JUMAMOSI WIKI YA 3 YA KWARESMA-
Somo:
Hos 6:1-6
Injili:
Lk 18:9-14
Nukuu:
“Maana nataka fadhila
wala si sadaka, na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa,” Hos 6:6
“Lakini yule mtoza
ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali
alijipigapiga kifua akisema, ‘Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi,” Lk
18:13
TAFAKARI:
“Majuto
ya kweli, na Msamaha wa dhambi.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo tutafakari: “Majuto ya kweli, na Msamaha wa dhambi.” Toba na majuto ya
kweli ni kumrudia Mungu bila kujibakiza. Mungu hujua yote katika maisha yetu na
hata yale ambayo yapo mbele yetu. “Je! Mashomoro watano hawauzwi kwa sentí
mbili? Wala hasahauliwi hata mmojawapo mbele za Mungu. Lakini hata nywele za
vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora ninyi kuliko mashomoro
wengi,” Lk 12:6-7.
Somo la kwanza linatupa
picha hiyo na mwono huo wa Mungu. Anachoitaji kwako, ni wewe wenyewe na siyo
yale uyafanyayo. Yakupasa kumjua Mungu, na hii ndiyo fadhila mbele za macho
yake. “Maana nataka fadhila wala si sadaka, na kumjua Mungu kuliko sadaka za
kuteketezwa,” Hos 6:6.
Ndugu yangu, huyafuti
makosa yako mbele za Mungu kwa wingi wa sadaka za kuteketezwa uzifanyazo au
uzitoazo. Leo hii katika jamii na makabila yetu, bado tupo na tunaendelea kutoa
sadaka za kuteketezwa. Mitambiko isiyokoma, na kwa mitindo mbalimbali. Sadaka
za mbuzi, na kuvishwa ngozi na mabangili ya shaba kwa kushikamanishwa na sadaka
hizo. Wingi wa matendo na sadaka hizi, hauondoi kosa letu mbele za Mungu.
Tunachofanya ni kujiongezea hofu pasipo hofu.
Kukiri na kufanya toba
ya kweli ndiyo salama ya maisha yetu. Sadaka hizi hazimpendezi Mungu. Ni
chukizo mbele ya Mungu. “Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za
dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati),
ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili
kusudi alisimamishe la pili,” Ebr 10:8-9. La pili limeshasimamishwa na sadaka
ya mwanaye Mpenzi Yesu Kristo. Kasadaka kako na matambiko yako yana nafasi gani
mbele ya Kristo? Acha maigizo hayo!
Habari Njema-Injili
yetu ya leo yatufundisha namna ya kufanya toba ya kweli na mkao wetu mbele ya
Mungu kwenye kiti chake cha Huruma na Msamaha. Ndugu yangu, tuwapo mbele ya
Kiti cha huruma na Msamaha wa Mungu, Yeye haitaji historia ya mema yetu
tufanyayo kwa sababu wema na uzuri ni asili na ni tabia ya Mungu. Haitaji
kusikia ubaya wa wengine, ila makosa yako. Mfarisayo anatoa historia ya mazuri
yake na namna afanyavyo mfungo wake. “Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si
kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza
ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote,”
Lk 18:11-12.
Ndugu yangu, mbele za
Mungu hatujihesabii haki, bali tunapewa haki hiyo baada ya kufanya yampendezayo
Mungu. Tunachohitaji mbele ya Mungu ni Huruma na Msamaha wake. Tukiwa mbele ya
kiti hiki cha Huruma ya Mungu, hatufanyi malinganisho ya dhambi wala
uhalalishaji wa dhambi, ila makosa yetu tuliyoyafanya kwa kujua au kutokujua.
Labda nitoe mfano: Huwezi kwenda kuungama na kusema hivi; “nimechukua pesa ya
mume wangu na kulipa zaka kwa sababu yeye hapendi kulipa zaka.” Kosa la wizi
lipo pale pale, licha ya kwamba nia yako ilikuwa nzuri, yaani kulipa zaka kwa
niaba ya mume wako. Njia mbovu na ovu, haziwezi kamwe kuhalalisha tendo lolote
lile hata kama malengo yake ni mazuri.
Mfano wa kuigwa ni wa
Mtoza ushuru. Mtoza ushuru anajiachia kwenye kiti hiki cha Huruma na Msamaha wa
Mungu kama alivyo na kama alivyoyatenda makosa yake. “Ee Mungu, uniwie radhi
mimi mwenye dhambi,” Lk 18:13. Kwa maneno haya yanatosha kupewa dhawabu na
kuinuliwa katika hali yake ya unyonge iliyotokana na dhambi zake. Mtoza ushuru
alikuwa amejawa na hofu ya Mungu kiasi kwamba hakuthubutu hata kuinua macho
yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifuani mwake. Hii ndiyo toba ya kweli na
aibu juu ya dhambi. Ndugu yangu, uwapo kwenye kiti cha Huruma na Msamaha wa
Mungu, unachoitaji ni uponyaji wa mwili na roho. Mponyaji wetu ni Mungu
anayejua makandokando yetu yote. Kamwe usione aibu kuziungama dhambi zako, na
tena kwa uwazi kabisa.
Ndugu yangu, mara
nyingine waona baadhi ya dhambi zako ni kubwa sana, na mbele ya kiti hiki cha
Huruma na Msamaha, unaishia kusema na “nyingine nilizosahau,” ilihali unajua
hujazisahau. Huku ni kuchezea Kiti hiki cha Huruma ya Mungu na Msamaha, na
zaidi, kumkufuru Roho Mtakatifu. “Na kila mtu atakayenena neno juu ya Mwana wa
Adamu atasamehewa, bali aliyemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa,” Lk 12:10.
Hakuna dhambi kubwa mbele ya Mungu ambayo atashindwa kukusamehe, na hakuna
dhambi ndogo mbele ya Mungu ambayo hata ichukulia maanani. Neema na huruma ya
Mungu ni KUBWA kuliko dhambi zako. Ikiwa dhambi ni ukosefu wa kutenda mema na
kwenda kinyume cha upendo wa Mungu, basi hakuna uzito wa dhambi kubwa wala
ndogo mbele ya Mungu kwa kusamehe. Tuziungame zote bila aibu.
Kwa kuziungama dhambi
hizo kama alivyofanya Mtoza ushuru, unahesabiwa haki, na kukwezwa mbele za
Mungu. “Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko
yule (Mfarisayo); kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye
atakwezwa,” Lk 18:14.
Ndugu yangu, mali yako halali
mbele ya Mungu ni dhambi zako. Vingine vyote ni mali na uzuri wa Mungu.
Kuviishi kwa amani na uhuru alivyokupa Mungu kama sehemu ya uzuri wake,
yakupasa kusalimisha mali zako kwake, yaani dhambi zako. Hivyo, twende muda na
wakati wo wote kupatanishwa naye kwenye kiti chake hiki cha Huruma, Msamaha, na
Upendo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye
dhambi,” Lk 18:13b
Tusali:-Ee Yesu, nijalie neema ya kuziona na kuziungama
dhambi zangu zote bila aibu mbele ya kiti chako cha Huruma, Msamaha, na Upendo.
Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario