ALHAMISI WIKI YA 4 YA KWARESMA
Somo:
Kut 32:7-14
Zab:
106:19-20, 21-22, 23
Injili:
Yoh 5: 31-47
Nukuu:
“Na Bwana akaughairi
ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake,” Kut 32:14
“Wala hamtaki kuja
kwangu mpate kuwa na uzima. Mimi siupokei utukufu kwa wanadamu. Mwawezaje
kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa
Mungu aliye wa pekee hamwutafuti?” Yoh 5:40-41,44
TAFAKARI:
“Huruma ya Mungu, Uzima, na Utukufu ndani na katika Yesu Kristo.”
Wapendwa wana wa Mungu,
“Huruma ya Mungu, Uzima na Utukufu ndani na katika Yesu Kristo.” Somo la kwanza
Mungu anaonyesha huruma kwa watu wake kupitia Mtumishi wake Musa “…alipokuwa
amekwisha zungumza na Musa katika mlima wa Sinai, akampa hizo mbao mbili za
ushuhuda, mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa chanda cha Mungu,” Kut 31:18,
waliobaki chini wakisubiri maelekezo hayo ya Mungu, walijifanyia mambo yao kwa
kujichongea sanamu zoa kama utambulisho wa Mungu wao wa kutengeneza. Hili
lilikuwa ni chukizo kubwa kwa Mungu. Kwa hasiri hii Mungu anataka kuliangamiza
taifa lote la Israeli kwa kutokuwa na subira. Bwana akamwambia Musa, “Mimi
nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu. Basi sasa niache,
ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize,” Kut 32:9-10.
Musa analiombea taifa
lake, kwa kumkumbusha Mungu ahadi zake alizozitoa na kuzifanya na Ibrahimu,
Isaka na Israeli. Kwa huruma yake Mungu, “…akaughairi ule uovu aliosema ya
kwamba atawatenda watu wake,” Kut 32:14. Mungu wetu ni Huruma na mara zote yupo
tayari kuturumia na kutusamehe tunapoyakiri makosa yetu na kumrudia. Huruma hii
ya Mungu iwe pia ndani yetu hasa pale ninapotakiwa kutoa huruma hiyo bila
masharti katika kusamehe. Huu ndiyo mwito wetu pia sisi sote tunaomwamini
Mungu, na Mwanaye Yesu Kristo.
Injili yetu ya leo
inatupa msingi wa kile tuaminicho na malengo yetu kama wafuasi wake Kristo.
Ndugu yangu, uzima wako na utukufu wako hauwezekani pasipo kuwa ndani ya Kristo
na katika Kristo. Wayahudi hawaukubali ukweli huu, na badala yake wanamdhihaki
Yesu Kristo kwa kutokuamini kwao. Hawatambui pia yale yote yaliyofunuliwa juu
ya Kristo katika safari nzima ya historia hii ya wokovu. Yesu anasema mshitaki
wao mkuu ni kazi zake, na yale yote yasemwayo kuhusu Yeye katika Maandiko
Matakatifu. “Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba; yuko anayewashitaki, ndiye
Musa, mnayemtumaini ninyi. Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi;
kwa sababu yeye aliandika habari zangu,” Yoh 5:45-46.
Uzima na utukufu wetu
wapatikana katika Kristo kwani Yeye yupo kwa ajili ya hayo na ameyafia hayo.
Yatupasa kuyaamini atufundishayo. Na kama hatuyaamini atufundishayo tuziamini
kazi zake. “Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima. Mimi siupokei utukufu
kwa wanadamu. Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na
utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti?” Yoh 5:40-41,44.
Utukufu wa kweli ni ule utokao kwa Mungu, ambao kwa namna ya pekee ndiyo Yesu
Kristo anatujalia sisi kutipitia mateso, kifo na ufufuko wake. Hakuna utukufu
kwa Mkristo bila msalaba. Uzima huu twaupata kwa kula na kunywa damu yake
katika mastahili 1Kor 11:27, ikiwa ndiyo njia ya pekee ya kushiriki mateso,
kifo, na utukufu wa Kristo. “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao
uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:54.
Ndugu yangu, wakati
ndiyo sasa wa kujipanga sawa sawa na kujua uzima na utukufu wako unatoka wapi.
Ishi imani yako ipasavyo na “msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine
nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si
kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida.” Ebr 13:9.
Tumsifu Yesu Kristo
“Lakini
ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohana; kwa kuwa zile kazi
alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya
kwamba Baba amenituma,” Yoh 5:36
Tusali:-Ee
Yesu Kristo, nakiri na kuamini kwamba Uzima na Utukufu vya toka kwako tu Wewe
uliye yote katika yote. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario