lunes, 20 de marzo de 2017

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 3 YA KWARESMA


JUMATANO WIKI YA 3 YA KWARESMA

Somo: Kumb 4:1, 5-9

Zab: 147:12-13, 15-16, 19-20

Injili: Mt 5:17-19

Nukuu:

“Na sasa, ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende, mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu,” Kumb 4:1

“Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua Torati au Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiza,” Mt 5:17

TAFAKARI: “Sheria ya Bwana ni kamilifu, nayo ni uhai wetu.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo na tutafakari “sheria ya Bwana na ukamilifu wake.” Sheria ya Bwana ni utaratibu wa kuyaishi yale yampendezayo Mungu, na kuwa na mahusiano mazuri naye kwani Yeye ndiye uhai na uzima wetu. Wana wa Israeli walipewa sheria kama mwongozo wa kutenda na kuwa na mahusiano mazuri na Mungu. “Bwana akamwambia Musa, Njoo huku juu kwangu mlimani, uwe huku; nami nitakupa mbao za mawe na ile sheria na hiyo amri niliyoiandika ili uwafundishe,” Kut 24:12. Sheria hizi zilipaswa kufuatwa kiaminifu na bila kuzichakachua. “Mioyo yenu na iwe kamili kwa Bwana, Mungu wetu, kuenenda katika sheria zake, na kuzishika amri zake, kama ilivyo leo.” 1Fal 8:61.

Ukamilifu na uaminifu wa mtu ulipatikana katika kuzishika sheria za Bwana. Kwa sababu, “sheria ya Bwana ni kamilifu, huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa Bwana ni amini, Humtia mjinga hekima.” Zab 19:7. Hivi ndivyo ilivyopaswa kuzishika sheria za Bwana. Na hilo ndilo lililokuwa kusudi la sheria. Jambo la kushangaza wakati wa Yesu, Wayahudi hawakuwa wanafuata Torati kama iliyokuwa mwanzo, yaani, nyakati za Musa. Wayahudi walikuwa wanafuata tafsiri ya Torati ambayo iliendana na matamanio yao na siyo ya Mungu. Huu ndio ugomvi uliokuwepo kati ya Yesu na Waandishi na Mafarisayo.

Jambo muhimu sana la kujua ni kwamba kipindi cha Yesu, Wayahudi na hasa mafarisayo na waandishi hawakuwa wanaifuata Torati kama iliyokuwa, ila tafsiri yake (maisha ya dini na matendo yake kupitia masimulizi), iliyojulikana kwa ujumla kama TALMUD. Talmud ilibeba mambo mawili: MIDRASH (tafsiri ya mambo mbalimbali toka Torati), na MISHNAH (marudio/waliyorudia au mafundisho)

Kwa mantiki hiyo hapo juu ya TALMUD, vitabu vile vitano vya Torati vingewezwa kuandikwa kwa kurasa 350 tu; wakati TALMUD ilichukuwa hadi vitabu 523; vilivyo rudufiwa (printed) katika mabando (volumes) 22. Haya ndiyo yanayonukuliwa na mafarisayo na waandishi kama mapokeo ya wazee. Sehemu nyingi za mafundisho ya Yesu anapinga jambo hili la kufuata mapokeo ambayo ni tafsiri kutoka Torati, (Mt 15:2-3, 6; Mk 7:3, 5, 8, 9, 13). Naye Yesu anawaambia, “Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu,” Mk 7:8. Mapokea haya ni ukweli wa Mungu uliopotoshwa. Mtume Paulo baada ya kuongoka na kuujua ukweli kuhusu sheria ya Bwana anawaambia Wakolosai, “Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo,” Kol 2:8. Ukweli ni kwamba, Mtume Paulo kama Mfarisayo kabla ya kuongoka kwake aliyafuata mapokea haya ya wazee ambayo yalikuwa ni ‘ukweli wa Mungu uliopotoshwa.’ Paulo anakiri jambo hili na kusema, “Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu,” Gal 1:14.

Kwenye jambo hili, yaani kweli ya Sheria ya Bwana, Yesu anawakemea Mafarisayo na Waandishi na kusema, “Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua Torati au Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiza,” Mt 5:17. Hapa Yesu akubaliani nao kwa swala la kuichakachua Torati kama walivyokwisha kufanya. Yesu anarudisha mpango mzima wa Mungu katika safari nzima ya ukombozi wa mwanadamu. Yesu anatoa zaidi maana ya sheria na ushikaji wa sheria hiyo. Yesu anawakosoa Mafarisayo kwa unafiki wao katika sheria na kusema, “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache,” Mt 23:23

Utimilifu wa sheria kadiri ya mpango mzima na mtazamo wa Yesu umebebwa katika upendo. Hii ndiyo amri mpya. “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo,” Yoh 13:34. Mtakatifu Agustino anatuambia kwamba, “ukipenda utafanya yote.” Ni katika mantiki hii kwamba, “mkipenda, mtazishika amri zangu,” Yoh 14:15. Ndugu yangu, ukiona viongozi wetu serikalini au kwenye taasisi yoyote ile wanang’ang’ana kubadili katiba kwa matamanio yao na vyama vyao bila kujali maslahi ya wengi, ni wazi kabisa mwisho wake ni upotoshaji wa kweli na kwenda kinyume na mpango wa Mungu kupitia watu wake.

Katika kweli hili niliyosema kuhusu ung’ang’anizi wa kubadili mambo kadiri ya matamanio ya wachache, bado tunao Mafarisayo na Waandishi katika jamii yetu kama ilivyokuwa nyakati za Yesu. Leo tuna mkwamo mkubwa wa kisiasa visiwani Zanzibar kwa sababu tu ya wachache wenye kutanguliza matamanio yao ya kuenzi umilele katika ‘utawala’ bila hofu ya Mungu. Hiki ni kitu kisichowezekana hata kidogo. Katiba haitafsiriwi kama ilivyo, bali inapewa tafsiri kadiri ya matamanio ya wachache ili kukidhi tamaa na makusudi yao huku wengi wakiteseka pasipo sababu za msingi. Yatupasa kila mmoja wetu kadiri ya Imani na itikadi zake aone hili ni tatizo kubwa na linahitaji kutatuliwa haraka. Katiba ndio msahafu wetu sote bila kujali Dini, Imani, na itikadi zetu. Katiba haipaswi kuhodhiwa na Chama chochote kile cha siasa. Tukifanya hivyo tu, tujiandae kwa machafuko makubwa. Na pasipo shaka joto la machafu hayo linaanza.

Ndugu yangu, nawe uliye Mkristo, Ukristo wetu bila UPENDO wa kweli ni Ukristo MFU. Kwa Mkristo kuwa na upendo wa dhati ni kuzishika amri za Mungu katika ukamilifu wake. “Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake,” Yoh 14:21. Na kukaa katika pendo la Mungu ni kuzishika amri zake. “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake,” Yoh 15:10.

Ndugu yangu, ni wakati wa kijitazama, na hasa tukianzia kwenye familia zetu, Jumuiya zetu ndogondogo za Kikristo, na za kitawa, na dhamana tuliyopewa na umma kama viongozi kuishi katika kweli na haki. Huwezi kutenda kweli na haki kama huwapendi wale unao waongoza. Mwenye nafasi hii ya uongozi bila upendo kwa watu wake, ni rahisi sana kusukumwa na ubinafsi wake, na matamanio ya wachache wasio na uchungu na mateso ya wengi. Je, kama kiongozi waishi upendo wa kweli na haki? Mt. Yohane wa Msalaba anasema hivi, “When evening comes, you will be examined in love. Learn to love, as God desires to be loved and abandon your own ways of acting.” Kunapokuwa na upendo wa kweli, sheria ufanya kazi dogo sana, na wakati mwingine sheria hiyo hutoweka kabisa.

Upendo wa kweli utusukuma kufanya zaidi ya yale yanayohainishwa na sheria husika. “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Huu ndio mfano wa kuigwa kutoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Tupendane! “The soul that walks in love neither tires others nor grows tired,” Mt. Yohane wa Msalaba.

Tumsifu Yesu Kristo

“Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua Torati au Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiza,” Mt 5:17

Tusali:-Ee Yesu, nijalie Upendo wa kweli na kukuona kwa kila mmoja ninayekutana naye katika maisha yangu. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario