domingo, 5 de marzo de 2017

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 1 YA KWARESMA


JUMATATU WIKI YA 1 YA KWARESMA

Somo: Wal 19:1-2, 11-18

Zab: 19:8, 9, 10, 15

Injili: Mt 25: 31-46

Nukuu:

“Usimdhulumu jirani yako, wala kumnyang'anya mali yake; ijara yake aliyeajiriwa isikae kwako usiku kucha hata asubuhi,” Wal 19:13

“Msitende yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki,” Wal 19:15

Na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto,” Mt 25:32-33

Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele,” Mt 25:46

TAFAKARI: “Changamoto katika imani ya kweli na matendo halisi, na yenye uhusiano wa wazi na Hukumu ya Mwisho.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, masomo yetu ya leo yanatualika kutafakari kwa kina katika kuhusisha imani ya kweli na matendo halisi. Kwa maana nyingine kuhusisha nadharia ya jambo na tendo halisi. Hii ndiyo “Changamoto katika Imani ya kweli na Matendo halisi, na yenye uhusiano wa wazi na Hukumu ya Mwisho.” Kama wewe na mimi ni wakristo na wafuasi waaminifu wa Kristo, tutakuwa si wa kweli kama tutasema hatujui nadharia ya Ukristo wetu. Bila shaka tunazijua vyema Amri za Mungu, na za Kanisa kwa upana wake. Ni kweli kwamba mara nyingi huzirudia amri hizi kama ndege yule Kasuku bila tafakari ya kutosha na mwisho kupoteza maana yake.

Kuna tofauti kubwa sana kati ya kukijua kitu kinadharia, na kuchukua nadharia ile katika matendo. Somo la kwanza linaongelea Amri za Mungu na Utakatifu wake katika maana pana, yaani, nadharia. Na Mungu analiweka jambo hili ili tumtambue kuwa yeye ndiye Bwana (Wal 19: 14b, 16b, na 18b). Injili ya leo inatutoa kwenye nadhari ya jambo na kutupeleka kwenye uhalisia wa jambo, yaani tendo halisi linalo akisi nadharia yenyewe. Ni katika mantiki hii, Yesu anazifupisha Amri hizi za Mungu katika mambo makuu mawili; Kumpenda Mungu na Jirani. Yesu anasema, “nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi,” Mk 12:30-31. Injili ya leo (Mt 25:31-46) inatudai kuziweka amri hizo kwenye matendo. Na swali kubwa na la wazi la kujiuliza ni hili; nimefanya nini kumjali mwenye njaa, mgonjwa, aliye uchi, mfungwa, nk. Haya ndiyo mazingira wewe na mimi tunayoishi kila siku na yakawaida kabisa.

Wapendwa wana wa Mungu katika ukweli huu hakuna cha kujitetea na wala kujihesabia haki. Mimi na wewe tutapigwa na mshangao mkubwa siku hiyo ya mwisho. Mara nyingi na walio wengi kati yetu huonekana wakiwa karibu sana na wahitaji na hata kuwapigia upwatu wa nguvu. Bila shaka ukaribu wao kwa wahitaji si kwa lengo la kuumizwa na kutaka watoka katika hali zao, bali ni njia moja wapo ya kujiinua nafsi zao na kutafuta kuhurumiwa na jamii kwa matendo yao hayo yasiyokuwa na chembe yoyote ya huruma ya Mungu. Hawa ndio Yesu anaosema wanayafanya hayo yote ili wajihesabie haki pasipo haki. “Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia?” Mt 25:37-39. Je, ni kweli kabisa kwamba vituo vyote vyenye kutoa huduma na kuwalea mayatima vinafanya hivyo kwa dhamiri iliyo safi? Ndugu yangu, tusisahau maneno haya ya Mfalme siku ya hukumu, “Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi,” Mt 25:40. Je, nifanye nini basi?

Kila mmoja wetu na ayatazame mazingira yake, na aanze pale alipo kwa kujiuliza maswali haya mawili; Je, hao wahitaji anaowazungumzia Yesu hawapo hapa nilipo? Kama wapo, ninampango gani nao kadiri ya uwezo wangu na mazingira yangu? Ni kweli kama Waswahili wasemavyo, “mbuzi hula urefu wa kama yake.” Hivyo kadiri ya nguvu na uwezo alionijalia Mungu yanipasa kufanya chochote kwa wahitaji walioainishwa na Kristo Yesu katika Injili ya leo. Tukumbuke pia kosa la Tajiri yule na Lazaro masikini (Lk 16:20-31) halikuwa juu ya ubaya wa utajiri wake. Kosa la yule tajiri lilikuwa hali yake ya kutokujali hitaji la Lazaro na siyo utajiri wake. Hii ni dhambi ya kutokutimiza wajibu. Utajiri na vipawa tulivyopewa na Mungu vina maana tu pale tunapofaidiana. Huku ndiko Yesu anaposema siku ya mwisho kutakuwa na mtengano kati ya Kondoo na Mbuzi, akimaanisha Kondoo ni wale walioenenda njia ya Bwana kwa kuishi wanayoamini na kuwajibika katika matendo (Mt 25:34-36), na  mbuzi ni wale walioenda kinyume kwa kuamini wasiyoishi kwa matendo (Mt 25:41-43). Ndugu yangu tuliyesafiri sote katika tafakari hii, wajiandalia uwepo wa kundi gani kati ya Kondoo na Mbuzi?

Hakika hapa wengi tutapigwa mshangao. Ni wazi kabisa kama bado ningali hapa duniani na kwa hiari yangu nimeamua kuwa kama mbuzi, ni kwa namna hiyo hiyo nitakavyo jiandalia mahali pangu mara baada ya maisha ya hapa duniani ambayo ni jukumu la muda mfupi. "Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele," Mt 25:46. Basi ndugu zangu, tuchague haki na kuishi imani ya kweli katika matendo halisi na ya kweli ili tuishi milele mara baada ya maisha haya ya hapa duniani.

Tusifu Yesu Kristu!

Mwenye haki atasitawi kama mtende, Atakua kama mwerezi wa Lebanoni. Waliopandwa katika nyumba ya Bwana Watasitawi katika nyua za Mungu wetu. Watazaa matunda hadi wakati wa uzee, Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi,” Zab 92:12-14

Tusali:-Ee Yesu Mfalme wa Amani, tujalie amani na upendo wa kweli katika jamii yetu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario