lunes, 20 de marzo de 2017

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI 3 YA KWARESMA


ALHAMISI WIKI YA 3 YA KWARESMA

Somo: Yer 7:23-28

Zab: 95:1-2, 6-7, 8-9

Injili: Lk 11:14-23

Nukuu:

“Taifa hili ndilo lisilosikiliza sauti ya Bwana, Mungu wao, wala kupokea mafundisho; uaminifu umepotea, umekatiliwa mbali na vinywa vyao,” Yer 7:28

“Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia,” Lk 11:20

TAFAKARI: “Huwezi shindi vita na Mungu. Ushindi ni kuishi kwa ajili yake na katika yeye tu, yaani, kujisalimisha kwake.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo tutafakari kwa undani juu ya neno hili, “Huwezi shindi vita na Mungu. Ushindi ni kuishi kwa ajili yake na katika yeye tu, yaani, kujisalimisha kwake.” Wengi wetu kwa kufahamu au kutokufahamu, tunaishi kwa kupingana na Mungu. Mfumo huo kimaisha hautaweza kuleta mafanikio yo yote hata kama tukiweka bidii zetu zote, yaani, nguvu, akili, na moyo katika mpango huo. Tendo hilo kiimani ni kuwekeza pasipo na usalama. Huu ndio wito wa masomo yetu yote ya leo.

Somo la kwanza linatueleza hasara ya kutosikiliza sauti ya Mungu kupitia watumishi wake manabii. Waisraeli wanasahau kwamba hakuna kushinda bila uwepo wa Mungu. Kinyume chake wanakosa baraka na msaada wa Mungu kwa kila wafanyacho. Hii ni laana ya wazi kabisa. Mungu anasema kupitia kinywa cha Nabii Yeremia, “Taifa hili ndilo lisilosikiliza sauti ya Bwana, Mungu wao, wala kupokea mafundisho; uaminifu umepotea, umekatiliwa mbali na vinywa vyao,” Yer 7:28.

Ndugu yangu, unapokosa uaminifu mbele ya Mungu, hakuna mafanikio yo yote uwezayo kupata kwa sababu huamini nguvu ya Mungu, nafasi ya Mungu, na msaada wa wake katika maisha yako. Huku ni kujihesabia haki mbele ya Mungu pasipo mastahili. Uaminifu mbele ya Mungu hujengwa kwa kujisalimisha kwako. Kujisalimisha mbele ya Mungu ni tendo zima la KUABUDU.

Tendo hili la kujisalimisha kwa maana nyingine ni kujiweka kwa ajili ya Mungu tu. Ni kujiweka wakfu kwa ajili yake, Kumfanya Yesu Bwana wako, Kuchukuwa msalaba wako, Kuifisha nafsi, na Kujitoa kwa Roho Mtakatifu. Ni kitu ambacho kibinadamu ni vigumu kufanya kwa sababu hakuna anayetaka kupoteza kwa ajili ya kupoteza, hasa kwa ulimwengu wetu huu wa ushindani. Tupo kwenye ulimwengu wa kushinda tu, na mashindano muda wote. Lakini Yesu anatupa angalizo na kusema, “Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?” Mk 8:36-37. Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, njia sahihi ya maisha yako ni kujisalimisha katika mikono salama ya Mungu.

Nini maana ya kujisalimisha?

Kujisalimisha kwa Mungu si kujiuzulu na kukaa tu kusubiri, au kuamini kuwa yote yameandikwa binadamu hana hiari, au kuwa na udhuru na wivu. Siyo kukubali hali hiyo hiyo uliyo nayo. Inaweza kumaanisha kinyume cha haya; kujitoa sadaka maisha yako au kuteseka ili kubadilisha yanahitajika kubadilishwa. Mara nyingi Mungu huwaita watu waliojisalimisha kwake kupiga vita kwa jina lake. Kujisalimisha sio kwa uoga au mazulia. Mungu asingependa kupoteza akili alizokupa! Mungu hapendi watu wawe kama mitambo (robots) ili kumtumikia. Kujisalimisha siyo kukomesha utu wako. Badala ya kukomesha utu wako, kujisalimisha hukutia nguvu. C. S Lewis alisema, “kadiri tunavyomruhusu Mungu atutawale ndivyo tunavyozidi kuwa sisi wenyewe, kwa sababu yeye ndiye aliyetuumba. Alibuni namna mbalimbali za watu wote tofauti ambao mimi na wewe tulikusudiwa kuwa… Ni pale ninapomgeukia Kristo, ninapojikabidhi nafsi yangu kwake, ndipo ninapokuwa na ule utu wangu halisi.”

Kujisalimisha kunadhihirika vyema katika KUTII. Unasema ‘ndivyo, Bwana’ kwa chochote anachokueleza. Kusema “hapana, Bwana” ni kutamka vinyume. Hatuwezi kumwita Yesu Bwana na wakati huo huo hatutaki kumtii. Baada ya usiku kucha bila kupata samaki, Simioni alionyesha kujisalimisha pale Yesu alipomwambia kujaribu tena” “Bwana tumefanya kazi kwa bidii usiku wote na hatujakamata samaki yeyote. Lakini kwa sababu umesema, nitatia nyavu majini,” Lk.5:5. Watu waliojisalimisha hutii neno la Mungu hata kama linaonekana kutokuwa na maana.

Jambo lingine katika kujisalimisha ni IMANI. Ibrahimu alifuata maelekezo ya Mungu bila kujua alikokuwa akienda. Hana alisubiri wakati wa Mungu bila kujua ni lini. Mariamu alitarajia muujiza bila kufahamu utatendekaje. Yusufu aliamini lengo la Mungu bila kujua kwa nini mazingira yalikuwa hivyo. Kila mmoja wa watu hawa alikuwa amejisalimisha kwa Mungu alipomtegemea.

Utafahamu umejisalimisha kwa Mungu unapomtegemea Mungu akutengenezee mambo yako badala ya kujaribu kuwafanyia hila wengine, ukapitisha jambo lako, na mwisho ukatawala mazingira hayo. Unamwachia Mungu afanye, Huhitaji wakati wote kuwa, “mwangalizi.” Mzaburi anasema, “Jisalimishe nafsi yako kwa Bwana, na umsubiri kwa uvumilivu.” Zab. 37:7a. Baada ya kujaribu sana, umwamini zaidi. Pia unafahamu kwamba unajisalimisha unapokuwa huchukizwi na lawama na kukimbilia kujitetea. Mioyo iliyojisalimisha huonyesha mahusiano mazuri na wengine. Huwatupilii mbali wengine, hudai haki zako, na hutumikii nafsi yako kama umejisalimisha.

Eneo gumu sana kwa watu wengi kujisalimisha ni PESA zao. Wengi wamefikiri, “Nataka kuishi kwa ajili ya Mungu lakini pia nataka kupata pesa nyingi ili niishi kwa raha baadaye nipumzike.” Kupumzika siyo lengo la maisha ya kujisalimisha, kwa sababu huku ni kushindana na Mungu kwa sababu ya kuweka mkazo kwanza kwa maisha yako. Yesu anasema, “Huwezi kutumikia Mungu na pesa,” Mt. 6:24 na kwamba “popote hazina yako ilipo ndipo na moyo wako upo,” Mt. 6:21. Yesu anatupa angalizo la shamba la mtu yule mmoja tajiri lililo kuwa limezaa sana. Mtu huyu alipanga kujibohofisha; kupumzika, kula, kunywa na kufurahi. Naye Yesu anasema, Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu,” Lk 12:20-21. 

Wapendwa wana wa Mungu, kielelezo kikubwa cha kujisalimisha ni Yesu. Usiku ule kabla ya mateso Yesu alijisalimisha kwa mpango wa Mungu. Alisali, “Baba kila kitu kinawezekana kwako. Tafadhali niondolee kikombe hiki cha mateso. Lakini nataka mapenzi yako, siyo yangu,” Mk.14:36

Yesu hakuomba, “Baba, kama unaweza kuniondolea maumivu haya, tafadhali fanya hivyo.” Alikuwa tayari amethibitisha kuwa Mungu ana uwezo wa kufanya lolote! Badala yake aliomba, “Mungu, kama inapendeza kwako kuniondolea mateso haya, tafadhali fanya hivyo. Lakini kama yanatimiza kusudi lako, ndivyo ninavyotaka pia.

Kujisalimisha halisi husema, “Baba, kama tatizo hili, maumivu, ugonjwa, au hali yoyote inahitajika kutimiza lengo lako na utukufu kwako katika maisha yangu au ya mwingine, tafadhali usiliondoe.” Kiwango hiki cha ukomavu hakiji kwa urahisi. Kwa upande wa Yesu, aliugua sana kuhusu mpango wa Mungu kiasi cha kutoa jasho la damu. Kwa upande wetu, ni vita kali dhidi ya asili yetu ya ubinafsi.

Kujisalimisha ndiyo njia bora ya kuishi:

Kila mtu hatimaye hujisalimisha kwa mtu au kitu fulani. Kama sio kwa Mungu, utajisalimisha kwa matarajio au maoni ya watu wengine, au pesa, chuki, hofu, au kwa kiburi chako au tamaa mbaya, au ubinafsi. Ulibuniwa kumwabudu Mungu-na kama utashindwa kumwabudu, utatengeneza vitu vingine (sanamu) ili uvipe maisha yako. Unao uhuru wa kuchagua usalimishe maisha yako, lakini huko huru na matokeo ya uchaguzi huo. E. Stanly Jones alisema, “kama hutajisalimisha kwa Kristo, utajisalimisha kwa machafuko.” Kujisalimisha si njia bora ya kuishi; ni njia pekee ya kuishi. Hakuna kitu kingine cha kukufanikisha.

 Njia nyingine zote hukuongoza kwenye kukukatisha tamaa, na kuziangamiza nafsi. Tafsiri ya King James huita kujisalimisha “huduma yenu yenye maana.” Rum 12:1. Tafsiri nyingine inasema, “njia yenye maana zaidi ya kumtumikia.” Rum 12:1 Kusalimisha maisha yako si hisia za kipumbavu lakini ni tendo la akili na busara ambalo unaweza kulifanya kwa ajili ya maisha yako. Ndiyo maana Paulo alisema, “Ni lengo letu kwamba tumpendeze yeye,” 2Kor 5:9. Nyakati zako za busara zitakuwa zile ambazo unasema NDIYO kwa Mungu.

Wakati mwingine huchukua miaka, lakini hatimaye unagundua kwamba kizuizi kikubwa kwa Baraka za Mungu maishani mwako sio watu wengine, ni wewe mwenyewe, yaani, matakwa yako binafsi, kiburi cha hali ya juu, na matarajio yako. Huwezi kutimiza lengo la Mungu kwa maisha  yako huku ukikazania malengo yako binafsi.

Kama Mungu ataenda kufanya kazi ya kina ndani yako, itaanza hivyo. Kwa hiyo mpe yote Mungu: kushindwa kwako hapo nyuma, matatizo yako ya sasa, matarajio yako ya mbele, hofu zako, ndoto, udhaifu, tabia, maumivu, na madhara yoyote uliyo nayo. Mweke Yesu katika kiti cha dereva wa maisha yako na uondoe mikono yako toka kwenye usukani. Usiogope; hakuna chochote katika uongozi wake kinaweza kupoteza dira. Chini ya uongozi wa Kristo kunaweza kudumu chochote. Utakuwa kama Paulo, “Niko tayari kwa lolote na kuwa sawa na chochote kwa njia ya yeye anayetia nguvu ndani yangu, yaani, ninajitosheleza katika utoshelvu wa Kristo.”Flp 4:13

Kujisalimisha kwa Paulo kulitokea katika njia ya Dameski alipoangushwa chini na mwanga mkali uliompofusha. Kwa watu wengine, Mungu anapata mwitikio wao bila kutumia njia ya ajabu sana. Pamoja na hayo, kujisalimisha siyo tukio la wakati mmoja tu. Paulo anasema, “Nakufa kila siku.” I Kor 15:3 Kuna wakati wa kujisalimisha, na kuna tendo la kujisalimisha, ambalo ni la muda-hadi-muda na maisha yote. Tatizo la sadaka iliyo hai ni kwamba inaweza kutambaa na kutoa madhabahuni, hivyo unaweza kutakiwa kujisalimisha hata mara hamsini kwa siku. Ni lazima ufanye jambo hili kuwa tabia yako ya kila siku. Yesu anasema,” kama watu wanapenda kunifuata ni lazima waache mambo wanayoyapenda. Lazima wawe tayari kuacha maisha yao kila siku na kunifuata,” Lk 9:23

Ngoja nikuonye: unapoamua kuishi maisha ya kujisalimisha kikamilifu, uamuzi huo utapimwa. Wakati mwingine itamaanisha kufanya mambo yasiyostahili, ya gharama, au yanayoonekana hayawezekani. Mara nyingi itamaanisha kufanya kinyume cha unavyojisikia kufanya.

Lakini tukijipima nguvu zetu na Mungu, kamwe vita hii hatuwezi kushinda. Ni kupiga ngumu kwenye upepo au ukuta. Ni kujaza maji kwenye gunia la katani, kamwe halitajaa. Tujisalimishe kwake, kwa kuwa, “Mungu wako, ni Mungu wa rehema; hatakukosa wala kukuangamiza, wala hatalisahau agano la baba zako alilowaapia,” Kumb 4:31. Katika historia ya wokovu wetu, mara zote binadamu ameshindwa kwa kosa la kutojisalimisha kwa Mungu.

Injili yetu ya leo inafafanua kwa undani zaidi namna ya kujisalimisha, na hasa kujisalimisha kwa ufalme wa Mungu. Ndugu yangu, katika miaka ile mitatu ya mwisho ya Bwana watu Yesu Krisito, alisisitiza mambo makuu matatu; kwanza, kufanya toba ya kweli kwa kuwa ufalme wa Mungu u karibu (Mk 1:15), Pili, kuwachagua na kuwaandaa wafuasi wake kwa kazi hii ya kuhubiri habari njema (Mk 1:16-20, Mt 28:19-20), na tatu, kulitakasa Hekalu (kama jengo na nyumba ya sala, na mwili ambao ni hekalu la Roho Mtakatifu; Yoh 2:14-21, 1Kor 6:19)

Injili ya leo Yesu Kristo analifanya jambo hilo la tatu; kulitakasa Hekalu-Mwili ambalo ni makazi ya Roho Mtakatifu. “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.” 1Kor 6:19-20.

Ndugu yangu, kwa vile tusivyojisalimisha kwa Mungu, hujisalimisha kwa vitu au watu. Watu waliokuwepo katika uponyaji wa bubu aliyekuwa na pepo bubu, wanamuhukumu Yesu kuwa anayafanya hayo kwa nguvu za Beelzebuli. Mara nyingi huwa tunawahukumu watu kwa namna tunavyofikiri na kutenda. Kwa vile wao huamini juu ya nguvu hizo za Beelzebuli, wanafikiri na Yesu Kristo anayafanya hayo kwa nguvu hizo. La hasha! Yesu anawaambia, “Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia,” Lk 11:20. Yesu anayafanya hayo kwa mkono wa Mungu.

Ndugu yangu, leo wapo watu ambao hawaamini nguvu ya Mungu, na uwepo wa Kristo katika maisha yao. Watu wa mtindo huu, wapatwapo na majaribu kidogo tu, hukimbilia kupata ishara nje ya Kristo. Kristo kwetu anatosha. Hatuitaji ishara zaidi yake. Mateso, kifo na ufufuko wake ni Ushindi mkubwa wetu na Ishara ya kutosha kabisa. Ndugu yangu, kiguru na njia kila siku kwa waganga utaacha lini? Kama wewe ni Mkristo na waamini uwepo wa Kristo katika maisha yako, mganga wa kienyeji ana nafasi gani kwako? Kwa nini wajisalimisha kwa mwanadamu na wakati mwingine kwa shetani?

Ndugu yangu, elewa jambo hili, “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana,” Yer 17:5

Tumsifu Yesu Kristo!

“Taifa hili ndilo lisilosikiliza sauti ya Bwana, Mungu wao, wala kupokea mafundisho; uaminifu umepotea, umekatiliwa mbali na vinywa vyao,” Yer 7:28

Tusali:-Ee Yesu Kristo, hakuna usalama na hata ushindi nisipojisalimisha kwako. Nisaidie mara zote kuelewa kuwa Wewe  ndiye Njia, Uzima, na Ukweli. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario