IJUMAA WIKI YA 3 YA KWARESMA
Somo:
Hos 14:2-10
Zab: 81:5c-7a, 7bc-8, 9-10ab, 13, 16
Injili:
Mk 12:28-34
Nukuu:
“Mimi nitawaponya
kurudi nyuma kwao, nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo, kwa maana hasira yangu
imemwacha,” Hos 14:4
“Mpende Bwana Mungu
wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa
nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii: Mpende jirani yako kama nafsi yako.
Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.” Mk 12:30-32
TAFAKARI:
“Kumpenda Mungu, Nafsi, na Jirani”
Wapenda wana wa Taifa
la Mungu, kadiri ya masomo ya leo na tufakari kwa pamoja, “kumpenda Mungu,
Nafsi, na Jirani.” Wapendwa neno upendo si geni katika masikio yetu. Ni neno
linalotumika sana, na kwa mizania hiyo ni neno linaloongoza kwa kuchakachuliwa
sana na kupoteza ule umaana wake. Neno hili upendo limebeba maana tofauti kwa
kila kundi au rika la watu, hasa katika jamii yetu ya leo. Kwa watoto neno
upendo huwa na maana na tafsiri nzuri pale tu wazazi wao wanapoishi na
kuonyesha upendo huo wao kwa wao, na kwa familia. Wazazi wakiishi hovyo basi na
watoto huwa na mwono mbaya wa upendo.
Neno upendo kwa vijana
walio wengi linatafsiri ya usaliti. Waliosalitiwa kwa upendo hukosa kuamini
uhalisia wa upendo, na hivyo hubaki katika hofu na majuto muda wote. Humfanya
kijani kuishi katika hatia. Hatia hii huondoa umaana wa maisha na makusudi
halisi ya uumbaji wake. Maisha na uzuri wake hukosa mwelekeo wa Kimungu, na
kubaki katika hali ya kutofahumu muda wote. Ni vigumu kuamini tena kama kuna
upendo wa kweli. Mara nyingi kijana huyu anapoyajenga mahusiano na kijana mwenzake
baada ya usaliti wa kwanza, swala la kwanza na la msingi kujua huwa hivi,
“tafadhili sipendi kuumizwa tena, kama upo ‘serious’ na utakacho niwe mimi na
wewe.”
Kwa walio na umri wa
kati-wazazi walio wengi, neno upendo linatafsiri ya “yawezekana,” katika hali
ya sintofaumu bado. Wengi katika kundi hili bado wanatafuta upendo wa kweli na
kuishi katika mahangaiko yasiyo na kikomo. Wazazi walio wengi, upendo haupo
tena, na hivyo huamisha mapendo yao kwa watoto kama wamebahatika kuwa nao. Ndoa
yao ina uhai kwa sababu ya watoto. Nyumbani wazazi hawa huishi kama wapangaji.
Wote wawili yaani baba na mama wanaishi katika mfumo wa “kukubaliana kwa
kutokubaliana,” yaani ilimradi liende tu.
Kwa kundi la wazee,
upendo hutegemea historia nzima ya ujana wao, na uzazi wao ulivyokuwa. Kama
waliishi vizuri hatua hizo, basi uzee wao hujaa matumaini makubwa na furaha.
Kama waliishi hovyo, basi uzee wao huwa na mateso makubwa sana. Hutamani wakati
kwingine kufa mapema. Kila kitu kwao huwa kibaya. Kila siku kwao huishi kwa
kulalamika na kutoa laana.
Ndugu yangu, hata wewe
unayesoma tafakari hii, unayo mengi ya kusema kuhusu upendo na hasa ukiyatazama
maisha yako unayoishi sasa, uliyaishi na mtazamo wako wa baadaye. Upendo wa
Binadamu yeyote anayemjua Mungu na asiye mjua Mungu, huegemea katika mambo
matatu; kwa mwenye imani na uwepo wa Mungu, basi atampenda Mungu; Nafsi yake;
na jirani yake. Asiyeona uwepo wa Mungu, basi badala ya Mungu atapenda kitu
fulani ua nguvu fulani, nafsi yake, na jirani yake.
Somo la kwanza, msisitizo
upo katika kumpenda Mungu. Tunampenda Mungu kwa sababu ya kile tulicho, kwamba
tumeumbwa kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27, na hivyo ipo nguvu ndani yetu
inayotuvuta kwake, ingawa twaweza kumsaliti, na kufuata njia zetu kutoka na
uhuru aliotuachia. Twampenda Mungu pia kwa sababu Yeye ni UPENDO, MSAMAHA, na
yote MEMA upatikana kwake. Ukamilifu wote upo kwake. Yeye ni yote katika yote.
Naye Mungu anasema, “Mimi nitawaponya kurudi nyuma kwao, nitawapenda kwa
ukunjufu wa moyo, kwa maana hasira yangu imemwacha,” Hos 14:4.
Ndugu yangu, Mungu ni
mwema na hutuwazia mema muda wote. Tunapoasi na kumsaliti, huadhibiwa kadiri ya
makosa yetu. Ila tunapojirudi na kukiri wema wake, Yeye husamehe yote na kuanza
mpya nasi. “Kwa maana Bwana asema hivi, Kama nilivyoleta mabaya makuu haya yote
juu ya watu hawa, vivyo hivyo nitaleta juu yao mema yote niliyowaahidia,” Yer
32:41. Tunachotakiwa kufanya nyakati zote ni kutenda mema na kutafuta mema kwa
watu wote. “Yachukieni mabaya; yapendeni mema; mkaithibitishe haki langoni; yamkini
kwamba Bwana, Mungu wa majeshi, watawafanyia fadhili mabaki ya Yusufu,” Amo
5:15.
Ndugu yangu, leo katika
Taifa letu tumefikia hatua mbaya sana. Leo kuutoa uhai wa mtu na kuufanyia
mzaha mwili wa mtu ni jambo la kawaida na la kufikika. Jamii yetu leo ishaanza
kuzoe hali hii. Ndugu zetu kwenye ulemavu wa ngozi-Maalbino, hawaishi tena kwa
amani na matumaini. Viongozi wetu na wana harakati wanaosema na kukemea maovu
wanauwawa na hata kupotezwa au kupoteza baadhi ya viungo vyao kutoka na utawala
dhalimu tulionao.
Je, Mungu anasema nini
kuhusu jambo hili? Tusidhani kuwa Mungu hayaoni mambo haya. Mungu anasema,
“ninyi mnaoyachukia mema, na kuyapenda mabaya; ninyi mnaowachuna watu ngozi
yao, na nyama mifupani mwao. Naam, mnakula nyama ya watu wangu, na kuwachuna
ngozi zao, na kuivunja mifupa yao; naam, kuwakata vipande vipande kama kwa
kutiwa chunguni, na kama nyama sufuriani. Ndipo watakapomwomba Bwana,
asiwaitikie; naam, atawaficha uso wake wakati huo, kwa kadiri walivyotenda
mabaya kwa matendo yao,” Amo 3:2-4. Kwa matendo haya, tunajichumia laana kila
siku kama Taifa.
Ndugu yangu sipendi
kukuchosha, ila nivumilie kidogo nitakuacha. Injili yetu ya leo, inaliweka
jambo hilo katika matendo, yaani, kumpenda Mungu, nafsi, na Jirani. Mizania ya
kumpenda Mungu na jirani ni upendo ulionao wewe na hali uliyonayo kwa kujipokea
kama ulivyo. Ni vigumu kumpenda Mungu na Jirani, kama wewe mwenyewe hujipendi,
hujipokei, na hujithamini. Katika jambo hili,
Bwana wetu Yesu Kristo anasema, “Mtu mwema katika hazina njema ya moyo
wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa
yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake,” Lk
6:45. Wapendwa wana wa Mungu, binadamu ye yote yule hutoa kwa wengine kile
alichonacho. Huwezi kutoa usicho nacho. Hukumu yetu siku ya mwisho imejikita
katika kutenda mema. Fanya ufanyacho leo katika maisha yako, lakini usisahau
kutenda mema. Kutenda mema ikiwa ndiyo dira ya maisha yako kila siku, kamwe
hutowaza kutenda mabaya licha ya kwamba uwezo huo wa kutenda mabaya unao. Huu
ndio uhuru wa kweli kimaadili.
Tendo hili la wema
hutuinua hasa pale tunapolifanya hata kwa wabaya wetu. Tunainuliwa na kuwa wana
wa aliye juu. Hiki ndicho cheo chetu chenye thamani kubwa kuliko vyote
tunavyoweza kufikiri. Cheo hiki ni utakatifu wako. Katika jambo hili, Yesu
anasema, “Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini
kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu,
kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu,” Lk 6:35. Tendo hili licha
ya kutufanya wana wa Aliye juu, linatupa uhakika na mastahili ya Mungu kwa uzima wa milele. Kwetu kama binadamu ni
changamoto kubwa sana. Ukitenda mema utasemwa vibaya, na usipotenda mema
utasemwa pia vibaya. Kilichobaki ni kutenda mema na kutotazama macho ya watu na
maoni yao ikiwa jambo hilo linakibali mbele ya Mungu, kwani, “wale ambao kwa
saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika,
watapewa uzima wa milele,” Rum 2:7. Je, jambo hili maana yake nini?
Ndugu yangu, utendapo
mema fanya hivyo pasipo ubaguzi. Usifanye kwa vile huyu ni ndugu yangu au kwa
vile ninamfahamu. Fanya mema kwa vile wema ni sifa ya Mungu. Nitende sifa ya
Mungu na kwa ajili ya Mungu. Kwa mantiki hii, “msilipe mtu ovu kwa ovu.
Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote,” Rum 12:17. Kati ya vitu ambavyo
Mungu hutujibu mara moja tutendapo ni swala hili la wema. Na hapa ndipo
tunaposema kwamba Mungu ni “mwema kila wakati.”
Utendapo jambo jema, Mungu hukujibu kabla ya kuzimia roho yako. Mpendwa,
“tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si mbele za Bwana tu, ila na mbele ya
wanadamu,” na tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati
wake, tusipozimia roho,” 2Kor 8:21, Gal 6:9. Tenda wema ndugu yangu na uende
zako, wala usingoje shukrani.
Hii ndiyo sababu kubwa
ya maneno ya Yesu katika injili ya leo, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako
wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na
ya pili ndiyo hii: Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine
iliyo kuu kuliko hizi.” Mk 12:30-32. Ndugu yangu, elewa kwamba, unaweza kutoa
kitu bila kupenda hasa pale mtu huyo anaposisitiza kitu hicho, na ukasukumwa
kutoa ili uachane na karaha ya kusumbuliwa. Ila huwezi kupenda bila kutoa. Kwa
maana hiyo, upendo wetu kwa Mungu na Jirani unaonekana na kutulazimu kwa upendo
kujitoa na kutoa. Tunatoa kwa Mungu na Jirani; nafsi zetu, muda wetu, maarifa
yetu pamoja na vipaji vyetu, na mali tulizonazo. Anayeyaishi haya na kuyatenda
kesha mwona Mungu.
Ndugu yangu “mpenzi,
usiuige ubaya, bali uige wema. Yeye atendaye mema ni wa Mungu, bali yeye
atendaye mabaya hakumwona Mungu,” 3Yoh 1:11.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Lakini ninyi, Ndugu, msikate tamaa
katika kutenda mema,” 2Kor 3:13
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, uliufia ulimwengu kwa sababu ya kunipenda kuliko vitu vyote. Nami
nijalie neema hiyo ya kupenda kama ulivyonipenda. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario