domingo, 26 de marzo de 2017

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 4 YA KWARESMA


JUMANNE WIKI YA 4 YA KWARESMA

Somo: Eze 47:1-9, 12

Zab: 46:1-2, 4-5, 7-8

Injili: Yoh 5:1-3a, 5-16

Nukuu:

“Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko, maana maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi popote utakapofikilia mto huo,” Eze 47:9

“Akawajibu, “Yeye aliyenifanya kuwa mzima ndiye aliyeniambia, ‘Jitwike, uende,’” Yoh 5:11

TAFAKARI: “Uzima na uponyaji upo ndani na katika Yesu Kristo.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, “uzima na uponyaji upo ndani na katika Yesu Kristo.” Maono ya Nabii Ezekieli juu ya mto wa uponyaji ambao chanzo chake ni patakatifu, unatupa maandalizi ya Mungu katika uponyaji ambao umekamilika ndani na katika Yesu Kristo. Ndani ya maji hayo kutakuwa na uzima na kila kiumbe kitapata uhai. “Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu. Na matunda yake yatakuwa ni chakula, na majani yake yatakuwa ni dawa,” Eze 47:12

Ndugu yangu, neema na baraka kadiri ya maono ya Nabii Ezekieli kulingana na  mto huu zipo ndani ya Kristo, na Kikanisa zinajidhihirisha katika sakaramenti zake. Katika Injili ya leo, uzima na uponyaji wajidhihirisha katika Kristo. Ndani ya Kristo tunapata uhai na uzima tele. Ndani ya Kristo tunapata neema na baraka. Ndani ya Kristo tunatambua njia, kweli, na uzima kuelekea umilele.

Katika uponyaji huu, Yesu anamuuliza huyu asiyejiweza, “Wataka kuwa mzima?” Yoh 5:6. Ingawa jibu la huyu asiyejiweza haliendani na swali (“Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu wingine hushuka mbele yangu,” Yoh 5:7), Yesu anajua mateso na mahangaiko yake, na hivyo analitenda jambo kuu kwa ndugu huyu.

Yawezekana kutokana na mahangaiko na mateso tuliyonayo, iwe ni ugonjwa au kitu kingine, yameshatufanya tupoteze ufahamu na mwelekeo wa matumaini. Lakini tukumbuke kwamba katika hali hiyo Yesu anatuuliza kama twataka kuwa wazima. Yesu anaturudishia hadhi yetu na utu wetu kuufanya upya na kutufanya tuanze maisha mapya. Angalisho kubwa katika maisha haya mapya, ni kutokutenda dhambi. “Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi,” Yoh 5:14.

Ndugu yangu, tunaishi katika neema na baraka zake Mungu tunapokuwa katika hali ya usafi kiroho na kimwili, yaani hali ya kutokutenda dhambi. Kwa kipindi hiki cha kwaresma tunapotafakari mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, ni kipindi pia cha kujitakasa kwa sala, na kuziungama dhambi zetu. Ndugu yangu, “tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala nena lake halimo mwetu,” I Yoh 1:8-10

Tumsifu Yesu Kristo!

 Maana kwako Wewe iko chemchemi ya uzima, Katika nuru yako tutaona nuru,” Zab 36:9

Tusali:-Ee Yesu, ndani yako na katika wewe upo uzima na uponyaji. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario