JUMAPILI
YA 1 YA KWARESMA-A
Somo I: Mwa 2:7-9; 3:1-7
Zab: 51:3-4, 5-6a, 12-13,
14, 17
Somo II: Rum 5:12-19
Injili: Mt 4:1-11
Nukuu
“Bwana Mungu akamfanya
mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi
hai.” Mwa. 2:7
“kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi
walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake
mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi,” Rum 5:15b
“Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili
ajaribiwe na Ibilisi,” Mt 4:1
“Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika
wakamtumikia,” Mt 4:11
TAFAKARI: “Kisha Ibilisi akamwacha;
na tazama, wakaja malaika wakamtumikia.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya kwanza ya Kwaresma mwaka “A.” Masomo
yetu yote matatu yanatualika tusimame katika Imani ya kweli, na hasa katika
matendo. Pili, yatupasa kuwa imara hata baada ya kuyashinda majaribu katika vita
hivi vya Imani, kwa sababu yule mwovu shetani kushindwa kwake siyo mwisho wake
wa kutujaribu. “Kisha
Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia,” Mt 4:11. Ibilisi
kumwacha Yesu haikumaanisha ndiyo mwisho wa jaribu, (Rejea Lk 4:13). Tatu, Huruma
na upendo wa Mungu kwetu ni waajabu.
Wapendwa katika Kristo,
Mungu ni Upendo na kwake yote huyafanya kwa sababu ya upendo. Wazazi wetu wa
mwanzo wanapewa upendeleo ukiambana na utaratibu wa kuishi kwenye hii bustani.
Bustani ina mambo makuu matatu; a) Aina zote za miti ya matunda, b) Matunda ya
mti wa uzima, na c) Matunda ya mti wa
ujuzi wa wema na mabaya.
Pamoja na kupewa ruksa
ya kula matunda yote, waliwe pia angalizo la kutokula matunda ya mti wa ujuzi
wa wema na mabaya, Mwa 2:17. Tendo la kwenda kinyume na agizo hili ni KIFO. Cha
kujifunza leo ni kwamba tangu mwanza kifo hakikuwa katika mpango wa Mungu.
Mungu anatutakia uzima wa milele.
Madhara ya kutokufuata
maangalizo na utaratibu fulani iwe ni kazi au aina yeyote ya stadi za maisha
yapo mengi. Tazama milipuko ya magonjwa mengi sugu na yasiyoponyeka! Yote
yametokana na kutumia utashi wetu vibaya. Mara nyingi binadamu twapenda kujua
kwa bidii sana kile kilicho jificha nyuma ya "pazia." Je, haitoshi
kuyajua haya yaliyomahitaji yetu na yale tu yenye uzima ndani yake? Ni vizuri
tukatumia udadisi wetu kumjua Mungu, kuboresha maisha yetu kuelekea utakatifu,
na kuifanya dunia hii kuwa sehemu nzuri zaidi ya kuishi licha ya kwamba ni
sehemu ya kujiandaa kwa maisha ya umilele.
Ndugu yangu tunaye
safiri sote katika tafakari hii, ni vyema tukazama ndani kidogo kwenye fumbo
hili la mtu kama alivyo, ili tuweze kujua ujumbe wa Injili ya leo. Mtu kamili
anakuwa katika sehemu kuu tatu:-Nafsi, Roho, na Mwili. “Mungu wa amani mwenyewe
awatakase kabisa; nanyi Nafsi zenu na Roho zenu na Miili yenu mhifadhiwe mwe
kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.” I The 5:23
Katika hili Roho na
Nafsi huwa pamoja na ndizo wewe mwenyewe. Mwili ni nyumba ya roho na nafsi.
Katika uumbaji Mungu aliumba mwili kwa udongo halafu akapulizia pumzi puani
ambayo ni roho yake ndipo mtu huyo akawa nafsi iliyo hai. “Bwana Mungu
akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa
nafsi hai.” Mwa. 2:7. Miili tuliyonayo ni nyumba ya Nafsi na Roho. Kwa hali hii
sisi binadamu ni wawili. Kuna mtu wa ndani na mtu wa nje. Mtu wa ndani ni Nafsi
na Roho, na mtu wa nje ni Mwili lakini watu hawa wapo pamoja hatuwezi
kuwatenganisha wala kumwona kwa macho ya nyama huyu mtu wa ndani, ila yupo.
Ndugu yangu, pamoja na
malengo mengi tuliyonayo kwa kutafuta fahamu mbalimbali (elimu) tuzipatazo toka
kwenye familia zetu, shule, vyuo, hadi hapo ulipo, moja na la msingi ni
kukusaidia kujijua katika maana ya uwezo wako (capacity), karama zako, na
mazingira yako ili mwisho wa siku uipate furaha ile ya kweli ndani yako.
Ukichepuka katika kweli hii huwezi epuka kuwa kivuli cha kitu kingine. Hicho
kivuli hakitoweza kukupa furaha. Ni sawa na kuvaa kinyago na kuificha sura yako
halisi.
Kutojipokea
ambapo kunapelekea kuishi maisha linganishi na uvuli wa vitu ndicho kisemwacho
hapa. Mungu alipomuumba mwanadamu, wazazi wetu wa mwanzo Adam na Hawa, aliwapa
pia sehemu nzuri ya kuishi. Na panapokuwa zaidi ya mmoja kuna kuwa na utaratibu
wake wa kuishi, na hiyo ndiyo akili. Penye akili kuna utaratibu, na pasipo na
utaratibu hapana akili. Kweli hii anaikiri mwanamke yule (Hawa) kwa nyoka yule
anayemrubuni ‘kula matunda yote ya bustani’ katika bustani ile Mungu
aliyoiandaa yao na kusema, “Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini
matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse,
msije mkafa,” Mwa 3:2-3. Nyoka kwa kujua udhaifu wao, yaani, wa kutojipokea
kama walivyo, anawapa hakikisho la hofu yao, yaani, kifo, na kuwaambia, “Hakika
hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti
huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya,” Mwa
3:4-5. Kutokujua uwezo wako ndani yako, ni rahisi sana kurubuniwa kwa sababu
nafasi ya kutokuwa na utoshelevu ni kubwa sana ndani yako. Na matokeo yake,
“Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni
mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa
na mumewe, naye akala,” Mwa 3:6. Tendo hili la kwenda kinyume cha utaratibu
(kutokutii) ni kujipatia utoshelevu ambao ni tokeo la kutojipokea kama walivyo.
Je,
ni mara ngapi tunaona vituko mtaani mwetu watu wanavyojipodoa na mwisho wa siku
wanabadilika na kuwa vinyago vya kutisha? Leo binadamu amefika mbali zaidi hata
anamkosoa Mungu kwa kubadili maumbile yake. Siku ya ufufuo wa wazima na wafu
hakika vitashuhudiwa vituko vingi!!! Tokeo la moja kwa moja kwa kile
walichokitaka wazazi wetu wa mwanzo kwa kuuvunja utaratibu ule ni hili la kuwa
na soni. “Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona
majani ya mtini, wakajifanyia nguo,” Mwa 3:7. Sijui siku hiyo ya ufufuo wa
wazima na wafu kama kutakuwa na majani ya mtini kuifunika soni itakayojitokeza.
Ndugu yangu, Yesu
angezifuata hisia zake, hakika hasingeweza kuyashinda majaribu kule jangwani. Yesu
hakuziruhusu hisia zake zimtawale kwa sababu alimruhusu Roho wa Mungu ayatawale
maisha yake. Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani,
akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Ni Roho huyu
aliyeyasukuma yote aliyoyafanya na hasa pale alipotangaza rasmi mapambano ya
kweli na haki katika lile lililo ovu na kumkomboa mwanadamu. “Roho wa Bwana yu
juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma
kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha
huru waliosetwa,” Lk 4:18. Na ni Roho huyu
huyu aliyemwezesha kuyaona yote kwa mwelekeo wa Mungu Baba. “Saa ile ile alishangilia kwa Roho Mtakatifu,
akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya
umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa
kuwa ndivyo ilivyokupendeza,” Lk 10:2.
Huyu
ndiye Roho aliyemwezesha kuyashinda yale majaribu jangwa juu ya Sifa, Umaarufu
na Utajiri [Mt 4:4, 5-6, 9]. Baada ya ushindi huu wa Yesu, Ibilisi alimwacha,
na malaika wakaja kumtumikia. “Kisha
Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia,” Mt 4:11. Unaposhinda
majaribu katika maisha yako usije ukajisahu na kubweteka kana kwamba vita hiyo
ishafikia ukomo. Yakupasa kuwa macho muda wote kama asemavyo Mtume Petro, “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi,
kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze,” 1Pet 5:8.
Kila
mmoja wetu anajangwa lake ambalo ukitaka uzima wa milele utaupata na ukitaka ya
hapa duniani utayapata pia. Ila ni vigumu sana kuyapata ya milele kama utabobea
kwa haya ya leo na kesho, yaani ya hapa duniani. Ukiyachuchumilia ya umilele,
kuna uhakika wa kuyapata yote ya duniani kwa amani na furaha. Basi “utafuteni
ufalme wa Mungu, na hayo mtaongezewa,” Lk 12:31. Maisha yangu kama Mtawa na
Padre ni yanipasa kuyaisha kwa uaminifu huku nikiyashinda majaribu yangu ya
kila siku kwa nguvu ya sala na uwezo wa Roho Mtakatifu. Nawe ule mlei na kadiri
ya wito wako, ni vyema ukajua yakupasayo kuishi na hasa uaminifu kwa kile
ulichoitiwa. Kipindi hiki cha kwaresma tunapata nafasi ya kuzama ndani ya nyoyo
zetu kwa lengo la kujitakasa na kumrudia Mungu katika kumwabudu kuliko sahihi,
halisi, tafakari, na kwa matendo hai. Ibilisi utuacha tu kwa muda ila
hajaghairi nia yake ya kutudondosha. Basi tukeshe tukiomba na kushikamana na
Kristo aliyeyashinda majaribu yake jangwani.
Maisha yetu leo yana
maana sana “kwa maana ikiwa kwa
kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa
kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya
wale wengi,” Rum 5:15b. Yesu Kristo katurudishia hadhi ya kuwa tena wana wa
Mungu na warithi wa ufalme wake wa mbinguni.
Jambo la ajabu ona tunavyoishi na jirani
zetu! Unaweka wigo "fence" kiasi kwamba unamzuiya hata jirani yako
kufungua mlango. Ona! tusivyo wajali wengine afya zao! Tunaelekeza maji taka
kwenye makazi yao bila huruma. Eti kwa vile unapesa, na unajulikana hadi usalama
wa Taifa. Eti kwa vile wewe ni kiongozi wa ngazi za juu kwenye utawala dhalimu.
Eti kwa vile wewe ni mfanya biashara maarufu nchini. Je, hili ndilo kusudi la
Mungu kwa maisha yako hapa duniani?
Ndugu yangu, usisahau
kuwa maisha ya hapa duniani ni sawa na kuwa ugenini. Haya si makazi yako ya
kudumu, au hatma yako ya mwisho. Unapita tu!
Unatembea tu duniani. Mfalme Daudi anatukumbusha, "Mimi ni mgeni
katika nchi, usinifiche maagizo yako," Zab 119:19, na Mtume Petro
anasema, "na ikiwa mnamwita Baba,
yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa
hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni." 1Pet 1:17. Waamini wa
kweli wanafahamu wazi kwamba kuna mambo mengi ya maisha kuliko hii miaka
michache tunayoishi hapa duniani. Uhakika huu tunapewa na Kristo mwenyewe baada
ya kukishida kifo kwa sadaka yake pale msalabani. Sote tumehesabiwa haki kwa
kifo cha Kristo. “Basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa
adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye
uzima,” Rum 5:18
Ndugu, kitambulisho
chako kiko katika umilele, na nchi yako ni mbinguni kwa sadaka ya Bwana wetu
Yesu Kristo aliyekubali kuutoa uhai wake ili mimi na wewe tuwe huru kutoka
utumwa wa dhambi. “Na dhambi ilipozidi, neema ilikuwa
nyingi zaidi; ili kwamba, kama
vile dhambi ilivyotawala katika mauti, vivyo hivyo kwa njia ya haki neema
itawale hata uzima wa milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu,” 5:20b-21. Yote haya
yawezekana kwako na kwangu kwa neema tu ya Mungu. Unapofahamu ukweli huu,
utaacha kuwa na wasiwasi wa "kupata kila kitu" hapa duniani. Mungu
yupo wazi kabisa kuhusu habari za kuishi kwa ajili ya "hapa" na
"sasa" tu huku ukijifananisha na watu wa dunia hii katika kipaumbele
na mtindo wa maisha.
Ndugu yangu hapana shaka wa mfahamu
vizuri "inzi!" Mdudu huyu kadiri ya utafiki wa kisayansi huishi siku
saba tu. Ni wiki moja kati ya wiki 52 katika mwaka mmoja. Tazama fujo na papara
za inzi. Hutua kila mahali kwa siku hizo saba; kwenye vyakula (vilivyo chacha
na visivyo chacha), kwenye vinjwaji, kwenye vidonda, kwenye vinyesi, nk. Tulio
wengi leo maisha yetu hayana tofauti na haya ya inzi. Hutaka kufanya yote na
kujaribu yote katika maisha. Ila “mali bila daftari, huisha bila habari.”
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kwa
maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya
Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi
kwa ajili ya wale wengi,” Rum 5:15b
Tusali:-Ee Yesu Mwema, nijalie neema na nguvu ili nivishinde
vilema vyangu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario