martes, 28 de febrero de 2017

TAFAKARI: ALHAMISI BAADA YA JUMATANO YA MAJIVU


ALHAMISI BAADA YA JUMATANO YA MAJIVU

Somo: Kumb 30:15-20

Zab: 1:1-4, 6

Injili: Lk 9:22-25

Nukuu:

Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako,” Kumb 30:19.

kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa,” Kumb 30:20

“Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate,” Lk 9:23

Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha,” Lk 9:24.

Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?” Lk 9:25

TAFAKARI: “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.”

Wapendwa wana wa Mungu, maelekezo ya Mungu juu ya maagizo yake iwe amri au sheria, hayana lengo la kuukandamiza uhuru wetu, bali endapo tutakuwa ndani ya mwongozo huo hapo ndipo ulipo uhai na umilele wetu. Kwa maana nyingine, Mungu wetu siyo mfano wa Jitu katili ambalo lengo na kiini cha utendaji wake ni kwa ajili ya ubinafsi wake. Mungu alipenda na kupendezwa kumuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake si kwa kujifaidia mwenyewe, bali kwa sifa na utukufu wake. Uwepo wetu haumpunguzi wala kumwongezea Mungu chochote na hasa katika utukufu wake. Ila kuishi kadiri ya maagizo ya Mungu kuna faida kwetu ikiwa ni kuishi katika Amani ya kweli, na mwisho wa maisha haya hapa duniani tuwe na maisha ya milele pamoja naye.

Hata pamoja na nia njema hii, Mungu hatushurutishi kumtii ili tufaidike na utukufu wake, ila kwa kumfuata kwa hiari bila kuburuzwa ni njia mojawapo ya kufunuliwa utukufu wake. Hivyo leo ni hiari yako na yangu kuchagua uzima au umauti. “Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya; kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki,” Kumb 30:15-16. Ndugu yangu, Mungu tu ndiye apaswa kuabudiwa kuliko kwa kweli na haki. Kinyume cha hapo ni balaa tupu, Kumb 30:18. Ni katika ukweli huu kwamba “kujisalimisha” kwa Mungu ndiyo njia pekee na sahihi ya kumjua, kumpenda, kumtumikia na mwisho kurudi kwake mbinguni. Kujisalimisha huku kwa hiari ndiko Yesu anakosema “kuikana nafsi.” “Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha,” Lk 9:24. Ingawa uhai na umauti kuwa sehemu ya ubinadamu wetu, ipo nafasi kubwa ya umilele kama wewe na mimi tutaamua vyema hatma ya maisha yetu kwa kujisalimisha huko kuliko kwa hiari. Naye Mungu anasema, “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako,” Kumb 30:19.

Wapendwa wana wa Mungu, uzima wetu upo pale tunapozishika amri za Mungu siyo kwa woga mbali kwa kuzipenda kwani mwisho wake ni umilele. “Kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa,” Kumb 30:20. Hivyo tafsiri ya sheria ya Bwana siyo teso bali ni njia ya kuyajua mapenzi yake kwako. “Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya Bwana,” Zab 119:1

Kwa maana hiyo, ni lazima nichague kumtii Mungu katika Imani. Kila wakati unapoamini hekima ya Mungu na kufanya kila analosema, hata pale unapokuwa huelewi, unakuza urafiki wako na Mungu. Mara nyingi hatufikiri utii kama sifa ya urafiki na Mungu wa sababu ya mausiano yasiyo ya afya kati yetu na mzazi, mkubwa wa kazi, na hata majirani zetu. Lakini Yesu aliweka wazi kwamba utii ni kigezo cha uhusiano na Mungu. “Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo,” Yoh 15:14. Sisi ni marafiki na Mungu, lakini siyo sawa na Yeye. Yeye ni kiongozi wetu atupendaye, na tunamfuata. Tunamtii Mungu, si kama wajibu au kwa hofu au kwa kushurutishwa, bali kwa sababu tunampenda na tunaamini kwamba anajua kile kilicho bora kwetu. Tunataka kumfuata Kristo kwa shukrani kwa yote aliyotufanyia, na tunapomfuata kwa karibu, ndipo urafiki wetu naye unakuwa wa kina zaidi.

Wasioamini mara nyingi hudhani kwamba Wakristo hutii kwa sababu ni wajibu, au kuogopa lawama, au kuogopa hukumu, lakini ukweli ni kinyume cha hayo. Kwa sababu tumesamehewa na kuwekwa huru, tunatii kwa upendo, na utii wetu hutuletea furaha kubwa! Yesu anasema, “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe,” Yoh 15:9-11.

Angalia jinsi ambavyo Yesu anatutazamia kufanya yale tu aliyotenda kwa Baba yake. Uhusiano wake na Baba yake ni kielelezo cha uhusiano wetu naye. Yesu alifanya chochote Baba alichomwagiza kufanya, kwa upendo. Urafiki wa kweli si wa kukaa tu, bali ni wa vitendo. Yesu anapotuagiza kuwapenda wengine, kusaidia wahitaji, kuwagawia wengine mali zetu, kuwa na maisha safi, kusamehe, na kuwaleta wengine kwake, upendo hutuchochea kutii mara moja. Mara nyingi tunapewa changamoto ya kumfanyia Mungu “mambo makubwa.” Ni dhahiri kwamba Mungu anafurahishwa zaidi tunapotenda mambo madogo madogo kwa ajili yake kutokana na utii wa upendo. Yawezekana huwa hayaonekani kwa wengine, lakini Mungu anayaona na kuyahesabu kuwa matendo ya kuabudu.

Nafasi kubwa inaweza kutokea mara moja katika maisha, lakini nafasi ndogo ndogo zinatuzunguka kila siku. Hata katika matendo madogo kama vile kusema kweli, kuonyesha wema, kuwatia moyo wengine, tunaleta tabasamu katika uso wa Mungu. Mungu anathamini matendo rahisi tu ya utii kuliko sala zetu, sifa na sadaka. “Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu,” 1Sam 15:22.

Yesu alianza huduma yake ya hadharani katika umri wa miaka thelathini kwa kubatizwa na Yohane. Katika tukio hilo Mungu alizungumza kuto mbinguni; “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye,” Mt 3:17. Je, Yesu alikuwa anafanya nini kwa miaka thelathini ambacho kilimfurahisha Mungu? Maandiko Matakatifu hayasemi kitu kuhusu miaka hiyo iliyojificha, isipokuwa kwa maneno machache kutoka Mwinjili Luka, kwamba “Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake,” Lk 2:51. Miaka thelathini ya kumpendeza Mungu ilijumlishwa katika maneno: “naye alikuwa akiwatii.” 

Hivyo wapendwa katika Kristo, kama tuonavyo masomo yetu ya leo yanatuelekeza kufanya maamuzi ya kweli kuhusu maisha yetu na kumfuata Kristo. Je, Yesu anasema nini juu ya AMRI? Yesu yupo wazi kabisa kuhusu amri na mahusiano yake na umilele. Amri ni ‘Upendo’ ambao kwa kupitia Yeye, yaani Kristo, upendo wa Mungu Baba ni dhahiri kwetu. “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo,” Yoh 13:34. Hivyo kumpenda Kristo na Mungu Baba ni kuishika amri hii ya Mapendo. “Mkinipenda, mtazishika amri zangu,” Yoh 14:15. Hivyo mara zote yanipasa mimi na wewe nimwone Kristo kwa yeyote yule nitakaye kutana naye bila kujali itikadi zetu za maisha, familia zetu, koo zetu, makabila yetu na utaifa wetu.

Wapendwa wana wa Mungu, kumtambua Kristo katika maana ya kuwa na amri zake Kristo na kuzishika ni kumpenda Kristo na huko ndiko kupendwa na Mungu Baba. Hili ndilo dhihirisho la Kristo kwetu, yaani, kuishi ndani na katika Kristo Yesu. Naye Yesu anasema, “Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake,” Yoh 14:21. Ndugu yangu, wewe na mimi tu wafuasi wa Kristo kwa kuzishika amri zake na huko ndiko kukaa katika pendo la Kristo. “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake,” Yoh 15:10. Licha kwamba hapa Yesu katumia muda mwingi kuelezea amri, ukweli ni huu anaousema kuhusu amri; “Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi,” Yoh 15:12. Sadaka ya Yesu pale msalabani yanipasa ihakisi na isadifiwe na kutukuzwa daima kwa kupendana sisi kwa sisi. Tusipofanya hivyo, ni kwamba tunaendelea kumsulubisha Yesu pale msalabani.

Kati ya mtihani mgumu wa maisha ni kuamua kuacha jambo fulani ulilolizoea na kuanza njia nyingine. Hapa ndipo wengi hushindwa. Mara nyingi tunajawa hofu ya sintofahamu ya mambo yajayo na tusiyo yajua. Ila kama kweli tunataka kuwa karibu na Mungu, na kuokoa nafsi zetu yatupasa kufanya maamuzi. Maamuzi ye yote yale katika maisha yana gharama zake. Na uamuzi utakaochukua lazima utapimwa. Wengi watakushangaa na hata kukucheka. Wala usihofu kwa sababu duniani hapa ni mahali tu pa kujiandaa kwa ajili ya umilele.

Somo la kwanza kwa mantiki hiyo, linatupa angalisho; kuchagua kati ya kifo au uhai. Uzuri na utamu wa maisha haya ya leo na sasa unatutia upofu wa kuona uzuri wa maisha ya umilele. Jambo hilo Yesu analiongelea katika mfumo wa msalaba. Tusipokuwa tayari kujikana, kuchukua misalaba yetu, na kumfuata, hatufai kuwa wanafunzi wake. “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate,” Lk 9:23.

Jambo hili la maanisha nini?

Kuikana nafsi ni tendo la kuvua mwelekeo na mvuto wa yale uyapendayo na yasiyo na tija ukilinganisha na maisha ya umilele. Na maisha yasiyo na tija ni pamoja  na "ponda mali kifo chaja." Ni maisha ya kutokuwa na hofu ya Mungu. Ni maisha ya kujipenda kupita kiasi na kujihurumia. Ni maisha ya kuukataa ubinadamu wako na mipaka yake na kujiona mungu mtu. Huku ni kutoikana nafsi.

Kuubeba msalaba ni kukubali kuongozwa. Ni kukubali mapungufu yako kama binadamu ili iwe changamoto kwako kuelekea ukamilifu. Ni kujipokea. Ni hali ya uitaji wa neema ya Mungu. Ni hatua muhimu ya awali kuanza kukua kiroho. Ni kukubali kujiachia mikononi mwa Mungu na kumtegemea yeye tu. Ni kuwa na imani juu ya Mungu ingawa mapungufu yapo kama binadamu.

Kumfuata Yesu, ni kumfanya Yesu kuwa njia, na ukweli, na ulizi, Yoh 14:6. Yesu ni njia kuelekea uzima wa milele. Hakuna njia nyingine ndugu yangu. Na njia aliyochagua Yesu ni msalaba. Nasi kama wafuasi wake, msalaba haukwepeki. Yesu ni ukweli. Ukweli huu ndio utakao tuweka huru, Yoh 8:32. Yesu Kristo ndiyo uzima wetu. Mwili na damu yake Yesu ni uzima na uhai kwetu, Yoh 6:54.

Ndugu yangu, wakati wa kukata shauri ni sasa na kumrudia Mungu. Kishawishi kikubwa ni kudhani kuwa muda bado upo. Linalowezekana leo, lisingoje kesho.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria, ili kila aaminiye ahesabiwe haki. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu,” Rum 10:4, 10

Tusali:-Ee Yesu na Ngome yangu, nijalie neema ili niweza kujinasua katika vifungo vyangu vya kimwili na kiroho. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario