JUMAPILI
YA 5 YA PASAKA YA MWAKA-C
Somo
I: Mdo 14:21-27
Zab:
145:8-13
Somo
II: Ufu 21:1-5a
Injili:
Yoh 13:31-33a, 34-35
Nukuu:
“wakifanya imara roho za
wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia
katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi,” Mdo 14:22
“Na walipokwisha
kuwachagulia wazee katika kila kanisa, na kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka
katika mikono ya Bwana waliyemwamini,” Mdo 14:23
“Hata
walipofika wakalikutanisha kanisa, wakawaeleza mambo yote aliyoyafanya Mungu
pamoja nao, na ya kwamba amewafungulia Mataifa mlango wa imani,” Mdo 14:27
“Naye atafuta
kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala
kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha
kupita,” Ufu 21:4
“Na
yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa
mapya,” Ufu 21:5
“Enyi
watoto wadogo, bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi” Yoh 13:33
“Amri
mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo
hivyo,” Yoh 13:33, 34
“Hivyo
watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo
ninyi kwa ninyi,” Yoh 13:35
TAFAKARI: “Amri mpya nawapa, Mpendane. Naye
Mungu atafuta kila chozi katika macho yenu. Mlikutanishe Kanisa mara zote na
kuwaeleza mambo yote aliyoyafanya Mungu pamoja nanyi.”
Wapendwa
wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya tano ya Pasaka ya mwaka
“C” wa Kanisa. Dominika hii ya tano ya Pasaka, masomo yetu ya leo yanatutaka
kutafakari neno hili, “Amri mpya nawapa, Mpendane. Naye Mungu atafuta kila
chozi katika macho yenu. Mlikutanishe Kanisa mara zote na kuwaeleza mambo yote
aliyoyafanya Mungu pamoja nanyi.” Amri mpya kwa mfuasi wa Kristo na yeyote yule
mwenye hofu ya Mungu ni UPENDO. Na kama
hofu ya Mungu ni kutambua kwa kina yale yote yakuzungukayo kwamba yapo kama
yalivyo kwa sababu fulani, basi hakuna mwanadamu ye yote chini ya jua ambaye
hata wajibika kwa amri hii mpya.
Msisitizo
wa amri hii mpya-Upendo, Yesu anautoa katika saa yake ile ya mwisho, yaani muda
ule na mazingira yale halisi ya kujongea kifo kile Kitukufu na kilichobeba
simanzi kubwa la aibu kwetu sisi wanadamu kwa namna kilivyotendwa- kifo cha
Msalaba. Lakini huu ndio upendo mkubwa wa Mungu kwetu sisi wanadamu ambao ndiyo
sababu ya kifo chake kutokana na dhambi zetu. “Hakuna
aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki
zake,” Yoh 15:13. Na hili ndilo fumbo lililotanda mazingira na kifo cha yule
mwenye haki-Yesu Kristo na mwokozi wetu.
Hivyo ndugu yangu tunayesafiri sote
katika tafakari hii, saa hii ambayo Bwana wetu Yesu Kristo anatoa agizo hili zito
na muhimu la amri mpya, ni ukamilifu wa Yesu kama Mwana wa Mungu, aliyekuja
kuufunua upendo wa Mungu, na upendo binafsi kwa watu wake. “Kwa maana jinsi hii
Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye
asipotee, bali awe na uzima wa milele,” Yoh 3:16. Ni kwa mtazamo huu, kifo cha
Kristo kinawajengea uhusiano mpya wanafunzi wa Yesu, na Wewe na Mimi leo. Kifo
hiki kinatupa uwepo wa wazi na ule wa kujificha-(fumbo) wa Mungu. Upendo huu
ndiyo dira yetu na utambulisho wetu kama Wakristo na Wafuasi hai wa Kristo hadi
mwisho wa nyakati. “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa
wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi,” Yoh 13:35. Upendo huu kwa
namna ya pekee, uwe dira ya maisha yako na utambulisho wako kila siku kadiri ya
agano lako na Mungu (Mwenye hofu ya Mungu, Mlei, Mtawa, au Mtawa na Mkleri).
Upendo
huu una gharama zake. Yesu kwa kutupenda upeo, kilele chake kilikuwa kifo cha
Msalaba. Ndugu yangu, unaweza kutoa bila kupenda, ila hauwezi kupenda bila
kutoa. Kwa kutupenda upeo, Yesu anayatoa maisha yake kwa ajili yako na yangu. “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda
ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo,” Yoh 13:33, 34. Gharama ya kwanza kufa kifo
Upendo ni kuwa tayari kujinyenyekesha. Unyenyekevu ni msingi wa fadhila zote.
Unyenyekevu si ujinga pale ufanyapo kitu hicho kukiwa na sababu za kufanya
hivyo, na kama kadiri ya ufahamu wako
kuna ukinzani kati ya tendo lile na sababu ya kufanya hivyo, tazama mafaa
mapana ya kile kitarawajiwacho kwa wakati ule na ujao. Hali hii ilimkuta Yesu
pale Bustanini Gestemani kama Mungu na Mwanadamu. “Mwenyewe akajitenga
nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi
yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke,”
Lk 22:41-42. Licha kuna uwezekana wa mtu kufa kwa ajili ya mwingine na katika
hali ya upendo wa mashaka, ila pale tendo hilo linapoongozwa na unyenyekevu
kama nilivyosema hapo awali, tendo hilo ubeba maana mpya hata kama kibinadamu
kujongea au kukabiliana na jambo hilo huleta maumivu makubwa. Maumivu hayo
ukoleza upendo uliopo ndani ya mtenda tendo, na mwisho maumivu hayo huwa furaha
kwa sababu hutoa maana mpya ya teso katika tendo lile. Jambo hili pia linawatokea Mtume Petro na
wenzake pale Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, Mdo
5:35, alipotoa ushauri kwenye baraza la Kiyahudi juu ya kukamatwa kwa Mitume
isije wakawa wanapigana na Mungu. “Wakakubali
maneno yake; nao walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina
lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao. Nao
wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili
kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo,” Mdo 5:40-41. Hivyo ndugu yangu, sababu ya
teso huwa furaha na kikolezo cha kusonga mbele licha ya magumu katika njia
hiyo. Kristo Yesu ndiye sababu ya mateso na kuaibishwa wa Mitume. Kama Kristo
alikubali kufa kifo cha aibu na mateso pale Msalabani, mateso yangu na yako ni
kitu gani katika kweli hii? Je, naweza kuyalinganisha na mateso yale
aliyoyakabili Yesu kwa upendo mkubwa pale Msalabani? Ninapoutazama Msalaba
Mtakatifu, iwe nafasi pia ya kutazama changamoto za mateso ninayokutana nayo
kila siku.
Gharama
ya pili ya kufa kifo Upendo ni kutii. Utii pia siyo ujinga ufanyapo utii huo
kwa sababu, na mafaa mapana ya kile unachotii. Utii ni bora kuliko sadaka. Utii
ni fadhili kubwa mbele ya Mungu. Utii ni kujua kwa upana kile ukifanyacho.
Nabii Hosea anasema, “Maana nataka fadhili
wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa,” Hos 6:6. Kufa
kifo Upendo kwa kutii ni gharama kubwa sana kwa sababu unapingana na kwenda
kinyume kabisa na takwa la ufahamu wako-“will.” Hivyo ni vyema nifahamu tena
kwa hofu kubwa kwamba ni kwa ajili yako na yangu kama tulivyo (katika udhaifu
wetu), Kristo Yesu anakuwa mtii hadi kifo cha Msalaba ili wewe na mimi tuwe
huru kutoka minyororo ya dhambi. “Iweni
na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; tena, alipoonekana ana umbo kama
mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba,” Flp
2:5, 8. Ndugu yangu, ni mara ngapi umeziacha neema na baraka pale uliposhindwa kufa-kifo upendo kwa
kutii? Kwa tendo hili la kufa-kifo upendo kwa kutii, Yesu anainuliwa na
kutukuzwa na Baba yake wa Mbinguni kwa haya: “Kwa
hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti
lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU
KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba,” Flp 2:9-11
Wapendwa wana wa Mungu,
kwa kujitoa nafsi yako kwa kuishi vyema na kwa uaminifu agano lako katika maisha
u mtumwa wake Kristo, na kwa njia hiyo u mtumishi wa Kristo katika haki na
kweli aliyoifia pale msalabani. Mtume Paulo anaamsha dhamiri zetu kwa kuhoji na
kusema, “Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye
mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule
mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa
utii uletao haki,” Rum 6:16. Kumbe kama mimi ni Baba katika familia yanipasa
kila siku nijitahidi kupungua (kufa kifo-utii) ili mke na watoto wangu waongeze
kiufahamu na kimaadili katika hofu ya Mungu. Vile vile kama mimi ni Mama katika
familia yanipasa kupungua (kufa kifo-utii) ili mme wangu na watoto wangu
waongezeke kiufahamu na kimaadili katika hofu ya Mungu. Na kama mimi ni mtoto
katika familia yanipasa kupungua (kufa kifo-utii) ili familia yangu (mimi,
ndugu zangu na wazazi wangu) waongezeke kiufahamu na kimaadili katika hofu ya
Mungu. Na kama mimi ni (Mtawa, Mtawa na Mkleri, na Mkleri) yanipasa kupungua
(kufa kifo-utii) ili jumuiya yangu, utume wangu, na wale wote niliopewa dhamana
waongezeke kiufahamu, kimaadili, na kujawa hofu ya Mungu pale nilipo. Kupungua
huku ni ile hali ya kujali na kuwajibika ipasavyo.
Kifo upendo katika utii
hutupa nguvu kushinda majaribu hasa pale tunapoishi katika Kristo, ndani ya
Kristo, na kwa ajili ya Kristo tukishirikishana wote na vyote kwa ukarimu yale
tuliojaliwa na Mungu. Hivyo, “kwa kuwa
mkijaribiwa kwa utumishi huo, wanamtukuza Mungu kwa ajili ya utii wenu katika
kuikiri Injili ya Kristo, na kwa ajili ya ukarimu wenu mliowashirikisha wao na
watu wote,” 2Kor 9:13. Ukarimu huu ni kielelezo cha kufa kifo-Upendo katika ufukara. Ufukara ni ile hali ya kuwa
na furaha kwa kuwa na machache katika maisha yako huku ukiwajali wengine. Baada
ya Yohana Mbatizaji kutangaza ule ubatizo wa toba, makutano walimjia na
kumuuliza katika hali ile waliyo kuwa nayo wafanye nini? “Akawajibu akiwaambia, Mwenye kanzu mbili na ampe
asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo,” Lk 3:11. Ufukara huu unalenga kujinyima kwa
ajili ya wengine, na kuwa na furaha kwa tendo hilo. Hili ndilo agizo pia ya
Yesu kwa wanafunzi wake (Thenashara) anapowatumwa kutangaza ufalme wa Mungu, na
kupoza wangonjwa. “Akawaambia, Msichukue kitu kwa safari yenu,
fimbo, wala mkoba, wala mkate, wala fedha, wala mmoja wenu asiwe na kanzu
mbili,” Lk 9:3. Ndugu yangu, kadiri ya uchache wa vitu unavyokuwa navyo ndivyo
kwa namna hiyo unakuwa na muda wa kutosha wa utulivu wa ndani. Bila kuwa na
utulivu wa ndani mambo mengi katika maisha yako hayawezi kwenda sawa, hasa
katika swala la kufanya maamuzi ya kina katika maisha-“fundamental decisions in
your life.”
Mwono
huu wa maisha katika maana nzima ya upendo na kufa kifo upendo (unyenyekevu,
utii, na ufukara), ulikuwa msingi imara wa jumuiya ya kwanza ya Wakristo.
Mateso waliyoyapata yakiambatana na dhuluma ha hujuma kwa kuteswa na hata kuuwa
kwa wafuasi wa kwanza wa Kristo, tendo hilo lilikuwa na kubeba tafsiri halisi
ya ‘mlango wa kuingia katika Ufalme wa Mungu.’ Mtume Paulo anawapa moyo jumuiya
ya Filipi kutokana na nguvu ya kusimama imara katika roho moja, kwa moyo mmoja wakishindania imani
ya Injili, na kusema, “wala
hamwaogopi adui zenu, katika neno lo lote; kwao hao ni ishara mathubuti ya
kupotea, bali kwenu ninyi ni ishara ya wokovu, huo utokao kwa Mungu. Maana
mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake; mkiwa
na mashindano yale yale mliyoyaona kwangu, na kusikia kwamba ninayo hata sasa,”
Flp 1:28-30. Kwa vyovyote vile jumuiya hii ya kwanza ya Wakristo ilikuwa na mshikamano
wa kweli.
Umoja
na mshikamano wao (katika kweli, haki, na upendo) ndiyo pona yao. Na umoja na
mshikamano wetu leo Kanisa katika kweli, haki na upendo ndiyo pona yetu. Dhambi
ya usaliti waliepukana nayo kwa maneno na matendo. “Kama
tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana
sisi,” 2Tim 2:12. Jumuiya hii kwa kuishi mshikamano na umoja huu, waliutazama
umilele na faida zake kuliko haya ya leo na kesho. “Maana
mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile
ahadi,” Ebr 10:36. Saburi na utulivu wa
jumuiya kwa kiasi kikubwa ulitegema uongozi ule uliowekwa na Kanisa-jumuiya mahalia
na kusimikwa na Mitume, ambao uongozi huu haukutegemea maslahi binafsi bali
hitaji la jumuiya husika. Viongozi hawa walikuwa wazee walioaminika na wenye
hofu ya Mungu. Wote waliochaguliwa waliwakabidhi kwa nguvu ya Roho Mtakatifu
kwa kuwawekea mikono “Na
walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila Kanisa, na kuomba pamoja na
kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana waliyemwamini,” Mdo 14:23. Hata
safari ya kwanza ya kimisionari kwa watu wa mataifa ilikuwa ni msukumo ya Roho
Mtakatifu. Roho Mtakatifu aliwaongoza katika kila jambo. “Basi
hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema,
Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia,” Mdo 13:2.
Mafanikio
makubwa ya Jumuiya hii ya kwanza yalichochewa na maisha yao ya uwazi. Kila
jambo lilisemwa katika uwazi wake, na kwa namna hiyo walitoa shukrani zao kwa
Mungu kwa yote aliyowatendea. ‘Moyo usio na shukrani ukausha mema yote.’ Ni kwa
namna hii ya uwazi, “Hata walipofika
wakalikutanisha Kanisa, wakawaeleza mambo yote aliyoyafanya Mungu pamoja nao,
na ya kwamba amewafungulia Mataifa mlango wa imani,” Mdo 14:27. Jumuiya yoyote
ile inayoishi kwa kujitolea kwa watu wake hasa mambo ya maendeleo yahitaji uwazi.
Kadiri uwazi unavyojidhihirisha kwa watu, ndiyo kwa namna hiyo hiyo watu
hujitolea kwa nguvu na mali zao kwa hitaji la Kanisa mahalia. Hivyo, tunahitaji
uwazi katika matumizi na matapato katika jumuiya zetu ndogo ndogo za Kikristo,
Vigango vyetu, na Parokia. Tuliopewa dhamana na kuhesabiwa haki na Mama Kanisa
kwa usimamizi wa mali hizo za Kanisa mahalia, yatupasa kuwa waaminifu kwa kutoa
taarifa sahihi kwa yale tuyapatayo na namna tulivyoyatumia kwa wakati ufaao. La
sivyo mbele huko ni giza tupu. Tuelewe kwamba tu wakili na wazimamizi wa mambo
yote yale yampendezayo Mungu.
Namna hii ya utendaji
ndiyo njia sahihi ndani na katika Kristo, na kupata ushindi dhidi ya uovu na
maovu. Hii ndiyo Yerusalemu Mpya. “Maana,
tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza
hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni,” Isa 65:17. Kutenda kwetu
kunakosababisha ulimwenguni hapa kuwe sahemu salama ya kuishi ndiyo baraka na
neema tuzipataza. Tendo hilo pia huufunua Uzuri na Utukufu wa Mungu. “Kama vile mbingu mpya na nchi mpya, nitakazofanya,
zitakavyokaa mbele zangu, asema Bwana, ndivyo uzao wenu na jina lenu
litakavyokaa,” Isa 66:22. Mungu kamwe hawezi kutuacha tukaangamia katika janga
lolote lile tunaposimama katika kweli, haki na upendo. Mungu hatoacha kuyafuta
machozi yetu tuyafanyapo yote kwa ajili yake na Utukufu wake. “Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala
mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo
tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita,” Ufu 21:4. Mungu ni ngome
imara kwa wale wote wanaomlilia na
kumwelekea. Na katika shida na mateso hayo kwa sababu ya kweli, haki na upendo,
hatutakosa faraja kutoka kwake. “Na
yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa
mapya,” Ufu 21:5. Ndugu yangu, tukiwa tumefika mwisho wa safari ya tafakari, bila
shaka umegundua ni kitu fulani si sawa sawa katika maisha yako. Linalowezekana
kufanyika leo lifanye na wala lisingoje kesho.
Wapendwa katika Kristo,
Frank Kisoli alijulikana sana kwa fani yake ya ufundi viatu, na zaidi
kurekebisa soli za viatu. Umaarufu huu ndio ulimpa jina lake la pili yaani, “Kisoli.”
Frank Kisoli alifahamika na kila mtu na marika tofauti kwa huduma hii ya
kurekebisa viatu. Alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kukaa muda mrefu kwenye
huduma hiyo ya kushona viatu, na hasa kurekebisha soli.
Pamoja na huduma hiyo,
alikuwa mcheshi sana na alipokeleka na wote. Mara mteja ajiapo viatu vyake humuuliza
swali hili, “wavitambua tena viatu vyako na visigino vyake? Huyu ndiye Frank
Kisoli mrekebishaji. Karibu sana.” Basi kwa maneno haya ilikuwa furaha sana kwa
wateja wake. Hivyo kila wakati huwezi kumkosa mtu kwenye kibaraza kile cha
nyumba yake. Kutokana na kazi hii, aliweza kujipatia mahitaji yake ya kila
siku, na kuwasomesha vizuri watoto wake.
Lakini jambo la ajabu
ni hili, licha ya mafanikio mengi aliyoyapata kuwa na nyumba nzuri, kuvaa
vizuri yeye na familia yake, watoto wake kusoma na kuwa na maisha mazuri, Frank
Kisoli hakuacha kazi yake ile. Siku moja mteja na rafiki yake alimuuliza, “hivi
kwa nini pamoja na maendeleo vyote uliyokuwa nayo kwa nini usiache kazi hii na
kufanya kazi nyingine zenye hadhi, au basi ufungue kiwanda kikubwa?” Frank
Kisoli alimjibu hivi, “kwa vile watu wanaendelea kuvaa viatu na siyo wote wenye
uwezo wa kununua viatu vipya kila mara, naona sitawatendea haki watu hao kama
nikiacha kazi hii. Najisikia furaha kuifanya licha ya changamoto zake kwa mfano
vipo viatu vingine huwa vinanuka sana,” wote (Frank Kisoli na rafiki yake) waliangua
kicheke! “Basi na iwe hivyo,” rafiki yake alimjibu.
Ndugu yangu, yapo mengi
ya kutafakari na kujifunza kutoka kwa Frank Kisoli. Ila haya ni dhahiri:
-Hakuna kazi yenye
heshima au isiyo na heshima. Jambo la msingi ni utayari wa hutuma ile uitowayo,
na furaha ile uipatayo kwa kile ukifanyacho. Je unawafikia wahitaji wako kila
mmoja na uzito wa shida yake ile katika huduma uitowayo? Kwa hili Frank Kisoli
alifanikiwa sana.
-Kwa vile tunaishi na
tunatembea hapa na pale, na kukutana na hili na lile ndiyo kwa namna hiyo
tunadondoka hapa na pale. Hali hii ni sawa na soli ya kiatu. Tunamwitaji Frank
Kisoli, yaani Sakramenti ya utapanisho. Hapa tunapatanishwa tena na Kristo na
kuwa wapya. Kumbuka swali la Frank Kisoli kwa mteja ajiaye viatu vyake, na jibu
alilolitoa kwa rafiki yake yule aliyemshauri kuacha kazi yake ya ushonaji na
viatu.
-Mama Kanisa kama
alivyo Frank Kisoli, ataendelea kufanya kazi yake kama Sakramenti ya Wokovu kwa
watu wote katika kweli, haki, na upendo akitambua kuwa familia yake ni familia
ya wakosefu (wadhambi) na watakatifu. Kazi hii ya wokovu watu Mama Kanisa
ataifanya hadi mwisho wa nyakati.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi
wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi,” Yoh 13:35
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, bila wewe hatuwezi kufanya lolote. Tujalie nguvu ya kuyafanya yote
ya kupendezayo na tukuone kwa wote tunao wahudumia kila mmoja wetu kadiri ya
wito na nafasi yake. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario