sábado, 25 de marzo de 2017

TAFAKARI: JUMAPILI YA 4 YA KWARESMA-A


JUMAPILI YA 4 YA KWARESMA-A

Somo I: 1 Sam 16:1b, 6-7, 10-13a

Zab: 23:1-3a, 3b-4, 5, 6

Somo II: Efe 5:8-14

Injili: Yoh 9:1-41

Nukuu:

Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo,”

“Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake,” Yoh 9:3

“Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu,” Yoh 9:5

“Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho,” Yoh 9:6

“Basi yule mtu akajibu, Kwamba yeye ni mwenye dhambi sijui. Najua neno moja, kuwa mimi nalikuwa kipofu na sasa naona,”Yoh 9:25

“Yesu akasikia kwamba wamemtoa nje; naye alipomwona alisema, Wewe wamwamini Mwana wa Mungu?” Yoh 9:35

“Akasema, Naamini, Bwana. Akamsujudia,” Yoh 9:38

“Yesu akasema, Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, nao wanaoona wawe vipofu,” Yoh 9:39

 “Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa,” Yoh 9:41

“Enendeni kama watoto wa nuru,” Efe 5:8c

“kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli,” Efe 5:9

“Lakini yote yaliyokemewa hudhihirishwa na nuru maana kila kilichodhihirika ni nuru,” Efe 5:13

TAFAKARI: “Enendeni kama watoto wa nuru,” Efe 5:8c

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya nne ya Kwaresma ya mwaka “A” wa Kanisa. Mwaliko wa Dominika ya leo watutaka sote tuenende katika nuru na kama watoto wa nuru. Nuru ni alama na uwepo wa Mungu kati yetu, na kwa namna hiyo hiyo ni vita dhidi ya giza, yaani, uovu. Hivyo kuenenda katika nuru ni kuvipiga vita vya giza, yaani, aina zote zile za uovu.

Katika kweli hii, vita dhidi ya uovu vinaushindi katika mpango mathubuti wa Mungu kupitia watu wake aliowachagua na kupendezwa nao. Kunapotokea udhaifu katika vita hivi, Mungu umwinua mwingine katika kundi shindwa lile na kufanikisha hadhma yake.

Ni katika mantiki hiyo kwamba, baada ya Sauli kukosa sifa mbele za macho ya Mungu, Mungu anafanya zaidi kwa manufaa ya watu wake. Hivyo Mungu anawachagulia tena Mfalme wana wa Israeli. Samweli mtumishi wa Mungu anapewa maelekezo na Mungu na anafanya kadiri ya maelekezo hayo. Yese alikuwa na wana wazuri na wenye uwezo. Pamoja na hayo yote, Mungu anamchagua yule amtakaye kwa makusudi yake na watu wake.

Baada ya kukosekana yule amtakaye Mungu, Samweli mtumishi mwaminifu  wa Mungu anamuuliza Yese, “Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku,” 1Sam 16:11.

Mtazamo wa leo na msukumo wa kijamii na kisiasa ni vigumu sana kusikia sauti ya Mungu ndani ya mioyo yetu. Tunaishi sana katika ushabiki na wakati mwingine tunaingiwa upofu na kutokuona vitu sawasawa. Leo si jambo la ajabu kuona mtu asiyependwa na watu ndiye anayetangazwa kuwa mshindi na aliyechakuliwa na watu kwa kishindo. Demokrasia (iliyovikwa kama koti la dharura) kwa nchi zenye mfumo wa kimla ni kwamba wengi usema ila baadhi na wacheche sana ndio wanaoamua. Udhalimu huu hauna nafasi mbele ya Mungu. Kilicho cheupe na kiwe cheupe na kilicho giza na kitambulike kuwa giza. Kwa nini tunatanguliza nafsi zetu mbele zaidi ya kile atakacho Mungu kupitia watu wake?

Mungu wetu hatazami kama sisi tutazamavyo katika hulka na ushabiki wetu. Mungu hufanya kadiri ya ukamilifu wake. Nasi kama wanadamu tunaalikwa kila siku kuwa wakamilifu kama Yeye Mungu alivyo. “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mk 5:48. Ni vyema ufahamu uwepo wako hapa duniani. Ndugu yangu unanye safiri nami katika tafakari hii elewa kwamba upo hapa nduniani kupigana kufa na kupona juu ya cheo chako ambacho ni utakatifu wako. Mengine yote na fahari zake ni mbwembe tu. Huwezi kumwona Mungu kama si mtakatifu. Je, unajua hilo? Msema kweli ni mpenzi wa Mungu hakumaanishi “mbainisho wa hiki kizuri na hiki kibaya, bali kusimama katika kweli na haki pale ulipo, ukitambua dhamana uliyopewa na umma wa watu.” Bila hili kufanyika hayo yote utakayoyaainisha hubaki kuwa mbwembwe tu kama ulivyo upepo wa kisulisuli.

Hivyo, Daudi anapata sifa mbele za Mungu ingawa hakuwa matarajio ya familia ya Yese. “Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo,” 1Sam 16:7. Mungu utazama moyo ule unaomwelekea na kufanya mapenzi yake. Na katika jambo hili, kutenda lililo jema hakuwezi kugubikwa na mila na desturi zetu, bali katika kweli na haki.

Injili ya leo inachanganua taswira tatu katika vita hivi vya mwanga dhidi ya uovu. Moja; -Kristo Yesu ndiye mwanga halisi, Yoh 1:9, na kielelezo halisi cha upendo, huruma, kweli, na haki ya Mungu, Yoh 13:1. Na kwa kinywa chake Yesu anasema, “Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu,” Yoh 9:5.

Pili; -ni taswira ya wakumbatia uovu kulikotokana na kufa kwa dhamiri zao. Kwa nyakati zile za Yesu kundi hili lilibeba Mafarisayo, Waandishi, Masadukayo, na wale wote kwa namna moja au nyingine waliupinga mwanga ambao ndiye Kristo mwenyewe. Na leo kama ilivyokuwa nyakati zile za Yesu, watu hawa ni wale wote wanaojihesabia haki pasipo haki na kweli yenyewe. Ni wale wote wasiona upendo na huruma ya Mungu, na kutaka kuwa wasemaji wa Mungu kwa kujihesabia urafiki na Mungu. Ni wale wenye uhakika pasipo uhakika kwani hata wao wenyewe hawajijui sawasawa. Na hivi ndivyo wanavyojiinua, na kusema, “Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo,” Yoh 9:31. Je, mwenye dhambi hana sura na mfano wake Mungu? Na kwa maana hiyo Mungu hana upendo na huruma tena kwa huyu aliyedondoka katika tope la dhambi? Ndugu yangu, Mungu mwenyewe anakuambia wewe na mimi tulio wadhambi kwamba, “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu,” Isa 1:18.

Tatu; -ni taswira ya uovu wenyewe ikiwa ndilo giza lenyewe. Katika Injili ya leo Ndugu yetu kipofu ndiyo giza lenyewe ambalo Kristo aliye Mwanga analiondoa ingawa wakumbatia uovu hawapenda tendo hilo. Na sababu kubwa ya kutokupenda ni kwamba kile kilicho katika giza hufurahia kuwa katika hali hiyo hiyo isiyo kinzani. Ila kwa Mungu hali hii siyo ya kawaida na isiyovumilika. Naye Yesu anasema, “Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, nao wanaoona wawe vipofu,” Yoh 9:39. ‘Wanaoona wawe vipofu’ kwa maanisha wale wote wanaojiaminisha kuwa wanajua ilhali hawajui hubaki katika hali hiyo hiyo. Ni ulemavu katika ufahamu.

Maneno haya ya Yesu ‘Wanaoona wawe vipofu’ yanamtofautisha mtu ‘mjinga’ na ‘mpumbavu.’ Mjinga hujifunza kutoka katika hali yake ya kutokujua na kufika katika hali/hatua ya kujua asichokijua. Mpumbavu hana muda wa kujifunza kwa sababu anajiaminisha katika upumbavu wake kwamba anajua ilhali hajui chochote. Na hili ndilo jibu la Yesu kwa Mafarisayo waliotaka kujua kama na wao ni vipofu, Yoh 9:40. “Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa,” Yoh 9:41. ‘Kama mngekuwa vipofu msingkuwa na dhambi,’ kwa maneno mengine Yesu anawakumbusha kwamba, ‘kama mngekubali ujinga wenu wa kutokujua isingelikuwa kosa kwa sababu mngeukubali mwanga/kweli nanyi mngekuwa huru, Yoh 8:32.

Tukija kwenye taswira ya tatu, yaani, giza lenyewe ambalo katika Injili ya leo linawakilishwa na Ndugu yetu mwenye upofu halisi, Yesu anaweka wazi uhalisia wa tatizo lenyewe na kusema, “Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake,” Yoh 9:3. ‘Kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake’ kwa maanisha kwa upande mmoja hakuna lisilowezekana kwa Mungu hata kama kwa upeo na uwezo wetu wanadamu jambo hilo lishafika mwisho wake. Na kwa upande mwingine maneno haya ya Yesu yalibeba ujumbe mzito kwa kile alicho Kristo mwenyewe (Asili, Nguvu, na Mamlaka), yaani, Njia, kweli, na uzima, Yoh 14:6. Ndani na katika Kristo Yesu yote hayo matatu (Njia, Kweli, na Uzima) yawezekana pasipo shaka yo yote. Na hivi ndivyo ilivyokuwa kwa ndugu yetu yule Kipofu: “Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho,” Yoh 9:6, naye akapata kuona.

Pamoja na kuzongwa sana na kundi lile la wakumbatia uovu na vipofu wa kujinadi kama alivyo wathibitisha Yesu mwenyewe kuwa ni vipofu wanaoona, Ndugu yetu aliyepata kuona anatoa ushuhuda juu ya Kristo Yesu na kusema, “Kwamba yeye ni mwenye dhambi sijui. Najua neno moja, kuwa mimi nalikuwa kipofu na sasa naona,”Yoh 9:25. Huu ni ujumbe mzito sana kwa Mafarisayo na kwa wakati mwingine wewe na mimi tunaishi hali hii ya kifarisayo kwa nyakati tofauti tofauti. Je, tunaona sawasawa? Ndugu yetu aliyekuwa kipofu katika uhasili wake sasa anaona. Je, ndugu yangu unaona sawasawa? Yesu aliposikia wanamsonga sana kwa sababu la kile alichomtendea, alitaka kujua msimamo wa Ndugu yetu aliyeponywa kama kweli anaamini tendo lile. Yesu akamuuliza, “Wewe wamwamini Mwana wa Mungu?” Yoh 9:35. Naye akamjibu, “Naamini, Bwana. Akamsujudia,” Yoh 9:38. ‘Bwana akamsujudia,’ ni tendo la heshima kubwa sana mtu kupewa na hasa kutoka kwa Kristo mwenyewe.

Ndugu yangu, unaposimama katika kweli na haki ni tendo la furaha kubwa sana kwa Mungu ingawa katika ulimwengu wa giza yakupasa kulipa gharama yake. Tendo hili ni kuishi kweli ile na chapa ile ya Mungu ndani yako, Mwa 1:27. Ni kuwa kielelezo halisi cha upendo na furaha ya Mungu kama kiumbe chake. Chapa hii ya Mungu na uhasili wake ndani yetu tunaipoteza au kuififisha kwa kutenda dhambi.

Wito kwako na kwangu leo ni kwamba, ili tuwe salama mwili na roho yatupasa kuenenda “kama watoto wa nuru,” Efe 5:8c. Hapa ndipo tunadhihirisha kweli tu wanafunzi wa Kristo katika kweli na haki. Tuepuka bla bla nyingi zenye kumpamba Mungu kwa uzuri wa maneno yetu majukwani ili hali twatembea na upofu ulio tukuka kimwili na kiroho. Ndugu yangu tuliye safiri wote katika tafakari hii, “…tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli,” Efe 5:9. Kwa kuwa “…yote yaliyokemewa hudhihirishwa na nuru maana kila kilichodhihirika ni nuru,” Efe 5:13. Kristo Yesu ndiye Nuru yetu halisi, na kielelezo halisi cha hofu ya Mungu ndani mwetu. Tumwogope Mungu kwa kusimama katika kweli na haki.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa,” Yoh 9:41

Tusali:-Ee Yesu, tuondolee upofu wetu kama tunda la upumbavu wetu. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario