domingo, 3 de abril de 2016

TAFAKARI: KUPASHWA HABARI YA KUZALIWA BWANA

 KUPASHWA HABARI YA KUZALIWA BWANA

Somo I: Isa 7:10-14
Zab: 40:7-8a, 8b-9, 10, 11
Somo II: Ebr 10:4-10
Injili: Lk 1:26-38
Nukuu:
“Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanaume, naye atamwita jana lake Imanueli,” Isa 7:14

“Ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili,” Ebr 10:9

“Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho,” Lk 1:30-33

TAFAKARI: “Mpango wa Mungu wa wokovu wa mwanadamu; kupitia wanyenyekevu wa Moyo.”

Wapendwa wana wa Mungu, Mama Kanisa leo anapoadhimisha sherehe ya kupashwa habari ya kuzaliwa Bwana, tutafakari “Mpango wa Mungu wa wokovu wa mwanadamu; kupitia wanyenyekevu wa Moyo.” Mungu aliye kusudi la mwanadamu, alikuwa na mpango naye tangu kabla ya kuumba ulimwengu. Hakuna shaka kwamba uumbaji wa ulimwengu huu pamoja na uzuri wake ni kwa mafaa ya binadamu na ufunuo wa Utukufu wa Mungu. Binadamu huyu aliyekuwa kusudi la Mungu tangu kabla ya kuumbwa ulimwengu, kwa bahati mbaya tendo hili ya pekee kwake hulichukulia la kawaida tu, na wakati mwingine kama mastahili yake. Kiburi hiki cha mwanadamu ndicho kimtiacho majaribuni na kutenda dhambi.

Hata baada ya kuanguka kwa sababu ya dhambi, Mungu kwa upendo wake hakuacha mpango wake wa kumkomboa mwanadamu. Huu ni upendo wa ajabu sana wa Mungu kwetu. Mungu kwa mara hii, anakubali kuchukua umbo letu na kufanana nasi-“Kumwilishwa,” ili awe karibu zaidi nasi. Mpango huu anaufunua kwa njia ya Ishara kupitia Nabii Isaya, na kusema, “Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanaume, naye atamwita jana lake Imanueli,” Isa 7:14. Ishara hii inakuwa wazi kupitia wale waliojawaliwa maisha ya unyenyekevu.

Bikira Maria anakuwa kati ya wanyenyekevu wa Moya wa Mungu na aliyempendeza kwa namna ya pekee. Bikira Maria anachukua jukumu la mzazi wetu wa kwanza-Eva, aliyeshindwa kwa anguko la dhambi. Bikira Maria anapewa mastahili haya kwa unyenyekevu wake, na siyo kwa sababu alikuwa mzuri sana au binti wa pekee sana katika mtaa wake au kijiji chake, au maarufu yake binafsi na familia yake. Mastahili haya anapewa Bikira Maria kwa sababu ya udogo wake na unyenyekevu wake.

 Malaika anatoa siri hii na mpango huu wa Mungu kwa Mama Bikiria Maria. Tendo hili linampa Bikira Maria hofu kubwa sana. Anapata hofu kwa kuona mpango mkubwa kama huu utakuwaje na yeye ni nani hata Mungu ayafanye hayo yote kwake? Malaika anapoona hofu hii, anamwambia, “Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho,” Lk 1:30-33

Ndugu yangu, kama hili lingetokea kwako, ungelibeba moyoni kwa unyenyekevu kama wa Bikira Maria? Leo mmoja wetu anapochaguliwa kwa nafasi mfano ya Ubunge, tena wakati mwingine kwa wizi wa kura, ona anavyojipambambanua kwa sifa bungeni. Nusu saa nzima kutoa shukrani zilizojaa majigambo, na mwisho wa siku hakuna anachofanya kwa kujitoa kwa wale waliomchagua. Ipo mifano mingi sana ya kutokuwa na unyenyekevu kama huu wa Bikira Maria. Tujifunze kwa Mama yetu Bikira Maria.

Yesu Kristo, ambaye anabeba dhambi za sisi wanadamu, analo jambo moja tu la kufanya. Nalo ni kufanya mapenzi ya Mungu, na si yake. Huu pia ni unyenyekevu wa hali ya juu. Ni sadaka kubwa sana mtu anapoazimia kuutoa uhuru wake wote kwa sababu ya mtu mwingine. Kuwa tayari kufanya yote bila kujibakiza kwa maelezo ya mtu mwingine bila kuhesabu faida ni sadaka kubwa sana. Hii ni sadaka kubwa sana isyo na kipimo. “Ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili,” Ebr 10:9. Utii ni sadaka kubwa sana unayeweza kutoa. Huwezi kuwa mtii kama si mnyenyekevu.

Ndugu yangu, tunaposheherekea siku hii ya leo, tujifunze kuwa wanyenyekevu kama Mama yetu Bikira Maria. Anza zoezi hili pale ulipo. Lianze kwenye familia yako na lifanye kadiri ya nafasi yako katika hiyo familia kwa kuyatimiza yote yanayokuhusu kwa unyenyekevu. Pili, lifanye jambo hili katika sehemu yako ya kazi, na sehemu yeyote unapowajibika kwa ajili ya wengine. Ndugu yangu, ukilifanya hili kwa moyo mkunjufu hakika Mungu atatenda mambo makuu kwako.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili,” Ebr 10:9


Kwa maombezi ya Bikira Maria Mama Yetu, Ee Yesu nijalie fadhila ya unyenyekevu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario