JUMAMOSI
WIKI YA 2 YA PASAKA
Somo: Mdo 6:1-7
Zab: 33:1-2, 4-5, 18-19
Injili: Yoh 6:16-21
Nukuu:
“Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu
na kuhudumu mezani,” Mdo 6:2
“Basi
ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa
na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na
kulihudumia lile Neno,” Mdo 6:3-4
“Ambao
wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu
yao,” Mdo 6:6
“Na
bahari ikaanza kuchafuka kwa kuvuma upepo mkuu,” Yoh 6:18
“Naye
akawaambia, Ni mimi, msiogope,” Yoh 6:20
TAFAKARI:
“Msiogope”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo kwa namna ya pekee tulitafakari neno hili, “Msiogope.” Hofu ni moja ya
dalili za maumivu ya ndani. Hofu
tunayotaka kuiongelea hapa si hofu ya nyoka au simba, na vingine kama hivyo. Ni
hofu ya vitu vya kawaida kabisa kama asemavyo Mzaburi, “hapo waliingiwa na hofu
pasipokuwapo hof” Zab. 53:5a.
Mfano:- Kuogopa giza sana kiasi cha
kutothubutu kutoka chumba kimoja kwenda kingine wakati wa usiku, Kuogopa kutembea
barabarani mpaka uwe na mtu; Kuogopa wadudu na viumbe kama mende, chura, panya,
kinyonga, mjusi; Kuogopa watoto wachanga na wazee. Mtu akiona kikongwe anapita
yupo tayari hata kubadili njia ili asipishane naye.
Hofu ya maisha yatakavyokuwa magumu;
Hofu ya maisha ya kesho; Hofu ya kuolewa na kuoa: wakijiuliza itakuwaje
watakapoanza maisha ya ndoa? Hofu ya matukio magumu ya maisha huleta mapepo “HALI
KINZANI” inayotufanya tumchukie MUNGU na kutenda dhambi. Hofu huzaa kushtuka
shtuka na kufanya mtu kuugua magonjwa ya mwili, na pia hofu ni mbaya zaidi inapokutawala.
Jumuiya ya kwanza ya wakristo kadiri ya somo la leo,
wanaingiwa hofu kutokana na jumuiya hiyo kuongezeka, na huduma kutokwenda sawa.
“Haipendezi
sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani,” Mdo 6:2. Hivyo wanaona ipo
hatayari ya kuacha kulihubiri neno wakabaki kutatua matatizo yanayotokana na
manung’uniko kati ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania
kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku.
Jumuiya hii kwa
kuongozwa na nguvu ya Kimaadili, Unyenyekevu, na Roho Mtakatifu, wanakabiliana
na hofu hii kwa kufanya uteuzi wa watu saba “Mashemasi,” kutatua tatizo hilo.
Mitume wanatoa agizo na vigezo vya kuwachagua wasaidizi hao na kusema, “basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu,
walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya
jambo hili; na sisi tutadumu katika
kuomba na kulihudumia lile Neno,” Mdo 6:3-4.
Baada ya vigenzo na
masharti kuzingatiwa, wateuzi hawa wanawekwa wakfu kwa tendo “ambao
wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu
yao,” Mdo 6:6. Tendo hili
linamsisitizo wa umoja wa Mitume ambao leo tungesema umoja wa maaskofu,
“Collegiality of Bishops.” Umoja huu ni
muhimu sana leo katika Kanisa letu. Tunapoona mmoja katika kundi hili akitamka
yake kama anavyojisikia, ni wazi taasisi hii muhimu na fundishi inaingiliwa.
Tulio wengi tunajiuliza, hilo alinenalo kalitoa wapi, na kwa baraka ya nani? Na
kama jambo hilo asemalo linaukweli, Je, ni kwa manufaa ya nani?
Leo katika Injili
wanafunzi wa Yesu wakiwa wanasafiri wenyewe wanaingiwa na hofu kwa sababu ya
mabadiliko ya hali ya hewa ndani ya baharí.
“Na bahari ikaanza kuchafuka kwa
kuvuma upepo mkuu,” Yoh 6:18. Katika mtafaruku huu, Yesu anajitokeza akitembea
juu ya baharí na kuwaambia, “Ni mimi, msiogope,” Yoh 6:20. Hata leo Yesu anakuambia wewe na
mimi “usiogope.” Yesu analiambia Kanisa pia kama Sakramenti ya wokovu, chombo
kinachosafiri, na chombo ambacho kipo hija, kwamba, “Msiogope,” ni MIMI. Swali
ni hili, Je, tunaweza kumwona Yesu katika hatari hii ya kuangamia na tukabaki
na msimamo na imani yetu? Tunaitaji jicho la Imani na ufahamu wa kutosha
kuzisoma alama za nyakati zetu. Yapo mambo mengi leo hayaendi sawa hasa kwenye
jamii yetu. Tumeingiwa hofu hata pale pasipo na hofu kusema mzaburi, Zab 53:5a.
Mpendwa, neno “usiogope”
lipo mara 366 katika Biblia. Hii ina maana Mungu anatuambia kila siku “usiogope”. Unapokuwa na hofu ya kitu
chochote, basi kitu hicho ndicho chenye uwezo wa kuamua hatima yako. Kwa mwenye
Imani ya kweli, na watu wa Mungu
tunatakiwa tuelekeze hofu yetu kwa Mungu tu na si kwingineko kwani
tutakapoielekeza kwa Mungu yeye ni mwaminifu na atatuelekeza kufanya ya
Mbinguni.
Maandiko matakatifu yanatuambia ni nani twapaswa kuwa na
hofu naye; “Bwana wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu,
na awe yeye utisho wenu,” Isa 8:13. Yesu anasema hivi kuhusu hofu, “Nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili,
kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi. Lakini nitawaonya mtakayemwogopa; mwogopeni
yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam,
nawaambia, Mwogopeni huyo,” Lk 12:4-5. Katika kitabu cha Ufunuo wa Yohani
tunaona adhamu ya watu mwenye woga. “Bali
waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao
waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto
na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili,” Ufu 21:8
Ndugu yangu, Hofu haileti madhara ya kiroho tu bali hata ya
kimwili. Huleta mshtuko na penye hofu pana wasiwasi, palipo na haya huleta
magonjwa ya “Organic” {sehemu za
mwili zifanyazo kazi maalumu} na hitilafu katika shehemu hizi husababisha
vidonda vya tumbo {ulcers} shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya ini,
upungufu wa damu mwilini, n.k. “Kwa
sababu hiyo viuno vyangu vimejaa maumivu, utungu umenishika, kama utungu wa
mwanamke azaaye; ninaumwa sana, nisiweze kusikia; nimefadhaishwa wa hofu,
nisiweze kuona. Moyo wangu
unapiga-piga, utisho umenitaabisha, gizagiza la jioni nilipendalo limegeuka
likanitetemesha,” Isa 21:3-4.
Wapendwa
wana wa Mungu, kuna mambo kwa binadamu ni ya wazi kabisa na lazima tutayapitia
tupende tusipende. Kifo ni mojawapo ya jambo ambalo halipingiki katika uhasilia
wake. Wote lazima tutakufa. Kitu cha kuogopa hapa si kifo, bali hofu. Yatupasa
kuishinda hofu dhidi ya kifo. Uhakika wa maisha baada ya kifo tunayo. Kristo
ndiye kielelezo chetu katika uzima huo baada ya Kifo. Acha hofu! Wote tupo
safarini kuelekea tukio hili muhimu, kwenda upande wa pili wa ukweli kuhusu
Maisha ya UMILELE. Katika jambo hili Yesu anasema, “Amin,
amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo
hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi,” Yoh 12:24. Kwa mantiki hii,
yatupasa kufa ili kuishi maisha hayo ya UMILELE.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Naye
akawaambia, Ni mimi, msiogope,” Yoh 6:20
Ee Yesu uliye
kielelezo chetu, tuondolee hofu, tujaze matumaini na ujasiri wa kukabiliana na
sintofahamu zote katika maisha yetu ya kila siku. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario