jueves, 21 de abril de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 4 YA PASAKA

JUMAMOSI WIKI YA 4 YA PASAKA
Somo: Mdo 13:44-52
Zab: 98:1.2-3ab, 3cd-4
Injili: Yoh 14:7-14 
Nukuu:
 “Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa,” Mdo 13:46

 “Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao,” Mdo 13:50

 “Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?” Yoh 14:9

“Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba,” Yoh 14:12

Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana,” Yoh 14:13

TAFAKARI: “Jumuiya ya kwanza ya wakristo na Changamoto za uinjilishaji; Yote yawezekana ndani na katika Kristo.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo ni jumamosi ambapo kwa namna ya pekee Mama Kanisa anatualika tutafakari neno hili, “Jumuiya ya kwanza ya wakristo na Changamoto za uinjilishaji; Yote yawezekana ndani na katika Kristo.” Ni ukweli usio tia shaka kwamba kukua na kuongezeka kwa Kanisa letu kumekuwa hivyo kama kulivyo kutokana na changamoto mbalimbali katika huinjilishaji. Tukitazama jumuiya ya kwanza ya Wakristo kama ilivyo, walikalibiliana na upinzani mkubwa juu ya kile walichoamini sambamba na tukio zima la ufufuko wa Yesu Kristo. Tendo hili kwa ujumla wake liliweza kuwaunganisha watu na wakati mwingine kuwatenganisha kutokana na kile walichokuwa wakikiamini awali juu ya maisha yao na maana halisi ya Masiha.

Kutokana na wimbi hili la sintofahamu, jumuiya hii ya kwanza ya Wakristo iliwapasa kusema juu ya Yesu Kristo waliyemjua, waliyeishi naye, na yale aliyotenda kwa maisha yao na ufunua mzima wa historia ya wokovu wa mwanadamu kadiri ya Maandiko Matakatifu yalivyofumbua ukweli huu. Ni katika hali hii ya kumtangaza Kristo kadiri ya mguso wa maisha ya kila siku ya yule waliyemwamini (Yesu Kristo) na ufunuo wa Maandiko Matakatifu yalivyoufunua ukweli huu kupingana na ufahamu ya Wayahudi kuhusu Masiha, Wayahudi hawa hawakuwa tayari kusikia alichokisema Mtume Paulo. Hivyo Mtume Paulo analazimishwa kukaa kimya na Wayahudi kutokana na wingi wa watu kuukubali ukweli juu ya Kristo. Hapa ndipo tunapoongelea kuhusu wivu wa Wayahudi kuhusu ukweli juu ya Kristo. Bali Wayahudi, walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana,” Mdo 13:45.

Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, aliloanzisha Mungu hatuwezi kulizuia kwa ufahamu wetu mdogo tuliokuwa nao. Tunapoukataa ukweli wa Mungu, Mungu ufikisha ukweli huu kwa watu wengine. Licha ya kwamba Taifa la Israeli lilipendelewa kufanya maagano na Mungu katika safari hii ya ukombozi, Mungu katika kutimiza hazma yake hakujali kufikisha ujumbe wake wa wokovu kwa wale waliomridhia. Ni katika namna hii wewe na mimi leo tunahesabiwa haki tunapoishi kweli hii ya kimungu tuyafanya na kuyatimiza kwa uaminifu yale yampendezayo Mungu. Hivyo, Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa,” Mdo 13:46. Ninapotafakari hazma ya Mungu katika malengo yake ya umilele ndani yetu, nimegundua kitu hiki; binadamu huweza tu kuchelewesha hazma ya Mungu katika ukamilifu wake kwa wakati ufahao, ikiwa ni subirá tu ya Kimungu kwa kujali uhuru aliokuwa nao binadamu kwa kujirudi na kumrejea muumba wake, ila binadamu huyu hawezi kubadili mpango wa Mungu kwa kile anachoona kinafaa kwa maisha yetu na malengo yake ambayo kwa wakati wote na nyakati zote ni mema.

Ndugu yangu, ni kwa namna hii lile aliloazimia Mungu linabaki kuwa na mashiko kwamba, Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini,” Mdo 13:48. Mara zote ushindi kama huu hauachi kuwa na upinzani. Unapoona umepita katika msuguano wa kiimani wa mtindo huu, yakupasa kujiandaa vyema katika hali kinzani kwa kile ulichokisimamia. Nalisema hili si kwa nadharia ila kwa vitendo kutokana na mang’amuzi yangu ya kichungaji kwa miaka sita niliyokaa Parokiani kama Paroko mara tu baada ya upadirisho wangu. Kile ulichokisimamia katika kweli na haki katika Kristo bila tuterereka, yakupasa kujiandaa katika ukinzani wake. Jambo hili na ukweli huu unawakuta Mtume Paulo na Barnaba. Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao,” Mdo 13:50. Katika hali ya namna hii, wewe kama mchungaji nikimaanisha mwenye dhamana kiimani mathalani Paroko, yakupasa kusimama imara katika kweli na haki Kristo akiwa msingi wa yote. Yatakayotokea kutokana na msuguano huu ni mapito tu. Yatakuja kwa kasi kubwa, ila yatatoweka kama moshi wa mabua angani. Mwisho wa msuguano huu ni ukamilifu wa kweli ya Mungu, na furaha ya kweli kwa kile ulichokisimamia kama mpakwa mafuta. Jambo hili lilitokea pia kwa Mtume Paulo na Barnada. Roho wa Bwana hatoacha kutufariji na kutujaza matumaini ya kulinena neno la Mungu licha ya magumu tunayokutana nayo. Na wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu,” Mdo 13:52. Kanisa leo na kama ilivyokuwa mwanzo lapaswa daima kuishi katika ukweli huu wa Kristo ndani na katika yeye.

Wapendwa wana wa Mungu, msingi wa haya yote tunayoyaona kutoka jumuiya hii ya kwanza ya Wakristo yanatokana na msingi wa imani waliyokuwa nayo juu ya Yesu Kristo na yale aliyoyafundisha. Ni ukweli usiotia shaka kwamba jumuiya hii ya kwanza ya Wakristo waliamini barabara yule wamfuatao na kumshuhudia mbele za watu. Mtume Filipo anapomwuliza Yesu tuonyeshe Baba nayo yatosha kumwamini, Yesu anamjibu na kusema, “Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?” Yoh 14:9. Kristo anafumbua ukweli wa kumwilishwa kwake, si tu kwa Filipo, hata kwetu pia. Kumwilishwa huku kwa Yesu Kristo ni ukweli wa Mungu mwenyewe katika fumbo na umbo hili la kibidamu kama sisi ila utofauti wake ni kwamba hakutenda dhambi kama mwanadamu. Yesu Kristo anakazia ukweli huu na kusema, “Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake,” Yoh 14:10b. Ufunuo huu wa Mungu kupitia Yesu Kristo ni wa wazi na wakati mwingine wakujificha. Ila hapana shaka hata kidogo kwa umungu wa Kristo kunakojieleza kwa yale aliyoyafanya yaani kazi zake.

Wapendwa wana wa Mungu, Kristo analifumbua jambo hili pale tunapokuwa na shaka juu yake kwa kusema, “La! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe,” Yoh 14:11b. Imani ya kweli juu ya Kristo ndiyo inayotufanya kuishi na kutenda kama alivyofanya Yesu Kristo. Ukweli huu anausema Kristo mwenyewe, na wale wote waliouishi ukweli huu, Kristo amefanya makuu kupitia kwao kwa mkono wake. “Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba,” Yoh 14:12. Matendo makuu hufanyika kwa mtu huyu aaminiye juu ya Kristo si kwa faida yake binafsi, ila kwa kupitia mtu huyu Mungu anatukuzwe na kuabudiwa milele ndani ya Yesu Kristo mwanaye. Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana,” Yoh 14:13. Je, ndugu yangu, hupendi kuwa sababu ya utukufu huu wa Mungu kupitia mwanaye Yesu Kristo?

Wapendwa, jibu la swali hili ndilo kiini cha Imani yetu, na maisha yetu kama Wakristo na Wafuasi wa Kristo leo katika dunia hii tunayoishi: “KUWA SABABU YA UTUKUFU WA MUNGU KUPITIA MWANAYE YESU KRISTO, na si vinginevyo.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba,” Yoh 14:12


Tusali:-Ee Yesu, tufanye kuwa sababu ya Utukufu wa Mungu kupitia kwako. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario