IJUMAA WIKI YA 4 YA PASAKA
Somo:
Mdo 13:26-33
Zab:
2:6-7, 8-9, 10-11ab
Injili:
Yoh 14:1-6
Nukuu:
“kwetu sisi neno la
wokovu huu limepelekwa,” Mdo 13:26b
“Na ijapokuwa
hawakuona sababu ya kumfisha wakamwomba Pilato auawe,” Mdo 13:28
“Lakini
Mungu akamfufua katika wafu; akaonekana
siku nyingi na wale waliopanda naye kutoka Galilaya hata Yerusalemu, ambao sasa
ndio walio mashahidi wake mbele ya watu,” Mdo 13:30-31
“Na
sisi tunawahubiri habari njema ya ahadi ile waliyopewa mababa, ya kwamba Mungu amewatimizia watoto
wetu ahadi hiyo, kwa kumfufua Yesu; kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili,
Wewe ndiwe Mwanangu, mimi leo nimekuzaa,” Mdo 13:32-33
“Msifadhaike
mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi,” Yoh 14:1
“Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena
niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo,” Yoh 14:3
“Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu
haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6
TAFAKARI:
“Ili nilipo mimi, nanyi mwepo. Mimi ndimi njia na kweli, na uzima; mtu haji kwa
Baba ila kwa njia ya mimi.”
Wapendwa wana wa Mungu,
ingawa upo uwezekano wa mtu yeyote kuupata wokovu na kuifikia Mbingu kutokana
na msukumo wa maisha yake wenye kuongozwa na dhamiri yake njema na hofu ya
Mungu hata kama hakuwahi kusikia habari njema za Kristo Yesu, wewe na mimi
tuyeunganishwa na Kristo kwa Sakramenti ya Ubatizo, Kristo hubaki kuwa njia,
kweli, na uzima katika usahihi wake. Kwa wale ambao bado hawajafikiwa na habari
njema ya wokovu ila wanaishi kwa dhamiri zao njema, Kanisa kupitia Mamlaka yake
fundishi-Magisterium, linasema hivi juu ya wokovu wao; -Mafundisho ya Kanisa hasa tunaposoma Katekisimu ya Kanisa Katoliki,
namba 847 inafundisha juu ya dhamiri hai na safi ambapo hata wale wasiomjua
Kristo ndiyo ponya yao. Ukweli huu pia umefafanuliwa vizuri katika mafundisho
ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano, Konstitusio ya Kichungaji juu ya Kanisa katika
Ulimwengu wa leo, “Gaudium Et Spesteaches,” “Furaha na Matumaini,” inaelezea
ukweli huu kama ifuatavyo; “Jambo hilo
haliwahusu wakristo tu bali pia wanadamu wote wenye mapenzi mema, ambao neema
ya Mungu hufanya kazi mioyoni mwao, kwa namna isiyoonekana. Maana Kristo
alikufa kwa ajili ya watu wote na
wito halisi wa binadamu ndio mmoja, ule wa kimungu. Kwa hiyo lazima tuwe na
wazo kwamba Roho Mtakatifu anawajalia watu wote uwezekano wa kushiriki fumbo la
kipasaka, kwa jinsi anayoijua Mungu,” (no. 22)
Pamoja na ukweli huo,
ikiwa wewe na mimi tumeunganishwa na Kristo kwa Sakramenti ya Ubatizo na kuwa
warithi wa ufalme wa mbinguni, yatupasa kuishi ndani na katika Kristo. Hivyo ni
wajibu wangu leo na daima kumjua Kristo, kumpenda, kumtumikia–(kupitia wote
wale walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, Mwa 1:27), na mwisho ni Yeye tu
atakaye nihesabia haki mbele ya kiti chake cha uzima wa milele mbinguni. Masomo
yetu ya leo yamefafanua kwa undani kweli hii.
Wapendwa wana wa Mungu,
ikiwa wewe ni mfuasi wa Kristo na Mungu aliye hai, katika maana ya kuziishi
vyema na kwa uaminifu ahadi zako za ubatizo, yakupasa kuelewa ukweli huu juu ya
Kristo Yesu. Ukweli ni kwamba, bila Kristo hatuwezi kufanya lo lote, liwe dogo
au kubwa. Kama Kristo ni Mzabibu nasi tu matawi yake, twawezaje basi kushamiri
na kupata uhai pasipo shina lenyewe? Kitendawili hiki kinateguliwa na Kristo
mwenyewe. Naye anasema, “Mimi ni mzabibu;
ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana
pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote,” Yoh 15:5. Ndugu yangu na
Mbatizwa mwenzangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, kwa weledi wako na yote
uliyonayo, Je, waweza kutoboa mbingu bila Kristo Yesu? Na kama vile haitoshi,
Yesu anaenda mbali zaidi na kujifananisha yeye na Mlango. Ndugu yangu na
Mbatizwa mwenzangu, Kristo tu ndiye Mlango wa kufikia huo upande wa pili,
yaani, Mbingu. Naye Yesu anatuambia hivi, “Amin,
amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia
kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho,” Yoh 10:7, 9.
Upekee wa Kristo kama ndiyo Mlango sahihi umebebwa na maneno haya mazito ya Yesu.
Naye anasema hivi, “Wote walionitangulia ni wevi na wanyang'anyi; lakini kondoo
hawakuwasikia,” Yoh 10:8. Maana yake ni
kwamba, kama hapo-“wakati fulani” iliwezekana wachache kwa ujanja ujanja wao
kupita, au waliojitangazia na hata kujiinua kwamba wao ni “milango,” hawakuwa
sahihi, na hata leo kama wapo si milango au mlango sahihi. Habari Njema kwa
sasa ni kwamba Yeye mwenyewe-Yesu Kristo ndiyo HABARI NJEMA HIYO, na ndiyo
MLANGO SAHIHI na wa KWELI.
Kweli hii ndiyo anayoihubiri Paulo na
wenzake pasipo shaka yoyote wakimjua yule wanayemuhubiri na kumtumikia, yaani
Yesu Kristo. Ni kwa kumfahamu Kristo na kwa sababu yake tu, Mtume Paulo
anasema, “kwetu sisi neno la wokovu huu
limepelekwa,” Mdo 13:26b. Ni wazi kabisa tena pasipo shaka yoyote kama Wayahudi
wangalimfahamu vizuri Kristo wasingefanya waliyofanya. Hivyo ni jukumu la kila
mmoja wetu aliyepata neema ya kufikiwa na habari njema juu ya Kristo na mwokozi
wetu kuwa hai na shahidi wake. Ni katika ukweli wa jambo hili Paulo Mtume
anasisitiza, “Kwa
maana wakaao Yerusalemu, na wakuu wao, kwa kuwa hawakumjua yeye, wala maneno ya
manabii yanayosomwa kila sabato, wameyatimiza kwa kumhukumu,” Mdo 13:27. Hata
pale walipokosa sababu za msingi kuuondoa uhai wa mwenye haki-Yesu Kristo,
Wayahudi walitunga uongo mwingine na kulazimisha kifo chake. Hivyo, “ijapokuwa hawakuona sababu ya kumfisha
wakamwomba Pilato auawe,” Mdo 13:28.
Ndugu yangu, kutokuona
vizuri kwa wezwa sababishwa na matatizo ya macho na hata upofu nyemelezi, na
mwisho upofu wenyewe. Ila nachelea kusema kwamba upofu mbaya ni upofu wa
ufahamu, yaani, upofu wa kutokuona kitu kama kilivyo, na badala yake wakiona kitu kile kama ulivyo.
Hivyo kwa kufahamu udhaifu huu juu ya Wayahudi, Paulo anasema hivi juu ya
Kristo, “Lakini Mungu akamfufua
katika wafu; akaonekana siku
nyingi na wale waliopanda naye kutoka Galilaya hata Yerusalemu, ambao sasa ndio
walio mashahidi wake mbele ya watu,” Mdo 13:30-31. Ndugu yangu, huwezi kumfamu
Kristo na kufikiwa na habari njema hii ya wokovu ukaendelea kukaa kimya na
kuyafumbia macho yaliyo kinyume na wokovu huu aliotupatia Kristo Yesu kwa
gharama ya damu yake pale Msalabani.
Mimi na wewe yatupasa
kufanya kitu kwa ajili ya Kristo Yesu. Yapo mengi ya kufanya kwa ajili ya
Kristo, ila anza hapo hapo ulipo. Na swali elekezi ni hili; Ee Yesu na Mwakozi
wangu, kwa mazingira yangu na hali yangu naweza kukufanyia nini kwa ajili ya
watu wako? Yesu Kristo aliye hai atakuongoza na utamfanyia mengi mazuri. Anza
na yale madogo na yaliyo chini ya uwezo wako. Haya yaliyo madogo mara nyingi si
rahisi kuonekana na wengi, ila hubeba neema na baraka kubwa sana. Kwa upande
wake Mtume Paulo hakukaa kimya. Alifanya kitu kwa ajili ya Yesu. Na hapa anatoa
ushuhuda huo na kutuambia, “Na sisi
tunawahubiri habari njema ya ahadi ile waliyopewa mababa, ya kwamba Mungu amewatimizia watoto
wetu ahadi hiyo, kwa kumfufua Yesu; kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili,
Wewe ndiwe Mwanangu, mimi leo nimekuzaa,” Mdo 13:32-33
Hapana shaka yoyote
kwamba msukumo wa maisha ya Mtume Paulo ulipata msingi imara katika fundisho
hili la Mtume Petro, kwamba
“Wala hakuna wokovu katika
mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa
wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo-Yesu Kristo,” Mdo 4:12. Ufahamu huu
ndio, yaani, ‘Kristo ndiye kila kitu katika maisha yetu,’ ndio unaotupeleka
kuyafahamu maneno ya Yesu katika Injili ya leo. Naye Yesu anasema, “Mimi
ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh
14:6. Yesu Kristo ni njia kama ulivyo Mlango
pekee wa kuufikia uzima wa milele. Na njia aliyoichagua Yesu ni Msalaba. Kwa
kuibeba misalaba yetu na kuchukulia kindugu katika misalaba ya wenzetu kwa
uaminifu na hofu ya Mungu tunakutana naye Kristo katika hali na mazingira hayo.
Yesu Kristo ni kweli halisi. Kweli hii tunakutana nayo katika neno lake hasa
pale tunapokuwa tayari kulisikia neno, kulipokea neno, kulitafakari neno,
kulishirikisha neno, na mwisho kuwa shahidi wa neno.
Na Yesu Kristo ni
uzima halisi. Kristo ni uzima halisi tunaposhiriki Ekaristi Takatifu katika
mastahili yake. Yesu anatuambia, “Mimi
ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye
hataona kiu kamwe” Yoh 6:35. Ni katika kula chakula hiki-mwili na damu yake, Yesu anahaidi mambo mawili makuu: Moja, ni
ufufuko siku ya mwisho. Naye anasema, “Aulaye
mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya
mwisho,” Yoh 6:54. Na katika kula chakula hiki-mwili na damu yake, Kristo hukaa
ndani yetu. Naye anasema, “Aulaye mwili
wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake,” Yoh
6:56. Hata hivyo Mtume Paulo anatupa angalizo
la chakula hiki cha uzima. Naye anasema, “Basi
kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili,
atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana,” 1Kor 11:27. Yatupasa
kuijongea Meza ya Bwana tukiwa na mastahili ya kufanya hivyo-usafi wa mwili na
roho, yaani, pasipo hatia yoyote. Zaidi ya hapo ni kuikufuru Meza ya Bwana.
Wapendwa wana wa Mungu,
kwa kupitia Sakramenti ya kitubio tunapatanishwa tena na Kristo kutoka katika
hatia zote. “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu
zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu
kama bendera, zitakuwa kama sufu,” Isa 1:18. Hakuna sababu ya kufa moyo pale
ambapo mambo huenda ndivyo sivyo. Mungu aliye Upendo na Huruma uanza upya nasi
pale tunapokuwa tayari kufanya hivyo. Hivyo ndani na katika Kristo hakuna
sababu ya kuwa na hofu. Tumwamini Kristo na tuziamini kazi zake na hasa kupitia
Masakramenti yake. “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu,
niaminini na mimi,” Yoh 14:1.
Ndani na Katika
Kristo kunautulivu wa kweli, naye kesha tuandalia makao ya milele. Duniani hapa
ndugu yangu tunapita tu. Ulimwenguni hapa ni sehemu ya maandalizi ya huo
umilele. Mbinguni ndipo kwenye nafasi ya kila mmoja wetu, na ndiyo makao ya
milele. “Nyumbani mwa
Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda
kuwaandalia mahali,” Yoh 14:2. Lengo la Kristo ni kumpata kila mmoja wetu. Hili
ndilo pia lengo msingi la Kanisa. Lilipo Kanisa katika maana ya Mwili wa Kristo
nasi tukiwa viungo hai vyake, Kanisa huwa Sakramenti ya Wokovu kwa sababu
Kristo yu hai mahali hapo. “Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali,
nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo,” Yoh 14:3.
Ndungu yangu, je, hu kiungo hai cha mwili wa Kristo, yaani Kanisa?
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Msifadhaike
mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi,” Yoh 14:1
Tusali:-Ee Yesu Mwema
na Hai, nifanya kiungo hai cha mwili
wako, ili nisiwe sababu ya kupooza kwa Kanisa pale nilipo. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario