JUMANNE WIKI YA 2 YA KWARESMA
Somo:
Isa 1:10, 16-20
Zab:
50: 8-9, 16bc-17, 21, 23
Injili:
Mt 23:1-12
Nukuu:
“Jiosheni, jitakaseni;
ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;
jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni
yatima haki yake; mteeni mjane,” Isa 1:16-17
“Bali ninyi msiitwe
Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu,” Mt 23:8
TAFAKARI:
“Utayari wa Mungu kusamehe; Yesu Kristo Mpatanishi wetu na Mungu na mwenye mamlaka
ya kusamehe dhambi.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, leo tutafakari kwa pamoja “Utayari wa Mungu kusamehe; Yesu Kristo
Mpatanishi wetu na Mungu na mwenye mamlaka ya kusamehe dhambi.” Ndugu yangu,
mwito wa Nabii Isaya kwa watu wa Sodoma na Gomora, ni kuacha njia mbaya na
kumrudia Mungu. Mungu yupo tayari muda wote kusamehe kwa sababu MSAMAHA ni moja
ya uhasili wake.
Mungu daima ni, “mwenye
kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala
si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza
watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha nne,” Kut
34:7.
Tendo la kuwapatiliza
watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha nne, ni
matokeo ya laana. Laana ni kinyume cha baraka. Kwa upande mwingine, laani
huenda hadi kizazi cha nne. Kwa mantiki hiyo, yapo mambo fulani watu huteseka
bila kujua, na chanzo chake yawezekana watu fulani, wakati fulani, hawakuenenda
katika njia ya Bwana.
Kuepuka tatizo hilo,
Nabii Isaya anawatahabarisha watu wa Sodoma na Gomora na kusema kwamba,
“Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu;
acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki;
wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteeni mjane,” Isa 1:16-17
Ndugu yangu, upendo wa
Mungu kwetu na utayari wake wa kusamehe hauna mfano. Kinachotokea kwa upende
watu, ni kukubali kufa na tai shingoni, ni kwa sababu ya kiburi chetu. Chapa
tulioyonayo ya sura na mfano wake Mungu, Mwa 1:27, ndiyo mvuto mkubwa wa hurama
yake kwetu. Mungu wetu hapendi kuona tunaangamia bure. Anasema hata kama
tungekuwa na dhambi nyekundu kama bendera, yupo tayari kusameha na kuzifanya
nyeupe kama sufu, Isa 1:18.
Mpendwa, kwa nini
unakubali kuumwa na mbwa aliyefungwa na kamba kwenye mti? Dhambi, ni kujipeleka
ukijua kabisaaa! Wokovu ni kumrudia Muumba wako ukijua uzuri na wema wake. Hata
hivyo, pamoja na madhaifu yetu, Mungu bado hajakata tamaa nasi.
Pamoja na watu
kutokutambua wema wa Mungu, “ila wakakataa kutii, wala hawakuyakumbuka maajabu
yako, uliyoyafanya kati yao; lakini wakafanya shingo zao kuwa ngumu, na katika
kuasi kwao wakaweka jemadari, ili wairudie hali ya utumwa; lakini wewe u Mungu,
uliye tayari kusamehe, mwenye neema, mwenye huruma nyingi, si mwepesi wa
hasira, u mwingi wa rehema, basi hukuwaacha,” Neh 9:17.
Ndugu yangu, watu wengi
hujihukumu wenyewe na kujifungia neema za kupatanishwa na Mungu. Ni kosa kubwa
kuishi katika hatia fulani. “Na kama mtu akifanya dhambi, na kutenda mambo hayo
mojawapo ambayo Bwana alizuilia yasifanywe, ajapokuwa hakuyajua, ni mwenye
hatia vivyo, naye atachukua uovu wake,” Wal 5:17. Lakini Mungu wetu hakai na
hasira yake milele. Kufanya hivyo ni kinyume cha uhalisia wake. Yeye hufurahia
rehema. “Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia
kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hashiki hasira yake milele, kwa maana
yeye hufurahia rehema,” Mik 7:18.
Katika Injili yetu ya
leo, Yesu anatoa angalizo kwa wanafunzi wake akisema wawe macho juu ya waandishi
na mafarisayo kwa kujihesabia haki na kukaa katika kiti cha Musa. Wapendwa,
Musa anawakilisha sheria. Mafarisayo na waandishi kukaa katika kitu cha Musa ni
kuwa juu ya Sheria za Mungu. Wanajichukulia mamlaka yasiyo yao, na kuwabebesha
watu mizigo mizito isiyo bebeka.
Ushauri wa Yesu kwetu
kuhusu Mafarisayo na Waandishi, ni kutenda na kuisha wasemayo, ila kwa mfano wa
matendo yao tusitende. Yesu Kristo anaona kasoro ya watu hawa na anawakemea kwa
kusema, “ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu
ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi
waingie,” Mt 23:13. Wanausema na kuusifia utakatifu bila kuuishi.
Badala yake, Yesu
anatutaka kufanya hili, “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja,
nanyi nyote ni ndugu,” Mt 23:8. Mwalimu wetu ni Yesu Kristo, na katika Yeye
sote kwa kupitia sakramenti ya Ubatizo tumerudishiwa urithi wetu na kuwa wana
wa Mungu. Kwa tukio hili la kupatanishwa na Mungu Baba kupitia mwanaye Mpenzi
Yesu Kristo, sisi sote leo ni ndugu. Kwa upatanisho huo, Yesu Kristo anayo
mamlaka ya kusamehe dhambi. “Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo
amri duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule mwenye kupooza) Ondoka,
ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako,” Mt 9:6
Ndugu yangu, nani aliye
tabibu zaidi ya Bwana wetu Yesu Kristo? Ni kwa Yesu Kristo tunaweza kuponywa na
kuwa huru tukiwa na haja hiyo. “Na makutano walipojua walimfuata;
akawakaribisha, akawa akisema nao habari za ufalme wa Mungu, akawaponya wale
wenye haja ya kuponywa,” Lk 9:11. Je, mwenzangu humuitaji Yesu? Kuponywa huku
na Yesu ni matokeo ya kuziungama dhambi na kuomba uponyaji huo. Tendo hili
linatupelekea kuwa na haja ya kuponywa. “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi,
na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa
bidii,” Yak 5:16. Amina
Tumsifu Yesu Kristo!
“Bali ninyi msiitwe Rabi, maana
mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu,” Mt 23:8
Tusali:-Ee
Yesu, usituache waja wako tunapoitaji uponyaji wako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario