jueves, 28 de abril de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 5 YA PASAKA

JUMAMOSI WIKI YA 5 YA PASAKA
Somo: Mdo 16:1-10
Zab: 100:1b-2, 3, 5
Injili: Yoh 15:18-21
Nukuu:
 “Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani,” Mdo 16:1 

Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Myunani,” Mdo 16:3

Basi walipokuwa wakipita kati ya miji ile, wakawapa zile amri zilizoamriwa na mitume na wazee walioko Yerusalemu, ili wazishike,” Mdo 16:4

Makanisa yakatiwa nguvu katika ile Imani, hesabu yao ikaongezeka kila siku,” Mdo 16:5

Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi,” Yoh 15:18

Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia,” Yoh 15:19

Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka,” Yoh 15:21

TAFAKARI: “Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi,” Yoh 15:18

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, leo kwa namna ya pekee tutafakari changamoto za uinjilishaji za Kanisa la mwanzo na changamoto tunazokumbana nazo leo katika utume wetu kama wabatizwa na wahudumu katika Kanisa. Bila shaka wiki nzima hii tumekuwa tukitafakari changamoto hizi na hatua waliyochukuwa Mitume kukabiliana nazo, hasa kwa kuitisha Mtaguso wa Yerusalemu.

Matokea ya Mtaguso huu ulikuwa: Wajiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu,” Mdo 15:29. Hata hivyo Kanisa bado linakumbana na changamoto za mila na desturi za Kiyahudi. Hivyo ili Timotheo afuatane na Mtume Paulo, inampasa kutahiriwa. Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani,” Mdo 16:1. Je kwa tendo hili Paulo atakuwa ameenda kinyume na maamuzi ya Mtaguso wa Yerusalemu? Ndugu yangu tunayesafiri wote katika tafakari hii, ni vyema tuelewe jambo hili. Licha ya kwamba Kanisa ni la kiulimwengu, na hili limethibitishwa katika mitaguso mbalimbali, maamuzi ya mitaguso hiyo hayaondoi upekee wa changamoto ya Kanisa mahalia, mfano Kanisa la Tanzania. Hapa ndipo tunapozungumzia busara za kichungaji kuenenda na mazingira husika bila kuwakwaza watu. Hivyo, tukio hili la kutahiriwa kwa Timotheo linaendana na mazingira maalumu bila kuwakwaza watu, ili kuweza kupenyeza ujumbe ule waliokuwa wameubeba au kusudiwa, na hapa ikiwa ni maamuzi ya Mtaguso wa Yerusalemu.

Mtume Paulo anatupa sababu ya kufanya hivyo ikiwa ndiyo busara ya kichungaji. Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Myunani,” Mdo 16:3. Je, Paulo alilifanya jambo hili kutowakwaza Wayahudi? Bila shaka Paulo analifanya jambo hili kwa malengo hayo, kama anavyosema Kristo, Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa,” Lk 17:1-2. Ni vizuri kutowakwaza wale tunaotaka waufahamu ukweli wa Mungu. Kwa upande wa kichunguaji, ni rahisi sana kumhubiri Kristo kwa kwale wasiomjua bado, kuliko kuwarudisha wale waliokatishwa tamaa hasa pale tunapowakwaza.

Kwa mambo yale ambayo hayaendi kinyume na imani yetu, yanapotokea bila kujua au kujiandaa, ni vyema tukayapa muda ili tuyaelewe na kutumia mbinu ya kuwaelimisha wale wayafanyayo, hasa tukilenga katika kutaka kujua ‘kwa nini wanafanya kama wanavyofanya.’ Hivyo kwa kulitambua jambo hilo, inakuwa rahisi kufikisha ujumbe ule uliokusudiwa. Basi walipokuwa wakipita kati ya miji ile, wakawapa zile amri zilizoamriwa na mitume na wazee walioko Yerusalemu, ili wazishike,” Mdo 16:4. Mambo haya huwa tunakutana nayo mara nyingi hasa pale tunapoanza utume mpya katika mazingira mageni kinyume na mila na desturi zetu tulizokulia na kuzizoea. Jambo la msingi ni kushikilia mafundisho sahihi ya Kanisa (katika kuyafundisha kwa lugha nyepesi na mifano hai ili yaeleweke kwa waamini) na yenye mwelekeo wa wokovu, na maisha ya umilele.

Ni dhahiri kwa Kanisa la mwanzo mengi yalifundishwa na yenye kuleta umoja kindugu na Kikanisa kwa ujula wake, ila haya manne yapo wazi, ususani tendo la kutahiriwa kuonekana kama kigezo cha kuchangamana pamoja; Kwanza, mafundisho yalisisitiza kuzishika amri za Mungu. “Kutahiriwa si kitu, na kutokutahiriwa si kitu bali kuzihifadhi amri za Mungu,” 1Kor 7:19.

Pili, kuishi maisha ya Ufufuko ndani na Katika Kristo Yesu, na hapa yakilenga haswa mila na desturi zetu zilizopotofu na zisizo na mwelekeo wa wokovu na maisha ya umilele. Msalaba wa Kristo ndiyo kielelezo cha huo Utukufu wenyewe. Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya,” Gal 6:14-15. Hapa tunakumbushwa pia hakuna Utukufu pasipo Msalaba kwa ye yote yule aliye mfusi mwaminifu wa Yesu Kristo.

Tatu, mafundisho ya Kanisa la mwanzo yalijikita kwenye kweli ya kuwa yote katika yote na Kristo Yesu. Kujitoa bila kujibakiza katika hali ya kusahau tofauti zetu zisizo na mwelekeo wa wokovu na maisha ya umilele. Hivyo hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote,” Kol 3.11.

Nne, yote yapo kama yalivyo kwa neema ya Mungu. Hakuna kati yetu mwenye kujihesabia haki mwenyewe. Zipo sehemu nyingi katika Maandiko Matakatifu, na hasa Agano Jipya zinazoonyesha kweli hii. Hivyo ndugu yangu, kujisifu kwetu ni huku, ushuhuda wa dhamiri yetu, ya kwamba kwa utakatifu na weupe wa moyo utokao kwa Mungu; si kwa hekima ya mwili, bali kwa neema ya Mungu; tulienenda katika dunia, na hasa kwenu ninyi,” 2Kor 1.12

Hivyo wapendwa wana wa Mungu, wewe na mimi yatupasa kujua kweli hii, kwamba, utamaduni wa mahali fulani ni sehemu ya Maisha yao, na hivyo ni Utakatifu wao. Kwa maana hiyo, tuwapo katika mazingira hayo ni kufanya kama alivyoambiwa Musa na Mungu, “Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu,” Kut 3:4-5. Yatupasa kuvivua viatu vyetu, ili kujua utakatifu wa mahali pale. Yatupana kuwa tayari kuona upya na watu wa mahali pale ili kujua ukweli halisi ya maisha yao. Uinjilishaji wetu na umisionari kwa ujumla wake unapokosa dhana hii ya kuona upya yale tunayokutana nayo, ukiambatana na  upole wa kujifunza, mwisho wa siku tunaishia kutokuwaelewa watu husika na kuwa na sintofahamu kubwa. Mtihani huu Mtume Paulo anaufaulu vizuri, na matokea yake ni kwamba, Makanisa yakatiwa nguvu katika ile Imani, hesabu yao ikaongezeka kila siku,” Mdo 16:5. Ukiona kila unayekutana naye anakukimbia ujue kunatatizo kubwa katika mahusiano yako na wale unaokutana nao. Kabla ya kumtafuta mchawi, zama kwanza ndani yako na jipekue vizuri namna yako ya kufanya mambo, na namna ya kufikisha kwao kile ulichotarajia-ujumbe.

Wakati mwingine yawezekana kabisa ukakumbana na pingamizi kubwa kutokana na mazoea yao ambayo yamekuwa sehemu ya tabia yao. Unapotenda jambo jema kwa watu na mapokeo yao yakawa mabaya, wala usikate tamaa. Tumia njia njingine ili ujumbe ule ule uwafike vyema. Na zaidi ya hayo Yesu anatuimarisha kwa kutupa moyo na kusema, Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi,” Yoh 15:18. Kama ulimwengu huo ulishamchukia yule kwa wakati huu unayemtumikia, hakika huyo huyo ndiye atakaye kupa njia na namna ya kufanya pale ukutanapo na mkwamo. Yesu anasema hivi kuhusu hali hii mara inapotoka: Na watakapowachukua ninyi, na kuwasaliti, msitafakari kwanza mtakayosema, lakini lo lote mtakalopewa saa ile, lisemeni; kwa maana si ninyi msemao, bali ni Roho Mtakatifu,” Mk 13:11. Kwa vile ujumbe uusemao na kuusimamia si wetu binafsi, kwa wakati huo Roho Mtakatifu atatusaidia kuyasema yale yatupasaya kuyasema kwa sifa na utukufu wa Mungu.

Ukweli ni kwamba yeyote anayekuwa ndani na katika Kristo, ujitenga na mwelekeo na mtazama wa yale tunayoyaishi na kukutana nayo kila siku. Mtu huyu huyaona mambo yote katika mtazamo mwingine. Unapokuwa na maisha yenye malengo, na hasa maisha katika ufuasi wa Kristo, utayaona yote katika umilele. Kukiona kitu katika umilele wake, ukweli huu hupingana na dhana ya leo na sasa. Tupo katika ulimwengu wa ‘ponda mali kifo chaja.’ Hivyo Yesu Kristo anatuambia kuhusu ukweli huu, kwamba,  “Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia,” Yoh 15:19. Hufanyapo kila kitu na kupigiwa makofu, jaribu kuchunguza makofi hayo. Wakati mwingine makofi hayo huashiria kejeri.

Mwisho tuwe tayari kutendwa vibaya kama Kristo alivyotendwa kwa sababu watesi hawa hawamjua yule aliyempeleka Kristo. Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka,” Yoh 15:21. Tusisahau pia matatizo na magumu katika utume wetu, yanatufanya kukua na kukomaa kiroho.

Tumsifu Yesu Kristo!

Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka,” Yoh 15:21


Tusali:-Ee Yesu, uliyeshinda uovu kwa wema, tujalie uvumilivu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario