ALHAMISI WIKA YA 1 YA KWARESMA
Somo:
Est 14:1, 3-5, 12-14
Zab:
138:1-2ab, 2cde, 7c-8
Injili:
Mt 7:7-12
Nukuu:
“Ee Bwana, Wewe ndiwe mwenye haki. Utukumbuke, Ee
Bwana; ujifunue wakati wa taabu yetu, unipe moyo thabiti, Ee Mfalme wa miungu
na Bwana wa milki zote,” Est 14:4
“Unitie kinywani mwangu maneno ya kufaa mbele ya
simba, ukaugeuze moyo wake apate kumchukia Yule anayepigana nasi, ili akomeshwe
pamoja na wote wenye nia moja naye,” Est 14:13
"Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona;
bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye
huona; naye abishaye atafunguliwa." Mt 7:7-8
“Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto
wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao
wamwombao?” Mt 7:11
“Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi
watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii,” Mt 7:12
TAFAKARI: “Kujiachia katika Sala: ‘Ee Bwana, Wewe ndiwe mwenye haki.’”
Wapendwa wana wa Mungu, leo tutafakari namna ya
"kujiachia katika sala." Masomo yetu ya leo
yanatuelekeza katika fundisho hilo. Somo la kwanza, Malkia Esta anatupa mfano
hai wa kujiachia kabisa katika sala. Kujiachia katika sala, kwanza kabisa ni
kutokuwa na shaka kwa kile unachoomba. Pili, kutokuwa na shaka kwa yule
unayejisalimisha kwake, yaani Mungu. Tatu, kuamini kuwa umeshapata hata kama
bado. Atua hii ya tatu inaitwa "atua ya utakatifu katika sala."
Wengi wetu hatufiki
hatua hii ya tatu kwa sababu zifuatazo; kwanza hatujiamini na hatuamini
tuombacho. Pili, uhusiano wetu na Mungu ni wamashaka. Mungu wetu kwa mtazamo
huu, ni yule ambaye, "labda inawezekana." Tatu, Hatuna utulivu wa
ndani katika kuomba. Tunamuharakisha Mungu atende tunavyotaka. Hatumpi Mungu nafasi
ya kutenda apendavyo na ifaavyo kwetu. Tunajilinganisha na Mungu na kusahau
kuwa sisi na yale tunayoomba ni mali yake na yanawezekana kwa uwezo wake.
Malkia Esta katika sala
yake anatambua kabisa nje ya Mungu hakuna lolote na yeye si lolote. Esta anajisalimisha
na kujiachia hivi: "Bwana wangu, Wewe peke yako u Mfalme wetu. Unisaidie
mimi niliye mkiwa, wala sina msaidizi mwingine ila Wewe; maana hatari yangu imo mikononi mwangu."
Est 14:4
Kutawanya mawazo katika
sala ni tatizo lingine la walio wengi. Mfano: unamwomba Mungu akuwezeshe
kununua gari, huku ukiwa na mashaka kama gari hilo litakuwa na "spare
tyre,"-tairi la akiba.
Ndugu yangu, sala ya
kujiachia ni kutotia shaka kabisa, na kumwambia Mungu atende kwa kadiri
impendezavyo Yeye. Itakuwa vigumu kufaidi minofu ya nyama ukiwa na kisu butu. Sala
kama kisu, kinapaswa kuwa kikali ili kitimize kazi yake kama kisu. Ikiwa ndivyo
sivyo, hatuwezi kupata yale tuombayo kama Mtume Yakobo anaposema, "hata
mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa
zenu." Yak 4:3. Uimara huu wa sala wenye kubeba nia nzuri tunajifunza
kutoka sala ya Malkia Esta. Naye anasali hivi: “Unitie kinywani mwangu maneno
ya kufaa mbele ya simba, ukaugeuze moyo wake apate kumchukia Yule anayepigana
nasi, ili akomeshwe pamoja na wote wenye nia moja naye,” Est 14:13.
Somo la Injili linatupa
hakikisho la yale tuombayo, tutafutayo na tuyasalimishayo kwa Mungu. Hakikisho
hili la kuyapata haya tuombayo ni pale tu tunapojiachia kwake. Hapa yatupasa
kwenda zaidi ndani. Je, kuomba, kutafuta, na kujisalimisha/kubisha hodi katika
sala kuna maanisha nini?
Wengi wetu katika jambo
hili tunashindwa mara zote kufahamu maana yake. Mungu kamwe habariki utupu
licha ya kwamba uwezo huo anao. Labda ni kukumbushe tu mifano miwili. Mfano wa kwanza
ni ishara ile ya kwanza kule Kana. Yesu anabadili maji kuwa divai (Yoh 2: 1-11).
Kabla ya ishara hii Yesu anawaambia, "jalizeni mabalasi maji. Nao
wakayajaliza hata juu." Yoh 2:7. Kuna maanisha nini? Je, isingetosha Yesu
kuinua mikono yake juu na mapipa ya divai kudondoka?
Ishara nyingine ni ile
ya mikate ambapo watu walikula mikate na samaki hadi wakasaza makapu 12. Kabla
ya kufanya ishara hii, Yesu anawauliza wanafunzi wake, "Mnayo mikate
mingapi? Nendeni mkatazame. Walipokwisha kujua wakasema, Mitano, na samaki
wawili," Mk 6:38. Kwa nini Yesu awaulize swali hili? Isingetosha kuinua tu
mikono yake na mikate na samaki kudondoka kama mvua ya mawe?
Ndugu yangu, huku ndiko
Yesu anapomaanisha, "kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona;
naye abishaye atafunguliwa." Mt 7:8
Ukweli ni kwamba Mungu
habariki utupu. Yatupasa kufanya kitu. Hubariki yale tujitahidiyo kufanya na
yale ambayo tuna malengo mathubuti nayo.
Haiwezekani kushinda
shindano la Coca-cola ikiwa wewe ni mpenzi wa Pepsi Cola. Hata ungekesha kusali
mwaka mzima utatoka pakavu. Yakupasa kunywa soda ya Coca-Cola ili upate fursa
ya kubandua visoda vyake, ikiwa ni njia mojawapo ya kushinda shindano hilo.
Unapoweka sala kwenye tendo hilo utakuwa umeshafanya yote matatu; kuomba,
kutafuta na kubisha hodi/kujisalimisha. Hapa hakika baraka utapata kwani huku
ndiko kujiachia. Na Yeye atakupa kadiri aonavyo inafaa. Kwani, "maana ni
yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki,
badala ya samaki atampa nyoka?" Lk 11:11.
Pamoja na kujiachia
katika sala kwa mtindo niliusema, yakupasa kufanya mambo makuu manne wakati
Mungu anapoonekana kuwa mbali. Mambo hayo ni haya yafuatayo: Kwanza, mwambie
Mungu ukweli unavyohisi. Pili, angalia zaidi Mungu ni nani, yaani asili yake
isiyobadilika [wema na upendo wa Mungu, Mungu mwenye nguvu zote, Mungu ajuaye
kila kitu katika maisha, Mungu mtawala wa kila kitu, Mungu ayeokoa]. Tatu,
mwamini Mungu katika kutunza ahadi zake, na nne, kumbuka yale Mungu
ameshakutendea. Katika mambo haya manne, leo tutafakari hili la nne, “kumbuka
yale Mungu ameshakutendea,” na haya matatu tutayatafakari kwa undani wakati
mwingine.
Ndugu yangu, kama Mungu
hajakufanyia chochote kamwe, bado anastahili sifa zako daima maisha yako yote
kwa sababu ya alichokifanya Yesu msalabani. MWANA WA MUNGU ALIKUFIA! Hii ni
sababu kubwa ya kuabudu. Kwa bahati mbaya, tunasahau mambo magumu ya kina ya
sadaka ya maumivu makali aliyoitoa Mungu badala yetu. Mazoea huleta kutosheka.
Hata kabla ya kusulubiwa kwake, Mwana wa Mungu alivuliwa nguo, akapigwa vibaya
sana, akadhihakiwa na kuchekwa, akavikwa taji ya miiba, na akatemewa mate.
Alidhalilishwa na kudhihakiwa na watu waovu,
akatendwa vibaya kuliko mnyama.
Kisha, akiwa karibu
kuzimia kwa sababu ya kupoteza damu nyingi, alilazimishwa kubeba msalaba kwenda
mlimani-[Golgotha-fuvu la kichwa (Mt 27:33, Mk 15:22, Lk 23:33, na Yoh 19:17)],
alipigwa misumari juu yake, na aliachwa afe pole pole, kifo cha mateso ya
kusulubishwa. Damu yake ya uhai ilipomwagika, watu wenye maudhi walisimama na
kumtukana huku wakimpa changamoto ya kuhoji uhusiano wake na Mungu.
Akisha Yesu kuchukua
dhambi ya binadamu na hukumu yake, Mungu alitazama pembeni mwa sehemu hiyo ovu,
na Yesu alilia katika hali ya kulemewa sana, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona
umeniacha?” Yesu angeweza kujiokoa mwenyewe lakini asingekuwa amekuokoa wala kuniokoa.
Maneno hayatoshi
kueleza giza la wakati huo. Kwa nini Mungu aliruhusu na kuvumilia mateso maovu
kiasi hicho. Kwa nini? Mungu aliyaruhusu na kuyafanya hayo yote ili wewe na
mimi tuweze kuokolewa na kuzimu ya milele! “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa
dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye,” 2Kor
5:21. Yesu aliacha vyote ili wewe na mimi tupate vyote. Alikufa ili wewe na
mimi tuishi milele. Jambo hilo tu linatosha kukufanya umshukuru na kumsifu
daima. Usijiulize kamwe jambo la kushukuru.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye,
mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au
akiomba samaki, atampa nyoka?” Mt 7:9-10
Tusali:-Ee
Yesu tujalie sala ya utakatifu kwa kwa yale tukuombayo na utupe kadiri ya
hitaji letu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario