JUMANNE WIKI YA 1 YA KWARESMA
Somo:
Isa 55: 10-11
Zab:
34:4-5, 6-7, 16-17, 18-19
Injili:
Mt 6:7-15
Nukuu:
“ndivyo litakavyokuwa neno langu,
litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi
yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma, Isa 55:11
“Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa;
maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi,” Mt
6:7
“Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji
kabla ninyi hamjamwomba,” Mt 6:8
“Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa
mbinguni atawasamehe ninyi,” Mt 6:14
“Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu
hatawasamehe ninyi makosa yenu,” Mt 6:15:
TAFAKARI:
"Basi msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi
makosa yenu."
Wapendwa wana wa Mungu,
masomo yetu ya leo yanatualika kutambua wema wa Mungu na nguvu ya msamaha hasa
kwa somo letu la Injili. Somo la kwanza, nabii Isaya anatupa wema wa Mungu
katika mfano wa mvua. Mvua inyeshapo katika ardhi, vyote vyenye uwezo wa kumea
humea bila upendeleo. Iwe michongoma, matunda, maua rozi nk. Wema wa Mungu
haubagui walio wema na wabaya. Na “ndivyo
litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure,
bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale
niliyolituma, Isa 55:11. Kila dakika ya uhai wetu Mungu anatupa nafasi
ya kuwa wema kama Yeye. Tunapopoteza nafasi hiyo kwa kubeba magunia ya chuki,
visasi, lawama, wivu, majungu na kutowatakia mema wengine, ndipo tunapopoteza
uhai wa Mungu ndani yetu.
Ni kweli usiotia shaka
kwamba wengi wetu tushakufa kiroho licha ya kwamba bado tunatembea. Wema wa
Mungu kwetu ni mwelekeo wa kuyaona yote katika Yeye. Ndugu yangu, achia gunia
hilo na uwe uru mwili na roho. Kwa nini unawabeba wengine katika roho yako na
Mungu kukosa nafasi?
Injili ya leo Yesu
anatufundisha namna ya kusali. Anatoa angalizo katika sala. Sala ya kweli na
yenye utulivu ni kule kusali bila kupayuka. Ni sala ya kumsikiliza “mtu wa
ndani.” Ni kujisikiliza na kusikiliza matakwa ya Mungu. Ni utulivu wa ndani
ambapo katika utulivu huo tunakutana na Mungu. Hivyo kuabudu kuliko kwa kweli
ni kuabudu katika usahihi, uhalisi, tafakuri, na matendo hai. Kama haya mambo
hayafanyiki, kuabudu kwetu huwa kwa kupayuka payuka. “Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa
mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa
mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi
hamjamwomba,” Mt 6:7-8
Sala hii ya Baba yetu
ni ufupisho wa yale yote tunayotakiwa kufanya kila dakika tunapopumua. Mahitaji
yetu, utulivu wetu, matakwa yetu, uhusiano wetu na wengine, mahangaiko na
vishawishi vyetu vyote hupata majibu katika sala hii. Je, tunatafakari hayo
tusalipo sala hii ya baba yetu? Mfano swala la MSAMAHA. Kusamehe ni amri na sio
ombi. Yatupasa Kusamehe na hiki kicho kipimo cha sisi kusamehewa. “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao,
na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi,” Mt 6:14. Ndugu yangu, kusamehe siyo
kusahau uliotendewa. Ukweli ni kwamba hatuwezi kufuta aliyofanyiwa Yesu na kufa
kifo kile cha aibu msalabani. Ila tunasema msalaba ni ushindi tunapotazama
Utukufu wa Msalaba. ‘Huu ndio ule uti wa msalaba, ambao wokovu wa dunia
umetundikwa uu yake.’ Maneno haya ya ushindi na matumaini husemwa siku ile ya
Ijumaa Kuu unapofunuliwa msalaba uliofunikwa.
Unapomsamehe mtu mbele
yako upo Utukufu. Tunapokumbuka uchungu tuliofanyiwa tunapata faraja kwani
katika hilo tumeshinda kwa kusamehe. Ni faraja ya kweli na matumaini mapya.
Tusibaki kwenye uchungu wa mateso ila tukumbatie Utukufu ule wa milele. Hili
ndilo fumbo la kusamehe na Utukufu unaopatikana katika tendo hilo. “Bali msipowasamehe watu makosa yao,
wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu,” Mt 6:15. Na kwa kufanya hivyo
ndugu yangu, yaani, kutokusamehe kwako hakuna Utukufu wala Mbingu-Uzima wa
milele.
Mpendwa embu tulia na
fikiri uliyembeba kwa muda mrefu bila kumsamehe. Leo au kesho tafuta njia ya
kumsamehe. Ni vizuri akijua pia umemsamehe. Kwa tendo hilo unaleta pia uponyaji
kwako na kwake. Na fanya hivyo kwa upendo na uhuru. Wakati ndio sasa!
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kwa
maana Wewe, Bwana, U mwema, Umekuwa tayari kusamehe, Na mwingi wa fadhili, Kwa
watu wote wakuitao,” Zab 86:5
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, uliyeteseka na kufa kifo cha aibu kwa ajili yangu, yaponye maumivu
yangu yote ya ndani, na nijalie neema ya kusamehe yote pasipo kipimo. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario