JUMAMOSI BAADA YA JUMATANO YA MAJIVU
Somo:
Isa 58:9b-14
Zab:
86:1-2, 3-4, 5-6
Injili:
Lk 5:27-32
“Na kama ukimkunjulia
mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako
itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri," Isa 58:10
“Ikawa Mafarisayo na waandishi wao kuwanung'unikia
wanafunzi wake, wakisema, Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na
wenye dhambi?” Lk 5:30
“Yesu akajibu akawaambia, Wenye afya hawana haja na tabibu,
isipokuwa walio hawawezi,” Lk 5:31
“Sikuja
kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu," Lk 5:32
TAFAKARI:
“Sikuja
kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
kipindi hiki cha kwaresma kinatutafakarisha na kutusogeza karibu zaidi na neema
na huruma ya Mungu. Kwa upande mwingine ni kuiona "furaha ya Mungu
ninapojirudi na kumrudia, pale ninapofanya toba ya kweli kama kieleleza cha
kuujenga tena uhusiano wangu na Mungu ulioathiriwa na dhambi zangu."
Pamoja na mapungufu yetu na ubinadamu wetu, bado Mungu hajakata tamaa kutupokea
kama tulivyo. Furaha yake ni kutupata hasa tunapofanya toba ya kweli. Huruma na
neema ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu.
Somo la kwanza la
tuonyesha namna ya kufanya toba hiyo. Baada ya kutubu na kuondolewa dhambi,
malipizi au toba yetu ya kweli ni kujifunua na kujiweka karibu na wale wote
wanaohitaji uwepo wetu, na kuwasaidia kadiri ya uwezo na nafasi aliyotupa
Mungu. Tunapolifanya tendo hilo kuwa letu kwa moyo mkunyufu, kiwi yetu na Mungu
inafanywa kama adhuhuri. "Na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako,
na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na
kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri," Isa 58:10
Ndugu yangu, unapoishi
hapa duniani kati ya moja ya mambo haya mawili waweza kuwa:-Ukiishi vizuri
unakuwa muhenga. Yaani mtu aliyeishi vyema na ameacha kitu cha kuigwa na
kusimuliwa kwa vizazi vyote. Na jamba la pili ni hili, usipokuwa muhenga basi
uwezekano wa kuwa mzimu ni mkubwa. Mzimu ni roho ovu/mbaya. Hapa hakuna cha
kuigwa wala kusimuliwa. Mtu anakosa na kupoteza historia yake. Na hata historia
hiyo ikikumbubwa hubeba yasiyo mema. Kuishi vyema na watu kwaitaji unyenyekevu
kama msingi wa fadhila zote. Unyenyekevu huu ni furaha ya Mungu. "Kumcha
Bwana ni maonyo ya hekima; na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu,"
Mit 15:33.
Ni unyenyekevu huu
unaotusukuma tena na tena kupenda kuishi na kila mmoja wetu. Ni unyenyekevu huu
unao tufanya kushuka chini kabisa kwa wahitaji. "Afadhali kuwa na roho ya
unyenyekevu pamoja na masikini, kuliko kugawanya nyara pamoja na wenye
kiburi." Mit 16:19. Kristo ndiye kielelezo cha unyenyekevu wa kweli.
Hakika huruma na neema ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu. Tendo la Yesu la
unyenyekevu na huruma linakuwa kero kwa Mafarisayo ambao kwa kiasi fulani
katika utendaji wao nasi tumo. “Ikawa
Mafarisayo na waandishi wao kuwanung'unikia wanafunzi wake, wakisema, Mbona
mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?” Lk 5:30. Ni mara ngapi wewe na mimi huendelea
kuwanyooshea vidole wale waliodondoka katika dhambi na uovu, na kutokuona tena
neema na huruma ya Mungu kwa watu hao wanapojirudi?
Injili yetu ya leo
inatupa furaha hiyo ya Mungu na toba ya mwanadamu kupitia mwanaye Yesu Kristo,
anaposema uwepo wake si kwa wenye haki, bali kwa wenye dhambi, na hilo ndilo
alilolijia, yaani, sote tuhesabiwe haki ya kuwa wana na warithi wa ufalme wake.
“Yesu akajibu akawaambia, Wenye afya hawana
haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki,
bali wenye dhambi, wapate kutubu," Lk 5:31-32. Mapaswa yetu wanadamu ni
kutambua tulipojikwaa na kumrudia Mungu. Mlango wa neema na huruma ya Mungu upo
wazi muda wote kupitia Sakramenti ya Upatanisho.
Wapendwa katika Kristo,
Maandiko Matakatifu yanatupa masimulizi mbalimbali kuonyesha furaha hii ya
Mungu-[neema na huruma yake]-mja wake anapofanya toba ya kweli. Tazama furaha
ya Baba kwa mwana mpotevu, (Lk 15:11-32). Mfano wa mwanakondoo aliyepotea na
shilingi moja iliyopotea. Vinapopatikana hivi vilivyopotea ni furaha kubwa sana
mbinguni. "Nawaambia, vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya
mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda
ambao hawana haja ya kutubu,"Lk 15:7.
Ndugu yangu, ni upendo
mkubwa sana kwetu kupata fursa hii na ukaribu huu na Mungu. Ni wakati mzuri wa
kupatanishwa naye. Tusisite kuijongea Sakramenti ya upatanisho. Wakati ufahao
ndiyo sasa.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Tena,
mtu mwovu atakapoghairi, na kuuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo
halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai. Kwa sababu atafakari, na kughairi, na
kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda,
hakika ataishi, hatakufa,” Eze 18:27-28
Tusali:-Ee Yesu na
Mwokozi wangu, asante kwa kuona na kuuthamini utu wangu hata katika hali ya
udhaifu wangu. Nijalie neema na nguvu ya kuziungama dhambi zangu zote bila aibu.
Amina.
No hay comentarios:
Publicar un comentario