IJUMAA WIKI YA 4 YA KWARESMA
Somo:
Hek 2:1a, 12-22
Zab:
34:16-17, 18-19, 20, 22
Injili:
Yoh 7:1-2, 10, 25-30
Nukuu:
“Ndivyo
walivyosemezana, wakakosea kabisa, kwa maana uovu wao uliwapofusha; hawakuzijua
siri za Mungu, wala hawakuutarajia mshahara wa utakatifu, wala kudhani ya
kwamba iko thawabu kwao wenye roho zisizo na hatia,” Hek 2:21-22
“Basi wakatafuta
kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu
saa yake ilikuwa haijaja bado,” Yoh 7:30
TAFAKARI:
“Mpango wa Mungu kwa mwanadamu; na njia ovu za mwanadamu”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo kwa namna ya pekee tutafakari neno hili, “Mpango wa Mungu kwa mwanadamu, na
njia ovu za mwanadamu.” Mpendwa, somo la leo ikiwa ni pamoja na Injili ya leo,
yote kwa ujumla wake yanaongelea Mpango wa Mungu kwa sisi wanadamu, na matendo
maovu tuyafanyayo kwa kujua au kutokujua ili mradi tu kwenda kinyume na matakwa
yake Mungu. Tunaona jinsi ya mtu wenye haki anavyodhulumiwa na kutendwa vibaya
bila hatia yo yote. Tuona katika somo hilo la kwanza binadamu anavyokaa vikao
vya kutenda maovu na kushauriana kufanya hivyo kwa utaratibu na kufanikisha
jambo hilo.
Mwisho Mungu analiona
jambo hilo na analiweka wazi. “Ndivyo walivyosemezana, wakakosea kabisa, kwa
maana uovu wao uliwapofusha; hawakuzijua siri za Mungu, wala hawakuutarajia mshahara
wa utakatifu, wala kudhani ya kwamba iko thawabu kwao wenye roho zisizo na
hatia,” Hek 2:21-22. Jambo lo lote ovu lifanyikalo gizani ipo siku litawekwa
hadharani. Mungu kwa uwezo na mamlaka aliyokuwa nayo aweza kuruhusu uovu kwa
lengo la kutoa fundisho. Na katika mantiki hii, lililo ovu haliwezi kushinda
kamwe! Na kamwe Mungu hawezi kuwa sehemu ya uovu ule kwa sababu Mungu ni
Mkamilifu katika ukamifu wote. Kwa hiyo, ye yote yule ajivuniaye kwa uovu
anapoteza muda wake bure na mwisho wa siku anajichumia mzingo wa dhambi.
Tunapoitazama jamii
yetu leo kama Watanzania, ni wakati wa kulitazama kwa ukaribu Taifa letu na
kuliombea sana. Wale wote wafanyao ovu kinyumbe na mpango wa Mungu hasa kwa
wale wasiokuwa na sauti, si kwamba hawana chembe ya umungu ndani yao, ila
wameamua kufanya hivyo kwa ajili ya nafsi zao na ubinafsi wao. Wamekubali
kupatwa na upofu wa kutokuona mema kwa faida ya wengi. Mtu huyu mwenye haki,
yaani, mwananchi asiye na sauti, akitegemea wenye hekima na busara wamtete,
anajikuta anasalitiwa. Mtu huyu ni Kristo anayeteseka leo na sasa. Wategemewa
hawa, wamekuwa vipofu kutumia hekima zao kwa kung’ang’ania madaraka na kusahau
cheo chao halisi, yaani, Utakatifu wao. Hakika adhabu yao mbele ya Mungu ni
kubwa.
Injili yetu pia
yatuonyesha mtu mwenye haki anavyowindwa na hata kufikia hatua ya kuutoa uhai
wake. Yesu Kristo usalama wake unaingia matatani kwa vile tu anasimamia kweli,
haki, huruma, msamaha na upendo. Hii ndiyo asili ya Kristo, na ndiyo asili ya
Mungu. Ndiyo kusema kwamba kweli ya Kristo ni kweli ya Mungu. Kristo akiwa neno
aliyefanywa Mwili, Yoh 1:14, ni Mungu yule yule tunayetaka kumwangamiza. Je,
ikiwa binadamu kaumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, Mwa 1:27, vita hii binadamu
ataiweza? “Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake
ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado,” Yoh 7:30. Hii ni
ishara wazi kwamba nguvu za binadamu katika uovu wake dhidi ya Mungu na hasa
kwa wanyonge hazitafanikiwa kamwe!
Mambo yote tuyaonayo
leo yaliyo kinyume na mpango wa Mungu yana mwisho wake. Hakuna uovu wowote
duniani, au tawala zozote duniani zilizodumu kwa muda wote. Uovu ni kinyume
kabisa na uwepo wa Mungu na mpango wake kwa ulimwengu huu. Yote haya tuyaonayo
yanasubiri saa yake. Je, tufanye nini katika nyakati hizi za sintofahamu?
Katika nyakati hizi za
sintofahamu, kamwe tusipoteze matumaini ndani na katika Kristo. Ni Kristo tu
aliyeshinda uovu kwa wema atakayetupitisha katika mkwamo huu. Kristo anateseka sana na wale wanyonge na wasio na
hatia katika jamii yetu leo. Kuwa na matumaini ni wito wa kuwa
na Imani na Kristo. Imani ya kwamba yote yana mwisho wake, ni swala la Muda tu.
Tutaweza kudumu katika matumaini na imani ndani na katika Kristo, kama tuna
upendo wa kweli ndani yetu na Kristo. Upendo ni msingi mkubwa wa Matumaini na
Imani. Ni katika kupenda twaweza kufanya yote ikiwa ni pamoja na kudumu katika
sala hasa kwa kipindi hiki kigumu.
Ndugu yangu, tuwe macho
kwa kila kitu tunachokumbana nacho leo, na kukitafakari kwa undani na kumwomba
Roho Mtakatifu atusaidie kuona yale yote yaliyojifisha sirini.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mimi mnanijua,
na huko nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye aliyenipeleka
ni wa kweli, msiyemjua ninyi,” Yoh 7:28
Tusali:-Ee
Yesu, uliyekubali kuzichukua dhambi zetu pasipo Wewe kutenda dhambi, tufungulie
hekima yako hii ili nasi tuwajibike kikamilifu katika kuliondoa giza nene hili
la uovu katika jamii yetu leo. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario