jueves, 30 de junio de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 13 YA MWAKA-C

JUMAMOSI WIKI YA 13 YA MWAKA-C
Somo: Amo 9:11-15
Zab: 85:9, 11-12
Injili: Mt 9:14-17
Nukuu:
Siku hiyo nitaiinua tena maskani ya Daudi iliyoanguka, na kuziba mahali palipobomoka; nami nitayainua magofu yake, na kuyajenga kama siku za kale; wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu, na mataifa yote yaitwayo kwa jina langu, asema Bwana, afanyaye hayo,” Amo 9:11-12

Angalieni, siku zinakuja, asema Bwana, ambazo huyo alimaye atamfikilia avunaye, na yeye akanyagaye zabibu atamfikilia apandaye mbegu; nayo milima itadondoza divai tamu, na vilima vyote vitayeyuka,” Amo 9:13 

 “Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga,” Mt 9:15

Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi,” Mt 9:16

Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika, na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote,” Mt 9:17

TAFAKARI: “Katika Kristo na ndani ya Kristo, yote yatafanywa upya. Tusife moyo huyu ni Mungu pamoja nasi, Imanueli, Mt 1:23.”

Wapendwa wana wa Mungu, ‘unabii licha ya kubeba ujumbe wa Mungu katika misingi ya kufundisha, kuonya na kutoa angalizo, sehemu kubwa ya ujumbe huu wa Mungu hubeba tumaini jipya la kule tunapokutamani ambapo ndipo kusudi zima la Mungu katika ukamilifu wake. Na wito wetu kila siku kama Yesu anavyotuamuri ni kwamba,  ‘tuwe wakamilifu, kama Baba yetu wa mbinguni alivyo mkamilifu,’ Mt 5:48. Kuwa mkamilifu kama Mungu alivyo ni kuwa Mtakatifu. Bila utakatifu huwezi kuwa katika himaya ya Mungu. Kuwa mwenyeji wa Mbinguni lazima uwe mtakatifu. Na hivi ndivyo asemavyo Mtume Paulo kwamba, “tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu,” Efe 2:19. Maneno haya ya Mtume Paulo yanatufikirisha uwepo wetu hapa duniani. Hapa tulipo, yaani, duniani, siyo makazi yetu ya kudumu. Tupo hapa kwa kujiandaa tu kwa uzima wa milele. “Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake,” Flp 3:19-20

Hili ndilo tumaini la Mungu na la kinabii kwa wale aliowaridhia kuupitisha ujumbe wake, yaani, manabii. Nabii Amosi anafikisha ujumbe huu wa Mungu wenye matumaini ambao ni uthibitisho wa Mungu aliye hai na mwenye kuiona historia ya watu, na mwenye kutembea nao katika historia hiyo yenye kila aina ya dhoruba. Dhoruba na misukosuko aipatayo mwanadamu katika historia yake na kuyakabili katika matumaini huwa ndiyo ponya yake ya mwili na roho. Na huu ndio ujembe wa kinabii na matumaini kwa wana wa Israeli baada ya mateso waliyoyapata ndani ya utawala wao, na nje ya utawala wao. Na Siku hiyo nitaiinua tena maskani ya Daudi iliyoanguka, na kuziba mahali palipobomoka; nami nitayainua magofu yake, na kuyajenga kama siku za kale; wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu, na mataifa yote yaitwayo kwa jina langu, asema Bwana, afanyaye hayo,” Amo 9:11-12. Mungu hachoki kufanya nasi agano pale tunapomrudia katika kweli na haki.

Hata pamoja na kufanya agano hilo la kweli na haki kama alama ya kujirudi na kufuata njia iliyo salama, Mungu haachi kutupa angalizo ilihali akijua fika hali zetu na ubinadamu wetu, yaani, ‘maanguko yetu.’ Naye mjumbe wa Mungu, Nabii Amosi, anasema, Angalieni, siku zinakuja, asema Bwana, ambazo huyo alimaye atamfikilia avunaye, na yeye akanyagaye zabibu atamfikilia apandaye mbegu; nayo milima itadondoza divai tamu, na vilima vyote vitayeyuka,” Amo 9:13. Neema na baraka tuzipatazo katika maisha si kitu cha kubeza, bali ni kitu cha kuthamini na kulindwa katika maana ya kukipigania kisipotee. Hata hivyo, ni vyema tuelewe tunda la amani ni haki hasa pale tunapoishi zaidi ya mtu mmoja. Na haki ni tunda la wajibu. Haki na amani huwepo pale kila mmoja anapotimiza wajibu wake kadiri ya nafasi na wito wake.

Mungu hatochoka kutuletea na kutukirimia yanayofaa kadiri ya mahitaji yetu pale tunapodumisha amani ambayo ni tunda la haki, na haki ikiwa ni tunda la wajibu. Na hivi ndivyo alivyowahaidia wana wa Israeli na kusema, Nami nitawarejeza tena watu wangu Israeli waliohamishwa, nao wataijenga miji iliyoachwa maganjo, na kukaa ndani yake; nao watapanda mizabibu katika mashamba, na kunywa divai yake; nao watafanyiza bustani, na kula matunda yake,” Amo 9:14. Ndugu yangu, ni ndoto ya mchana kweupe kutabiri kuijenga nchi ya maziwa na asali kwa kukanyaga haki za watu ambao kwa njia moja au nyingine wana wajibika kwa taifa lao kadiri ya wito na nafasi zao. Huwezi kuwa na amani kama hakuna haki. Na pasipo haki na amani hapana maendeleo. Na maendeleo yasiyotokana na utashi wa watu hukosa thamani mbele zao hata kama machoni mwako yatakuwa ya gharama kubwa. Na mwisho wa siku maendeleo hayo hufifia kama moshi wa mabua kwa sababu hayakugusa maisha ya watu na hayana maana kwao. Lolote lile lenye kugusa utashi wa watu ndilo lijengalo na kukuza maisha ya watu kwa sababu ni zao la kile walicho.

Pamoja na uwezo wako kama kiongozi wa kuona mbele kule wasipokuona sawa sawa wale unaowaongoza, jaribu mara zote kutembea nao na kuwaonyesha kule unapopaona. La siyo utafika kule utakapo ilihali wao bado hata hawajajianda kwa safari hiyo uliyokwisha imaliza. Unapotembea hatua kwa hatua na wale unaowaongoza Mungu anakuhakikishia hili kama kiongozi,  Nami nitawapanda katika nchi yao, wala hawatang'olewa tena watoke katika nchi yao niliyowapa, asema Bwana, Mungu wako,” Amo 9:15. Na hivi ndivyo uzalendo unavyojengwa. Uzalendo wa watu kamwe haujengwi kwa shuruti za kiimla, bali uhuru na utashi uliokomaa wenye kuthamini siyo tu kwamba hiki ni changu bali ni chetu na kina thamani kwa wote na umma. Zaidi ya hapo ni mbwembwe tu. Na mwisho wa mbwembe ni pale sherehe inapofikia kikomo chake. Je, maisha si zaidi ya sherehe? Tunahitaji tafakuri ya kina. Na ndiyo maana katika maisha tunahitaji nyakati za mafungo, yaani, kuyapitia yale tuliyokwisha yaishi (uzuri na ubaya wake), kuona pale tulipokosea, na kuanza upya kwa nguvu ili kutokurudia makosa na kufika pale tunapopatamani, yaani, ukamilifu ambao ndio maisha ya umilele na kusudi la kumbwa kwetu.

Hivyo wapendwa wana wa Mungu, kadiri ya Injili ya leo, kufunga ilikuwa moja ya mambo makuu matatu kadiri ya Imani, mila na desturi za kiyahudu. Kufunga iliendana na kusali, pamoja na kutoa sadaka. Haya mambo matatu yalikuwa ya msingi sana. Kitendo cha wanafunzi wa Yesu kuonekana kutokufunga kiliwashangaza na kuwakwaza wengi, na hasa wanafunzi wa Yohane Mbatizaji. Yesu anapoulizwa swali hili: kwa nini wanafunzi wako hawafungi, anajibu na kusema, “Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga,” Mt 9:15. Uhusiano wetu na Kristo una sura mbili; kuna wakati wa furaha na wakati wa huzuni, itupelekayo kwenye utukufu. Tukiwa na Yesu tu wana wa Bwana harusi na yatupasa kufurahi naye kuliko haki.

Kwa upande wa pili wa uhusianao wetu na Yesu unatukumbusha upo wakati wa kutoa ushuhuda wa kweli juu ya kile tunachoamini kuhusu Yesu. Huu ndio wakati wa kuteseka na hata kufa kwa ajili ya Kristo. Huu ndio wakati wa kufanya toba ya kweli kwa ajili ya maaondoleo ya dhambi zetu. Huu ndiyo wakati wa kufanywa upya ndani na katika Kristo. Na huu ndio wakati wa kutakaswa na kubeba bendera ya ushindi ya mwanakondoo.

Nyakati hizi mbili za mahusiano yetu na Kristo ndizo zitupazo kiini cha imani yatu. Sisi si Wakristo wa Jumapili tu, yaani, pasaka, bali tu wafuasi wa Kristo siku zote na hasa siku ile ya Ijumaa, yaani mateso na kufa kifo dini. Tunakufa kifo dini kwa kuIfia kweli siku zote za maisha yetu. Yatupasa kusimama katika kweli, kufundisha iliyo kweli, kuishi yaliyo kweli, na kushuhudia lililo kweli, hata kama litagharimu uhai wetu. Haya ndiyo maisha ya ufuasi wa Kristo ambao tuliowengi hatutaki kusikia.

Jambo lingine la muhimu kujua ni hili: Yatupasa kuelewa lile lililo la zamani ambalo kwa sasa linakamilishwa na hili jipya, mbalo tangia awali lilikuwa limejificha ndani ya lile la zamani. Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi,” Mt 9:16. Maana yake nini? Ndugu yangu, katika safari ya ukombozi wa mwanadamu, katika hatua ya mwanzo ya safari hiyo, imebebwa katika agano la mwanzo. Agano hili kama lilivyo laelezea historia ya mwanadamu hatua kwa hatua. Kwa lenyewe agano hili kama lilivyo lina maana ila limekosa ukamilisho au hitimisho. Ukamilisho wa Agano la kwanza ni Upya wa Agano jipya, ikiwa ni ufunuo wa wazi wa Mungu kwa tukio la neno kufanyika mwili. Agano hili jipya licha ya kwamba ni ukamilisho wa agano la kale, tangu mwanzo lilikuwa limejificha ndani ya agano la kale. Hivyo Yesu anatutaka kulijua jambo hilo na pia kutenganisha maagano haya mawili katika “ufahamu wake,”  “umaana wake” na “nafasi zake.” Na hii ndiyo maana ya maneno haya, Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika, na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote,” Mt 9:17. Hivyo katika jambo hili twapaswa kumfuata Kristo katika ukamilifu wote na kuachana na michanganyo. Ni heri kuwa baridi au joto, kuliko kuwa vuguvugu katika Imani. Hili vuguvugu kiimani ndilo litakalo pasua hekalu hili la Roho Mtakatifu.

Tumsifu Yesu Kristo!

Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi,” Mt 9:16


Tusali:-Ee Yesu na Mungu wetu, tupo tayari kuanza yote pamoja nawe. Amina

miércoles, 29 de junio de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 13 YA MWAKA-C

IJUMAA WIKI YA 13 YA MWAKA-C
Somo: Amo 8:4-6, 9-12
Zab: 119:2, 10, 20, 30, 40, 131
Injili: Mt 9:9-13
Nukuu:
 “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana,” Amo 8:11 

Nao watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione,” Amo 8:12

 “Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi,” Mt 9:12

Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi,” Mt 9:13

TAFAKARI:Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

Wapendwa wana wa Mungu, maneno haya ya Bwana wetu Yesu Kristo, “Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi,” kwetu ni mwito wa toba na wongofu. Ni maneno yaliyojaa neema na huruma ya Mungu. Ni maneno yenye uzima na yenye kutoa fursa kwa kila mmoja wetu kuziacha njia zake mbaya na ovu, na kumrudia Mungu. Ni maneno yasiyobeba hukumu kwa yeyote yule mwenye kuiona na kuitafakari huruma na neema ya Mungu. Na kwa maneno hayo ya Yesu, kila mmoja wetu ana nafasi ya pekee mbele ya uso wa Mungu licha ya mapungufu na udhaifu wake.

Huu ndio ujumbe wa Mungu anaoutoa Nabii Amosi kwa  matajiri na mwenye mamlaka waliokuwa sababu ya dhuluma kwa masikini. Ujumbe huu unawataka waziache njia zao mbaya na kumrudia Mungu. Naye anasema: Lisikieni hili, ninyi mnaopenda kuwameza wahitaji, na kuwakomesha maskini wa nchi, mkisema, Mwezi mpya utaondoka lini, tupate kuuza nafaka? Na sabato nayo, tupate kuandika ngano? Mkiipunguza efa na kuiongeza shekeli, mkidanganya watu kwa mizani ya udanganyifu; tupate kuwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu; na kuziuza takataka za ngano,” Amo 8:4-6. Leo Nabii Amosi angalikuwa katika jamii yetu angeongelea ugumu wa maisha uliosababishwa na unaosababishwa na watu wachache waliolifisidi taifa letu na wanaoendelea kulifisidi. Hawa ndio wale wajulikanao kwa ‘umaarufu wao’ kama ‘mafisadi.’ Wito ni kuonja moyoni na kughairi uovu kwa sababu waovu na uovu ni chukizo mbele ya uso wa Mungu. “Laana ya Bwana i katika nyumba ya waovu, Bali huibariki maskani ya mwenye haki,” Mit 3:33

Lolote lile lililo ovu halina umilele ndani yake. Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu (Yesu Krito), sadaka hii ya Mwana wa Mungu pale Msalabani, na ufufuko wake, ndicho kikomo cha uovu wote. Hii ndiyo njia aliyoichangu Mungu kuushinda uovu. Na tunaushinda uovu tukiwa ndani na katika Kristo Yesu. Na hivi ndivyo alivyotabiri Nabii Amosi kwamba, Tena itakuwa siku hiyo, asema Bwana MUNGU, nitalifanya jua litue wakati wa adhuhuri, nami nitaitia nchi giza wakati wa nuru ya mchana,” Amo 8:9. Tendo hili ndilo fumbo zima la kifo kile cha aibu pale Msalabani ambacho kwayo ‘wokovu wetu ulitundikwa.’ Hakuna uhai kwa yeyote yule mwenye kufurahia mateso ya wengine kwa namna yoyote ile, au mwenye kusukumwa na ghariba ya uovu. Kumbe njia salama ni kuukumbatia Msalaba Mtakatifu wa Bwana wetu Yesu Kristo ambao ni ishara hai ya huruma na neema ya Mungu. Naye Mtume Paulo anasema, Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14. Pamoja na Utukufu uliopo katika Msalaba Mtakatifu, Msalaba utuvuta kwenye neema na huruma ya Mungu.

Mvuto huu leo wa Msalaba wenye kutupeleka kwenye neema na huruma ya Mungu, Nabii Amosi anauzungumzia kwa nyakati zile ambazo zilikuwa bado kufunuliwa kwao kwa maneno haya;  Nami nitazigeuza sikukuu zenu kuwa maombolezo, na nyimbo zenu zote kuwa vilio; nami nitatia nguo za magunia katika viuno vyote, na upaa katika kila kichwa; nami nitayafanya haya kuwa kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, na mwisho wake kama siku ya uchungu,” Amo 8:10. Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, mwana huyu wa pekee anayezungumziwa hapa si mwingine bali ‘Neno aliyefanyika mwili na kukaa kwetu,’ Yoh 1:14. Kwake neno huyu kuna huruma, uelewa, na kujituma. Tufanyapo toba ya kweli na majuto kwake (Yesu Kristo) kuna huruma ya kweli. Kristo Yesu ni mwelewa na anaelewa hali yetu na ubinadamu wetu. Yesu kwa kumwilishwa kwake na kuchukua umbo la mwanadamu, aliishi kama sisi ila “Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake,” 1Pet 2:22. Na mwisho, Kristo Yesu alijituma bila kujibakiza. Uthibitisho huu wa kujituma kwake kwa sababu yako na mimi ni kuutoa uhai wake pale msalabani. Huu ni upendo wa hali ya juu. Hakika, “hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Na hivi ndivyo tunavyotakiwa kupendana. Kujitoa kwa kutotanguliza kupokea. Ni kwa namna hii ya kupendana tunakuwa rafiki ya Yesu, Yoh 15:14.

Upendo huu wa ajabu na urafiki huu wa Yesu pale tunapopendana kwa dhati ndiyo ile kiu na njaa kwa ujumbe ule wa Mungu kupita Nabii wake Amosi. Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana,” Amo 8:11. Neno la Bwana ni uzima kama anavyothibitisha Yesu mwenyewe. “Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote,” Yoh 15:3-5. Ndugu yangu, bila Kristo Yesu hutoweza kufanya lolote lile, ‘liwe dogo au kubwa!’ Na hivi ndivyo Mungu alivyoufunua ukweli huu wa  ‘maisha bila NENO-Yesu Kristo,’ kupitia Nabii wake Amosi; Nao watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione,” Amo 8:12. Ndugu yangu, ‘Kristo Yesu ndiye Njia, Kweli, na Uzima,’ Yoh 14:6. 

Wapendwa wana wa Taifa ya Mungu, kwa mantiki hiyo, kila mmoja wetu kadiri ya wito na hali yake, anapoishi hapa duniani yampasa kujua sababu ya kuumbwa kwake. Tunapojua sababu ya kuumbwa kwetu ni kwa namna hiyo twafahamu kuwa maisha ya kila mmoja wetu ni wito maalumu. Maisha kama wito, yanatudai kujitoa sadaka kwa kile tulichochagua kuishi kwa kuwezeshwa na Mungu mwenyewe. Leo katika Injili tunaona namna Mathayo alivyoitwa na Yesu na mara kuacha mpangilia wa maisha yake ya zamani. Kuujua wito wako ni kuanza mpangilia mpya wa maisha yako. Na ndivyo ilivyokuwa,Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata,” Mt 9:9. Ukweli ni kwamba tendo hili la kumfuata Yesu katika mazingira aliyokuwa nayo Mathayo, linamlazimu muhusika kujimamanua kutoka yale aliyojifungamanisha nayo. Mathayo anaamua kuiacha kazi yake ya ukarani na kumfuata Yesu ambaye hana chochote katika maisha linganishi (mali na utajiri) ingawa vyote ni vyake, Zab 24:1, ila uzima wa milele. Yesu anasema, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake,” Lk 9:58. Kumfuata Yesu kwa ukaribu na uthabiti, kunatualika kuitafakari changamoto hii.

Kitendo cha Yesu kumchagua Mathayo kuwa mmoja wa Mitume wake na kula pamoja na wenye dhambi kinawakasirisha sana Mafarisayo. Yesu anawajibu Mafarisayo kwa kulenga sababu ya uwepo wake hapa duniani: Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi,” Mt 9:12. Yesu amekuja kwa sababu ya wale wenye uhitaji wa mwili na roho. Yesu amekuja kwa ajili ya wadhambi na wale wote wenye moyo wa hofu ya Mungu. Hili ndilo fumbo tunalotakiwa kulitafakari kila siku. Pili, kama nilivyokwisha kusema hapa mwanzo wa tafakari hii, ‘ni Mungu peke yake wenye kutuhesabia haki.’ Hivyo, Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi,” Mt 9:13. Ndugu yangu, embu ona Yesu anavyokupenda kupita upeo. Kuuthaminisha upendo huu ni kuishi kadiri ya mpango wa Mungu na yale yote Mwanaye Mpendwa aliyotufundisha.

Tumsifu Yesu Kristo!

Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi,” Mt 9:12


Tusali:-Ee Yesu ninakuhitaji daima. Amina

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 13 YA MWAKA-C

ALHAMISI WIKI YA 13 YA MWAKA-C
Somo: Amo 7:10-17
Zab: 19:8, 9, 10, 11
Injili: Mt 9:1-8
Nukuu:
Ndipo Amazia, kuhani wa Betheli, akapeleka habari kwa Yeroboamu, mfalme wa Israeli, akisema, Amosi amefanya fitina juu yako kati ya nyumba ya Israeli; nchi haiwezi kustahimili maneno yake yote,” Amo 7:10 

Kwa maana Amosi asema hivi, Yeroboamu atakufa kwa upanga, na bila shaka Israeli atachukuliwa mbali, hali ya kufungwa, atoke katika nchi yake,” Amo 7:11 

 “Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako,” Mt 9:2

Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule mwenye kupooza) Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako,” Mt 9:6

TAFAKARI:Na kazi ya haki itakuwa amani; na mazao ya haki yatakuwa ni utulivu na matumaini daima,” Isa 32:17 

Wapendwa wana wa Mungu, pasipo haki hapana amani, utulivu, na matumaini. Hata hivyo haki uendana na wajibu. Aliyetimiza wajibu wake anastahili haki yake kwa namna yoyote ile. Mfano: ni wajibu wangu kuwa raia mwema ikiwa ni pamoja na kulipa kodi kadiri ya utaratibu uliowekwa kisheri na kikatiba inayoakisi matakwa ya raia wenyewe. Kama hili limefanyika, basi nastahili kupata haki zangu kwa mujibu wa Katiba ambayo ndiyo dira na sheria mama. Na sheria hiyo Mama au Katiba, ndipo watu huamua namna wanavyotaka waongozwe, kuwajibika, na kuwajibishwa pale inapokuwa ndivyo sivyo. Fujo na machafuko utokea pale ambapo haki haitolewi licha ya wajibu kutimizwa.

Ila Mungu wetu aliye Amani anatutaka tuwe na amani na hili ndilo fumbo la uumbaji wetu, ‘kwa sura na mfano wake,’ Mwa 1:27. Penye fujo na machafuko Utukufu wa Mungu hufifishwa tu ila hatuwezi kuuondoa au kuutokomeza. Naye Mungu asema hivi, watu wangu watakaa katika kao la amani; na katika maskani zilizo salama, na katika mahali pa kupumzikia penye utulivu,” Isa 32:18. Haki, utulivu, na amani havitolewi na mtu kutoka mfukoni mwake. Ni wajibu wa kila mtu/raia pale alipo kuhakikisha vinakuwepo. Wote waliopewa dhamana na umma yawapasa kusimamia hilo pasipo upendeleo na kwa mujibu wa Katiba husika, na siyo dhania binafsi kwa malengo binafsi au kikundi fulani cha waliojihalalishia haki hiyo. “Wabaya wanafanana na bahari iliyochafuka; maana haiwezi kutulia, na maji yake hutoa tope na takataka. Hapana amani kwa wabaya; asema Mungu wangu,” Isa 57:20-21

Chini ya utawala wa Mfalme Yeroboamu haki za watu zilikanyagwa. Mfalme hakupaswa kuguswa wala kukosolewa. Ilikuwa ni kosa kufanya hivyo. Kuhani Amazia alikuwa mtetezi na mtu wa karibu wa Mfalme Yeroboamu. Watu wote waliotaka kumkosoa mfalme walizimwa midomo au kuamuriwa kuikimbia nchi na kuishi uhamishoni. Ni katika mazingira haya Nabii Amosi anapata misukosuko kutoka kwa kuhani wa Betheli juu ya kumkosoa mfalme na kuonya tabia yake ya ukandamizaji. Ili kumnyamazisha Nabii Amosi, Amazia, kuhani wa Betheli, akapeleka habari kwa Yeroboamu, mfalme wa Israeli, akisema, Amosi amefanya fitina juu yako kati ya nyumba ya Israeli; nchi haiwezi kustahimili maneno yake yote,” Amo 7:10. Yaani, kwa maneno mengine, Amosi anashitakiwa kwa kosa la uchochezi. Ndugu yangu hapa ndipo tunapotakiwa kujua maana ya sauti ya kinabii.

Sauti ya kinabii ni sauti ya Mungu iliyojaa maono. Mungu uwafunulia watu wake na hasa wenye utulivu wa ndani, wenye uwezo wa kuliona jambo au hali kama lilivyo au ilivyo, na siyo kama walivyo. Ni msukumo wa ndani uliojaa hofu ya Mungu na kwa watu wa Mungu. Ni maono yaliyobeba kweli, haki, upendo, na amani. Nabii na unabii si kitu cha mkurupuko kama ilivyo ‘bendera fuata upepo.’ Na siyo utabiri kama ilivyo kwa wapiga ramli wenye kulenga hisia binafsi au za watu, bali ni kweli katika kweli, na haki katika haki.

Wapendwa wana wa Mungu, mwenye sauti hiyo ya unabii ni mwiba wa hatari palipojaa dhuluma na giza la uonevu. Watu wa mtindo huu kama alivyo Amosi Nabii, hawakoswi kusingiziwa yasiyo kweli na hata kuhalalishiwa makosa yasiyo kweli. Lengo ni kuwafunga midomo na kuwaangamiza. Mungu anaujumbe huu kwa wote wasimamao katika kweli na haki: Nyakati zao zitakuwa nyakati za kukaa imara; za wokovu tele na hekima na maarifa; kumcha Bwana ni hazina yake ya akiba. Angalia, mashujaa wao wanalia nje, wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu.” Isa 33:6-7. Ni kwa namna hiyo Nabii Amosi anashitakiwa kwa Mfalme na kuhani Amazia, na kusema, Yeroboamu atakufa kwa upanga, na bila shaka Israeli atachukuliwa mbali, hali ya kufungwa, atoke katika nchi yake,” Amo 7:11. Na kama haikutosha,  Amazia akamwambia Amosi, Ewe mwonaji, nenda zako, ikimbilie nchi ya Yuda, ukale mkate huko, ukatabiri huko; lakini usitabiri tena huku Betheli; kwa maana ni mahali patakatifu pa mfalme, nayo ni nyumba ya kifalme,” Amo 7:12-13.

Amazia kuhani anamvika umungu Mfalme Yeroboamu. Jambo hili ni hatari sana machoni mwa Mungu. Mungu ndiye mwenye mastahili ya kuabudiwa na kuogopwa, Zab 15:11; 111:9, na siyo mwanadamu mwenye nyama na mifupa, na kifo kikiwa ndiyo rafiki yake wa karibu kama kilivyo kivuli chake kisichosema chochote bali ufuatana nacho daima. Pamoja na vitisho hivyo vya kuhani Amazia, havikuweza kuufunga mdomo wa Nabii Amosi. Ndipo Amosi akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu; naye Bwana akanitwaa, katika kufuatana na kundi; Bwana akaniambia, Enenda uwatabirie watu wangu Israeli,” Amo 7:14-15. Nabii Amosi anajua wazi kabisa hayafanyi hayo kwa malengo yake binafsi, bali anawakilisha ujumbe wa Mungu kwa watu wake. Hivyo Amosi asiti kuzitema cheche za moto wa kweli na haki kutoka kwa Mungu. Naye alikuwa na ujumbe huu wa Mungu kwa Amazia kuhani, Basi, sasa lisikie neno la Bwana; Wewe unasema, Usitabiri juu ya Israeli, wala usitoe neno lako juu ya nyumba ya Isaka; kwa hiyo, Bwana asema hivi, Mke wako atakuwa kahaba mjini, na wana wako na binti zako wataanguka kwa upanga, na shamba lako litagawanywa kwa kamba; na wewe mwenyewe utakufa katika nchi iliyo najisi; na bila shaka Israeli atachukuliwa mbali hali ya kufungwa kutoka nchi yake,” Amo 7:16-17. Hayo ndiyo yaliyomkuta Amazia kuhani kwa tendo lake la kutetea uovu na udhalimu.

Ndugu yangu, Mungu hachezewi wala hajaribiwi. Yatupasa mimi na wewe kuchunguza mienendo yetu. Ikiwa sauti ya watu ni sauti ya Mungu, basi wayasemayo watu yaliyomabaya juu yako na yangu, yatusaidie kufanya tafakari ya kina kujisahihisha. Hakuna malaika watakaoshuka kutoka mbinguni na kukuambia kweli hiyo tukijua kila mtu ni hekalu la Roho Mtakatifu, 1Kor 6:19, anayetuongoza katika kweli.

Wapendwa wana wa Mungu, Yesu katika Injili ya leo anadhihirisha amani na utulivu wa kweli anapoletewa mgojwa aliyepooza katika kitanda mzegamzega.  Kwa Yesu, watu waliiona amani, utulivu, upendo, haki, na matumaini ya kweli. Kwa Yesu, watu walikuwa na Imani kwani walipata faraja na utulivu wa kweli. Na kwa Yesu watu waliona huruma na msamaha wa dhambi zao. Yesu kuona imani ya watu wale walivyokuwa wakimtaabikia ndugu yao mgonjwa akamwambia yule aliyepoonza, “Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako,” Mt 9:2. Maneno haya ya Yesu ni maneno yenye kubeba ubaba na umama ndani yake. Maneno haya ya Yesu siyo tu ya uponyaji, bali ya kuumba  na kuleta uzima mpya. Tendo hili linawachukiza baadhi ya waandishi kwani walilitafsiri kama ni kukufuru Mungu. Watu hawa hawaoni Umungu ndani ya Yesu. Kuwakata kimbelembele chao, Yesu analiweka wazi jambo hili machoni mwao na kusema, Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule mwenye kupooza) Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako,” Mt 9:6. Kwa maneno na msimamo huu wa Yesu mbele ya waandishi hawa anadhihirisha mamlaka yake kamili, kwamba, Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:3. Pamoja na mamlaka hayo yaliyotukuka, Yesu alibaki kuwa mfano wa pekee katika ‘unyenyekevu na utii. Na “tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba,” Flp 2:8. Huyu ndiye Yesu, na Huyu ndiye Mungu, Bwana wangu na yote yangu. Amina!

Wapendwa katika Kristo, tendo alilolifanya Yesu la uponyaji linakuwa kikolezo cha Imani, na ule mkutano unafunuliwa juu ya Mambo makuu ya Mungu. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii,” Mt 9:8. Je, wewe ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii, umefunuliwa jambo gani ambalo waweza kumsifu Mungu? Ndugu yangu, nikuache na maneno haya mazito ya Mtakatifu Paulo yanayoweza kutusaidia kuzama katika unyenyekevu. Kwanza, ni kukubali kufa kila siku na Kristo na kwa sababu ya Kristo. Naye anasema, “ndugu, kwa huku kujisifu kwangu niliko nako juu yenu katika Kristo Yesu Bwana wetu, ninakufa kila siku,” 1Kor 15:31. Ni kufa kila siku katika ‘kweli, haki, upendo, na amani, kwa watu na kwa ajili ya watu na kwa mapenzi ya Mungu. Pili, kujisifu katika kupambana na udhaifu wako. Kuyatambua madhaifu yako na kujisahihisha kuelekea nuru ile ya kweli, yaani, “mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu,” Kol 3:1. Na kujisahihisha katika hali ya udhaifu Mtume Paulo anasema, Ni nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu nami? Ni nani aliyekwazwa nami nisichukiwe? Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu. Mungu, Baba wa Bwana Yesu, aliye mtukufu hata milele, anajua ya kuwa sisemi uongo,” 2Kor 11:29-31. Tulenge kila siku katika ukamilifu hata kama udhaifu upo.

Tumsifu Yesu Kristo! 

Mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu,” Kol 1:10


Tusali:-Ee Mungu, ilikupendeza na ukaona inafaa tukuumba kama tulivyo wanadamu kwa sura na mfano wako. Tujalie hofu yako ndani yetu ili tuushinde ubinadamu wetu na kuifikia nuru yako. Amina

martes, 28 de junio de 2016

TAFAKARI: SHEREHE YA MT. PETRO NA PAULO, MITUME

SHEREHE YA MT. PETRO NA PAULO, MITUME
29/6
Somo: Mdo 12:1-11
Zab: 34:1-3, 4-5, 6-7, 8-9
Somo II: 2Tim 4:6-8, 17-18
Injili: Mt 16:13-19
Nukuu:
Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi,” Mdo 12:11

Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda,” 2Tim 4:7

Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina,” 2Tim 4:18

Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai,” Mt 16:16

Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda,” Mt 16:18

Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni,” Mt 16.19

TAFAKARI: “Utume si lelemama, bali ni kuvumilia hadi ushindi wa kweli.”

Wapendwa wana wa Mungu, neno utume si geni masikioni mwenu. Ila tusikiapo neno utume yatupasa kwanza kabisa tuelewa ukweli huo na uhasilia wa maisha hayo ya kiutume kwamba hayana uhusiano na faida binafsi. Ni utumishi uliotukuka, na usiojifungamanisha na maslahi binafsi. Ni msukumo wa maisha unaotutaka kujitoa zaidi kwa ajili ya wengine bila kujali faida yetu binafsi. Utume kamwe hauwezi kuwa na malengo ya faida binafsi. Mtu anapokuambia ametoka utume, au anaenda utume ni vyema kuelewa kwamba anaenda kumenyeka, kutaabika na kujichosha kwa ajili ya wengine. Msukumo huu haupaswi usukumwe na ufahamu au vigezo vya wale tunaowahudumia, ila kwa kila tunayemuhudumia bila kujali anatujua au la.

Hivyo leo Mama Kanisa anavyosherehekea siku ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, anasadifu ukweli huu, yaani watu hawa walikuwa ni MAJITU YA SIFA, katika maana ya kwamba waliyatoa maisha yao bila kujibakiza pasipo woga wowote. Ingawa sitazama sana katika wasifu wa Petro na Paulo Mitume, ila historia ya maisha yao inaonyesha jambo hili. Petro anajulikana zaidi kama kiongozi na mwakilishi wa Kristo katika kundi la wale wa mwaminio Kristo na kuyaishi maagizo yake. Paulo anasimama kama mmisionari shupavu aliyeyafanya yote ndani na kwa ajili ya Kristo. Hivyo leo Kanisa linasheherekea zawadi ya maisha yao katika kutenda na kulisimamie lile alilolianzisha na kuliacha Kristo, na kulipeleka duniani kote kama Kanisa la kimisioni na Sakramenti ya wokovu.

Ni wazi watu hawa wawili yaani Petro na Paulo wanayafanya mambo haya makubwa katika maisha yao ‘kwanza kwa kujitambua wao wenyewe,’ na pili ‘kuishi utambuzi huo katika kukutana na Kristo kila siku.’ Ukomvu wao wa Imani ni matokea ya kumtaabikia Kristo kila siku katika kuutoa ushuhuda wa kweli. Somo la kwanza linaeleza kwa undani ni kwa namna gani Petro aliutoa ushuhuda huo bila woga. Mwisho anasema maneno haya baada ya kutoka gerezani kwa miujiza. “Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi,” Mdo 12:11. Ufahamu huu kwa Petro hauna tena shaka juu ya kile anachokiamini.

Injili ya leo kwa namna nyingine inatupa wasifu wa Petro kwa undani na kutuelekeza nini hasa maana ya kiti chake na nafasi yake kati ya Mitume. Mtume Petro ndiye pekee aliyejibu swali ya Yesu kwa ufasaha, licha kwamba kwa mujibu wa Yesu jibu lile ni ufunuo kutoka kwa Mungu. Yesu anapowauliza wanafunzi wake, Je, watu wanasema kuwa mimi ni nani, Petro anajibu baada ya ukimya mkuu (tafakari): “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai,” Mt 16:16. Yesu anaridhika na jibu hili, na hapo hapo anamnyenyekesha Petro kwa kusema, “Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 16:17. Ufahamu huu wa Petro, na kufunuliwa huku kwa siri hii juu ya Kristo, kunamhesabia haki juu ya kiti kile alichokikalia hadi leo, Petro kama halifa wa kwanza, na Mababa watakatifu waliomfuata kama maalifa wa Kristo. Yesu mwenyewe anaweka kiti hiki rasmi kwa kusema, “wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda,” Mt 16:18. Wapendwa, Kanisa letu linamisingi yake. Moja ya misingi yake hiyo ni uongozi Imara usio wa yumbishwa.

Wapendwa wana wa Mungu, baada ya kuwekwa rasmi kiti hicho kama alama ya uongozi imara kichungaji, anayekalia kiti hicho anapewa mamlaka kamili juu ya wale watakao kuwa chini ya uongozi huo. Yesu anayatoa mamlaka hayo kwa kusema, Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni,” Mt 16.19. Kwa kupitia kiti na mamlaka haya, Kanisa linakuwa rasmi chombo cha msamaha na huruma ya Mungu. Na hii ndiyo maana ya Kanisa kama Sakramenti ya wokovu. Kanisa pia linapewa mamlaka ya kufundisha, kuonya, kukataza na hata kufungia yale yanayoenda kinyume cha Imani na ufuasi wa Kristo.

Ndugu yangu, chuma kinapoitwa “Iron Steel,” kimepita katika moja mkali sana. Uimara wa chuma hiki ni tokeo la chuma hicho kuvumilia joto hilo kali bila kupoteza uhasilia wake. Mitume, na hasa Petro na Paulo ambao leo Mama Kanisa anawasherekea, walitaabika vya kutosha kuhusu jina la Yesu. Somo la Pili linaeleza kwa undani mahangaiko na taabu alizozipata Mtume Paulo. Mtume Paulo anasema kama ni vita ameishinda na mwendo ameumaliza. Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda,” 2Tim 4:7. Faida kubwa aliyoipata katika utume wake huo wa pekee ni kuilinda Imani ambayo si kwa faida yake mwenyewe, bali kwa Kanisa zima. Msingi wa maisha ya Mtume Paulo ni kauli mbiu yake hii: “kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.” Flp 1:21. Hii ni hatua ya juu kabisa kwa mfuasi wa Kristo. Hapa ni kuishi kile unachokiamini na kukubali kuyapata yote kutokana na imani hiyo.

Wapendwa wana wa Mungu, hatua aliyoifikia mtume Paulo ni hatua ya kutokutishika na jambo lolote. Ni hatua ya kuishinda hofu na kuukumbatia uzima wa milele ingawa tunajua wote lazima tutakufa. Ni kujiachia katika mikono ya Kristo, na kuacha yeye atende kadiri apendavyo. Ni kutokuwa na shaka yoyote juu ya: sababu ya kuja kwake Yesu Kristo kwetu, kuteseka kwake, kusulubiwa kwake, kifo chake na ufufuko wake. Mtume Paulo analiweka fumbo hili kwa maneno haya: Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina,” 2Tim 4:18. Je, ninaweza kuyatamka maneno haya bila hofu yoyote ninapokabiliwa na changamoto za maisha yangu ya kila siku? Ndugu yangu Utume si lelemama, bali kuvumilia hadi ushindi wa milele.

Tumsifu Yesu Kristo!

Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda,” Mt 16:18


WATAKATIFU PETRO NA PAULO MITUME, MTUOMBEE. AMINA.

domingo, 26 de junio de 2016

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 13 YA MWAKA-C

JUMANNE WIKI YA 13 YA MWAKA-C
Somo: Amo 3:1-8; 4:11-12
Zab: 6:5-6, 7, 8
Injili: Mt 8:23-27
Nukuu:
Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake,” Amo 3:7

Simba amekwisha kunguruma, ni nani asiyeogopa? Bwana MUNGU amenena, ni nani awezaye neno ila kutabiri?” Amo 3:8 

Baadhi yenu nimewaangamiza, kama hapo Mungu alipoiangamiza Sodoma na Gomora, nanyi mkawa kama kinga kilichonyakuliwa motoni; lakini hamkunirudia mimi, asema Bwana,” Amo 4:11 

Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia,” Mt 8:25

Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu,” Mt 8:26 

Wale watu wakamaka wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?” Mt 8:27

TAFAKARI: “Kila jambo lina sababu yake. Simba amekwisha kunguruma, ni nani asiyeogopa? Bwana MUNGU amenena, ni nani awezaye neno ila kutabiri? Simama imara katika imani ya kweli.”

Wapendwa wana wa Mungu, ‘kila jambo lina sababu yake. Simba amekwisha kunguruma, ni nani asiyeogopa? Bwana MUNGU amenena, ni nani awezaye neno ila kutabiri? Simama imara katika imani ya kweli.’ Bila shaka katika maisha yako yapo mambo mengi mazuri na mengine yaliyojaa sintofahamu nyingi ambazo hadi sasa hujui sababu yake. Mambo haya yawe mema au mabaya kwetu kadiri ya mazingira na mitazamo yetu, jambo hilo au mambo hayo yana sababu yake. Hivyo chochote kile kitokeacho katika maisha yako au mazingira yako usikipuuze au kukipotezea hivi hivi. Mungu hutumia njia nyingi na tofauti kutufundisha, kufikisha ujumbe wake, na kuufunua Utukufu wake kwetu. Yale yote yanayotokea katika maisha yetu tuyajuayo na tusiyoyajua hubeba siri nzito ya Mungu kama mweza wa yote. Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake,” Amo 3:7. Jambo lolote litokealo katika maisha yako usiwe mwepesi wa kulaumu, bali kuwa na mazungumzo rafiki na Mungu, na muulize kama rafiki yako hivi, ‘Ee Mungu, wataka kunifundisha nini katika hili lililonitokea?’

Hakika alifanyalo Mungu na lolote lile litokalo kwa Mungu lina sababu katika maisha yako. Katika mazingira kama hayo wahitaji imani thabiti katika ufahamu, na maana kwa kile ukihojicho kuelekea ufahamu halisi. Ndugu yangu, alifanyalo Mungu ni sawa na Simba aliyekwisha kunguruma, ni nani asiyeogopa? Bwana MUNGU amenena, ni nani awezaye neno ila kutabiri?” Amo 3:8. Jambo la muhimu katika mazingira kama haya ni kuona kile alichokufunulia Mungu kama kilivyo na siyo kama ulivyo kadiri ya historia yako, mazigira yako, tamaduni yako, na mitazamo yako. Lolote lile lenye kubeba Umungu ndani yake ni Tatakatifu. Hivyo yakupasa kabla ya kulisogelea uvivue viatu vyako kama alivyofanya Musa katika kijiti kile kilichokuwa kikiwaka moto. Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti, akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu,” Kut 3:2b, 4b-c, 5.” Kuvua viatu ni kuvua ‘kinyago tafsiri cha uhalisia wa mambo kama ulivyo.’ Kila mtu ana kinyago chake, ‘mask’ kuona uhalisia wa kitu au mambo. Ni kama nilivyosema, yawezekana watumia uzoefu wako kuukabili ukweli ambao wakati mwingine hukudanganya. Watumia mila na desturi zenu kuutazama uhalisia ambao wakati mwingine hukudanganya.

Tunaposukumwa na kinyago hiki, ‘mask’ ni rahisi kuanguka kusiko kweli na halisi. Tunaporuhusu hali hii licha ya kupewa maangalizo mbalimbali, kifuatacho ni maanguko makubwa kwa sababu hakuna njia nyingine. Na hivyo ndivyo ilivyo kama asemavyo Mungu kwamba, Baadhi yenu nimewaangamiza, kama nilipoiangamiza Sodoma na Gomora, nanyi mkawa kama kinga kilichonyakuliwa motoni; lakini hamkunirudia mimi,” Amo 4:11. Mungu hupenda tuwe kama alivyotuumba, yaani, kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. 

Ni kwa namna hiyo, Injili ya leo inatutaka tuwe watu wa Imani ya kweli. Hatuwezi kumkiri Yesu kuwa ni njia, kweli na uzima, na wakati huo huo kukosa Imani naye. Imani hii thabiti ni kwa vipindi vyote; wakati wa mambo yakiwa shwari na wakati wa migogoro katika jamii. Leo swala la uzazi, familia, na mahusiano ni changamoto kubwa sana. Yatupasa kusimama katika kweli, na kulisema jambo hilo kwa Imani iliyo kweli. Haitoshi kupiga kelele tu kuwa tunaangamia, bali tunapopiga kelele tunaangamia tuwe tumesimama imara katika Imani.

Ni kweli yatupasa kumwendea Yesu muda wote, na hasa katika mikwamo iliyozidi akili na maarifa yetu. Mitume wanalifanya jambo hilo wanapoona chombo chao cha kusafiria kikiwa matatani. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia,” Mt 8:25. Kanisa kama chombo kielekeacho uzima wa milele, na sakramenti ya wokovu wetu kwa wabatizwa wote, mara zote hukaa kama familia na kupeleka maombi mbele ya Kristo ambaye Kanisa ni mwili wake. Tufanyapo jambo hilo kama mwili wa Kristo ulioingiliwa na udhaifu (dhambi), twapaswa kusimama katika Imani ya kweli. Yesu anatoa karipio kwa wanafunzi wake nasi pia katika nyakati zetu na kusema, “Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu,” Mt 8:26. Je, ndugu yangu, una imani kweli kwa kile umwombacho Mungu? Au waenda kwake ukiwa na mashaka? TUZIOMBEE FAMILIA ZETU ILI ZIBAKI SALAMA!

Tumsifu Yesu Kristo!

Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?” Mt 8:27


Tusali:-Ee Yesu na Bwana wangu, niondolee mashaka juu yako pale napokumbana na sintofahamu katika maisha yangu. Amina