domingo, 26 de marzo de 2017

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 4 YA KWARESMA


JUMAMOSI WIKI YA 4 YA KWARESMA

Somo: Yer 11:18-20

Zab: 7:1-2, 8bc-9, 10-11

Injili: Yoh 7:40-53

Nukuu:

“Lakini mimi nalikuwa kama mwanakondoo mpole, achukuliwaye kwenda kuchinjwa, wala sikujua ya kuwa wamefanya mashauri kinyume changu, wakisema, “Na tuuharibu mti pamoja na matunda yake, na tumkatilie mbali atoke katika nchi ya walio hai, ili jina lake lisikumbukwe tena.”” Yer 11:19

“Je, torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua atendavyo?” Yoh 7:51
 
TAFAKARI: “Haki ya mnyonge ni haki ya Mungu; dhuluma dhidi ya mnyonge ni dhuluma dhidi ya Mungu, binadamu hawezi kushinda kesi hii.”

Wapendwa wana wa Taifa ya Mungu, leo kadiri ya masomo yetu, yanatualika tutafakari juu ya “haki ya mnyonge ni haki ya Mungu; dhuluma dhidi ya mnyonge ni dhuluma dhidi ya Mungu, binadamu hawezi kushinda kesi hii.” Katika mazingira ya Nabii Yeremia na hata mazingira na nyakati za Yesu Kristo, wanyonge walidhulumiwa na haki zao kuporwa au kukanyagwa. Hawakuwa na watetezi, na hata kwenye ukweli juu ya wanyonge, ulipindishwa kwa visingizio mbalimbali kama tutakavyoona kwa Yeremia na Yesu Kristo. Je, nyakati zetu hali imebadilika na kuwa bora zaidi, licha kwamba Yesu Kristo kuwa mtetezi wa wanyonge na hata kuutoa uhai kwake kwa ajili ya kweli?

Ndugu yangu, Nabii Yeremia anasema ni kwa namna gani mtu mnyonge anavyoonewa kutokana na hali na upole wake. Katika jamii yoyote ile ya watu, licha ya historia yao na utamaduni wao, wale waliojaliwa ufahamu wa kuelewa mambo, hutumika sana katika kutafuta ukweli, usawa, haki, amani, na kuzisimamia. Ni watu hawa hawa kwa kukosa hofu ya Mungu hutumia upole na hali za wanyonge kuwadhulimu haki zao. Katika uovu huu, Nabii Yeremia anasema, “Lakini mimi nalikuwa kama mwanakondoo mpole, achukuliwaye kwenda kuchinjwa, wala sikujua ya kuwa wamefanya mashauri kinyume changu, wakisema, “Na tuuharibu mti pamoja na matunda yake, na tumkatilie mbali atoke katika nchi ya walio hai, ili jina lake lisikumbukwe tena.”” Yer 11:19

Mnyonge huyu hanyimwi tu haki zake, bali huondolewa hata haki za kizazi chake kijacho na kufutwa kabisa. Lengo ni kuuharibi mti pamoja na matunda yake. Wapendwa wana wa Mungu, dhuluma kama hii afanyiwayo mnyonge, binadamu mwenye kufanya hayo kamwe hataweza kushinda katika dhuluma hii. Mungu mara zote hulia na wanyonge. “Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu yake,” I Sam 2:6-8.

Ndugu yangu, dhuluma dhidi ya mnyonge ni dhuluma dhidi ya Mungu mwenyewe. Tenda haki kwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake. “Usimnyang’anye maskini; wala usimdhulumu mtu mnyonge langoni; Kwa sababu Bwana atawatetea; Naye atawateka uhai wao waliowateka,” Mit 22:22-23. Kuna heri na baraka kubwa kutoka kwa Mungu unapotenda mema na kuwatetea wanyonge. “Heri amkumbukaye mnyonge; Bwana atamwokoa siku ya taabu,” Zab 41:1. Tuwe watu wa kutenda mema kwa wote na tuanze pale tulipo. Lifanye jambo hilo kuwa tabia yako nyumbani kwako, kazini kwako na hata kwenye utume wako, iwe jumuiyani na hata Kanisani. Tuwe watetezi wa wanyonge na hasa wale wasiokuwa na sauti na mahali pa kupeleka malalamiko na vilio vyao.

Watendao maovu na hasa kuwanyanyasa wanyonge kwa kunyonga haki zao, kamwe hawataishi kwa amani. Ninapolitazama taifa letu leo, na harakati zake hasa kwa swala zima la Katiba, napata mashaka sana. Wasomi wetu na wale tuliowapa dhamana ya kutetea na kusimamia haki kwa wote na hasa kwa wanyonge, wamekuwa watu wa kwanza kupora haki za wanyonge na kufanya Katiba pendekezwa kuwa na taswira yenye mwelekeo wa kulinda maslahi yao na familiza zao, kulinda utajiri waliokwisha pora kwa wanyonge, kuweka uwezekano wa familia zao na marafiki zao kuwa madarakani daima, na hata kuzuia mnyonge kupata haki yake pale atakapoidai kwa haki.

Katika hili na mazingira kama haya, Mungu anasema, “hukumu hii imekuja kwa agizo la walinzi, na amri hii kwa neno la watakatifu; kusudi walio hai wapate kujua ya kuwa Aliye juu anatawala katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, tena humtawaza juu yake aliye mnyonge,” Dan 4:17. Dhuluma yeyote juu ya wanyonge, Bwana ataijibu mara moja. Tuwe na hamu na matumaini ya kutenda mema siku zote, na tuendelee kutenda haki. Kwa kuwa, “Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu,” Isa 66:2. Kumdhulumu mnyonge ni kugusa mboni ya jicho la Mungu.

Injili letu ya leo yaonyesha ni kwa namna gani mnyonge anavyodhumiliwa haki zake na hasa swala zima la kutoa hukumu. Yesu Kristo anahukumiwa hata bila kusikilizwa. Wanapanga njama za kuutoa uhai wake kwa vile tu ananena iliyo kweli na kutenda mema. Hata licha ya kusutwa na dhamiri zao, Mafarisayo bado wanasukumwa na dhamiri zao mbaya kutenda uovu. “Je, torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua atendavyo?” Yoh 7:51. Nikodemu, aliyekuwa mfuasi wa siri wa Kristo, na aliyekuwa anamwendea usiku kupata habari za ufalme wa Mungu, anajaribu kutoa ushauri ili kuunusuru uhai wa Yesu. Ushauri huu haukubaliki machoni mwa Mafarisayo kwa sababu binadamu  akishachagua kumtumikia shetani, uwepo wa Mungu unatoweka. Dhamiri iliyo mbovu na ufu, husahau hata yale mazuri tuliyojiwekea kwa ajili ya kutenda haki.

Ndugu yangu, Taifa letu linautaratibu mzuri tu wa kutoa haki licha ya kwamba yapo maeneo fulani yanaitaji marekebisho. Hata hivyo, bado haki za wanyonge zinakanyagwa kiasi kwamba hata aibu hatuna tena. Kujilimbikizia mali za wizi uliotokana na kodi za wanyonge, ni dhambi ambayo ukiifanya itakutafuna wewe na hata kizazi chako hadi kizazi cha nne baada ya wewe. Fedha na mali zisizo halali ni kujiwekea sanamu na kuanza kuziabudu. Tukianza kuambudu mali na vitu, Mungu hana tena nafasi ndani yetu. “Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Bwana wako, ni Mungu mwenye wivu, nawapatiliza wana wa uovu wa baba zao; hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,” Kumb 5:9. Hii ni laana kubwa sana. Ufisadi kwenye Taifa letu la Tanzania,  umekuwa moja ya sifa, na tunaaminishwa kupokea jambo hilo kama la kawaida. Uovu huu dhidi ya masikini na wanyonge binadamu hawezi kushinda kamwe kwani ni uovu dhidi ya Mungu mwenyewe. Leo tupo kwenye mkakati na harakati wa kutumbua ‘majipu.’ Je, tutafikia malengo kweli ikiwa hata watumbuaji wa majibu kikanuni nao wanamajipu hadi mikononi? It is just a play within a play!

Bwana wetu Yesu Kristo ni neno aliyefanyika mwili. Hivyo ni Mungu mwenyewe. Kutokumpatia haki stahili Yesu Kristo, ni kutokumpatia Mungu mastahili yake. Je, vita hii binadamu mwenzangu tutashinda, au ndiyo tunazidi kujichumia laana tu kila kukichwa. Ndugu yangu kilio cha wanyonge katika Taifa letu leo kwa ujumla wake ni kilio cha Mungu.

Mpendwa, mara zote kuwa na hofu ya Mungu na tenda wema kwa wote bila kujali historia ya mtu na hata hali yake kijamii. Sote mbele ya Mungu tunamizania na mastahili sawa. Wayahudi wanatafuta histori ya neno aliyefanyika mwili-Yesu Kristo, kwenye kumbukumbu zao. Wanampa Yesu Kristo nafasi ya Nabii. Yesu Kristo siyo nabii, bali ni nafsi ya Pili ya Mungu. Bado Wayahudi wanawaza kibinadamu. Tusimsaidie mtu au kumsikiliza mtu shida zake kwa kuanza kutazama historia yake. Hili ni kosa kubwa sana kufanya. Tumtazame mtu kadiri ya kile anachohitaji kwetu na tufanye kwa haki na stahili zote.

Tumsifu Yesu Kristo

“Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena,” Yoh 7:46

Tusali:-Ee Yesu, nipe neema ya kukuona mara zote kwa wale ninao wahudumia. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario