IJUMAA BAADA YA JUMATANO YA MAJIVU
Somo:
Isa 58:1-9a
Zab:
51:3-4, 5-6a, 18-19
Injili:
Mt 9:14-15
Nukuu:
“Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je!
Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na
kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga,
na ya kukubaliwa na Bwana?” Isa 58:5
“Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo
vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje
kila nira?” Isa 58:6
“Je,
Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje
nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe?" Isa 58:7
“Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya
yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata
nyuma ukulinde,” Isa 58:8
“Ndipo
utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa,” Isa 58:9
“Yesu
akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo
pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo
watakapofunga," Mt 9:15
TAFAKARI:
“Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga. Na
wakati huo ndio sasa. Mfungo na matendo ya huruma.”
Wapendwa wana wa Mungu,
masomo yetu ya leo yanatutaka kutafakari kwa kina maneno haya; “lakini siku
zitakuja watakapoondolewa Bwana arusi; ndipo watakapofunga. Na wakati huo ndio
sasa. Mfungo na matendo ya huruma.” Sehemu ya kwanza katika tafakari ya maneno
haya, ni jibu la Yesu kwa wanafunzi wa Yohane Mbatizaji walioshangazwa na tendo
la wanafunzi wake Yesu la kutokufunga. Nao walimuuliza Yesu, “kwa nini sisi na
Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi?” Mt 9:14. Bila shaka jibu
la Yesu lililenga dhana nzima ya uelewa wa kufunga.
Jibu la Yesu linaibua
ufahamu huu kwa wanafunzi wa Yohane Mbatizaji kwamba, ‘tusipende kufanya mambo
kwa mazoea bila kujua kiini chake na kwa nini tunafanya kama tunavyofanya.’ Kwa
mantiki hii, jibu la Yesu linaeleza asichokisema Yesu moja kwa moja kwamba, ‘kwa
sasa wanafunzi wake wapo shuleni kujifunza fumbo zima la mfungo.’ Basi nyakati
zitakapotimia, yaani kuondolewa kwa Bwana Arusi-[Yeye mwenyewe, kwa njia ya mateso,
kifo na ufufuko wake], ndipo watakapo funga na kuelewa vizuri sababu ya kufunga,
huku wakiendeleza yale yote aliyowafundisha.
Mafarisayo na hata
baadhi yetu leo twafikiri mfungo ni ‘kufanya tu yale yanayoonekana nje kwa faida
ya kujitukuza wenyewe, ikiwa ni pamoja na kutokula kwa ratiba ya kawaida, na
kujiweka katika hali ya huzuni na kuhurumiwa na watu.’ Mafarisayo walipoteza
lengo zima na maana ya mfungo. Kipindi hiki cha siku 40, yaani ‘muda wa
kutosha,’ hatufanyi maonyesho kwa lengo la kujiinua nafsi zetu, na wala
hatufanyi mazoezi ya mwili kwa lengo la kuuweka mwili vizuri ingawa tuifanyapo
saumu yetu vizuri twaweza kufaidika pia kimwili.
Nabii Isaya katika somo
la kwanza ameeleza vizuri sana lengo la Saumu, yaani Mfungo. Mfungo si maonyesho ya namna yoyote
ile ya kuziinua nafsi zetu. Naye anasema kwa mtindo wa kuhoji na tafakari; “Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je!
Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na
kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga,
na ya kukubaliwa na Bwana?” Isa 58:5. Hakika hili silo lengo la mfungo. Lengo
la Mfungo au Saumu ni pamoja na haya ayasemayo Nabii Isaya kwa kuihoji nafsi; “Je!
Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza
kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?” Isa 58:6. Saumu ya kweli ni pamoja
na kupatazama pale ulipokosea kutokana na uovu wako, na kupigania haki za watu
ikiwa ni pamoja na wale walioonewa kijamii kutokana na mifumo miovu ambayo nawe
ni sehemu ya mfumo huo. Haya ndiyo matendo ya huruma yanayopaswa kuendana na
Saumu ya kweli.
Matendo hayo ya huruma
ndiyo anayoyahoji Nabii Isaya; "Je, Siyo kuwagawia wenye njaa chakula
chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye
uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe?" Isa
58:7. Kama najinyima kwa lengo la kufunga, kile ninachojinyima kiwalenge
wahitaji. Kundi hili la wahitaji tunao pande zote na siku zote. Anza hapo
ulipo! Naye Yesu anatuambia ukweli huu kama alivyowaambia wale waliomnung’unikia
juu ya Marhamu ambayo alimwagiwa kichwani na Mwanamke yule mkosefu, ingeuzwa
ili fedha ile wapewe maskini. Naye akawajibu na kusadifu tendo lile la mwanamke
yule kwa kusema, “maana sikuzote mnao maskini pamoja nanyi, na kila mpendapo
mwaweza kuwatendea mema; lakini mimi hamnami sikuzote,” Mk 14:7
Wapendwa katika Kristo,
tunapofanya matendo haya ya huruma tunakutana na Yesu katika sura na maumbo
tofauti tofauti. Ni kwa namna hii somo la kwanza kutoka nabii Isaya linalandana
kabisa na ayasemayo Yesu katika Injili ya Mathayo 25:31-46. Hapa tunakutana na
Yesu mwenye njaa, mgonjwa, mfungwa, aliye uchi, mwenye kiu, aliye kifungoni nk.
Huku ni kukutana naye katika maisha yetu ya kawaida na ya kila siku. Mwisho wa
siku Yesu anasema, "Amin nawaambia, kadiri msivyomtendea mmoja wapo wa hao
walio wadogo, hamkunitendea mimi," Mt 25:45.
Ndugu yangu, hapa ndipo
ilipolala hukumu yetu ya mwisho. Wenye haki watakwenda kwenye uzima wa milele,
na wasio haki wataingia katika adhabu ya milele, (Mt 25:46). Bwana harusi
hatunaye tena. Huu ndio wakati muhafaka wa kufunga na kufanya toba. Zoezi hili
kwa Mkristo na kwa yeyote yule mwenye hofu ya Mungu ni zoezi na tendo endelevu
maisha yake yote. Yesu kesha tufundisha mengi tulipokuwa naye katika makuzi
yetu ya maisha ya kiroho, na sasa yatupasa kuyaishi. "Lakini siku zitakuja
watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga," Mt 9:15b. Kuyafanya
haya kwa uhakika, uaminifu, na ukamilifu wake ndiyo baraka na neema kwetu. “Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya
yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata
nyuma ukulinde, Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi
hapa,” Isa 58:8-9. Amina!
Hivyo ndugu yangu
niliye safiri nawe katika tafakari hii, usisahau kamwe kundi la wahitaji katika
mfungo wako. Daima uwe mtu wa kutenda haki na kuitetea pia pale haki hiyo
inapokosekana au kukandamizwa kadiri ya nafasi yako na wito wako.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Walioalikwa arusini wawezaje
kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja
watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga," Mt 9:15
NA
“Heri amkumbukaye
mnyonge; Bwana atamwokoa siku ya taabu. Bwana
atamlinda na kumhifadhi hai, Naye atafanikiwa katika nchi; Wala usimtie katika
hali wamtakiayo adui zake,” Zab 41:1-2
Tusali:-Ee Yesu na
Mwalimu wangu, katika mfungo huu nijalie nikuone kwa kila nitakayekutana naye,
na iwe sehemu ya shukrani yangu kwako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario