ALHAMISI WIKI YA 4 YA PASAKA
Somo: Mdo 13:13-25
Zab: 89:2-3, 21-22, 25, 27
Injili: Yoh 13:16-20
Nukuu:
“Katika
uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama
alivyoahidi,” Mdo 13:23
“Lakini, angalieni,
anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu
yake,” Mdo 13:25b
“Sisemi
habari za ninyi nyote; nawajua wale niliowachagua; lakini andiko lipate
kutimizwa, Aliyekula chakula changu Ameniinulia kisigino chake,” Yoh 13:18
“Tangu
sasa nawaambia kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa
mimi,” Yoh 13:19
TAFAKARI: “Wokovu wetu ni
katika Kristo; na hukumu yetu itatokana na mahusiano yetu na Kristo”
Wapendwa
wana wa Mungu, kama kweli tu wafuasi wa Kristo, ukweli huu ni ni bayana na
sehemu muhimu sana ya maisha yetu kama wafuasi wake KRISTO: “Wokovu wetu ni
katika Kristo; na hukumu yetu itatokana na mahusiano yetu na Kristo.” Hatuwezi
kuongelea wokovu wa Mkristo pasipo Kristo, na ni kwa namna hiyo hiyo hatuwezi
kuongelea hukumu ya mwisho pasipo uhusiano wetu na Kristo. Je, Mkristo ni nani?
Kwanza kabisa Mkristo ni yule aliyebatizwa katika Mungu mmoja nafsi tatu kadiri
ya kanuni ya ubatizo ilivyo: “Nakubatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la
Roho Mtakatifu.” Kwa kanuni hii tu haitashi wewe kuwa Mkristo.
Hatua
ya pili ya Mkristo kamili ni ufuasi wake katika Kristo katika fumbo zima la
kifo, mateso, na ufufuko wake Kristo. Ni katika fumbo hili tunazifia dhambi
zetu pamoja naye, na kufufuka naye katika hali ya upya pamoja naye. Upya huu wa
maisha katika Kristo na ndani ya Kristo unamapaswa yake. Mapaswa yake ni kuisha
kama Kristo mfufuka, yaani maisha safi na yasiyo na hatia yoyote. Tunapoisha
katika hatia tunaendeleza mateso ndani na katika Kristo. Kristo Mfufuka ni
mshindi dhidi ya dhambi na kifo. Kufurahia na kuisha katika hali ya dhambi ni
kuendeleza mateso ya Kristo Mfufuka, na kutothamini sadaka hii kubwa ya Kristo
kwa maisha yetu kama wafuasi wake. Ni katika mateso, kifo na ufufuko wake
Kristo, ndipo kwenye kilele kizima cha historia ya wokovu wetu. Kristo ndiye
mkamilisho wa kilele hiki.
Jambo
hili muhimu katika maisha ya Mkristo, ndilo ambalo Mtume Paulo katika safari
yake ya umisionari huko Pafo na Perge analiwekea msingi. Mtume Paulo anasema, “Katika uzao wake mtu
huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi,” Mdo
13:23. Ndugu yangu, wakovu wako pasipo Kristo ni sawa na maisha ya samaki
jangwani. Je, inawezekana? Ndugu yangu, usipolielewa jambo hii muhumu katika
maisha yako kama Mkristo, kuruka ruka kwako kutoka kikundi kimoja cha kitume
kwenda kingine ndani ya Kanisa hakuna maana yoyote. Kuhama kwako dhehebu moja
la Kikristo kwenda likingine hakuna maana yoyote. Kubadili dini yako ndani ya
Kristo kwenda dini nyingine hakuna maana yoyote. Kusimama leo mbele ya kadamnasi
na kusema umeokoka hakuna maana yoyote.
Ukweli wa Yesu Kristo
na nafasi yake katika historia nzima ya wokovu wetu, unasemwa na Yohane
Mbatizaji, ambaye leo katika somo letu la kwanza Mtume Paulo ananukuhu ukweli
huo na kusema, “Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi
sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake,” Mdo 13:25b. Maneno haya yanatafsiri hii: “HAKUNA WA
KULINGANISHWA NA YESU KRISTO KATIKA HISTORIA NZIMA YA WOKOFU WETU.” Kulegeza
kamba za viatu vya Yesu kungemaanisha uwezekano wa mbadala wa Yesu Kristo, kitu
ambacho kadiri ya mpango huu wa wokovu hakipo. Hapa ndipo penye fumbo zima la
UFUNUO WA MUNGU KWA MWANADAMU. Tunapoona baadhi ya binadamu wenzetu wanajiinua
na kujitanua kuwa wao ndio kweli na uzima, ni kichekesho na mshangao mkubwa.
Umepata wapi mamlaka hayo ndugu yangu? Kanisa kama chombo elekezi cha wokovu
wetu-Sakramenti ya wokovu, na uzima wetu kuelekea umilele, ni mwili wa Kristo
mwenyewe ambao sisi wabatizwa na waishio mapaswa ya ubatizo huo tu viungo
vyake. Ni makosa makubwa sana, leo tunaposikia mtu anajiinua na kusema nakwenda
kusali katika “KANISA LA EDGAR.” Kanisa ni la Kristo; ndani na katika Kristo.
Kuujua ukweli huu na kutokuuishi ni
usaliti mkubwa mbele ya Kristo aliyekufa kwa sababu yako. Yesu katika injili ya
leo anasema, “Sisemi habari za ninyi nyote; nawajua wale niliowachagua;
lakini andiko lipate kutimizwa, Aliyekula chakula changu Ameniinulia kisigino
chake,” Yoh 13:18. Aliyewachagua Kristo ni pamoja na sisi tunaohesabiwa haki
hiyo na Mama Kanisa kwa Sakramenti ya Ubatizo. Mama Kanisa anafanya kazi hiyo
leo kwa niaba ya Kristo mwenyewe. Kwa tendo hili la Sakramenti ya ubatizo,
tumeshiriki na kula chakula chake, yaani kuwa warithi wa ufalme wa Mbingu ambao
tayari umeanza katika ubatizo wetu ila bado kukamilishwa. Fumbo hili tunalisema
sana hasa wakati wa maziko ya Mkristo. Padre huyasema maneno haya
anapomnyunyuzia maiti (akiwemo kaburi) maji ya baraka: “Katika maji ya
ulibatizwa Mungu akamilishe ndani mwako aliyoanzisha katika ubatizo.” Kumgeuzia
kisigino Kristo ni kutokutambua ukweli huu.
Wakristo
wengi leo ni wamajina tu na matukio, nikimaanisha; katika ukweli wake wa nje
yaani usio wa kisakramenti. Ukweli huu wa kimatukio ni pamoja na Ubatizo,
Sakramenti ya Ekaristi, Kipaimara na Ndoa kwa wenye bahati. Leo wengi wanaishi
tu bila Sakramenti hii ya Ndoa na kujihalalishia. Sakramenti ya Kipaimara au
kuimarishwa leo imekuwa kama Sakramenti ya kuliaga Kanisa, “The send off
Sacrament.” Mkristo huyu ataonekana tena Kanisani akiwa mfu. Maisha katika
ufufuko hayapaswi kuwa ya mtindo huu. Yesu Kristo anatupa angalisho la mtindo
huu ya maisha bila yeye, na kusema, “Tangu
sasa nawaambia kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa
mimi,” Yoh 13:19. Angalisho hili ya Yesu leo linatutaka tufahamu kiini cha
maisha yetu na Imani yetu kipo wapi. Ndugu yangu, hauna wakati mwingine wa
kujipanga zaidi ya wakati huu na sasa. Usomapo habari hii, usiutafute ukweli
huu pengine zaidi ya kwenda ndani ya moyo wako na uguse pale ambapo mara nyingi
hupendi kupagusa na umepafunika licha ya kwamba ukweli wa kilicho ndani yake
unakijua. Hapo usipopataka kupagusa na kupaongelea ndiyo wewe mwenyewe, na
ndipo kwenye ufunguo wa kwenda pale alipo Kristo.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Tangu
sasa nawaambia kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa
mimi,” Yoh 13:19
Tusali:-Ee Yesu, najua
sasa hakuna wokovu pasipo wewe. Niwezeshe kila siku ya maisha yangu kuishi
kweli hii. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario