JUMATANO WIKI YA 4 YA KWARESMA
Somo:
Isa 49:8-15
Zab: 145:8-9,
13cd-14, 17-18
Injili:
Yoh 5:17-30
Nukuu:
“Je, mwanamke aweza
kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa
waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe,” Isa 49:15
“Yeye alisikiaye neno
langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii
hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani,” Yoh 5:24
TAFAKARI:
Usikivu wa Upendo wa Mungu Baba na Mwana, hu na uzima wa milele ndani yake.
Wapendwa wana wa Mungu,
“Usikivu wa Upendo wa Mungu Baba na Mwana, hu na uzima wa milele ndani yake.”
Yesu Kristo anaudhihirisha upendo wa Mungu Baba kwetu, na kwa njia yake twaweza
kumjua Baba Mungu. Hili ndiyo fumbo kubwa la kumwilishwa kwa neno wa Mungu na
kuwa mwanadamu.
Ahadi ya Mungu kwetu ni
kutokutusahau katika hali zote hata kama kibinadamu jambo hilo linawezekana.
Mungu hawezi kutusaha. “Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata
asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi
sitakusahau wewe,” Isa 49:15
Maisha yetu ni mpango
wa Mungu na kwa malengo ya Mungu. Mpango huu unarahisishwa kwa uwepo wa Mwanaye
Yesu Kristo, ambaye hajifanyii mambo yake pasipo Mungu Baba aliyempeleka. “Mimi
siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu
yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake
aliyenipeleka,” Yoh 5:30
Wayahudi wanapinga
ufundishi na utendaji wa Yesu, hasa kwenye uelewa wa Mungu mmoja tu, na si
katika nafsi tatu. Kadiri ya uelewa na mtazamo wa Kiimani wa Kiyahudi, kama
ilivyopia kwa dini nyingine kama Waislamu, Mungu hawezi kuwa na mtoto, na Yesu
kusema yeye ni Mwana wa Mungu, wakati wanajua yeye binafsi na wazazi wake, ni
kufuru kubwa sana. Lakini ukweli ni kwamba, nafsi hizi tatu hujitofautisha katika
utendaji. Na katika utendaji huu wa nafsi mojawapo, hauondoi uwepo na
ushirikiano wa nafsi nyingine.
Ndugu yangu, yawezekana
kupenda bila kujua na wakati mwingine kutokufanya chochote, ila huwezi kujua
ukaacha kufanya na kupenda. Mbali zaidi ni kwamba, kupenda na kufanya huku
msingi wake ni kuamini yale ayafanyayo Yesu Kristo pamoja na uelewa wetu kibinadamu
kutotosheleza kuzama kabisa katika fumbo la Utatu Mtakatifu. Tuanze na
kuyaamini haya ayasemayo na kuyafanya Yesu Kristo, na katika safari hiyo tutajua
taratibu siri ya fumbo hili la Utatu Mtakatifu na kupenda.
Ahadi ya kuyafanya hayo
yote, Yesu Kristo anaweka wazi jambo hili, na kusema, “Yeye alisikiaye neno
langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii
hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.” Yoh 5:24. Jambo hili la
kusikia neno na kumwamini Yesu Kristo liongoze dira nzima ya maisha yetu ya
kiroho. Mpendwa, kuwa na uzima ndani ya Kristo na katika Kristo ni kumfanya
Kristo kuwa pumzi ya maisha yako kila siku; katika kufikiri, kutenda, na
kuishi.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Tena
Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote; ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile
wanavyomheshimu Baba,” Yoh 5:22-23
Tusali:-Bwana Yesu, uwe
pumzi na uhai wangu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario