JUMATANO WIKI YA 2 YA KWARESMA
Somo:
Yer 18:18-20
Zab:
31:5-6 14, 15-16
Injili:
Mt 20:17-28
Nukuu:
“Niangalie, Ee Bwana,
ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya mema?
Maana wameichimbia nafsi yangu shimo,” Yer 18:19-20a
“Lakini haitakuwa hivyo
kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na
mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana
wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya
wengi,” Mt 20:26-28
TAFAKARI:
Tenda mema nyakati zote; KUTUMIKA ndiyo sababu ya UKRISTO wetu, na UTAMBULISHO
wetu mbele ya Mungu.
Wapendwa wana wa Mungu,
tumshukuru Mungu kwa zawadi ya kila mmoja wetu, kwa maisha na wito anaouishi.
Leo niwakaribishe tena kwa namna ya pekee tutafakari kiini cha maisha yetu kama
wafuasi wa Kristo, yaani, “Tenda mema nyakati zote; KUTUMIKA ndiyo sababu ya
UKRISTO wetu, na UTAMBULISHO wetu mbele ya Mungu.” Wapendwa tulio wengi katika
hili huwa tunakosa mwelekeo na kuanza kujilinganisha kimaisha. Wapo leo walio
kwenye maisha ya Ndoa wangependa kuishi kama watawa na Makleri; na wapo pia
walio watawa na Makleri wangependa leo kuishi kama wana Ndoa. Haya ni matamanio
ya kawaida ya mwanadamu aliye kamilika.
Ndugu yangu, hakuna wito
ulio bora zaidi ya mwingine mbele ya Uso wa Mungu. Kila mmoja wetu ni uzuri wa
Mungu, na Mungu anataka iwe hivyo kwa kumpendeza. Umoja wetu katika utofauti
ndio uzuri wa Mungu. Sote mbele ya Mungu tunamizania iliyo sawa. Na cheo chetu
sote ni kimoja tu, nacho ni UTAKATIFU wetu. Ni ukweli usiotia shaka kwamba,
kila mmoja wetu katika maisha na wito anaoishi, atapimwa kwa maswali haya
mawili mbele ya Mungu;
Swali
la kwanza: Umefanya nini kuhusu Mwangu Yesu Kristo, kwa
kuutoa uhai wake kwa ukombozi wako, na kadiri ya wito wako?
Swali
la pili: Je, umefanya nini na vipaji nilivyokupa?
Tusipokuwa tayari
kuyafanyia kazi maswali haya mawili tungali hai hapa duniani; tuwe tayari kulia
na kusaga meno, na tusio na meno hakika tutasaga fizi. Usicheke! Ndugu yangu
katika hili, haijalishi hapa duniani ulikuwa nani, una umaarufu gani, cheo
gani, nafasi gani, na jina gani. Sote tunaitwa kuwa wakamilifu-watakatifu kama
Baba yetu alivyo mtakatifu, Mt 5:48. Tukiwa tu waaminifu kwa kuyaishi hayo
maswali mawili, tutahuzunishwa na kukatishwa tamaa kama Nabii Yeremia
alivyofanyiwa. Nabii Yeremia kwa uchungu na unyonge, anamlilia Mungu kwa
kusema, “Niangalie, Ee Bwana, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je!
Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo,” Yer
18:19-20a.
Ndugu yangu, wapo
wanaotenda mema kila wakati lakini mwisho wa siku ni kuambulia masengenyo na
lawama. Tunapoona jambo hilo, tusikate tamaa kabisa. Hiyo ni alama ya kwamba
kazi uifanyao yampendeza Mungu na si mwanadamu. Hakuna mti wa mwiba upigwao
mawe. Ni mti ule tu ulio na matunda, tena yalikomaa na kuwiva ndiyo
hushambuliwao kwa mawe. Katika hili Yesu anatuambia wazi, “Heri ninyi
watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili
yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa
maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu,” Mt 5:11-12. Ndugu
yangu, wana heri tu wale wafanyiwayo hayo kwa jina la Yesu.
Tunapata neema na heri
tunapoteseka kwa ajili ya Yesu, na si vinginevyo. Kuteseka kwa ajili ya Yesu ni
kuishi, kutenda, kufikiri, na kupenda kama Yesu. Ni katika maana ya Ufalme wa
Yesu tunaweza kujifunza namna ya kutenda, kufikiri, kuishi, na kupenda. Kristo
Yesu, ni Mfalme wa Amani, Haki, Utii, Unyenyekevu, na Upendo. Kristo huyafanya
haya yote si kwa kutazamwa na watu, au kujipatia sifa binafsi, bali kwa
KUTUMIKA, na kuueneza Ufalme wa Baba yake. Hii ndiyo sababu ya Ukristo wetu.
Nabii Yeremia,
anahuzunishwa na mapigo anayoyapata kutoka kwa wale aliowapigania kwa jina la Mungu.
Mema yote aliyowatendea hawayaoni na badala yake wanakubali kuwa vipofu.
Yeremia, anasema, “Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili niseme mema kwa
ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate,” Yer 18:20b.
Ndugu yangu, wakutulipa
mema tunapoteseka kwa ajili ya Mungu na Mwanaye Yesu Kristo, na kwa kujua
sababu ya mateso hayo, si mwanadamu. Ukweli ni kwamba, “wasio haki watapotea,
nao wamchukiao Bwana watatoweka, kama uzuri wa mashamba, kama moshi
watatoweka,” Zab 37:20. Tuwe tayari kutumika muda na nyakati zote. Tuwe tayari
kusema na kuimba, “Bwana ni jabalí langu, na boma langu, na mwokozi wangu,
Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu
wangu, na ngome yangu. Na wokovu wa wenye
haki una Bwana; Yeye ni ngome yao wakati wa taabu,” Zab 18:2; 37:39.
Injili yetu ya leo
inalizungumzia kwa mapana swala hili la kutumika kwa ajili ya Ufalme wa Mungu,
na ndiyo sababu ya Ukristo wetu, na utambulisho wetu mbele ya Mungu.
Utambulisho wetu mbele ya Mungu hautokani na sababu ya kukaa kushoto kwake au
kulia kwake. Jambo la msingi ni kuyaishi yale maswali mawili ya Msingi. Tukiwa
waaminifu katika hayo, Yesu anasema, “kuketi mkono wangu wa kuume na mkono
wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu,”
Mt 20:23b. Waliowekewa tayari kwa maanisha wale walioyafanya mapenzi ya Mungu
kwa uaminifu. Swala hili halipo mwishoni mwa maisha yetu kama kupokea tunzo
fulani, bali kila siku ya maisha yetu twaishi tunzo hiyo, au kupokonywa tunzo
hiyo. Kila siku ya maisha yetu tupo darasani, na mtihani wetu ni UPENDO. Upendo
ndiyo mizania ya kila kitu tufanyacho.
Ndugu yangu
tunayesafiri pamoja katika tafakari hii, UTAMBULISHO wetu mbele ya Mungu, si
maisha ninayoishi, mfano; Maisha ya ndoa, Utawa, na Ukleri, au cho chote kile
ninachoishi kadiri ya wito wa Mungu, bali utambulisho wetu ni kwa namna
tunavyotumika kwa kuyatoa maisha yetu bila kujibakiza kwa upendo wake Mungu kwa
kile tulichoitiwa, na kama alivyofanya Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo. Utambulisho
huu kwa maana nyingine ni UTAKATIFU tunaojichotea kwa maisha tunayoyaishi hapa
duniani kila mmoja kadiri ya wito wake. UTAMBULISHO huu ndiyo tunzo na
UTAKATIFU wetu mbele ya Mungu.
Ndugu yangu, kwa Mungu
hatuendi na “CV” (Currículum vítae) zetu, kama tulivyozoea kusikua
historia fupi ya Marehemu. Huko mbinguni hakuna kazi tena zaidi ya kuishi
umilele tulioandaliwa, au kuteseka katika umilele tuliojiandalia kwa kuishi
ndivyo sivyo. Vyeti vyako, na historia yako kitaaluma ikuwezeshe kuupata
utakatifu huo kwa kutumika vyema. Kielelezo chetu kama wafuasi wa Kristo, ni
Kristo Yesu Mwenyewe.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Na mtu ye yote anayetaka kuwa wa
kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja
kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi,” Mt 20:27-28
Tusali:-Ee
Yesu, nipe ufahamu wa kuelewa vyema sababu ya yale yote unayonikirimia katika
maisha na wito ninaoishi, nami nitumike vyema kwa ajili ya wengine. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario