sábado, 9 de abril de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 3 YA PASAKA

JUMATATU WIKI YA 3 YA PASAKA
Somo: Mdo 6:8-15
Zab: 119:23-24, 26-27, 29-30
Injili: Yoh 6:22-29
Nukuu:
Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati;  maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa,” Mdo 6:13-14

Watu wote walioketi katika ile baraza wakamkazia macho yao, wakamwona uso wake kuwa kama uso wa malaika,” Mdo 6:15

Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba,” Yoh 6:26

Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu,” Yoh 6:27

Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye,” Yoh 6:29

TAFAKARI: “Mwenye haki ataishi Milele, kazi ya Mungu, ni kumwamini Kristo mwana wa Mungu.”

Wapendwa wana wa Mungu, masomo yetu la leo yanatualika kutafakari neno hili, “mwenye haki ataishi Milele, kazi ya Mungu, ni kumwamini Kristo mwana wa Mungu.” Stefano anakuwa shahidi wa kwanza anaposimama katika kweli na kuishi. Akiwa mtu aliyenena na kuongozwa na Roho Mtakatifu, Shahidi Stefano anajikuta katika mzozo mkubwa na Wayahudi ambao hawakupenda, kusikia, wala kusadiki mambo yote aliyoyafanya Yesu Kristo. Stefano anaundiwa genge na zogo na mwisho kutungiwa uongo ili kumwangamiza. Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati;  maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa,” Mdo 6:13-14

Stefano shahidi anakuwa mbegu ya kwanza ya Imani kuoteshwa katika jumuiya ya kwanza ya Wakristo. Watu wenye mtazamo wa Stefano katika jumuiya ya Wakristo hata sasa wapo. Unapojaribu kusimama katika kweli, na kuishi ujiandae kusongwa na mambo mengi. Kwanza utatungiwa majina ya ajabu ili tu ukatishwe tamaa. Utatungiwa uongo mwingi tu, ili uchafuliwe na Kristo achafuliwe. Unapomkiri Kristo katika kweli na haki, unatangaza vita dhidi ya giza. Je, katika hali hii nini cha kufanya? Kamwe usiache kusimama katika kweli na kunena lililo kweli hata ikikubidi kufa. Stefano shahidi hakuacha kulisema lililo kweli na hata kulisimamia. Jibu katika kweli hii inaonekana hata kabla hajakijongea kifo kile cha kupigwa mawe hadi kufa. Watu wote walioketi katika ile baraza wakamkazia macho yao, wakamwona uso wake kuwa kama uso wa malaika,” Mdo 6:15

Ndugu yangu, Kristo pekee ndiye mwenye kutuhesabia haki katika vita hivi vya mwanga dhidi ya giza. Ni katika Kristo, na ndani ya Kristo tunaweza kushinda vita hivi kwa sababu yeye kesha vishinda. Je, unamwamini Kristo? Wapo wengi waliokuwa wanamfuata Kristo ila kwa malengo ya hapa na sasa tu, wala siyo imani ya kweli. Wengi walipenda kumfuata Kristo kutokana na miujiza aliyokuwa akiifanya. Hivyo walikuwa watu wa mshangao tu, na matukio. Wengi walimfuata wakijua kwa uwepo wake utawahakikishia shibe. Mtazamo wa Kristo na watu hawa wa shibe, hauna tofauti ma mahusiano ya fisi na Simba. Fisi anamatumaini makuwa kuwa akiwa na Simba hawezi kukosa masalia ya mzoga.

Yesu Kristo analiona hili mapema na kuwakemea wale waliokuwa wanamtafuta na kumwulizia kwa shahuku. Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba,” Yoh 6:26. Swali ni kwamba, je, ukipata mahitaji yako yote ya kila siku, Kristo ana nafasi tena katika maisha yako? Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu,” Yoh 6:27
Wapendwa, tunaye Mtu mmoja tu anayeweza kutufunulia siri za mbinguni na uzima wa milele. Mtu huyu ni Kristo. Kujua siri za ufalme wa mbingini hatunabudi kumjua Kristo na kufuata matafundisho yake. Kristo ndiye mwenye mamlaka yote ya ufalme wa mbinguni. Ndiye aliyetiwa muhuri na Baba. Je, ni nini cha kufanya? Jambo la msingi kupita yote ni kumwamini Kristo. Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye,” Yoh 6:29. Ulimengu tunaoishi sasa, siyo kwamba tu watu hawamwamini Kristo, bali hawapendi kusikua habari zake.

Ni jukumu la kila Mbatizwa na hasa wale waliopewa mamlaka hayo kutoa katekesi ya kina kuhusu uhusiano nadharia kati ya maisha ya kila siku ya Mkristo na kile anachoamini. Mara nyingi, wanachohubiriwa watu hakigusi maisha yao. Kristo anabaki kuwa ni ukweli fulani unaoelea katika urefu fulani ambao hatuwezi kufika kwa urahisi. Kristo anakuwa si tena yule Emmanuel, yaani Mungu pamoja nasi. Mfanye Kristo kuwa Rafiki yako wa karibu, na anza kumuishi kuanzia hapo ulipo na hao uliokuwa nao. Kulifanya jambo hili kwa ukweli na kumwamini, ni kielelezo tosha cha uinjilishaji wako mpya hapo ulipo. Leo tunaitaji sana ushuhuda huu wa ukimya.

Tumsifu Yesu Kristo!

Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu,” Yoh 6:27


Ee Yesu Kristo, tujalie neema ya kuijua kweli yako na kuishi kweli hiyo katika maisha yetu ya kila siku. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario