KUPASHWA HABARI YA KUZALIWA BWANA
Machi
25
Somo
I: Isa 7:10-14
Zab:
40:7-8a, 8b-9, 10, 11
Somo
II: Ebr 10:4-10
Injili:
Lk 1:26-38
“Kwa hiyo Bwana
mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanaume,
naye atamwita jana lake Imanueli,” Isa 7:14
“Ndipo aliposema,
Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi
alisimamishe la pili,” Ebr 10:9
“Usiogope, Mariamu, kwa
maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto
mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa
Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki
nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho,” Lk 1:30-33
TAFAKARI:
“Mpango wa Mungu wa wokovu wa mwanadamu; kupitia wanyenyekevu wa Moyo.”
Wapendwa wana wa Mungu,
Mama Kanisa leo anapoadhimisha sherehe ya kupashwa habari ya kuzaliwa Bwana,
tutafakari “Mpango wa Mungu wa wokovu wa mwanadamu; kupitia wanyenyekevu wa
Moyo.” Mungu aliye kusudi la mwanadamu, alikuwa na mpango naye tangu kabla ya
kuumba ulimwengu. Hakuna shaka kwamba uumbaji wa ulimwengu huu pamoja na uzuri
wake ni kwa mafaa ya binadamu na ufunuo wa Utukufu wa Mungu. Binadamu huyu
aliyekuwa kusudi la Mungu tangu kabla ya kuumbwa ulimwengu, kwa bahati mbaya
tendo hili ya pekee kwake hulichukulia la kawaida tu, na wakati mwingine kama
mastahili yake. Kiburi hiki cha mwanadamu ndicho kimtiacho majaribuni na
kutenda dhambi.
Hata baada ya kuanguka
kwa sababu ya dhambi, Mungu kwa upendo wake hakuacha mpango wake wa kumkomboa
mwanadamu. Huu ni upendo wa ajabu sana wa Mungu kwetu. Mungu kwa mara hii,
anakubali kuchukua umbo letu na kufanana nasi-“Kumwilishwa,” ili awe karibu
zaidi nasi. Mpango huu anaufunua kwa njia ya Ishara kupitia Nabii Isaya, na kusema,
“Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, Bikira atachukua mimba, atazaa
mtoto mwanaume, naye atamwita jina lake Imanueli,” Isa 7:14. Ishara hii inakuwa
wazi kupitia wale waliojawaliwa maisha ya unyenyekevu.
Bikira Maria anakuwa
kati ya wanyenyekevu wa Moya wa Mungu na aliyempendeza kwa namna ya pekee.
Bikira Maria anachukua jukumu la mzazi wetu wa kwanza-Eva, aliyeshindwa kwa
anguko la dhambi. Bikira Maria anapewa mastahili haya kwa unyenyekevu wake, na
siyo kwa sababu alikuwa mzuri sana au binti wa pekee sana katika mtaa wake au
kijiji chake, au umaarufu yake binafsi na familia yake. Mastahili haya anapewa
Bikira Maria kwa sababu ya udogo wake na unyenyekevu wake.
Malaika anatoa siri hii
na mpango huu wa Mungu kwa Mama Bikiria Maria. Tendo hili linampa Bikira Maria
hofu kubwa sana. Anapata hofu kwa kuona mpango mkubwa kama huu utakuwaje na
yeye ni nani hata Mungu ayafanye hayo yote kwake? Malaika anapoona hofu hii,
anamwambia, “Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama,
utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo
atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi
cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake
utakuwa hauna mwisho,” Lk 1:30-33
Ndugu yangu, kama hili
lingetokea kwako, ungelibeba moyoni kwa unyenyekevu kama wa Mama Bikira Maria?
Leo mmoja wetu anapochaguliwa kwa nafasi mfano ya Ubunge, tena wakati mwingine
kwa wizi wa kura, ona anavyojipambambanua kwa sifa bungeni. Nusu saa nzima kutoa
shukrani zilizojaa majigambo, mbwebwe, vijembe, na mwisho wa siku hakuna
anachofanya kwa kujitoa kwa wale waliomchagua. Ipo mifano mingi sana ya
kutokuwa na unyenyekevu kama huu wa Bikira Maria. Tujifunze kwa Mama yetu
Bikira Maria.
Yesu Kristo, ambaye
anabeba dhambi za sisi wanadamu, analo jambo moja tu la kufanya. Nalo ni
kufanya mapenzi ya Mungu, na si yake. Huu pia ni unyenyekevu wa hali ya juu. Ni
sadaka kubwa sana mtu anapoazimia kuutoa uhuru wake wote kwa sababu ya mtu
mwingine. Kuwa tayari kufanya yote bila kujibakiza kwa mafaa ya mtu mwingine
bila kuhesabu faida ni sadaka kubwa sana. Hii ni sadaka kubwa sana isiyo na
kipimo. “Ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la
kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili,” Ebr 10:9. Utii ni sadaka kubwa sana
unayeweza kutoa. Huwezi kuwa mtii kama si mnyenyekevu.
Ndugu yangu,
tunaposheherekea siku hii ya leo, tujifunze kuwa wanyenyekevu kama Mama yetu
Bikira Maria. Anza zoezi hili pale ulipo. Lianze kwenye familia yako na lifanye
kadiri ya nafasi yako katika hiyo familia kwa kuyatimiza yote yanayokuhusu kwa
unyenyekevu. Pili, lifanye jambo hili katika sehemu yako ya kazi, na sehemu
yeyote unapowajibika kwa ajili ya wengine. Ndugu yangu, ukilifanya hili kwa
moyo mkunjufu hakika Mungu atatenda mambo makuu kwako.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ndipo aliposema, Tazama, nimekuja
niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili,” Ebr
10:9
Tusali:-Kwa
maombezi ya Bikira Maria Mama Yetu, Ee Yesu nijalie fadhila ya unyenyekevu.
Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario