lunes, 4 de abril de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 2 YA PASAKA

JUMATANO YA WIKI YA 2 YA PASAKA
Somo: Mdo 5:17-26
Zab: 34:2-3, 4-5, 6-7, 8-9
Injili: Yoh 3:16-21
Nukuu:
Lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema, Enendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu,” Mdo 5:19-20

“Watu wale mliowaweka gerezani wako ndani ya hekalu, wamesimama wakiwafundisha watu,” Mdo 5:25

Ndipo yule jemadari akaenda pamoja na watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa maana waliogopa watu wasije wakawapiga kwa mawe,” Mdo 5:26 

Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele,” Yoh 3:16

Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu,” Yoh 3:18

Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu,” Yoh 3:21

TAFAKARI: “Kweli katika Kristo utuweka huru”

Wapendwa wana Mungu, leo tutafakari “kweli katika Krito utuweka huru.” Pamoja na upendo na umoja wa kindugu wa jumuiya ya kwanza ya Wakristo katika kuishi na kulinena neno la uzima, KWELI katika Kristo ilikuwa moja ya nguzo muhimu sana kwa kutoa na kusimania ushuhuda mbele za watesi wao. Kweli hii juu ya Kristo iliwagharimu sana, lakini mwisho wa siku iliwafanya wawe huru. Jumuiya hii ya Wakristo wa kwanza haikuogopa vitisho na mateso kutoka kwa watesi wao.

Walilisema lililo kweli na kukubali kuteswa kwa ajili kweli hiyo. Hawakuogopa magereza na hata kudhalilishwa kwa sababu ya Kristo. Na hivyo Mungu akuwaacha katika mateso yao. Waliposwekwa magerezani kwa ajili ya kweli, Mungu alituma malaika zake na kuwaweka huru. “Lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema, Enendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu,” Mdo 5:19-20. Neno la uzima lilihubiriwa licha ya mateso na vitisho. Je, hali ikoje leo mfano, Jumuiya zetu Ndogo ndogo za Kikristo-JNNK? Tupo tayari kusimama kwa lililo kweli?

Mara nyingi tunashuhudia muundo wa “jumuiya za wasio na usawa”-“communities of unequals.” Tunajilazimu kuwepo kwenye jumuiya ili mradi sheria inasema hivyo. Wale wasio na fursa nzuri kiuchumi hata wakitoa wazo kwenye jumuiya huwa vigumu kupokelewa na kuaminika. Mtazamo huu wakati mwingine haukomi tu kwenye jumuiya ndogondogo za Kikristo, bali hujitokeza hata kwenye jumuiya zetu za Kitawa. Historia mbaya na jeografia ya mtu atokako huwa kipimo cha kumuhukumu hata kama wazo lake kwa wakati ule ni wazo ya kujenga. Wazo hili hukataliwa kwa vile tu wakati fulani au kipindi fulani mtu huyu alikuwa na maisha fulani ambayo hayakuwa na mwelekeo mzuri kwa mtindo wa maisha ya jumuiya husika.

Jambo hili katika jumuiya huwagawa wanajumuiya na kuwafanya wengine kama wageni na wasafiri tu wasiojua siku maalumu ya safari yao kwa muda wote. Mchango wao hauna nafasi, na kweli yao haina maana tena. Hii ni saratani mbaya kabisa kwenye jumuiya yeyote ile ya Wakristo. Mwisho wa siku jumuiya hii haiwezi kutoa ushuhuda mbele za watu kwa sababu ndani ya jumuiya hii hakuna kweli yeyote. Jumuiya hizi hubakia tu kama vikundi vya waigizaji fulani wa mtindo wa maisha wasiyoyajua bado. Jumuiya ya kwanza ya wakristo kwa kusimama na kushuhudia kweli iliyo ndani yao waliweza kufundisha kweli hiyo kwa wengine hata pale walipokuwa wamedhulumiwa kama jumuiya kwa sababu walikuwa kitu kimoja katika umoja na Kristo. “Watu wale mliowaweka gerezani wako ndani ya hekalu, wamesimama wakiwafundisha watu,” Mdo 5:25. Mtindo huu wa maisha uliwatia hofu hata watesi wao kwa sababu kweli iliyo ndani yao ilionekana wazi kwa watesi wao. Hivyo kweli hii iliwaweka huru. Ndipo yule jemadari akaenda pamoja na watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa maana waliogopa watu wasije wakawapiga kwa mawe,” Mdo 5:26.

Hatuwezi kusimama katika kweli ndani ya Kristo kama hatumwamini Kristo. Na hatuwezi kumwamini Kristo kama tunamuishi Kristo wa Historia. Yesu Kristo katika maisha yetu na ufuasi wetu kwake ni Kristo aliye hai. Ni kristo tunayekutana naye kila siku ya maisha yetu. Ni Kristo tunayekutana naye katika mateso yetu na furaha yetu. Mateso na furaha kwa Mkristo yanamaana tu pale Kristo anapokuwa kielelezo cha mambo yote. Na hii ndiyo sababu ya Mungu kumtoa Mwanaye katika historia nzima ya wokovu wetu. Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele,” Yoh 3:16.

Wapendwa wana wa Mungu, Imani yetu juu ya Mwana wa Mungu ndiyo hukumu yetu. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu,” Yoh 3:18. Kuamini huku si kwa yale tu tuyapendayo kuyaona na kuyasikia katika maisha yetu, bali ni kuamini hata yale ambaye yapo juu ya uwezo wetu na mara nyingine hatuyaoni kwa uwezo wetu wa kibinadamu. Ni kuamini pia yote yawezekana kwa njia yake na kwa uwezo wake. Huku ndiko kuliamini jina pekee la Mwana wa Mungu. Jina hili lina mamlaka juu ya umilele wako na mimi. Kuamini huku huendana na kutenda kweli kadiri ya imani juu ya Kristo, Maandiko Matakatifu, Kanisa na Mapokea yake. Huwezi kuamini mtu fulani na kutenda kinyume cha imani iliyojenga juu ya mtu yule. Tunapofanya kinyume na imani ile ni wazi kwamba hatujui tunachoamini. Ni sawa na kuvaa miwani ya giza kuelekea usipokujua ili hali unaitaji mwanga. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu,” Yoh 3:21.

Ndugu yangu tuliyesafari sote katika tafakari hii, jambo muhimu la kujihoji ni hili; je, ninachoamini juu ya Kristo, ndicho ninachokiishi? Je, bado najisemea moyoni ‘yawezekana ila sina uhakika?’

Tumsifu Yesu Kristo!

Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu,” Yoh 3:21


Ee Yesu uliyetupenda upeo, tuwezeshe kuishi kweli yako ili  tuwe huru. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario