jueves, 29 de septiembre de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 27 YA MWAKA-C


JUMATATU WIKI YA 27 YA MWAKA-C

Somo: Gal 1:6-12

Zab/Kit: 111:1-2, 7-8, 9, 10c

Injili: Lk 10:25-37

Nukuu:

“Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine,” Gal 1:6

“Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe,” Gal 1:8

 “Na tazama, mwana-sheria mmoja alisimama amjaribu; akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Lk 10:25

“Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako,” Lk 10:27

TAFAKARI: “Nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?

Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na mbwembwe zote za mwanadamu hapa duniani, ni wajibu wa kila mmoja wetu kujiuliza swali hili la msingi alilouliza mwana-sheria mmoja wa Kiyahudi kwa Yesu kuhusu uhai. Mwana-sheria huyu anamuuliza Yesu hivi; “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Lk 10:25. Msingi wa swali hili haupo kwenye uhai tu wa leo na kesho, bali uhai katika umilele wake. Tuelewe kwamba mwanadamu ameumbwa kuishi milele, na hayo ndiyo makusudi ya Mungu katika uumbaji wa mwanadamu.

Tatizo kubwa la mwanadamu ni mbwembwe nyingi alizonazo akisahau kuwa muda aliopewa hapa duniani hausimami kumsubiri. Mhubiri anatuwasa na kusema, “mwanadamu hadumu katika heshima, bali amefanana na wanyama wapoteao,” Zab 49:12. Fahari ya mwanadamu ni yule aliyemuumba, yaani Mungu wake. Mengine yote ni mbwembwe tu! Mche Bwana, Mungu wako, umtumikie yeye; ambatana naye, na kuapa kwa jina lake. Yeye ndiye fahari yako, na yeye ndiye Mungu wako, aliyekutendea mambo haya makubwa, ya kutisha, uliyoyaona kwa macho yako,” Kumb 10:20-21. Ndugu unayesafiri nami katika tafakari hii, elewa kwamba utajiri wako, ufahamu wako (kiwango cha elimu ulicho nacho), umaarufu wako, nk, bila Mungu ni bure kabisa.

Yesu kabla ya kumjibu vizuri mwana-sheria yule wa kiyahudi alitaka kujua uelewa wake wa Maandiko Matakatifu (Torati) yanasema nini kuhusu uhai wa Milele. Mwana-sheria yule akamjibu kwa staha, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako,” Lk 10:27. Yesu anaridhika na jibu hili na anamwambia hivi; “Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi,” Lk 10:28. Kuishi kwetu hapa duniani ambapo kunatupelekea kuishi milele baada ya kifo, kama wanadamu kwatuwajibisha kufanya kwa weledi mkubwa mambo makuu mawili.

Moja, mpende Mungu wako kwa moyo wako wote, roho yako yote, na nguvu zako zote. Kwa maana nyingine ni kutumia vyote Mungu alivyokujalia ili umpende na ubaki kumpenda daima. Afya yako njema, akili yako ya pekee, utajiri wako, na umaarufu wako hapa nduniani isiwe sababu ya kujitenga na upendo huu wa Mungu. Hayo Mungu aliyokujalia kwa namna ya pekee isiwe sababu ya kuwakejeli wenzako ambao kwa mtazamo wako wa kibinadamu waona hawastahili mema yoyote mbele ya uso wa Mungu.

Ndugu yangu, hata yale tunayoyaona kwa macho yetu kama udhaifu wa mtu na wengine, Mungu wakati mwingine utumia udhaifu huo kutufundisha siri ya maisha na uhai tuliopewa na Mungu mwenyewe. Maisha  na uhai tuliyonayo ni mali na zawadi yake Mungu. Mimi na wewe tumepewa uhai huu na kuazimwa kwa muda tu hapa duniani kama sababu ya kuutumia vyema uhai huu ili tuishi milele baada ya muda ambao kila mmoja wetu kapewa kadiri ya mapenzi yake Mungu. “Maana siku zangu zinatoweka kama moshi, Na mifupa yangu inateketea kama kinga,” Zab 102:3.

Pili, nimpende jirani yangu kama nafsi yangu. Jirani yangu ni yeyote yule ninayekutana naye na wale wote wanaonizunguka, yaani, wahitaji na wasio wahitaji. Jirani yangu ni kama kioo cha kujitazama ukamilifu wangu mbele ya Mungu. Je, udhaifu wa jirani yangu unasema nini kuhusu maisha yangu mimi niliyejiinua na kujiona safi na mwema kuliko wengine? Yesu, anakemea hali hii kwa Mafarisayo na Waandishi, na kwetu pia. Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi,” Mt 23:2-3. Mtazamo huu wa ugeugeu na kujiinua mbele za Mungu pasipo mastahili yoyote ndio sababu ya mfano wa Msamaria mwema.

Wafarisayo ambao kwa kiasi kikubwa walijiinua na kuwa wepesi kuwahukumu wengine, wanashindwa kuokoa uhai ambao ni mali na zawadi ya Mungu kwa vile tu muhitaji huyu na mhusika huyu hakuwa Myahudi. Wakati mwingine tunashindwa kusimama katika kweli kwa vile tu mhusika siyo kutoka familia yetu, ukoo wetu, kabila letu, au kutoka Kanda yetu. Wenye mitazamo kama hii ilihali wanajiita wafuasi wa Kristo, basi Kristo huyo huendelea kusulubiwa kwa matendo yao. Kristo huyo siyo fahari ya maisha yao. Mimi na wewe kama wafuasi wa Kristo hatuna kitu kingine cha kujivunia zaidi ya Msalaba wa Kristo.  Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14. Je, tusikemee maovu? La hasha! Mkemeapo Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote. Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa,” 1Pet 2:1, 21, 23-24. Je, nauona udhaifu wangu ninapoutazama udhaifu wa mwingine?

Wapendwa wana wa Mungu, Yesu anapomwambia mwana-sheria yule afanye tathimini kati ya wale wayahudi na yule Msamaria aliyetoa msaada kwa mhitaji yule aliyepata kipigo na wanyang’anyi, mwana-sheria anaelewa soma lile na kumjibu Yesu, “Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo,” Lk 10:37. Wapendwa katika Kristo, yatupasa kusimama katika kweli na haki, hivyo tutende yote kwa upendo na huruma ya kweli. Tusipolifanya jambo hilo basi tujiandae kusutwa na dhamiri zetu katika umiele wote.

Wapendwa wana wa Mungu, mamlaka aliyokuwa nayo Yesu ni vita dhidi ya uovu hapa duniani. Ni ukweli usiopingika kwa kupitia jina lake tunapata uponyaji wa kweli. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende,” Mdo 3:6.  Mamlaka ya Yesu yamejengwa chini ya mamlaka ya Mungu.

Hivyo hakuna jambo lolote alifanyalo Yesu Lisilo kuwa na uhusiano na Mungu, huku jambo lile likifunua siri ya Mungu kila kukichwa. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake,” Kol 1:16. Kwa nini basi nakuwa na mashaka juu ya utendaji wa Kristo katika maisha yangu?

Wapendwa katika Kristo, Yesu anapotoa mfano wa vazi kuukuu na jipya, na kwa upande mwingine divai ya zamani na kiriba kipya anataka kutufundisha jambo hili; “kwanza kabisa lazima tujue sababu na malengo ya maisha yetu hapa duniani. Hatupo hapa duniani kwa bahati mbaya hata kidogo. Tupo katika ulimwengu huu kadiri ya mpango wa Mungu ambao ni dhahiri na mathubuti. Hivyo lolote lile lililo jema mbele ya Mungu huwiishwa na kufanya upya.

Somo letu la kwanza, linauelezea uhali wa jambo hili, yaani,  Mungu ili awe sehemu ya maisha yako na kielelezo cha yale yote uyafanyayo, yakupasa kuushinda ubinadamu wako na matamaniyo yake. Kuushinda ubinadamu wako, yakupasa kujipokea na kujikubali kwamba wewe ni binadamu katika maana ya mafanikio yako na mapungufu yako. Katika uwezekano huu, ikiwa ni mafanikio na mapungufu yake, binadamu anabaki kuwa binadamu, na Mungu anabaki kuwa Mungu katika ukamilifu wake.

Hivyo kuwa wakamilifu kama Mungu alivyo mkamilifu kwake Yeye mwenyewe na kwetu sisi, twahitaji kuipokea hali yetu ya ubinadamu, na wakati huo huo kuushinda ubinadamu wetu huo kwa kuegemea ukamilifu ule tulioitiwa na Mungu. Naye Yesu katika kweli hii anasema, Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48. Huu ndio wito wetu wa kila siku na kulingana na mazingira yoyote yale tutakayokuwa, yaani, kuwa wakamilifu kama ‘Baba yetu wa mbinguni alivyo makamilifu.

Kwa kuujua ukweli huo, Mtume Paulo analiweka jambo hili wazi kwa watu wake na kusema, Paulo, mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka kwa wafu), na ndugu wote walio pamoja nami, kwa makanisa ya Galatia,” Gal 1:1-2. Ni wazi kabisa Mtume Paulo anataka tuwe makini kwa jambo hili: ‘kamwe tusijifananishe na matokeo ya mafanikio yetu, bali tuutazamie ule utukufu na ukamilifu tulioitiwa.’ Kuna anguko kubwa sana pale tunapojifananisha na kujilinganisha na mafanikio yetu binafsi.

Mazingira hayo ndiko kwenye chimbuko kubwa la majivuno, na penye majivuno hakuna ukuaji wa maisha ya kiroho. Mwenye majivuno hana nafasi ya Kristo ndani ya maisha yake. Nafasi ile ya Kristo imetawaliwa na ubinafsi wake na umimi wake. Katika hali hii kuna anguko kubwa sana la kurudi nyuma katika imani. Mtume Paulo haoni haya kuusema ukweli huu; Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine,” Gal 1:6. Ndugu yangu, yote yaliyo ya kibinadamu pasipo uhusiano na Mungu, hayana umilele.

Wapendwa wana wa Mungu, kilichohubiriwa na Kristo wakati ule katika historia ya wokovu wetu, na sasa kama kielelezo cha Kanisa lililo hai, na Sakramenti ya wokovu wetu ni habari njema ya wokovu wetu. Habari hii njema ya wokovu wetu hii hai muda wote na katika umilele wote.

Hivyo kwenda kinyuma na agizo hili la Yesu kabla ya kupaa kwake ili hali tunajua, ni kuipalilia ‘laana huku tukijua.’ Agizo hilo ndilo hili, ‘kwa Kanisa kama Sakramenti ya wokovu, na kwa Kanisa kama Mwili wa Kristo, yaani, kila aliyebatizwa na kuishi ahadi zake za ubatizo; Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa,”’ Mk 16:15-16.

Hiki ndicho akisemacho Mtume Paulo wa Wagalatia kuhusu mahusiano ya Habari Njema ya wokovu na laani ipatikanayo kwa kutokuhubiri kweli iliyo katika habari njema hivyo. Naye anasema, Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe,” Gal 1:8.

Kweli iliyo ndani ya habari njema ya wokovu wetu hubaki na kuhubiriwa kama ilivyo pale tunapoushinda ubinadamu wetu. Mtume Paulo anatutafakarisha kwa kusema, Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo,” Gal 1:10. Ndugu yangu, panapozidi ubinafsi wetu, Kristo hana nafasi.

Wapendwa wana wa Mungu, Kristo aliye Njia, Kweli, na Uzima wetu, Yoh 14:6, anapokosa nafasi katika maisha yetu, ni kwa namna hiyo hiyo, Mungu hana nafasi katika maisha yetu. Je, twawezaje kumfikia Mungu bila kupita kwake Kristo aliye na mamlaka yote? Kristo Yesu anaweka wazi ukweli huu na kusema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu,” Yoh 6:65. Kuupata au kuufikia Ufalme wa Mbinguni bila Kristo, ni sawa na samaki kuishi na kustawi bila maji. Je inawezekana?

Tumsifu Yesu Kristo!

“Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe,” Gal 1:9

Tusali:-Ee Yesu, nitumie kadiri ya takwa lako, ili ujulikane pale usipojulikana. Amina

TAFAKARI: JUMAPILI YA 27 YA MWAKA-C



Somo I: Hab 1:2-3; 2:2-4

Zab/Kit: 95:1-2, 6-7, 8-9

Somo II: 2Tim 1:6-8, 13-14

Injili: Lk 17:5-10

Nukuu

“Ee Bwana, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu, ila hutaki kuokoa,” Hab 1:2

“Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji,” Hab 2:2

“Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu,” 2Tim 1:6

“Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi,” 2Tim 1:7

“Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu,” 2Tim 1:14

“Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee imani,” Lk 17:5

“Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng'oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii,” Lk 17:6

“Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk 17:10

TAFAKARI: “Tuongezee imani Bwana.”

Wapendwa wana wa Mungu leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 27 ya mwaka “C” wa Kanisa. Mama Kanisa kwa namna ya pekee leo anatutaka tutafakari kwa makini kuhusu IMANI. Imani ikiwa ni kuamini pasipo shaka yanayoonekana na yasiyoonekana, Ebr 11:1, Imani thabiti ni suluhu ya mambo mengi tusiyoyajua bado. Imani thabiti utuzamisha kwenye fumbo zima la maisha. Ukweli ni kwamba ingawa twaishi katika ulimwengu huu yapo mambo mengi tusiyoyajua licha ya ufahamu wetu kama wanadamu.

Nabii Habakuki aliyefanya unabii wake katika jamii isiyo amini katika haki na baadaye kuwa chukizo kwa Mungu, anaona anguko kubwa sana mbele yake. Unabii huu unafananishwa na kile alichokiona Yesu kutokea juu ya anguko la Yerusalemu na mwisho wa nyakati, Mt 24. Pamoja na ukweli kwamba Nabii Hakukuki anaona uovu ndani ya jamii yake, na watesi wao, yaani, mataifa yaliyokuwa yanawazunguka, pona yao kama taifa kutoka ovu huo ni kusimama katika imani ya kweli na haki. Kuushinda uovu uliosababishwa kwa kutokutenda haki, Mungu anamjibu na kusema, “Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake,” Hab 2:4.

Hata pamoja na jibu hilo la Mungu, kuelewa ukweli huo na kuukubali kwa wezekana tu kwa Imani. Ni kwa imani tu twaamini ushindi wa mwisho katika uaminifu wetu kwa Mungu. Sehemu hii ya unabii wa Habakuki twaweza utafasiri katika mwelekeo wa fundisho kadiri ya vitabu vile vya hekima. Naye Nabii Isaya katika kweli hii anasema, “Nyakati zako zitakuwa nyakati za kukaa imara; za wokovu tele na hekima na maarifa; kumcha Bwana ni hazina yake ya akiba,” Isa 33:6. Na katika mwono huo huo na ulio wa juu zaidi, Mtume Paulo katika fundisho lake la kuhesabiwa haki kwa Imani, anasema, “Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani. Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani,” Rum 1:17; Gal 3:11. Hapa hakuna mkanganyo au kupingana kwa kweli hiyo. Uaminifu kwa Mungu ndiyo upekee huo uokoao, na uaminifu ndio uwezekano wa Imani kwa Mungu.

Mtume Paulo katika mantiki hii anatutaka tuelewe kwamba wokovu siyo tu swala la imani kwa wakati ujao, bali ni tendo la imani halisi, na chanzo cha uaminifu endelevu. Undani na uzito wa fundisho hili la Mtume Paulo ndilo alisemalo kwa Timotheo kwamba, “Shika kielelezo cha maneno yenye uzima uliyoyasikia kwangu, katika imani na upendo ulio katika Kristo Yesu. Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu,” 2Tim 1:13-14

Katika somo letu la Injili, Mitume wanamwomba Yesu awaongezee Imani, Lk 17:6. Kwa upande mwingine twaweza kuona tatizo  ambalo linawakabili wafuasi wake Yesu-Wakristo, ikiwa ni pamoja na wewe na mimi kama wabatizwa. Fundisho la Yesu, yaani, “Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng'oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii,” Lk 17:6, tunaweza lihusisha na habari ile ya uponywaji wa kijana yule aliyekuwa na pepo mwenye kumtesa sana, na wanafunzi wake Yesu kushindwa kumtoa, Mk 9:18. Baada ya Yesu kumkemea Baba wa kijana yule kwa kutokuwa na Imani, “Mara babaye yule kijana akapaza sauti, akasema, Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu,” Mk 9:24.

Ndugu yangu, Imani ya kweli na thabiti hata kama ingekuwa ndogo kiasi gani inatokeo kubwa na la ajabu katika maisha yetu, (Rej Mt 17:20, 21:21). Neno kuhusu mtumwa, Mt 17:7-10, linatupatia fundisho la pekee. Yesu mwenyewe akiichukulia hali ya maisha yake aliyokuwa akiyaishi licha ya ukuu aliokuwa nao-Mungu na Mwanadamu, mtumwa anatufundisha na kutuonyesha fundisho hususi kuhusu habari njema. Mtumwa hawezi jiinua na kujipongeza kwa kazi yake, zaidi ya kufanya na kutimiza wajibu wake. Na hivi ndivyo Mtume Paulo asemavyo, “Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili!” 1Kor 9:16. Hakuna la kujisifia, zaidi ya kutimiza kwa uaminifu kile upaswacho kutimiza.

Fundisho hili ya Yesu katika Injili ya leo linaenda kinyume kabisa na mwono ule wa mafarisayo waliojiongezea mapambio kwa kazi zao na kusahau ukweli kwamba siyo kazi katika kazi ndizo zinazotuhesabia haki, bali ni neema na kwanyo ni zawadi ya Kimungu kwetu. Kamwe hatuwezi jifananisha na vitu au idadi ya yale tuyatendayo, bali roho na upendo ule utusukumao kufanya mambo hayo hata kama ni madogo na macheche sana. Hivyo roho hiyo na upendo huo katika kutenda, na kwa kibali chake Mungu na kwa kadiri ilivyompendeza twahesabiwa haki. Na hii ndiyo maana ya maneno haya ya Yesu, kwamba, “Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk 17:10. Kuna furaha ya kweli tunapojibandua kutoka vitu na mali, na kutovifanya ndio mwisho wa kila kitu ingawa twavihitaji hapa na pale.

Kwa maana hiyo, wewe na mimi kama Wakristo tusipokuwa na Kristo Yesu katika maisha yetu tuna hasara kubwa sana. Na ukweli ni huu; bila Kristo Yesu huna njia, kweli, na uzima, Yoh 14:6. Na kama huna hivi, je, uzima wa milele unawezekana kwako? Tunapomwamini Kristo Yesu, Yeye hukaa kati yetu, naye huwa mwanga, kweli, na uzima wenyewe. Ni kweli hapa na pale tutakutana na magumu fulani katika ufuasi wetu kwake. Ila bila Kristo ni vigumu kuyabeba hayo na kuyashinda. Pamoja na udhaifu na uduni wa mwanadamu kama asemavyo Mhaburi, 103:14-15, mtu huyu mara zote na muda wowote anaitwa na Kristo Yesu.

Mtume Paulo licha ya kugundua kwamba Timotheo ameitwa na Kristo Yesu katika kuiishi na kuihubiri Injili, bado kuna mambo hayajakaa sawa. Katika kweli hii anamkumbusha Paulo anamkumbusha Timotheo na sisi pia, “kuichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi,” 2Tim 1:6-7. Nguvu na neema hii yapaswa kuonekana kwa Mkristo, na siyo kuwa goigoi.

Mtume Petro katika hili (kutokuwa na woga na hofu) anasema, “Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe,” 2Pet 1:10. Mkristo hana sababu ya kumwogopa mtu au kitu chochote kile, kwa sababu, “Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo,” 1Yoh 4:18. Jambo la ajabu leo baadhi yetu Wakristo na tuliopewa dhamana na Mama Kanisa tumekuwa goigoi hata kusimama tu katika kweli hofu imetupiga.

Je, Yesu anasema nini kuhusu kumwonea haya mbele za watu katika kweli na haki? Ni vyema tukayakumbuka vizuri maneno haya ya Yesu, Bwana, na Mwokozi wetu. Naye anasema, “Kila atakayenionea haya mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu,” Lk 9:26. Neno la Mungu ndilo litupalo nguvu na ujasiri. Na Imani na Upendo na nguvu ya Roho Mtakatifu ndivyo vinavyotuwezesha kuushika ujumbe na mafundisho ya Mungu. “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia,” Yoh 14:26.

Na Roho huyu Mtakatifu siyo roho mtakavitu, na mwenye kufanya kadiri ya matakwa yako au yangu. “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake,” Yoh 16:13. Huyu ndiye Roho Mtakatifu, na siyo roho mtakavitu. Siyo roho mtakavitu kwa sababu ya tabia yake kwamba; moja, ni kuongoza katika kweli yote. Pili, hunena kwa shauri lake mwenyewe. Tatu, huyasikia ayanenayo (kama upendo wa Mungu Baba na Mwana). Na mwisho, upasha habari yake kwetu.

Kijana Tumaini Ndewenga alitoka kijiji kilichoaminika sana kwa uchawi. Akiwa mwaka wa pili Chuo Kikuu Baba yake mzazi alifariki. Kifo cha Baba yake kilihusishwa na Mzee Change hapo kijijini. Mzee huyu akiisha kunywa pombe na kulewa huaza kujisifia kuwa yeye ndiye gwiji la uchawi hapa kijijini.

Akiwa kwenye msiba wa Baba yake, Mzee Change alisikika kilabuni akisema, “na hako katoto kake kasomi nakapa siku 7 nako katamfuata Baba yake huko aliko.” Maneno haya yalisambaa kwa haraka sana kijijini hapo kama moto wa petroli, kwa sababu wasifu wa Mzee Change hakuna asiyeujua. Habari hii ilipomfikia Tumaini alisema, “mwambieni Mzee Change yeye atakufa siku mbili kabla ya hizo saba alizonipa kuisha.”

Kijana Tumaini ambaye hakuwahi kuterereka hata siku moja kuhusu kile alicho amini juu ya uhai kuwa ni mali na zawadi ya Mungu, habari ile haikumshtusha hata kidogo. Hata hivyo Tumaini alitaka kutoa somo kwa wanakijiji wenzake. Somo lenyewe lilikuwa hivi; zikiwa zimebaki siku siku mbili ili neno la Mzee Change kutimia juu ya Tumaini, Mzee Change akiwa kilabuni anapata pombe muda wa saa moja usiku, Tumaini alimchukua jogoo na kumnyonyoa angali mzima na kwenda moja kwa moja nyumbani kwa Mzee Change na kumfunga Jogoo yule kwenye tendego la kitanda.”

Mzee Change kama kawaida yake alirudi nyumbani akiwa kesha lewa na kujilaza kitandani. Ilipofika majira ya saa kumi na moja alfajiri, jogoo yule alianza kuwika na sauti ilisikika ikitoka uvunguni mwa kitanda. Ghafla Mzee Change alishtuka na kutazama uvunguni. Mara alipomwona jogoo asiyekuwa na manyoya alifungasha kila kilicho chake na kukimbia kijiji kile akiamini kifuatacho ni kifo kama alivyosema Tumaini kabla ya siku mbili za mwisho alizotabiri Tumaini kufa yeye atakufa.

Ndugu yangu, simama katika imani ya kweli!

Tumsifu Yesu Kristo!

“Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu,” 2Tim 1:14

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tuongezee Imani, ili tuwaze mara zote na kutenda Matakatifu. Amina

miércoles, 28 de septiembre de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 26 YA MWAKA-C


JUMAMOSI WIKI YA 26 YA MWAKA-C

Somo: Ayu 42:1-3, 5-6, 12-16

Zab/Kit: 119:66, 71, 75, 91, 125, 130

Injili: Lk 10:17-24

Nukuu:

“Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika,” Ayu 42:2

 “Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; Bali sasa jicho langu linakuona,” Ayu 42:5

 “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru,” Lk 10:19

“Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni,” Lk 10:20

TAFAKARI: “Furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.”

Wapendwa wana wa Mungu, Wanafunzi wa Yesu wale sabini, wanarudi katika utume wao na kustajabia mambo makuu ya Mungu aliowatendea. Uhusiano wetu mzuri na Mungu ni chanzo kikubwa sana cha furaha yetu ya kweli. Lakini Yesu anawaambia wasiwe na furaha tu kwa sababu walimwona shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme, bali ndani yao Mungu aweza kufanya mambo makubwa zaidi ya hayo. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na n’nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru,” Lk 10:19. Huu ndio msingi wa furaha ya kweli kwa wale wote wenye hofu ya Mungu. Mahusiano mazuri na Mungu, hutujengea uwezo mkubwa sana wa kupambana na uovu.

Mara tuyaonapo haya makuu yakifanyika ndani mwetu tusibweteke. Dunia hii tunapoishi pamoja na uzuri wake na mambo yake, siyo mahali petu pa kudumu. Hapa ni mahali tu pa maandalizi ya umilele. Ni jukumu la kila mmoja wetu kupafanya hapa duniani kuwa sehemu nzuri zaidi ya kuishi huku tukijua siyo sehemu ya mwisho na ya umilele. Maandalizi mazuri ya hapa duniani ndiyo jibu la uhakika wa maisha hayo ya umilele. Hivyo furaha yetu kwa yote tutakayoyapata hapa duniani itupe taswira halisi ya maisha baada ya haya. Kuhusu ukweli huu Yesu anawaonya wanafunzi wake nasi pia kwa kusema, Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni,” Lk 10:20. Furaha yetu isiwe tu ya leo na kesho, bali furahi hii ipewe kibali na Mungu Baba wa Mbinguni. Tufurahi na Mungu milele mbinguni.

Wapendwa wana wa Mungu, ufahamu wa siri na ukweli huu,  Mungu anautoa kwa wanyenyekevu wake wa moyo. Wanyenyekevu wa moyo hufunuliwa siri za Mungu kwa sababu wapo tayari kusikia, kufanya, na kuishi kadiri ya mpango wa Mungu. Hivyo Yesu anamshukuru Mungu kwa niaba ya wanyenyekevu wote wa Moyo na kusema, “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza,” Lk 10:21b. Ni uchanga wetu kama watoto tupo tayari kujifunza, kusikiliza, kufanya, na kuishi kadiri ya matakwa ya Mungu.

Mara baada ya kuzama katika fumbo zima la maisha yake, na kugundua furaha na usalama wake upo kwa Mungu, na hasa pale alipojisalimisha kwake, Ayubu anayaona makusudi ya Mungu katika maisha yake. Naye anamwambia Mungu, “Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika,” Ayu 42:2. Mungu hujua mipango ya kila mmoja wetu kwa sababu kama Baba utuwazia yaliyo mema siku zote, Yer 29:11. Ayubu anaona udogo wake katika upendo huu wa Mungu ulio wa ajabu.

Ayubu kwa upande mwingine anatukumbusha kuweka lawama mbali mara tupatwapo na majanga katika maisha. Swali la kujiuliza katika hali hiyo ya sintofahamu ni hili; Je, Mungu anataka kunifundisha nini kwa hili lililonitokea? Naye Ayubu anaihoji nafsi yake na kusema, “ni nani huyu afichaye mashauri bila maarifa? Kwa maana, nimesema maneno nisiyoyafahamu, Mambo ya ajabu ya kunishinda mimi, nisiyoyajua,” Ayu 42:3. Mungu aliyeonekana kuwa mbali sana, na wa historia, sana anaonekana kuwa karibu na rafiki wa ajabu. Kwa kinywa chake Ayubu anakiri kweli hii na kusema, “nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; Bali sasa jicho langu linakuona,” Ayu 42:5. Kumbe furaha ya kweli ni kujenga urafiki wa karibu na Mungu.

Ukaribu na Mungu ukukumbusha udogo wako, na mapaswa yako katika kweli na haki. Ukaribu wako na Mungu ukuongezea hofu ya Mungu ndani yako, na hivyo kuwa mikono salama zaidi. Na ukaribu wako na Mungu ukunyenyekesha na kuwa tofauti katika, kuona, kuamua, na kutenda. Na ndivyo ilivyokuwa kwa Ayubu anapojitazama na kuchukua hatu. Ni kwa “sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu Katika mavumbi na majivu,” Ayu 42:6. Ukaribu wako na Mungu ukuongoza katika toba ya kweli na majuto. Unyenyekevu ule ukupelekeao kuona tofauti, kuamua tofauti, na kutenda tofauti, ni sawa na kuzaliwa upya na  katika nuru ya kweli, Mungu mwenyewe.

Kuzaliwa upya huku na kuwa katika nuru ya Mungu kunamrudishia hadhi yake Ayubu ikiwa ni pamoja na yale aliyoyapoteza hapo mwanzo, Ayu 42:13-15. Hakika mtu yule amtegemeaye Bwana hatopungukiwa na chochote. Mahangaiko na sintofahamu huwa za muda tu, na unapo simama imara kiimani katika hali na mazingira haya ya sintofahamu, Mungu ubaki kuwa mtetezi wako, mwaminifu kwako, na kukuongoza katika njia salama na kukubariki. “Basi hivyo Bwana akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng'ombe elfu, na punda wake elfu,” Ayu 42:12. Nani kama Mungu?

Ndugu yangu tulio safiri zote katika tafakari hii, furaha ya kweli siyo kwa haya tunayojibovusha nayo leo na sasa, bali pale tunapopewa kibali na Mungu na kutuheshabiwa haki. Ayubu anapata kibali mbele ya Mungu na kuhesabiwa haki kwani Mungu alipendezwa naye.  “Kisha baada ya mambo hayo Ayubu akaishi miaka mia na arobaini, naye akawaona wanawe, na wana wa wanawe, hata vizazi vinne,” Ayu 42:16. Mungu upendezwa na kila mmoja wetu tunapokuwa waaminifu katika Sura na Mfano wake, Mwa 1:27, kwa sababu ni kwa jinsi hiyo alikuumba, na kwa namna hiyo ataka uwe.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; Bali sasa jicho langu linakuona,” Ayu 42:5

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie furaha ya ndani kwako na ndani yako. Amina

martes, 27 de septiembre de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 26 YA MWAKA-C


IJUMAA WIKI YA 26 YA MWAKA-C

Somo: Ayu 38:1, 12-21, 40:3-5

Zab/Kit: 139:1-3, 7-8, 9-10, 13-14ab

Injili: Lk 10:13-16

Nukuu:

“Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza? Umeyajulisha mapambazuko mahali pake?” Ayu 38:12

 “Ndipo Ayubu akamjibu Mungu, na kusema, Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu,” Ayu 40:3-4

 “Ole wako Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu,” Lk 10:13

 “Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu,” Lk 10:15

“Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma,” Lk 10:16

TAFAKARI: “Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.”

Wapendwa wana wa Mungu, katika maisha yapo “mambo fulani” na hata wakati mwingine hutokea “mambo fulani,” ambayo kwayo kwa ufahamu wa ubinadamu wetu hukoswa na majibu. Huu “ufulani wa mambo” tusioujua katika maisha, huyafanya maisha hayo kuwa fumbo. Fumbo siyo tatizo na lingekuwa tatizo basi lingekuwa na jibu au suluhu yake. Fumbo halina suluhu zaidi ya kulizungumzia katika maana ya kulihusisha na kile tukifahamucho ili tuzame katika undani wa fumbo hilo. Lengo ni kupata mwanga katika fumbo hilo.

Ili kumfanya Ayubu azame ndani ya yale yaliyompata, Mungu kupitia upepo ule wa kisulisuli anamuuliza, “Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza? Umeyajulisha mapambazuko mahali pake?” Ayu 38:12. Msingi wa swali hili ni kumtaka Ayubu afahamu kuwa yapo mambo mengine ambayo kwayo kwa mazoea yetu twayaona ya kawaida, ila yamebeba fumbo zito kwa Yule anayeyaratibisha, yaani, Mungu mwenyewe.

Katika mwendelezo huo wa maswali ya kina, Ayu 38:13-20, yanamfanya Ayubu kufunguka na kuzama zaidi katika fumbo lile la maisha yake na yote yaliyompata. Yote tuyapatayo katika maisha yana kusudi la umilele kwa sababu tumeumbwa tuishi milele, na hili ndilo kusudi la Mungu kwako na kwangu. “Hukosi unajua, maana ulizaliwa wakati huo, Na hesabu ya siku zako ni kubwa!” Ayu 38:21. ‘Ukubwa wa hesabu za siku zako’ ni umilele wa maisha yako.

Baada ya kuzamishwa katika tafakari hii, na kupata mwanga wa fumbo la maisha yake, “ndipo Ayubu akamjibu Mungu, na kusema, Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu,” Ayu 40:3-4. ‘Mimi si kitu kabisa, naweka mkono wangu kinywani pangu,’ ni hali ya kujisalimisha kabisa bila kujibakiza kwa Mungu Mweza wa vyote. Kujisalimisha huku si kwa kijinga, bali ni kujisalimisha katika ‘ufahamu na umaana’-“rationality and significativity.” Akimaanisha ufahamu na umaana, Ayubu anasema, “nimenena mara moja, nami sitajibu; Naam, nimenena mara mbili, lakini sitaendelea zaidi,” Ayu 40:5. Hii ni hatua kubwa na ya ukomavu katika maisha ya kiroho.

Je, kuna uhusiano gani kati ya Imani na miujiza? Imani siyo miujiza! Ila miujiza usaidia imani changa kukua na kukomaa. Mkristo anayebaki katika hatua ya miujiza tu, huyo bado hajakomaa katika imani. Wapenda miujiza bila kukua katika imani, na wenye kuhama kutoka nyumba moja ya sala na kwenda nyumba nyingine ya sala, huku wakivutwa na ‘nani zaidi’, ni sawa na watoto wa ‘shule ya awali imani’ katika miaka yao yote. Na hili ndilo analolikemea Yesu katika Injili ya leo na kusema, “Ole wako Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu,” Lk 10:13. Miujiza ni mwito wa mabadiliko katika Imani kuelekea ukomavu, na siyo kigoto cha imani. “Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1

Watu waishio katika miji hiyo iliyotajwa na Yesu tungeweza kusema ni “watoto wazee,” katika imani. Na linganisho la ‘utoto uzee’ kiimani ni wakazi wa Tiro na Sidoni. Hawa wana hofu ya Mungu. Naye Yesu anasema, “Lakini, siku ya hukumu itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zake kuliko ninyi,” Lk 10:14. Wakazi wa  mji wa Kapernaumu ni sawa na mbegu zile zilizoanguka kwenye mwamba. Hawa ni “wale ambao wasikiapo hulipokea lile neno kwa furaha; nao hawana mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa hujitenga,” Lk 8:13. Katika hali hii kiimani, Yesu anasema, “Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu,” Lk 10:15. Kukuzwa hata mbinguni ni furaha kulipokea neno, ila wakati wa majaribu hukosa nguvu na kushuka hadi kuzimu.

Pamoja na hali na mazingira haya kiunjilishaji, Yesu anakuasa wewe na mimi tusivunjike moyo katika kuitangaza habari njema ya wokovu wetu. Hapa na pale tutahuzunishwa na hata kukatishwa tamaa, ila tusife moyo kwa sababu, “awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma,” Lk 10:16. Utume si lelemama. Utume ni kuvumilia ndani na katika Kristo Yesu.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu,” Ayu 40:3-4

Tusali:-Ee Yesu, tujalie Roho ya Kimisionari tukiazia pale tulipo. Amina

lunes, 26 de septiembre de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI; SIKUKUU YA MALAIKA WAKUU: MIKAELI, GARBIELI, NA RAFAELI


ALHAMISI WIKI YA 26 YA MWAKA-C

Sikukuu ya Malaika wakuu: Mikaeli, Gabrieli na Rafaeli

Somo: Dan 7:9-10, 13-14

Zab: 138:1-2ab, 2cde-3, 4-5

Injili: Yoh 1:47-51

Nukuu:

Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa,” Dan 7:14

Yesu akajibu, akamwambia, Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya,” Yoh 1:50

Akamwambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu,” Yoh 1:51

TAFAKARI: “Naye atayatenda yote kadiri ya mahitaji yetu. Tumwamini daima.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anasheherekea sikukuu ya Malaika wa Kuu; Mikaeli, Gabrieli, na Rafaeli. Hawa malaika wakuu wanatambulika hivyo kutokana na kazi zao na jumbe zao walizokuwa wakiziwakilisha kwa watu mbalimbali kutoka kwa Mungu. Tafsiri ya majina yao imebeba ujumbe na maana ya kile walicho. Malaika Mkuu Mikaeli, kutoka Kiebrania inamaanisha “Nani ni sawa na Mungu?” Ni malaika alikingaye Taifa la Mungu. Jina hili linamaanisha pia “zawadi kutoka kwa Mungu.” Kazi yake na namna alivyotumika tunaweza rejea sehemu hizi katika Maandika Matakatifu {Dan 10:21; 12:1, Kut 23:20, Yud 9, Ufu 7:12}.

Malaika Mkuu Gabrieli kwa Kiebrania inamaanisha “Bingwa au Mshindi wa Mungu.” Ni mpeleka ujumbe maalum kwa watu kutoka kwa Mungu. Tunaona Malaika huyu Mkuu akimsaidia Nabii Danieli kutafsiri ndoto {Dan 8:16; 9:21}. Gabrieli anapeleka pia ujumbe kwa Zakaria kuhusu kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji {Lk 1:19}. Tunaona vile vile Malaika huyu Gabrieli akimfikishia ujumbe Bikira Maria kuzaliwa kwa Mwokozi wetu Yesu Kristo {Lk 1:26}. Malaika Mkuu Rafaeli, kwa Kiebrania, “Aliyeponywa na Mungu. Vile vie ilimaanisha mlinzi wa geti la hekalu kwenye agano la kale.

Wapendwa wana wa Mungu, tunapotazama kazi za malaika hawa tunaona ni kwa namna gani Mungu amewatumia katika historia nzima wa wokovu wetu. Kanisa pasipo shaka leo linasheherekea kwa kutambua nafasi na kazi zao kwa wokovu wa Mwanadamu. Ni kweli kwamba malaika humzunguka Mungu pale alipo na kuwa tayari kufanya yale atakayo Mungu. Lakini leo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Padre ambaye ni Kristo mwingine, amepewa mamlaka na uwezo wa kumshusha Mungu kwa watu anaowahudumia kupitia Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Hivyo kwa kupitia Mwanaye Yesu Kristo, Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa,” Dan 7:14.

Ndugu zangu katika Kristo, tunapomwamini Kristo na kukaa katika njia, kweli na uzima wake, tunashirikishwa makubwa zaidi ambayo hatukuwahi kuyaona. Yesu anamwambia Nathanaeli ukweli huu, “Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya,” Yoh 1:50. Kristo akiwa ndiyo Jana yetu, Leo yetu, na Umilele wetu, anayafahamu yote kwa sababu kwa kupita yeye yote yalifanyika, Yoh 1:3. Kwa uwezo huu aliokuwanao Yesu, anawaambia wanafunzi wake na sisi pia kwamba, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu,” Yoh 1:51. Yatupasa kusadiki yote haya naye Mungu kupitia mwanaye Mpendwa Yesu Kristo atayatenda maishani mwetu kadiri ya mahitaji yetu.

Tumsifu Yesu Kristo!

Akamwambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu,” Yoh 1:51

Tusali:-Ee Yesu Mwema tujalie Imani thabiti. Amina

MALAIKA WAKUU WA MUNGU MTUOMBEE. AMINA

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 26 YA MWAKA-C


JUMATANO WIKI YA 26 YA MWAKA-C

Somo: Ayu 9:1-12, 14-16

Zab/Kit: 88:10bc-11, 12-13, 14-15

Injili: Lk 9:57-62

Nukuu:

 “Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake,” Lk 9:58

 “Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu,” Lk 9:62

“Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, Kweli najua kuwa ndivyo hivyo; Lakini mtu huwaje mwenye haki mbele za Mungu?” Ayu 9:1-2

 “Yeye ni mwenye hekima moyoni, na mwenye uwezo katika nguvu; Ni nani aliyejifanya kuwa mgumu juu yake, naye akafanikiwa?” Ayu 9:4

TAFAKARI: “Yeye ni mwenye hekima moyoni, na mwenye uwezo katika nguvu; Ni nani aliyejifanya kuwa mgumu juu yake, naye akafanikiwa?”

Wapendwa wana wa Mungu, kadiri ya Injili ya leo, Yesu anampa angalizo mtu yule aliyekutana naye njiani na kusema yupo tayari kufuatana naye ko kote atakapokwenda. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake,” Lk 9:58. Kwa maneno mengine Yesu anatuambia hakuna maslahi yo yote kibinadamu zaidi ya maisha ya umilele kutoka kwake. Kama ni swala la utajiri na kuwa na maisha mazuri siyo kipaumbele cha kwanza katika ufuasi wetu kwake. “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Mt 6:9. Kazi yetu ya kwanza ni kuutafuta ‘kwanza ufalme wa mbinguni’ na mengine yote tutapewa kwa ziada na kadiri ya mahitaji yetu.

Jambo la pili na la muhimu tunalofundishwa leo kuhusu Imani ya kweli na ufuasi usio na mawaa ni ‘utambuzi wa kweli na kujua nafasi ya Mungu katika maisha yako.’ Bila shaka wengi wetu tuna hofu ya kifo. Hata hivyo, kifo kipo pale pale upende au usipende. Na kama umezaliwa basi ipo siku utakufa. Kuzaliwa si lazima, bali kufa ni lazima kama umezaliwa. Kwa hiyo katika mantiki hii ya kifo na uhalisia wake, hatupaswi kukiogopa. Yatupasa kuishinda hofu ya kifo ili uwe tayari kukipokea kifo kama njia pekee ya maisha yale baada ya kifo hapa duniani, kuishi umilele. Hakutakuwa na maisha ya umilele baadaye bila kupita katika fumbo hili la kifo.

Hivyo Yesu anamtoa hofu ndugu yule aliyetoa hoja ya kwenda kwanza kumzika Baba yake ndipo amfuate. Naye Yesu anamwambia, “Waache wafu wawazike wafu wao; bali wewe enenda ukautangaze ufalme wa Mungu,” Lk 9:60. Je, Yesu anatukataza kuwazika wazazi wetu? La hasha! Kufanya hivyo angekuwa anaenda kinyumbe na ile amri ya nne ya Mungu, “waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako,” Kut 20:12. Yesu anachotaka kukuambia wewe na mimi leo ni kwamba, kifo ni ‘kweli isiyopingika na hivyo shughuli zake na mazingira ya yake, isiwe sababu ya kutokupokea ujumbe wake wa uzima wa milele.

Na jambo la tatu na la mwisho tunalofundishwa leo kuhusu Imani na ufuasi thabiti ni ‘kule kuwa na msimamo thabiti wa wito ulio nao na kutunza kile ulichoitiwa.’ Hii ni pamoja na kutokuwa ndumilakuwili au kigeugeu cha kutaka‘kutazama au kurudi nyuma ulikotoka kwa malengo ya kujaribu tena.’Bali lipaswalo ni kujenga uaminifu na utayari wa kutimiza kile ulichoitwa na kukubali bila shuruti kwa sifa na utukufu wake Mungu. Na hicho ulichoitwa na kukubali kwa hiari yako kiwe mwitikio chanya hasa pale linapojitokeza swala ya huduma kwa watu au umma.

Wengi wetu baada ya kubatizwa tumerudi kuishi maisha ya kipagani kabisa. Na wengi katika kundi hili wamekuwa washirikina wa kupindukia na kuongozwa na nguvu za giza ili hali wamejivika visakramenti mwili mzima. Ushirikina ‘ni kuamini nguvu fulani kutoka kitu fulani kisicho na uhusiano kimantiki.’ Katika hili Yesu anatupa angalizo, na kusema, “Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu,” Lk 9:62. Kwa maneno mengine ni heri kuwa baridi au joto, kuliko kuwa vuguvugu katika Imani.

Ayubu ni mfano mzuri na dhahiri wa kusimama katika imani thabiti. Siri kubwa aliyokuwa nayo Ayubu juu ya imani yake ni kutokushikamana na vitu na kujifananisha navyo. Ayubu alijisalimisha kabisa mikono mwa Mungu. Baada ya kuyatafakari maisha yake na uhusiano wake na Mungu, “ndipo Ayubu akajibu, na kusema, Kweli najua kuwa ndivyo hivyo; Lakini mtu huwaje mwenye haki mbele za Mungu?” Ayu 9:1-2. Mungu ndiye haki, na Yeye tu ndiye mwenye kutuhesabia haki. Hivyo mtu “kama akipenda kushindana naye, Hawezi kumjibu neno moja katika elfu,” Ayu 9:3. Katika hali na mazingira kama haya usalama wako upo pale tu utakapo jisalimisha mikononi mwake bila kujibakiza.

Ayubu kwa namna ya pekee pia anagundua kuwa Mungu ndiye kila kitu. Kwake hakuna linalomshinda, na vyote vipo kama vilivyo kwa nguvu zake, Ayu 9:5-12. Mungu huyu aliye hai na wapekee ndiye uiongoza mifumo yote hai (inayoonekana na isiyoonekana) kadiri apendavyo Yeye. Ni kweli pasipo shaka kwamba  “Yeye ni mwenye hekima moyoni, na mwenye uwezo katika nguvu,” Ayu 9:4a. Na vyote avifanyavyo Mungu vina lengo la umilele. Kushindana au kupingana na Mungu kwa ufahamu wako ni kushindwa kabla hata ya kuanza kutekeleza jambo hilo. Hivyo “ni nani aliyejifanya kuwa mgumu juu yake, naye akafanikiwa?” Ayu 9:4b. HAKUNA!

Tumsifu Yesu Kristo!

“Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu,” Lk 9:62

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie neema na nguvu na kupita katika majaribu ya Imani. Amina

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 26 YA MWAKA-C


JUMANNE WIKI YA 26 YA MWAKA-C

Somo: Ayu 3:1-3, 11-17, 20-23

Zab/Kit: 88:2-3, 4-5, 6, 7-8

Injili: Lk 9:51-56

Nukuu:

“Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu,” Lk 9:53

“Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?” Lk 9:54

“Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.]” Lk 9:55

“Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa,” Lk 9:56a

“Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake,” Ayu 3:1

TAFAKARI: “Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.”

Wapendwa wana wa Mungu, sehemu hii ya Injili n asomo letu la leo juu ya habari ile ya Ayubu, inafua ‘kweli ya Mungu’ ambayo hubaki kuwa ‘siri’ katika maisha yetu ya kila siku. Ni kweli kabisa katika hali na mazingira ambayo twateseka tu bila sababu ya teso hilo, maisha upoteza maana yake. Hii ndiyo hali aliyokuwa nayo Ayubu baada ya kupatwa na janga lile la majaribu na kuanza kulaani, Ayu 3:1. Kulaani kwa kile usichokijua vizuri hakutakufanya kuelewa fumbo la kile usichokijua vizuri. Kuzama katika fumbo usilolielewa ili upate maana yake ni kujiuliza swali hili; Je, katika jambo hili, Mungu wataka kunifundisha nini? Hakuna jaribu lisilo kuwa na mlango wa kutokea, 1Kor 10:13. Kuupata mlango wa kutokea ni kuachana na laana na laumu.

Yesu Kristo aliye Mungu na Mwanadamu anaelekea Yerusalemu kwa kile kinachosimuliwa na Mwinjili Luka kama “siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia.” Je, kupaa bila kupitia mateso, kifo, na ufufuko? Mwinjili Luka halisemi jambo hili kwa kukosea. La! Hasha. Kupaa kwa Yesu ni hitimisho linalo elezea Wokovu ikiwa ndiyo lengo lengwa katika historia nzima ya mwanadamu (Yoh 1:14, Gal 4:4-5). Wokovu huo unathibishwa kwa Ufufuko wake Kristo Yesu. Ufukuko huo ni alama ya wazi ya ushinda dhidi ya kifo kilichokuwa adui yetu mkubwa. Na Kifo hicho cha Kristo Yesu ni alama wazi ya upendo wa Mungu kwetu sisi wanadamu kutuweka huru kutoka utumwa wa dhambi. Kwa maana nyingine, kupaa kwa Kristo kusingekuwa na maana kama kusingesema chochote kuhusu wokovu, ufufuko, na kifo. Na kuelekea Yerusalema katika maana ya “kukaza uso wake kwenda Yerusalemu,” kulimaanisha, mateso, kifo, wokovu, ufufuko, na kupaa.

Hata pamoja na mpango huu mahususi uliobeba kilele cha historia mzima ya wokovu wa mwanadamu, jambo hili kwa ajabu kubwa na mshangao halimgusi mwanadamu. Hii ndiyo kweli ya Mungu inayobaki kuwa siri katika maisha ya mwanadamu. Na hii ndiyo maana ya maneno haya; “Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu,” Lk 9:53. Mwenye kufikiriwa kuhusu kesho na hatma yake itakuaje hana habari kabisa na kile anachofanyiwa.

Kwa bahati nzuri au mbaya siri hii haikufichwa kabisa kwa baadhi ya wateule wa Mungu.  Mwanga wa siri hii unafunuliwa kwa wanafunzi wake Yesu, kama asemavyo mwenyewe kwamba, “Ninyi mmepewa kuzijua siri za ufalme wa Mungu; bali wengine kwa mifano, ili wakiona wasione, na wakisikia wasielewe,” Lk 8:10. Kufunuliwa kwa siri hii kuna kuwa bahati mbaya kwa namna wanafunzi wake Yesu wanavyotafuta suluhu ya mambo hasa katika safari hii ya kuelekea Yerusalemu alipoyakazia macho yake Yesu. Na mambo yalikuwa hivi; “Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?” Lk 9:54. Yesu hakuja kufanya mwendelezo wa sheria ile ya jino kwa jino, bali kuitakatifuza na kuifanya kamili, Mt 5:17. Na lengo na uwepo wake Yesu siyo kuukumu ulimwengu bali ulimwengu  uukolewe na yeye, Yoh 3:17.

Ni wazi kabisa kwa kile walichoshupalia wanafunzi wake Yesu, Yakobo na Yohana cha onyesha kile kilicho ndani ya mioyo yao na ubinadamu wao. Na hapa ndipo Yesu “Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.]” Lk 9:55. Yesu anawakanya wao na sisi leo kama Wakristo na Wafuasi wake kwamba mtindo wa jino kwa jino siyo staha na maadili yetu kama Wakristo. Kufanya hivyo ni kutokujua fumbo zima la wokovu wetu. Ukweli ni kwamba, “Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa,” Lk 9:56a.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa,” Lk 9:56a

Tusali:-Ee Yesu, tuondolee ile roho ya kukata tamaa na kuwa watu wa visasi. Amina