JUMATANO
WIKI YA 4 YA PASAKA
Somo:
Mdo 12:24-13:5a
Zab:
67:2-3, 5, 6, 8
Injili:
Yoh 12:44-50
Nukuu:
“Basi
hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema,
Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia,” Mdo 13:2
“Ndipo
wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende
zao,” Mdo 13:3
“Naye
Yesu akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye
aliyenipeleka. Naye
anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenipeleka,” Yoh 12:44-45
“Mimi
nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae
gizani,” Yoh 12:46
“Na
mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili
niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu,” Yoh 12:47
“Yeye
anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo
nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho,” Yoh 12:48
TAFAKARI: “Ndani na katika Kristo Yesu kuna Nuru
ya Kweli.”
Wapendwa wana wa Mungu,
Mungu wetu aliye hai kwa nyakati tofauti katika historia ya wokovu wetu
anajitambulisha kama Mungu muumbaji wa nuru. Naye anasema, “Mimi
naiumba nuru, na kulihuluku giza; mimi nafanya suluhu, na kuhuluku ubaya; Mimi
ni Bwana, niyatendaye hayo yote,” Isa 45:7. Yesu Kristo anatuagiza tuwe Nuru na
Chumvi kila mmoja kadiri ya wito na nafasi yake pale alipo. “Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa
imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na
kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima,” Mt
5:13-14. Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, tu chumvi ya
ulimwengu pale tunapokuwa tayari kushuka katika hali zetu na kuchanganyika na
watu kwa lengo la kuwa kikolezo cha kumfanya Kristo ajulikane kwao na siyo sisi
kama tulivyo.
Kanisa
la Mwanzo na hasa baada ya hujuma zile zilizofanywa na Wayahudi waliompiga
Kristo na wafuasi wake, kamwe halikuacha kuwa nuru na chumvi. Kwa kulitambua
hilo hawakuacha kuwa kikolezo cha Kristo na kumfanya Kristo ajulikane kwa
wengine wasiomjua. Kwa kuwa kikolezo cha Kristo kwa mfano wa Chumvi, na Maadili
mema kwa mfano wa Nuru, Roho Mtakatifu aliyaongoza yote waliyofunga na kuomba. “Basi hawa walipokuwa
wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba
na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia,” Mdo 13:2. Hata pale walipojibiwa maombi
yao hawakuacha kuyakabidhi yote mikoni mwa Mungu ili Kristo aendelee kutenda
makuu juu yao. Na “ndipo wakiisha kufunga na kuomba,
wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao,” Mdo 13:3. Huu ni mfano mzuri wa mshikamano katika kweli ile
anayotufundisha Kristo katika Kanisa lake kila siku.
Wapendwa
katika Kristo, tusipo fanya hili ambalo ndila lengo na shabaha ya chumvi
hatutakuwa na maana yoyote hata kama tukibaki katika ubora wetu. Kutotimiza
lengo kwa kile ulichokusudiwa ni sawa na kutokuwepo. Hivyo ndivyo Yesu asemavyo
kama lengo hilo halitotimizwa, ‘chumvi hivyo hutupwa
nje na kukanyagwa na watu.’ Zaidi ya kushuka na kujichanganya na watu na kuwa
kikolezo kwao-kumfanya Kristo ajulikane, yatupasa kuwa nuru katika maana ya
kuwa na maadili mema. Maadili haya mema kama Wakristo ndiyo hututofautisha na
wengine katika ona yetu kama Kristo, fikiri yetu kama Kristo, tenda yetu kama
Kristo, na amua yetu kama Kristo. Kwa kuyafanya haya pasipo unafiki, Kristo
huinuliwa katika ulimwengu, na nuru yake usambaa kote, nasi kwa tendo hilo
huesabiwa haki na Mungu. Hivyo kimaadili yatupasa kuwa juu kama ilivyo kwa
mwanga ili usambae eneo kubwa taa yapaswa kuwekwa mahali pa juu. Naye Yesu
anasema, “Hakuna mtu ambaye akiisha washa
taa huifunika kwa chombo, au kuiweka mvunguni, bali huiweka juu ya kiango, ili
waingiao wapate kuona nuru yake. Hakuna mtu awashaye taa na kuiweka mahali
palipositirika, au chini ya pishi; bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate
kuuona mwanga,” Lk 8:16; Lk 11:33. Ni kwa maadili yetu mema huwa nuru
pale tulipo na kwa mataifa yote.
Matendo yako mema
yanayosukumwa na maadili yako mema kama Mkristo na Mfuasi ya Yesu Kristo ni
nuru hai pale ulipo. Hivyo Yesu anasisitiza na kusema, “Vivyo
hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema,
wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 5:16. Ndugu yangu, mtazamo wako katika
kuona, kufikiri, kuamua na kufanya hutegemea sana nuru uliyokuwa nayo, yaani,
maadili yako ambayo husukuma tenda yako kama mwili, nafsi na roho. Na hiki
ndicho ulicho, yaani, Mwili, Nafsi, na Roho-Mtu kamili. Katika kweli hii Yesu
anasema, “Taa ya mwili ni jicho; basi jicho
lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru. Lakini jicho
lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Basi ile nuru iliyomo ndani
yako ikiwa giza; si giza hilo!” Mt 6:22-23. Maadili mema husukuma matendo mema
ya mtu, na hili ndiyo taa la mwili.
Wapendwa
wana wa Mungu, Kristo katika mwono wa Nuru ndiye HUKUMU yetu katika wema na
haki, na hasa pale tunapomwamini. “Amwaminiye
yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina
la Mwana pekee wa Mungu. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na
watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu,” Yoh
3:18-19. Kwa nini basi twajisikia ahueni tungali katika giza? Bila shaka
kutokana na mwelekeo wa dhambi na anguko lake, shetani ujigeuza na kuwa mfano
wa nuru katika mtazamo wa giza na kutufanya kugaagaa katika dhambi. Mtume Paulo
anasema, “Wala si ajabu. Maana Shetani
mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru,” 2Kor 11:14. Ukweli ni kwamba
Yesu Kristo mwenyewe ndiye nuru halisi ya ulimwengu, na ndani na katika yeye
hakuna giza bali uzima wa milele. Yesu anatuhakikishia hili na kusema, “Mimi
ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa
na nuru ya uzima,” Yoh 8:12. Ndugu yangu bado tu wajisikia ahueni kuishi katika
giza?
Kumwamini Kristo ni
kukaa katika nuru na ndicho alichokijia ili wewe na mimi tuwe katika nuru. “Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila
mtu aniaminiye mimi asikae gizani,” Yoh 12:46. Kutokumwamini Kristo ni kukaa
katika giza kunakosukumwa na matendo maovu, Yoh 3:19. Nuru ambayo kwa Mkristo
na Mfuasi wa Kristo ni maadili mema ambayo husukuma matendo yake mema, tunda
lake ni haki na kweli. Ni kweli isiyotia shaka kwamba mwenye maadili mema huwa
na hofu ya Mungu, hivyo kutenda kwake huwa kwa haki na kweli. Mtume Paulo
anaweka wazi kweli kwa wale wamwaminio Kristo na kusema, “Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa
mmekuwa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru, kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema
wote na haki na kweli; mkihakiki
ni nini impendezayo Bwana,” Efe 5:8-10. Palipo na wema wote, haki na kweli,
kuna upendo wa kweli na watu huishi kindugu.
Hivyo ndugu yangu,
kupendana kindugu ni kukaa katika nuru na kinyume chake ni giza tupu. “Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru,
wala ndani yake hamna kikwazo. Bali
yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala
hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho,” 1Yoh 2:10-11. Ndugu yangu,
kwa nini basi hadi leo hupendi kupatana na ndugu yako? Kama kweli wamwamini
Kristo Yesu kuwa nuru halisi ya ulimwengu, mbona basi unashindwa kuwa chumvi na
nuru hapo ulipo? Ni jukumu lako kama mfuasi wa Kristo kumfanya Kristo aonekane
kwa watu wote hata wale wasio mwamini.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mimi
nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani,”
Yoh 12:46
Tusali:-Ee Yesu uliye Nuru
halisi, tufanye kuwa nuru na chumvi pale tulipo kila mmoja kadiri ya hali na
wito wake. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario