lunes, 6 de marzo de 2017

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 1 YA KWARESMA


JUMATANO WIKI YA 1 YA KWARESMA

Somo: Yon 3:1-10

Zab: 51:3-5, 12-13, 18-19

Injili: Lk 11:29-32

Nukuu:

Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo,” Yoh 3:5

"Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende." Yon 3:10

Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki,” Lk 11:30

"Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona." Lk 11:32

TAFAKARI: “Toba ya kweli na Msamaha wa dhambi kupitia Yesu Kristo.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, napenda leo tutafakari pamoja kuhusu "toba ya kweli na msamaha wa dhambi kupitia Yesu Kristo." Tendo la toba huturudisha katika uhalisia wetu kama viumbe na wanadamu. Toba utufikirisha na kutuongoza kwa undani kuhusu mianguko yetu iliyotokana na kutokuupokea ubinadamu wetu na kutaka kuwa sawa na Mungu.  Somo la kwanza, Yona anawaelekeza watu wa Ninawi kufanya toba ya kweli. Toba hii inasura ifuatayo: kwanza, kumfanya binadamu arudi kwenye hali yake na uhalisi wake. Hapa wote yaani wakubwa, watoto na watawala akiwemo mfalme wanafanya toba ya kweli. “Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo,” Yoh 3:5

Wanyama pia hawakuachwa. Wanashirikishwa kufanya toba hiyo. “Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake,” Yoh 3:7-8. Wazo kuu hapa ni kwamba, toba ya kweli ni kurudi kwenye hali yako na uhalisi wako. Hii ndiyo maana halisi ya kufanya toba ya kweli. Ni kushuka na kujishusha bila kujali nafasi, umaarufu, cheo, utajiri, na hata uwezo uliokuwa nao. "Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa." Mit 29:23

Mwenye kiburi na majivuno kamwe hawezi kufanya toba ya kweli. Bila toba ya kweli hakuna msamaha wa dhambi. Utimilifu wa kazi ya Yesu na mwendelezo wake kupitia Mitume na Kanisa leo ni kuhubiri habari njema ya wokovu, kufanya toba ya kweli na msamaha wa dhambi. Hili ni agizo alilolitoa Yesu kwa wanafunzi wake huko Emau mara baada ya ufufuko wake. Yesu akawaambia, "ndivyo iliyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanzia tangu Yerusalemu." Lk 25:46-47. Kanisa kwa kupitia Sakramenti ya kitubio, Yesu anafanya ondoleo hilo la dhambi kwa kupitia watumishi wake, yaani, Mapadre na Maaskofu kwa Sakramenti yao ya Daraja Takatifu. “Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa,” Yoh 20:22-23. Hii ni huruma ya Mungu kwetu kwa kupitia Kanisa lake Takatifu.

Somo letu la injili, yapo mambo mawili mazito ya kutafakari. Pamoja na Yesu kukemea uhitaji wao wa ishara, Yesu anajitabanaisha kuwa yeye ndiye Ishara halisi ya Toba na msamaha wa dhambi. Yeye ni Mungu aliyemwilishwa, Yoh 1:1-3, 1:14. Yeye ndiye njia, ukweli na uzima, (Yoh 14:6).

Ndugu yangu, wewe na mimi kama wafuasi wa Kristo, na ndivyo tulivyo Wakristo, ni ndoto na ni jambo lisilowezekana kwenda mbinguni bila kupitia kwa Yesu Kristo. Je, tunataka ishara gani tena zaidi ya Yesu? Katika hili Yesu anachukua nafasi mbili kwa wakati mmoja. Kwanza ni ishara kama kielelezo cha uhai kamili na umilele. Pili, Yesu ni mfanya ishara ambazo kwayo zaonyesha Umungu wake. Kwa nini basi ndugu yangu ukiwa na maangaiko kidogo tu unakimbilia kwa waganga wa kienyeji kupata ishara?

Ndugu yangu, kama umepoteza ufunguo wa maisha yako mwendee Yesu. "Jesus is the master key." Damu yake haikumwagika bure pale msalabani.  "The blood of Jesus is the master key." Ufunguo huu huwezi kuupata kwa mganga yeyote wa kienyeji na hata chuo kikuu chochote mashuhuri duniani. Ufunguo huu hupatikana kwake Kristo Yesu tu, na yawezekana kwa wale wenye unyofu wa moyo. "Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake, kuliko mpotofu wa njia ingawa ni tajiri." Mit 28:6. Wanyofu wa moyo ni wale wenye udongo mzuri na wenye kuzaa matunda kwa kuvumilia. "Mbegu zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao husikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia." Lk 8:15

Tumsifu Yesu Kristo!

"Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona." Lk 11:32

Tusali:-Ee Yesu Mwema, nijalie kuuona udogo wangu ili niweze kufanya toba ya kweli. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario