki mlimani pale. Yesu
inabidi ashuke na kuukumbatia Msalaba kama alama ya ushindi na hapo ndipo
wokovu wako na wangu ulipotundikwa. Hii ndiyo safari kuelekea kilele kile cha
wokovu kama Masiha wa Msalaba.
Tatu, ni hatma yetu
iliyojengeka katika agano la milele. Kristo ndiye kielelezo chetu na wokovu
wetu. Leo Mungu Baba anauweka ukweli huu hadharani na kusema, Huyu ni Mwanangu,
mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye,” Mt 17:5. Hili ndilo
agano la milele kati yetu na Mungu, na Kristo akiwa ndiye daraja na mlango
halisi wa sisi kupitia kwani ni kwake tu tutakuwa salama kama njia, ni kwa
Kristo tu tunalishwa kweli katika kweli, na Kristo tu ndiye uzima halisi. Hivyo
hapana tena ufunuo ulio wa wazi na kamili zaidi ya ufunuo huu wa Mungu kupitia
mwanaye Mpenzi. Tendo hili linathibitishwa na sauti ya Mungu mwenyewe kwa
viumbe vyote, Mt 17:5. Ndugu yangu, Je, unafuata sauti gani katika maisha yako?
Sauti hii kutoka mbinguni inampa Yesu Kristo Heshima, Mamlaka, na Utukufu.
“Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti
iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye,”
2Pet 1:17. Nasi tunapoisikia sauti hiyo na kuishi kweli hiyo, twajazwa nguvu,
heshima na utukufu kwa kuishi ndani na katika Kristo.
Wapendwa wana wa Mungu, zipo sauti nyingi katika
maisha yetu. Je, sauti hizo zinatupeleka karibu na Kristo Yesu au zinatutenganisha
na kweli yake? Kusikia sauti hii ni kuyafanya mapenzi yake. Na kufanya mapenzi
yake Mungu maana yake tuyafanye kila mmoja kadiri ya wito wake. Hapo ndipo
ulipo msalaba wako, na kufaulu kwako ndipo ulipo utukufu wa msalaba wako.
Ndugu yangu, “kuna
furaha ya kweli na heshima kuifia ‘kweli na haki’ kwa wajinga ili waijue kweli
na haki, kuliko kufa kama mfalme kwa pongezi na makofi ya wapumbavu wadhanio
kuijua ‘kweli na haki ilhali hawaijui na wao wenyewe hawajijui.” Leo kuwa Mkristo kwa kubatizwa tu haitoshi.
Leo kuwa Mkristo kunakuhitaji kuwa mpiganaji halisi wa Kristo kama Mfalme wa
haki, kweli, upendo, unyenyekevu, huruma, msamaha, na uwazi. Ulimwengu uliojaa
dhuluma, ufisadi, na matendo ya uvunjifu wa haki za binadamu, hauwezi kamwe
kuukubali Ufalme wa Yesu Kristo kama nilivyosema.
Leo tulio wengi, yaani
Wakristo, tumewekwa katika kikaangio cha kukubaliana na mtazamo huo (dhuluma,
ufisadi, na uvunjifu wa haki za binadamu) au kuukataa kwa gharama kubwa sana
hata kuutoa uhai wako. Hakika njia iliyo rahisi na isiyo na mawaa ni kuusaliti
Ukristo (kumkana Kristo) wako kwa gharama nafuu kama alivyofanya Yuda Eskariote
kwa vipande thelathini vya fedha. Ndiyo maana leo wale tuliotegemea waseme na
kuukemea uovu wapo kimya, na wale waliojaliwa ufahamu wa kupembua mema na
mabaya wamekuwa wasaliti wa iliyo kweli na haki.
Ndugu yangu
unayesafari nami katika tafakari hii, kuwa Mkristo leo ni changamoto kubwa
sana, kama ilivyokuwa kwake Yesu Kristo kuutangaza Ufalme wa Mungu kwa Wayahudi
kwa kauli mbiu yake ile, yaani, “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu
umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili,” Mk 1:15. Jamii ya Yesu wakati ule
ilikuwa kama ndoto kuupokea ujumbe huu-kutubu na kuiamini Injili. Je, katika
hali hii, Yesu alirudi nyuma katika hili kwa vigezo vya kutokukubalika? La
hasha!
Kwa kuushindilia msumari wa moto
katika kusisitiza na kumaanisha asemacho, Yesu aliwapa wapinzani wake silabasi
ya utendaji wake kwa miaka ile mitatu. Naye anasema juu ya utendaji wake kama
ifuatavyo na itakavyokuwa: “Roho
wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari
njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona
tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na
kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19. Silabasi hii ndiyo
iliyokuwa hatma ya kifo chake kile cha aibu, yaani, kifo cha Msalaba. Msukumo
wa kifo hiki ni Upendo na furaha ya kweli katika haki, kwa kujua kile akifiacho
siyo kitu cha kubumba bali ndio ukweli wenyewe. Yesu anakuambia wewe na mimi,
“Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya
rafiki zake,” Yoh 15:13. Bwana wetu Yesu
Kristo amelifanya hili, nasi kama wafuasi wake ni changamoto kubwa kwetu leo.
Hakika
Kristo amekupenda wewe na mimi upeo, na kwa sababu hiyo alikuwa tayari na yupo
tayari hadi sasa kufa kwa ajili yako na mimi. “Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka,
Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda
kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo,” Yoh
13:1. Kwa nini basi Mkristo
mwenzangu unakuwa na imani ya mwono wa chura? Hivi leo nikikuuliza uniambia
ukweli kuhusu Chura ‘kama amesimama au kachuchumaa waweze nipa jibu sahihi?
Kigugumizi hiki cha kujua mkao wa Chura, ndicho kigugumizi juu ya imani ya Wakristo
wengi wa leo.
Wapendwa wana wa
Mungu, yote niliyoyasema ni kukuandaa ili uzame vizuri katika tafakari ya leo
na kadiri ya masomo yake. Mtume Paulo licha ya changamoto alizozikuta baada ya
kuongoka kwake, hakuwa tayari kubadilishwa na mtazamo wa wakati wake na
kujivika koti la uovu. Haki na kweli ndani na katika Kristo Yesu ilibaki kuwa
msingi wa imani yake. Hivyo Barua yake ya pili kwa Timotheo anapenda wafahamu,
na tufahamu kiini na msimamo wa imani yake. Naye anasema, “Namshukuru
Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile
nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana,” 2Tim 1:3.
Anaye kumbukwa hapa bila shaka ni Timotheo mwenyewe aliye mfano halisi wa kweli
na haki katika jumuiya yake.
Leo mambo hayako hivyo
hata kidogo. Baadhi yetu kama viongozi wa dini, na wenye kuijua iliyo kweli, na
hata kama hatuiamini kwa kupitia utaratibu uliowekwa kwa taasisi husika kama
hatua ya kuhesabiwa haki ya kuwa kile ulicho, tumekuwa waogeleaji wa kufuata
mawimbi ya maji bila kujali ustadi wa kuogelea kwetu tukitazama ng’ambo ile na
iliyo salama tunayotamani wote kuifikia. Hapa ndipo penye chimbuko la unafiki.
Hapa ndipo kwa makusudi makubwa kabisa katika fikiri, amua na tenda yetu,
wafuasi wetu hutushangaa kwa kwenda kinyume kabisa cha matazamio ya kweli ile
tunayoihubiri na matamanio yake. Hapa ndipo tunapoonekana si tu vituko, bali
watu tusiokuwa na maono na uelewa wa kile tukisemacho, na mwisho kuutabiri
unabii tusioujua ili tuenende na mawimbi ya nyakati zetu tusiyoyajua.
Mkristo mwenzangu,
niyasemayo siyo mageni mbele ya macho yako. Manabii hawa wa kubumba hawaoni
shaka wala haya hata kidogo leo kusema Edgar ndiye “chaguo lile la Mungu” leo
kwa watu wa Mungu. Je, kwa nini wanasema kama wasemavyo? Je, wanajua kile walicho
na yale waliyoyalia kiapo kwa ajili ya taifa la Mungu? Kwa nini basi
wanadanganyika kiasi hicho? Je, wanaifahamu karama ya Mungu ndani ya maisha na
utume wao? Mtume Paulo anamwambia Timotheo hivi, “Kwa sababu hiyo nakukumbusha,
uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu,” 2Tim
1:6. Kutokuchoka maana yake, usitafute urahisi wa jambo na kuutafsiri
vinginevyo na karama uliyonayo kwa kuyaona mawimbi ya muda tu katika wakati
wako. Kwa maana nyingine, palipo na giza tusema giza, na tufanye kadiri
iwezekanapo kuuleta mwanga, na palipo mwanga tusema mwanga na uutetee mwanga
huo ili udumu. Kwa nin basi katika hali hii twaingiwa na woga? Kwa nini tunakufa gazi pasipo ganzi? “Maana Mungu
hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi,” 2Tim
1:7. Katika mazingira ya utata kama huu tufanye nini?
Wapendwa wana wa Mungu,
katika mazingira na utata kama huo yatupasa kusimama katika kweli, hata kama
nikibaki mwenyewe. Yesu Kristo kwa kutambua ugumu huu anakuambia wewe na mimi
leo kwamba, “tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru
kweli kweli.” Yoh 8:32, 36. Mwana anatuweka huru, unapokuwa tayari kujiachia
katika minyororo ya upumbavu kwa kuwa tayari kujifunza na kumsikiliza. Hii
ndiyo habari njema ya wokovu, yaani, kulisikia neno, kulipokea neno,
kulitafakari neno, kulishirikisha neno, na kuwa shuhuda ya neno hilo kwa maisha
yako ya kila siku. “Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee
haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili,
kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si
kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema
yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele,” 2Tim 1:8-9. Je,
hili lasema lolote juu ya maisha yako kama Mkristo leo?
Leo mimi kama mfuasi wa
Kristo na muhudumu wake wa karibu, habari njema ya wokovu, yapaswa kuwa kipaua
mbele changu. Na habari njema ya wokovu kwa ufupi kabisa ni kulishinda giza
(dhambi) kwa kuukumbatia mwanga (utakatifu). Kwa habari hii njema ya wokovu,
“inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili
mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili; ambayo kwa ajili ya
hiyo naliwekwa niwe mhubiri na mtume na mwalimu,” 2Tim 1:10-11. Leo mimi kama
mfuasi wa Kristo, na kwa upekee kama mhudumu wa karibu (Mkleri), bila kuijua
habari njema, na kusoma alama za nyakati kadiri ya habari njema ile, ufuasi
wangu na ukaribu wangu hautakuwa na mguso wowote kati ya kile nilicho na
ushuhuda ule nipasao kuutoa. Nitabaki kuwa tukio kama utaratibu wa kawaida bila
historia kama sehemu ya mang’amuzi.
Ndugu yangu, unakuwa
historia kama sehemu ya mang’amuzi unapoyachukulia yale yaliyotokea katika
maisha yako, ukitazama kule unapokutamani kama hitimisho la kila kitu. Hapa
tumaini lipo hata kama linachelewa au kucheleweshwa. Hapa ndipo mateso kama
matukio katika maisha ya kila siku yanapata maana kama asemavyo Mtume Paulo,
kwamba, “Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya, wala sitahayari; kwa
maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile
nilichokiweka amana kwake hata siku ile,” 2Tim 1:12. Hapa siku ‘ile’ ya
maanisha ‘uzima ule wa milele’ tunao utamani.
Tumsifu Yesu Kristo!
"Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye;
msikieni yeye,” Mt 17:5
Tusali:-Ee Yesu na Mchungaji wetu,
tupatatie masikio hai na yenye kuisikia sauti yako daima hata pale
tunapochanganywa na kelele nyingi katika maisha yetu ya kila siku. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario