JUMAPILI YA 3 YA
KWARESMA-A
Somo I: Kut 17:3-7
Zab: 95:1-2, 6-7, 8-9
Somo II: Rum 5:1-2, 5-8
Injili: Yoh 4:5-42
Nukuu
“Watu
wakawa na kiu huko; nao wakamnung'unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha
kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu?” Mwa 17:3
“Bwana
akamwambia Musa, Pita mbele ya watu, ukawachukue baadhi ya wazee wa Israeli
pamoja nawe; na ile fimbo yako ambayo uliupiga mto kwayo, uitwae mkononi mwako,
ukaende,” Mwa 17:5
“Akapaita
mahali pale jina lake Masa, na Meriba; kwa sababu ya mateto ya wana wa Israeli,
na kwa sababu walimjaribu Bwana, wakisema, Je! Bwana yu kati yetu au sivyo?”
Mwa 17:7
“Akaja
mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe,” Yoh 4:7
“Kila
anywaye maji haya ataona kiu tena; walakini ye yote atakayekunywa maji yale
nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani
yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele,” Yoh 4:13-14
“Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya
kuwa u nabii! Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko
Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia,” Yoh 4:19-20
“Yesu
akamwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye,” Yoh 4:26
“Kwa maana hapo
tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu,”
Rum 5:6
“Bali Mungu
aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili
yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi,” Rum 5:8
TAFAKARI:
“Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa
kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.”
Wapendwa
wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anadhimisha Dominika ya “3” ya Kwarema ya mwaka
“A” wa Kanisa. Niwaombe tuzame sote pamoja katika tafakari hii kwa maneno haya
yenye kufunua kweli kuhusu Mungu: -“Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe
kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye
dhambi.” Tendo hili, yaani, ‘upendo huu wa Neno kufanyika mwili na kukaa
kwetu,’ Yoh 1:14, ni dhihirisho la mpango mzima wa Mungu na ulio huru kabisa wa
kuumba ulimwenugu, Isa 45:18, kumuumba mwanadamu, Mwa 1:27, na kumkomboa
mwanadamu aliyelekwisha lemewa na mzigo mzito wa dhambi, Gal 4:4-5.
Hamu
hiyo, shahuku hiyo, chanzo hicho, na vuguvugu hili la upendo ni Mungu mwenyewe,
kama asemavyo huyu Neno aliyefanyika mwili na kukaa kwetu, yaani, Bwana wetu
Yesu Kristo; “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi;
nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba
lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Yoh 15:16. Je, ndugu yangu,
ulishawahi kuona ng’ombe aliyeshindwa kuibeba nundu yake hata kama inamkera?
Na
huu ndio wasifu wa Kristo Yesu kama kiongozi na hasa katika fumbo hili zima la
upendo wa Mungu katika historia ya wokovu wa mwanadamu, yaani, “ingawa ni
Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha
kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii; kisha ametajwa
na Mungu kuwa kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki,” Ebr 5:8-10. Ikiwa Agano
Jipya ndio utimilifu wa Agano la Kale ambalo kwalo limejificha katika Agano
Jipya, upendo, na huruma ya Mungu haujawahi kukoma tangu pale Mungu alipoona
inafaa na kumpendeza kuumba ulimwengu na mwanadamu hadi sasa. Kweli hii
inajidhihirisha katika somo letu la kwanza kama tulivyokwisha lisikia.
Musa
kama Nabii na kiongozi anashiriki sehemu hii maalumu ya historia ya wokovu wa
Mwanadamu kwa upendo na upendeleo wa Mungu kwake. Hata hivyo jambo hili
halikuwa rahisi sana kwake Musa. Ni rahisi kuwaswaga ng’ombe 1000 kichinjioni
kuliko kumpeleka mwalifu mmoja mahabusu. Kwa huyu mmoja, yaani, mwalifu,
unahitaji ulinzi wa hali ya juu, tena akiwa kafungwa pingu. Musa kama Nabii na kiongozi
anapewa wajibu wa kuliongoza Taifa zima la wana wa Israeli na kulifikisha
katika nchi ya ahadi. Haikuwa jambo rahisi kufanya hata kidogo kwa mwanadamu
mwenye nyama na mifupa. Tuelewe watu hawa katika mazingira ya somo la leo
hawakuwa na mwongozo wowote ule (leo tungezungumzia mfano wa Katiba). Amri zile
za Mungu wanakuja kuzipata baadaye, Kut 20:1-26, na Mbao zile mbili za
ushuhuda, Kut 31:1-18, ilhali aliowaacha chini ya mlima walishajifanyia
utaratibu wao (ndama yule wa dhahabu) baada ya yeye, yaani, Musa kuchelewa
kurudi kutoka mlimani, Kut 32:1-6.
Somo
hili la kwanza leo linafunua sifa ya Kiongozi, yaani, pamoja na mambo yote,
‘subira na utulivu wa ndani’ wenye kupelekea maamuzi yaliyo chanya na yakinifu.
Hii ndiyo busara katika uongozi. Kwa ufupi waswahili wana usemi huu kuhusu sifa
hii ya kiongozi, yaani, “Kiongozi ni jalala.” Je, siyo kwenye jalala kutupwapo
kila aina ya uchafu na yale yasiyofaa tena kwa matumizi? Kwa kuepuka milipuko
ya magonjwa jalala uyabeba yote katika yote. Hivyo Musa anakutana na changamoto
katika uongozi wake, nayo ni changamoto ya kiu. “Watu wakawa na kiu huko; nao
wakamnung'unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi
na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu?” Mwa 17:3. Watu hawa hawana maji na mazingira
yale yalikuwa mazingira ya jangwani. Malalamiko ya watu kwa Musa kama kiongozi,
hayarudishi kwa vijembe wala kujihami, ila anasikiliza ‘sauti ya Mungu’ ndani
yake. Hivyo “Bwana akamwambia Musa, Pita mbele ya watu, ukawachukue baadhi ya
wazee wa Israeli pamoja nawe; na ile fimbo yako ambayo uliupiga mto kwayo,
uitwae mkononi mwako, ukaende,” Mwa 17:5. Mungu anamkumbusa Musa kutumia ile
fimbo aliyompatia. Leo mimi na wewe kama viongozi tunakumbushwa kutumia vyema
ujuzi tulioupata kutokana na elimu tuliopitia, vipaji na karama tulizo nazo
kukabiliana na sintofahamu katika uongozi wetu. Huku ndiko kupambazuka kutoka
kiza kinene kwa tusichokifahamu. Ni jambo la kusikitisha na kumuhuzunisha Mungu
kwamba baadhi yetu huzaliwa, uishi, na kufa wakiwa wamelala usingizi mzito
licha ya elimu, vipaji na karama walizojaliwa na Mungu.
Mungu
asiyeshindwa lolote kwa wale wenye kumtegemea katika kweli na haki akanena na
Musa na wale wazee; “Tazama, nitasimama mbele yako huko, juu ya lile jabali
katika Horebu; nawe utalipiga jabali, na maji yatatoka, watu wapate kunywa.
Musa akafanya hivyo mbele ya wazee wa Israeli,” Mwa 17:6. Hapa tunajifunza sifa
nyingine na kubwa ya kiongozi, yaani, ‘kuwa na hofu ya Mungu,’ na imaanishe
kweli kwamba hofu hiyo ya Mungu imo ndani ya moyo wako kwa namna uonavyo,
ufikirivyo, uamuavyo, na utendavyo. La sivyo mwisho wa uongozi wako moja ya
mambo haya mawili yaweza kutokea, yaani, badala ya kuwa Mhenga kuna nafasi
kubwa sana ya kuwa Lihoka, yaani, roho ile ovu isiyo na chochote cha kukumbukwa.
Musa ni Mhenga wetu kwa sababu katika mapito yale, aliacha kitu cha kukumbukwa.
Na ndivyo ilivyokuwa kwamba baada ya changamoto ile ya kiu, Musa “akapaita
mahali pale jina lake Masa, na Meriba; kwa sababu ya mateto ya wana wa Israeli,
na kwa sababu walimjaribu Bwana, wakisema, Je! Bwana yu kati yetu au sivyo?”
Mwa 17:7.
Ndugu
yangu unaye safari name katika tafakari hii, Injili ya leo inafunua na kuficha
nguvu halisi ya Bwana wetu Yesu Kristo kama Masiha, na kiongozi wa kufuatwa
katika safari hii nzima ya wokovu wa mwanadamu, Yoh 14:6. Huu ndio wakati na
utimilifu wa yote, Gal 4:4-5. Katika jambo hili, Kristo anavunja ukimya
uliokuwepo kadiri ya mifumo, mitazamo, mila na desturi zetu ambazo baadhi ya
hizo kama zilivyo hazina uzima ndani yake. Yesu anavunja ukimya huo kwa yale
yaliyokuwa yakiendelea nje ya mila na desturi za watu wake kama Wayahudi kwa
mwanamke yule Msamaria wa Sikari na kumwambia, “Nipe maji ninywe,” Yoh 4:7.
Watu hawa -Wasamaria na Wayahudi- walikuwa na historia zao mbaya ambazo ziliwatenga
siku baada ya siku (kwa leo nisingependa kuzama sana katika jambo hili). Kristo
Yesu leo anavunja pia ukimya ndani ya Taifa lake mwenyewe kama Myahudi. Na hali
ilikuwa hivi; “Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa sababu alikuwa
akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini? Au, Mbona unasema
naye?” Yoh 4:27. Ujumbe uliwafikia barabara. Kiu yako na yangu leo ni kuutafuta
uso wa Mungu kwa kuishi vyema na impendezavyo Mungu, hasa upendo ule kwa
jirani. Na katika kiu hii Mtakatifu Agustino wa Hippo anasema, “Mioyo yetu
haitulii hadi hapo itakapo tulia kwako Ee Bwana.” Kristo Yesu ndiye kielelezo
na kitoshelezo cha kiu yetu kwa sababu ni kwake tu ipo Njia, kweli, na Uzima,
Yoh 14:6.
Kristo
Yesu kama mwalimu wetu, anachukuwa nafasi hii kutoa mafundisho/katekesi ya
kweli juu yake mwenyewe, na juu ya ufalme ule wa mbinguni ambao kwa upendo wa
Mungu Baba na kwa wale wote waliouridhia u urithi wao. Tendo hili la Yesu
kuomba maji kwa mwanamke huyu Msamaria ndio mlango wa ufahamu wote kwa yale
atakayoyazungumza juu ya kweli kuhusu Yeye mwenyewe na kila alichokijia kama
Masiha. Hata hivyo kutokkana na mahusiano yasiyo afya kati ya Wasamaria na
Wayahudi, kitendo kile cha Yesu kuomba maji kinamshangaza sana mwanamke yule
Msamaria. Naye anahoji, “Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni
mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.),” Yoh 4:9.
Yesu anaanza kuvunja kuta zile za hofu na ukimya ule wa muda mrefu na kusema,
“Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe,
ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai,” Yoh 4:10. Yesu anaondoa
hali ile ya kufa na kuleta uzima. Hii ni moja ya changamoto kubwa leo kuhusu
uinjilishaji mpya na katekesi ya kina kuhusu imani yetu. Hakuna usalama wowote
kuendelea kujenga kuta za utengano. Usalama upo pale tunapozivunja kuta hizo na
kujenga mahusiano katika kweli, uhuru na haki.
Pamoja
na kujifunua kwake Yesu kwa mara ya kwanza kama Masiha, bado somo hili -nipe
maji ninywe- linabaki katika hali ya nadharia kwa mwanamke huyu. Naye anamjibu
Yesu hivi, “Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata
wapi hayo maji yaliyo hai? Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo,
aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na
wanyama wake?” Yoh 4:11-12. Ndugu yangu, kila mmoja wetu huwa kile alacho
katika maana ya kwamba, kile ulicho ni tokea la historia yako (mila na desturi
ulizokulia).
Yesu
anamtoa mwanamke huyu Msamaria kwenye nadharia na kumpeleka kwenye tendo halisi
kuhusu -“nipe maji ninywe.” Na kweli ya akisemacho Yesu juu ya “nipe maji
ninywe ni hiki:-“Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; walakini ye yote
atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji
nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa
milele,” Yoh 4:13-14. Kweli ya hiki akisemacho Yesu kinafunua kile alicho,
yaani, Masiha, na kile alichokijia, yaani, Mkombozi wetu. Uwepo wa Yesu kwako
na kwangu ni kuufikia uzima wa milele, na ule ukamilifu wa Mungu, Mt 5:48,
ambao bila huo hatuwezi kumwona Mungu. Ukamilifu huu ni Mtakatifu wako kama
cheo chako. Yesu anasema wazi wazi kile alichokijia. “Mwivi haji ila aibe na
kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele,”
Yoh 10:10.
Mara
somo linaanza kueleweka katika hatua hii ya “tendo”-nipe maji ninywe ingawa
chembechembe za nadharia bado zinamsonga mwanamke huyu. “Yule mwanamke
akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka,” Yoh
4:15. Hata hivyo Yesu anataka kujua kweli iliyopo ndani ya nafsi yetu, kwa
sababu kama kweli hiyo ipo ndani yetu basi tu huru, Yoh 8:32. Hivyo “Yesu
akamwambia, Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa,” Yoh 4:16. Basi “Yule mwanamke
akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume; kwa
maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo
umesema kweli,” Yoh 4:17-18. Mguso wa maneno haya ya kweli juu ya maisha ya
mwanamke huyu Msamaria yanafunua ndani ya moyo wake kile alicho Kristo Yesu.
“Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii! Baba zetu waliabudu
katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo
kuabudia,” Yoh 4:19-20.
Ndugu
yangu, hadi hapa Yesu kesha yafanya yote mawili, yaani, kweli ya kile alicho,
na kile alichokijia. Kilicho baki sana ni Yesu kumwonyesha njia ya kufuata ili
afike pale ambapo kila mmoja wetu kwa kuumbwa kwa sura na mfano wake Mungu siyo
jambo la mabati mbaya. Tumeumbwa tuishi milele. “Yesu akamwambia, Mama,
unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule
Yerusalemu. Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa
wokovu watoka kwa Wayahudi. Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo
halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu
kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu
katika roho na kweli,” Yoh 4:21-24. Kumwabudu Mungu katika roho na kweli ni
kujisalimisha kwa Mungu pasipo kuwa na viambata. Viambata katika imani ni ile michanganyo
isiyoendana na kile alicho Mungu. Ili kupata uhakika wa kile akifanyacho, “Yule
mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi, (aitwaye Kristo); naye
atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote,” Yoh 4:25. Na Yesu akamaliza
katekesi yake kwa hitimisho hili lenye utoshelevu wote: “Mimi ninayesema nawe,
ndiye,” Yoh 4:26. Ndugu yangu, achia viambata vyako na ambatana na Kristo Yesu.
Kwake upo uzima wa milele.
Ndugu
yangu, furaha ni kama kikohozi huwezi kuizuia. Mara baada ya kupata kitoshelevu
cha kiu yake kwa muda mrefu, “yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake
mjini, akawaambia watu, Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote
niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?” Yoh 4:28-29. Kwa tendo
hili la mwanamke huyu Msamaria tunakumbushwa kushirikishana mambo yale makuu
aliyotutendea Mungu. Wokovu wako uwe faida pia kwa wengine. Na kwa tendo hilo
nawe unakuwa Kristo mwingine pale ulipo.
Kwa
upande wa wanafunzi wa Yesu wanabaki na maswali mengi kichwani mwao. Kwa vile
muda ulishakwenda, wanamsihi Mwalimu wao ale kile walichokwenda kuhemea mjini.
Naye “Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi. Chakula changu ndicho
hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake,” Yoh 4:32,
34. Kwa jibu hili la Yesu tunajifunza kwamba kiu na furaha ya Mungu ni kukupata
wewe na mimi bila kujipoteza katika haya ya leo na kesho tu. Kuondoa ile
sintofahamu kwa wanafunzi wake na hasa kwa tukio lile la mazungumzo baina yake
Yesu na yule mwanamke Msamaria, Yesu anawaambia upendeleo waliokuwa nao mbele
ya Mungu kama wahudumu, Yoh 4:35-41. Upendeleo huo unao wewe na mimi pia kwa
sakramenti ya ubatizo na kipaimara (uimarisho). Atimaye Yesu anawapata wote,
Wasamaria waliodharaulika na Wayahudi, na Wayahudi walio waliojitenga na
Wasamaria kadiri ya misimamo yao kiimani. Na huu ndio ushuhuda wa Wasamaria juu
ya Kristo Yesu: -“Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu
ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika
huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu,” Yoh 4:42.
Wapendwa
wana wa Mungu, somo letu la pili latufundisha kwamba, wewe na mimi leo
tunauishi Utatu huu Mtakatifu na umoja usiogawanyika tunapoambatana pasipo
kujipoteza katika malimwengu tukiwa ndani ya Utatu huu kila mmoja kadiri
alivyoitwa kutumika hapa duniani kama viumbe shirikishwa katika uumbaji wa pili
na Mungu-“co-creators of God.” Hivyo wito na maisha yako unayoyaishi kwa
uaminifu ni kwa namna hiyo hiyo unashiriki fumbo hili Takatifu katika (kuumba,
kukomboa, na kutakatifuza malimwengu). Hapa ndipo twawezwa kuhesabiwa haki
katika imani hiyo. Hivyo “Basi tukiisha kuhesabiwa haki
itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu
Kristo, ambaye kwa yeye tumepata kwa
njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi
katika tumaini la utukufu wa Mungu,” Rum 5:1-2. Na kuishi Imani hii katika kweli, tumaini na haki,
tunawezeshwa na Roho Mtakatifu tuliyepewa. “Na kazi ya uthabiti wa moyo
ni tumaini; na tumaini
halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo
yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi,” Rum 5:4b-5. Je, ninalo la kujivunia au
kuona fahari juu ya kufunuliwa siri na fumbo hili la Utatu Mtakatifu na umoja
usiogawanyika? Sina!
Ndugu
yangu, lazima uelewe jambo hili, kwamba, “Kwa maana hapo
tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu,”
Rum 5:6. Je, mimi nimekamilika? Kama nimekamilika, je, mazingira yangu na
kutenda kwangu kwa watu kuna akisi upendo huu alionifia Kristo? Ukweli ni kwamba,
“Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa
kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi,” Rum 5:8. Sadaka yangu kila
siku ni kuwa mwaminifu pale nilipo, na kuvuja damu kila siku kwa kujitoa
vilivyo kwa kile nikifanyacho kama moja ya huduma na kuwajibika kwangu.
Kutafuta huruma mbele za watu ili kuonekana mwema ni kupoteza muda na neema ya
Mungu ndani yako. Huu ndio mchezo haramu na usiopendeza mbele ya Mungu
unaofanywa na viongozi wetu, hasa wa kisiasa kucheza na hisia zetu.
Basi
nielewa kwamba pale nilipo na kwa kila mmoja kadiri ya wito na nafasi yake ni
kielezo cha mwanga kama mshumaa. Unapowaka mshumaa na kutoa kile kilicho kama
mshumaa -“kuliondoa giza”- mshumaa haubaki kama ulivyo. Hii ndiyo sadaka ya
kila mmoja wetu anapoishi kila alicho katika kweli na haki. Nilete uhai,
furaha, matumaini, upendo, na amani pale nilipo kama Kristo afanyavyo daima.
Tusifu
Yesu Kristo!
“Mimi
ninayesema nawe, ndiye,” Yoh 4:26.
Tusali:-Ee Yesu Mwema
na Mwalimu wetu, tuondolee woga pasipo woga ili tuweze kuabudu katika roho na
kweli. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario