martes, 26 de abril de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 5 YA PASAKA

JUMATANO WIKI YA 5 YA PASAKA
Somo: 15:1-6
Zab: 122:1-2, 3-4ab, 4cd-5                                 
Injili: Yoh 15:1-8
Nukuu:
Wakashuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka,” Mdo 15:1

Lakini baadhi ya madhehebu ya Mafarisayo walioamini wakasimama wakisema, Ni lazima kuwatahiri na kuwaagiza kuishika torati ya Musa,” Mdo 15:5

Mitume na Wazee wakakusanyika wapate kulifikiri neno hilo,” Mdo 15:6 

 “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote,” Yoh 15:5 

Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea,” Yoh 15:6 

Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa,” Yoh 6:7 

TAFAKARI: “Maandalizi ya Mtaguso wa Yerusalemu; kutahiriwa kama moja ya kigezo cha kuwa Mkristo na Mshiriki Kikanisa.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo tutafakari kwa undani changamoto za Kanisa la mwanzo, hasa swala zima la kupokelewa na kushiriki huduma za kikanisa kwa wale ambao hawakuwa Wayahudi. Tunaona Kanisa linapanuka na kuenea kila kona, ni kwa namna hiyo hiyo linakumbwa na kasumba ya ubaguzi uliolenga mila na desturi za Kiyahudi. Tendo la kutahiriwa kwa wayahudi lilikuwa na maana tofauti tofauti kadiri ya walivyokuwa wanaishi na hasa maagano yao na Mungu.

Kwa mara ya kwanza katika historia yao, tendo hili lilibeba maana ya usafi na kwa yule aliyetaka kuoa lilichukua maana ya “Bwana harusi wa damu.” Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi. Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri” Kut 4:25-26.  Kutahiri kulimaanisha pia agano kati yao na Mungu hasa kwa tendo la Mungu kuwatoa utumwani Misri, na hapa wanatairiwa kwa mara ya pili. “Wakati huo Bwana akamwambia Yoshua, Haya, jifanyie visu vya mawe ya gumegume, watahiri tena wana wa Israeli mara ya pili. Basi Yoshua akajifanyia visu vya mawe ya gumegume, akawatahiri wana wa Israeli huko Gibea-haaralothi. Na sababu ya Yoshua kutahiri ni hii; watu wote waliotoka Misri, waliokuwa waume, hao watu waume wote waendao vitani walikufa katika bara njiani, baada ya wao kutoka Misri,” Yos 5:2-4. Kutahiriwa pia kulimaanisha kushika torati kikamilifu. Basi ikiwa yeye asiyetahiriwa huyashika maagizo ya torati, je! Kutokutahiriwa kwake hakutahesabiwa kuwa kutahiriwa?  Rum 2:26. Pamoja na sababu nyingine zote tulizokwisha kuziona, hii ya mwisho ndiyo iliyotumika kama kigezo cha alisiye Myahudi kupokelewa katika jumuiya hii ya Wakristo wa kwanza ambayo kwa kiasi kikubwa walikuwa Wayahudi. Lakini baadhi ya madhehebu ya Mafarisayo walioamini wakasimama wakisema, Ni lazima kuwatahiri na kuwaagiza kuishika torati ya Musa,” Mdo 15:5. Watu wa mataifa yaani wale ambao hawakuwa wayahudi iliwapasa kufanya tendo hili la kutahiriwa. Hivyo Kanisa linafanya utaratibu wa kutatua tatizo hili ili upendo na amani udumu katika kundi. Mitume na wazee wakakusanyika wapate kulifikiri neno hilo,” Mdo 15:6.

Mambo haya ya nje hayapaswi kuwa sababu ya kutokuishi upendo wa Kristo katika Kanisa. Hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote,” Kol 3:11. Injili yetu ya leo inasema ukweli huu wa Kristo. Uzima wetu, na uhai wetu kiroho ni katika Kristo Yesu aliye mzabibu nasi matawi yake. Kuishi katika ukweli huu ni kuzaa matunda, yaani kuwa watu wa  upendo, haki na amani kama Kristo mwenyewe. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa,” Yoh 15:2

Ndugu yangu, njia salama na amani ya kweli kama mfuasi wa Yesu ni kukaa ndani yake na kuishi kadiri ya matakwa yake. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu,” Yoh 15:4. Je, hupendi kusitawi ndani ya Kristo? Bila Yesu Kristo katika maisha yako huku ukijiita Mkristo, hutoweza kufanya lolote lile liwe dogo au kubwa, “maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote,” Yoh 15:5b. Ni katika Kristo na ndani ya Kristo twaweza yote yawezekana katika maisha yetu kama wafuasi wake, na hasa pale tunapoishi vyema na kwa uaminifu ahadi zetu za ubatizo. Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa,” Yoh 6:7. Je, kinyume chake ni nini? Ndugu yangu, kinyume chake ni KUNYAUKA KIROHO NA KIMWILI. Na mwisho wa kadhia hii ni kutokufaa kwa chochote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea,” Yoh 15:6. Hakika kama mimi ni Mkristo bila Kristo katika maisha yangu, huko mbele ya safari ni giza tupu.

Tumsifu Yesu Kristo!

Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa,” Yoh 6:7


Tusali:- Ee Yesu, tudumishe katika upendo wako wa kweli.

No hay comentarios:

Publicar un comentario