ALHAMISI WIKI YA 2 YA KWARESMA
Somo:
Yer 17:5-10
Zab:
1:1 1-2, 3-4, 6
Injili:
Lk 16:19-31
Nukuu:
“Bwana asema hivi,
Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake
Na moyoni mwake amemwacha Bwana,” Yer 17:5
“Amebarikiwa mtu yule
anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake,” Yer 17:7
“Mimi, Bwana,
nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake,
kiasi cha matunda ya matendo yake,” Yer 17:10
“Wanao Musa na manabii;
na wawasikilize wao. Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu
akifufuka katika wafu.” Lk 16:29,31
TAFAKARI:
“Kuishi bila hofu ya Mungu; kutotimiza wajibu na kutokujali.”
Wapendwa wana wa Mungu,
niwaalike tena kwa siku ya leo, tutafakari pamoja, “kuishi bila hofu ya Mungu;
kutotimiza wajibu na kutokujali.” Somo letu la kwanza laelezea hathari za
kuishi bila kuwa na hofu ya Mungu. Injili yatuelezea hathari za kutotimiza
wajibu na kutokujali.
Ndugu, tuanze safari
yetu kwa kutafakari kwa undani hathari za kutokuwa na hofu ya Mungu. Je, hofu
ya Mungu ni nini? Mpendwa, hofu ya Mungu ni kuishi kwa kumtegemea Mungu kwa
kila jambo. “Ee Bwana, Mungu wangu, umefanya kwa wingi Miujiza yako na mawazo
yako kwetu; Hakuna awezaye kufananishwa nawe; Kama ningependa kuyatangaza na
kuyahubiri, Ni mengi sana hayahesabiki,” Zab 40:5.
Ni kujenga mahusiano ya karibu na Mungu
kiasi kwamba huwezi fanya lolote bila kumshirikisha Mungu. Ndugu yangu,
“mkabidhi Bwana kazi zako, na mawazo yako yatathibitika,” Mit 16:3. Mtu
anayeishi katika hofu ya Mungu, upanga na Mungu, uwaza na Mungu, ushauriana na
Mungu, na uyakabidhi maisha yake mwenyewe na mipango yake yote kwa Mungu. Huku
ni kuishi katika baraka kama asemavyo Nabii Yeremia, “Amebarikiwa mtu yule
anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake,” Yer 17:7
Kuishi bila hofu ya Mungu
ni kujiamini kusiko fikirika. Ni kuamini na kutegemea vitu na mali, watu na
vyeo vyao. Huku ndiko tunapochuma laana kama anavyosema Nabii Yeremia, “Bwana
asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa
kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana,” Yer 17:5. Mtu wa mwono huu
kimaisha hawezi pata baraka. Mungu hana nafasi katika maisha yake. Na hapendi
kumpa Mungu nafasi.
Mtu asiye na hofu ya
Mungu huishi maisha linganishi mara zote. Mtu wa mtindo huu kimaisha hawezi
jipokea alivyo; na hivyo ni vigumu kufanya mabadiliko kimwili na kiroho. Mtu wa
mtindo huu awezi kuwa na furaha ya kweli. Muda wote huishi maisha ya ushindani
na kusahau jambo lililo la msingi katika maisha yake, yaani, Mungu hupendezwa
nawe kama ulivyo. Uwepo wako ulimwenguni hapa si bahati mbaya. Maisha bila
Mungu ni sawa na samaki bila maji. Hivyo ni wajibu wangu na wako kuitafuta sura
ya Mungu kila siku. “Bali mimi nikutazame uso
wako katika haki, Niamkapo nishibishwe kwa sura yako,” Zab 17:15. Kwa nini basi
itakupasa kuitafuta sura ya Mungu kila siku? Mtume Paulo anasema, “Na
kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake
yeye aliye wa mbinguni,” 1Kor 15:49. Na sura ya yule wa mbinguni ni UTAKATIFU.
Ndugu yangu, bila Utakatifu hakuna mbingu. Kuitafuta Sura ya Mungu ni kuutafuta
Utakatifu na kuuishi huo utakatifu tungali hai kila mmoja wetu kadiri ya
mazingira na wito wake.
Furaha ya kweli
haipatikani kwa mali tulizonazo; bali twaipata kwa kujipokea kama tulivyo na
kujua upendo wa Mungu ndani yetu. Yeye Mungu yupo tayari kutupokea na kutufanya
tena wana wake tunapokiri kupotoka kwetu na kumuasi. Mungu huturudishia hadhi
yetu na mastahili yetu kama watoto wake. Hii ndiyo furaha ya kweli ndani mwetu.
Hakuna mamlaka yoyote au binadamu yeyote awezaye kuyafanya haya. Ni Mungu tu.
Somo la Injili la tupa
kisa cha tajiri na maskini Lazaro. Tajiri anajulikana kwa mwono wake, na maisha
yake ya anasa. Lazaro anajulikana kwa jina lake, umaskini wake na unyonge wake.
Kosa kubwa la tajiri huyu ni dhambi ya kutotimiza wajibu. Ndugu yangu, kabla ya
kuendelea na tafakari hii nikuombe usali kwanza sala ya “NAKUUNGAMIA.” Dhambi
ya kutotimiza wajibu, ni kosa la nne tunalokiri katika sala hii ya “nakuungamia
Mungu mwenyezi.” Lazaro tunaambiwa mara zote alikaa kwenye mlango, ikimaanisha
kwamba kwa vyovyote vile tajiri huyu alimwona Lazaro katika dhiki yake na
ilimpasa tajiri huyu afanye kitu. Kutotimiza wajibu, ni kosa la kutokufanya
kitu wakati ulitakiwa kufanya kitu. Tajiri huyu anahukumiwa kwa kutokujali na
kutokufanya chochote.
Ndugu yangu, tazama
mazingira unayoishi, Je, akina Lazaro hawapo? Wale Mungu aliotubariki kuwa na
Magari binafsi, Je, unapofunguliwa geti hujamwona Lazaro pembeni akisubiri wema
na upendo wako? Wale ambao hula vizuri kila siku na asubuhi kumwaga viporo vya
wali na vipande ya samaki, Je, huwaoni akina Lazaro wakilichungulia shimo taka
kwa masikitiko? Wewe ambaye kila siku huingia ofisini na mkoba wako, Je,
humuoni Lazaro kwenye ‘benchi’ akisubiri wema na huruma yako?
Ukweli ni kwamba, wote
tutakufa na kujongea kiti cha ukumu. Tunapoishi hapa duniani, tunaaswa na
mzaburi, “usiogope mtu atakapopata utajiri, na fahari ya nyumba yake
itakapozidi. Maana atakapokufa hatachukua cho chote; utukufu wake hautashuka
ukimfuata,” Zab 49:16-17. Mambo yote yatupayo ufahari ipo siku tutayaacha. Je
mbele ya Mungu tutafika na jambo gani kama utambulisho wetu?
Ndugu yangu, ijumaa
ijayo, nakualika wakati wa njia ya msalaba utafakari kituo cha tisa; Yesu
anaanguka mara ya tatu. Njia ya msalaba kwa kutumia misale ya waamini, kuna
maneno haya katika kituo hiki cha tisa; “Mara nyingi mno ninajibovusha kwa
kupenda mno starehe, anasa na tafrija. Ee Yesu mwema, nisaidie kuufuata mfano
wa Mtakatifu Paulo, niutese mwili wangu na kuutumikisha, ili nipate siku moja
tuzo mbinguni.” Katika kujibovusha huko, hujakutana na akina Lazaro?
Tunapojitesa na
kuwajali wengine, hakika tutapata tuzo mbinguni. Mateso aliyoyapata Tajiri,
alitamani na kuomba taarifa zile ziwafikie ndugu zake ili wasije patwa na mateso
yale. Ibrahimu anamjibu, “wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao.
Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu.”
Lk 16:29,31. Ndugu yangu, hapa Musa anawakilisha Sheri za Mungu na Amri zake. Manabii
hapa ni wale wahudumu wa neno la Mungu. Kwa maana nyingine tungesema, sisi kama
wafuasi wa Kristo tunajua taratibu zitupasazo kuishi, ikiwa ni pamoja na Amri
za Mungu. Na Amri kuu kupita zote ni Amri ya upendo. “Mpende Bwana Mungu wako
kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya
kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo
ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika
amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii,” Mt 22:37-40 Pili, tumepewa
wachungani, na wapo muda wote kwa kutuhudumia hasa kiroho. Tunaonywa na
kufundishwa kupitia mahubiri yao. Kwa kuyashika haya mawili na kuyaishi, basi
tuzo tutalipata. Nje ya hapo tutegemee mateso makali.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea
Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake,” Yer 17:7
Tusali:-Ee
Yesu, tuepushe na dhambi ya kutokujali na kutotimiza wajibu wetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario