viernes, 1 de abril de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 2 YA PASAKA MWAKA-C

JUMAPILI YA 2 YA PASAKA YA MWAKA-C
Somo I: Mdo 5:12-16
Zab: 118:2-4, 13-15, 22-23
Somo II: Ufu 1:9-11a, 12-13, 17-19
Injili: Yoh 20:19-31
Nukuu:
Na kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu,” Mdo 5:12a

hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao,” Mdo 5:15 

Nayo makutano ya watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa,” Mdo 5:16 

Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na subira ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu,” Ufu 1:9

Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu,” Ufu 1:17b-18

 “Akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu,” Yoh 20:19b

“akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana,” Yoh 20:20

“Akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa,” Yoh 20:22-23

“Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo,” Yoh 20:25

“Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye,” Yoh 20:27

Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu!” Yoh 20:28

“Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki,” Yoh 20:29

Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake,” Yoh 20:31

TAFAKARI: “Upendo wa kweli ndiyo msingi wa Ukristo wetu, ujidhihirisha tunapoishi ndani na katika Kristo na kuwa Mashahidi wake; na ndiyo njia pekee ya kuurithi Ufalme wa Mungu kila mmoja kadiri ya wito wake.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Jumapili ya Pili ya Pasaka ya mwaka “C” wa Kanisa. Mama Kanisa leo anapenda kutuongoza kwenye tafakari ya neno hili, “Upendo wa kweli ndiyo msingi wa Ukristo wetu, ujidhihirisha tunapoishi ndani na katika Kristo na kuwa mashahidi wake; na ndiyo njia pekee ya kuurithi Ufalme wa Mungu kila mmoja kadiri ya wito wake.” Mafanikio na maendeleo makubwa ya Imani katika jumuiya ya kwanza ya Wakristo yalijengeka katika msingi wa UPENDO KWA KWELI, WALIPOISHI NDANI NA KATIKA KRISTO. Tendo hili la upendo, Kristo akiwa kielelezo cha yote, uliwafanya wanajumuiya hawa wa kwanza kujitoa bila kujibakiza. “Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika,” Mdo 4:32

Ndugu yangu, hutoweza kuwa shahidi wa Kristo na neno lake kama haupo tayari kushirikisha wengine kweli ya Kristo iliyopo ndani yako. Kuishirikisha kweli ya Kristo ndani yako kwa wengine ni tokeo la kulitafakari neno la uzima kwa kina kila siku ya maisha yako. Hutoweza kusimama katika neno la Mungu kama hujalielewa na kuwa sehemu ya maisha yako. Kama neno hili ni uzima basi yanipasa kulisoma kila siku na kulitafakari ili liwe uzima ndani yangu. Ni vigumu pia kulitafakari neno la Mungu na kuwa sehemu ya uzima wako kama huwezi kulisikia.

Kulisikia neno la Mungu siyo tu kwa kupitia masikio yetu kama njia moja ya mlango wa fahamu, bali kulisikia kwa kila kiumbe alichokiumba Mungu, na zaidi kutoka mazingira yale unayoyaishi leo na sasa. Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko. Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya,” Lk 24:45-48. Neno “kuanza tangu Yerusalemu,” linaweza kutafsiriwa kuwa ni mazingira uliyopo na namna ile ulivyo kila mmoja kadiri ya wito wake. Kuwa shahidi wa neno hili la uzima yanipasa kuanzia pale nilipo. Neno hili lilete uzima ndani ya ndoa yako, maisha yako ya wakfu, na katika huduma unayoitoa watu. Hali hii ndiyo inayomkuta Mtume Petre; hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao,” Mdo 5:15 

Ni vigumu vile vile kusikia neno hili la uzima kama haupo tayari kulipokea. Kulipokea Neno la Uzima kamwe lisiwe Neno kihistoria, yaani simulizi fulani kwangu na lenye kunipa taarifa ya mambo yaliyopita, bali Neno hilo lanihusu mimi leo na sasa na siyo mtu mwingine. Huku ndiko kulipokea Neno la Uzima kutakapo kupelekea kulisikia, kulitafakari, kulishirikisha, na mwisho kuwa shahidi na kufa shahidi. Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na subira ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu,” Ufu 1:9. Na huu ndio ushuhuda wa Neno lililo hai. Ushuhuda huu wa Neno la Uzima ndio tunaoambiwa kwamba, Na kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu,” Mdo 5:12a.

Wapendwa katika Kristo, ushuhuda wa Neno la Uzima ulipelekea kujali na kutaabikiana kwa upendo wa kweli kwa jumuiya ya kwanza ya Wakristo, na kuliweza kutatua matatizo mengi makubwa. Hakuna miongoni mwao aliyeitaji akakosa mahitaji yake. Mt. Augustino ambaye alichukua kielelezo hiki cha maisha ya jumuiya ya kwanza ya Wakristo, na kufanya ndicho msingi wa jumuiya ya Kiagustino, anasema “UKIPENDA UTAFANYA YOTE.” Ni kwa msingi huu na upendo huu wa kweli, “wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa,” Mdo 4:34. Jambo la kushangaza leo katika familia zetu, licha ya wanafamilia, yaani Baba na Mama kuunganishwa kwa Sakramenti ya ndoa, wamekuwa wabinafsi kiasi kwamba kila mmoja wao hujifanyia mambo yake bila kumshirikisha mwenzake.

Tatizo kubwa hapa lipo kwa akina Baba. Utaona kila mmoja wao anasema hiki ni changu. Wakati mwingine Baba huwa na viwanja na hata biashara kubwa ambazo mkewe hajui lolote. Mwisho wa siku kinapotokea kifo kwa upande wa Baba, mali yote hupotea na familia kubaki umasikini uliokithiri. Hivi nyie akina Baba, inawezekanaje kumwamini rafiki wako wa kufikia, kuliko kumwamini mkeo na wanafamilia yako? Marafiki hawa wa kufikia ndio wanaojua mikataba yote ya mali na biashara za Baba huyu wa familia. Tujirekebishe! Mkeo ni zaidi ya ndugu na marafiki. Huyu umeunganishwa naye na kuwa kitu kimoja. Unapoanza kumtenga unajipasua mwenyewe na mwisho wake hutobaki salama.

Ndugu zangu, tusipouishi kweli hii hasa katika ngazi ya familia, hakika bado hatujamjua Kristo. Katika kitabu cha ufunuo tunaona namna Yesu anavyojifunua kwa Mtume Yohane kwa njia ya maona na kusema, “Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu,” Ufu 1:17b-18. Mimi na wewe tusipo ijua kweli hii tu bado katika giza, na tunaishi maisha ya kuigiza kwa miaka yote, kila mmoja  kadiri ya wito wake. Kila mtu aaminiye kwamba Yesu ni Kristo amezaliwa na Mungu. Na kila mtu ampendaye mwenye kuzaa, ampenda hata yeye aliyezaliwa na yeye,” 1Yoh 5:1. Upendo wa kweli ndiyo amri kuu kwa kila aliyebatizwa na kumwamini Kristo. Kwa yeyote anayejiita Mkristo na anayejitambua kuwa ni Mkristo, hakuna mbadala dhidi ya kupenda kuliko kwa kweli. Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito,” 1Yoh 5:3. Ukipenda kweli, utafanya yote kama asemavyo Mt. Augustino. Wepesi wa amri yeyote ni upendo katika agizo hilo na kwa kutimiza matakwa ya hiyo amri. Jumuiya ya kwanza ya Wakristo inaishi pendo la kweli na kuwa kivutio cha kweli katika huduma na huruma ya Mungu. Na ndivyo ilivyokuwa kwamba, Nayo makutano ya watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa,” Mdo 5:16 

Kupenda kuliko kweli ndiko kuzaliwa na Mungu, na kuushinda ulimwengu dhidi ya uovu. Silaha kubwa ya kuushinda ulimwengu huu dhidi ya uovu, ni kupenda kuliko kwa kweli. Wengi wetu ujikuta kufanya maovu kwa vile tu hawakuwahi kupendwa na mara zote hujisikia kusalitiwa na kuhuzunishwa. “Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu,” 1Yoh 5:4. Huu ndiyo msingi wa kila Mkristo mwenye Imani ya kweli.  Jambo hili la kutokupenda kutokana na majeraha na kuumizwa kwetu, linaonekana wazi katika Injili ya leo ambapo tunaona watu wawili (Yesu Kristo Mfufuka na Mtume Tomaso) waliojeruhiwa, ambao mwisho wa siku mmoja wao (Yesu Kristo Mfufuka) anamponya mjeruhiwa mwenzake (Tomaso).

Uponyaji wa kwanza anaoutoa Yesu Kristo kwa wanafunzi wake ni kuiondoa hofu kwa salamu yake ya upendo, “Akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu,” Yoh 20:19b. Tendo hili la kuwa na Amani ya kweli ndiyo mwanzo wa kuanza kupenda kuliko kwa kweli na furaha ya kweli. Wanafunzi wa Yesu wanaonyesha furaha hii, na kuanza kupenda tena, ingawa Mtume Tomaso hawakuwepo katika kundi. Naye Yesu baada ya salamu ya upendo iliyojaa matumaini mapya, “akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana,” Yoh 20:20. Furaha hii inaendana na maagizo ya kufanya anayoyatoa Kristo kwa wanafunzi wake. Naye Kristo akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa,” Yoh 20:22-23. Kristo hapendi furaha ya kweli aliyotupatia tubaki nayo wenyewe. Hivyo furaha hii twapasa kuisambaza kwa wengine kila mmoja kadiri ya wito wake, vipaji vyake, dhamana na nafasi yake katika jamii anayoishi. Ndugu yangu ukiona hapo unapoishi hata mbwa wanakukimbia bila sababu, ujue wewe ni shiiiiida!

 Tomaso aliporejea anakokujua mwenyewe kwa kupoteza imani yake juu ya Kristo, anapoambiwa jambo hili la kuonekana kwa Kristo, hakuamini hata kidogo. Naye kwa ufahamu wake anatoa vigezo vya kutambua ukweli aliousikia kutoka kwa wenzake. Naye anatoa vigezo na masharti ambavyo lazima vizingatiwe. “Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo,” Yoh 20:25. Kwa masharti haya na vigezo hivi tunaweza kuona ni kwa jinsi gani Tomaso alivyo jeruhiwa na kusononeshwa kwa tukio la kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo.

Wapendwa, baada ya siku nane, tunaona tukio la kukutana kwa wajeruhiwa hawa wawili, yaani Yesu Kristo Mfufuka na Mtume Tomaso. Mjeruhiwa wa kwanza ni Yesu Kristo. Yesu anamkuta Tomaso na kumwonyesha majeraha yake, na kusema, “Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye,” Yoh 20:27. Tendo hili la Yesu kumwonyesha Tomaso majeraha yake na kuumizwa kwake kunatoa picha ya majivuno ya Yesu na wakati mwingine kama kujigamba vile. Jambo hili lina ukweli wake kwa mtazamo huu wa majeraha na makovu aliyokuwa nayo Yesu. Majereha ya Kristo na maumivu yake hayakuwa majeraha ya kushindwa, bali majeraha ya UPENDO WA KWELI. Majeraha ya Kristo yalikuwa majeraha ya USHINDI uliotukuka. Hayakuwa majeraha ya kuuma, bali majeraha ya UTUKUFU. Ni majeraha ya UPENDO. Upendo ambao upo tayari kujitoa sadaka bila kipimo na kutojibakiza. Kristo anaonyesha ubavu wake na mikono yake ilivyotobolewa si kwa kujionyesha au kuhukumu, bali kuonyesha uzito na undani wa upendo wake kwa Mitume na kwetu sote.

Japokuwa Tomaso hakuwa na majereha kwenye ngozi yake, na hakuwa na kuvuja damu kutoka mwilini mwake, majeraha yake yalikuwa ndani ya moyo wake. Haya ni maumivu ya ndani. Moyo wake ulijeruhiwa kwa kusikishwa na kifo cha Bwana wake. Alijisikia kudanganywa na Bwana wake Yesu Kristo. Alijisikia kushindwa baada ya kuyaweka matumaini yote kwa Kristo kwa sababu alifikiri Yesu Kristo ni Masiha, Mfalme, na kuhoji kwa nini Yesu afe kifo katili kama kila cha msalaba. Alifikiri Yesu Kristo angeikomboa Israeli kutoka kwenye dola ya Kirumi. Anajiuliza hivi, kwa nini hata yeye mwenye-Yesu ameshindwa kujinasua kutoka watesi wake? Mtume Tomaso alisikitishwa na kusijikia kusalitiwa na Yesu. Tomaso alishawishika kabisa kwamba alifanya uchaguzi usio sahihi kumfuata mseremala huyu wa Galilaya. Kwa kweli Tomaso alikuwa na maumivu makubwa sana.

Wapendwa maumivu na majeraha ya Moyo huchukua muda mrefu kupona. Majeraha haya na maumivu ya Moyo yanachukua kuda mrefu kupona kwa sababu twaweza kuyaficha na kujifanya hayapo. Twaweza kuongea na kutenda mambo yetu kama vile hakuna jambo lolote baya au upungufu wowote kwetu. Wengi wetu twaweza kukaa katika hali hii kwa miaka mingi kwa kujivisha taswira nyingine na mwonekano mwingine ambao sio uhalisia wa kile kilicho ndani mwetu ingawa tunaendelea na mateso na maumivu hayo. Lakini ukweli ni kwamba hatuwezi kudumu katika hali hii kwa muda wote na nyakati zote. Mara tutaanza kujisikia vibaya na kujisikitikia na kufikiri marafiki zetu wametutenga na wapo mbali bila kutusikiliza maumivu yetu yanayotusonga moyoni. Mara tunajisikia kwamba hawajali na wanaubaridi kuhusu maumivu yetu, na hivyo kuwachukia pia.

Hivyo, katika kukutana kwa wawili hawa hasa kipindi hiki cha pasaka, mmoja wao yaani Yesu Kristo ana majeraha ya UTUKUFU, na mwingine yaani Tomaso ana majereha ya maumivu ya ndani. Yesu Kristo alikuwa tayari kujiponya kwa nguvu ya majeraha yake. Tomaso alihitaji kuponywa majeraha yake lakini hapakuwa na mtu wa kumponya. Hapa ndipo wanapokutana wajeruhiwa hawa wawili. Mjeruhiwa wa kwanza anamponya wa pili. Uponyaji huu unajionyesha kwa maneno ya Tomaso mwenyewe anapomjibu Kristo baada ya Kristo kumtaka kuvitia vidole vyake kwenye makovu na majeraha yake, akisema, “Bwana wangu na Mungu wangu!” Yoh 20:28. Mwisho wa kukutana huku, kila mmoja anapata majeraha ya UTUKUFU, na kuwa tayari kuponya wengine wenye maumivu.

Wapo maelfu ya watu wameumizwa na kujeruhiwa miongoni mwetu. Wengine wanabeba chuki kwa usiri mkubwa ndani ya mioyo yao kwa kusalitiwa  kulikotokana na kutokuwa na uaminifu kwa wenzi wake wa ndoa. Wengine wanabeba chuki dhidi ya wanaofisi wenzao kwa kuwaenezea umbea na uongo mitaani. Wengine pia wanabeba ndani ya mioyo yao chuki na manung’unika kwa milongo ya miaka iliyopita kwa kukosa sehemu ya kuponyeshwa na kusikilizwa. Wengine maumivu haya wanayabeba tangu kuzaliwa kwao hadi sasa kutokana na namna ya kutungwa mimba kwao kuliko kataliwa na kwa bahati mbaya au nzuri akazaliwa. Wengine wamesalitiwa na wapenzi wao na kuyabeba hayo hadi sasa hata kama wanaishi maisha yao ya ndoa. Wapo wengi sana waliojeruhiwa na kuumizwa vibaya kwa namna tofauti tofauti. Jambo hili linaweza kutokea kwa yeyote yule, iwe mlei, mtawa na hata mtawa na mkleri.
Ndugu yangu, hata kama tutayaficha majereha na maumivu yetu, kwa binadamu itafika wakati lazima atayaonyesha tu wazi kwa kutafuta uponyaji. Ni njia mojawapo ya kurudisha mizania ya ndani katika uumbaji wetu. Ukweli ni kwamba walioumizwa kweli na kupata majeraha ya ndani hawawezi kuficha na kuvaa kinyago hicho kwa muda mrefu. Wanaweza kuwadanganya wanaowazunguka kwa wakati tu, ila hawawezi kujidanganya wenyewe na kuficha ukweli huu. Maumivu ya ndani ni vigumu sana kuyavumilia.

Watu hawa wanaitaji uponyaji. Wangepewa nafasi na uchaguzi, wote wangependa kugusa majeraha ya Kristo. Wanapenda kujua kwa uhakika kama kuna mtu anayewapenda vya kutosha kwa kujeruhiwa kwao na mtu huyo yupo tayari kufa kwa kuwapenda. Tatizo kubwa ni kwamba hawawezi kumwona tena Kristo. Wanaweza tu kuwaona watu wanaojiita Wakristo. Wakristo ambao wanajulikana kwa kujinadi kulibeba jina la Kristo na siyo kumuishi Kristo. Swali ni hili: Je wakristo hawa wapo kweli kama Kristo? Je, wakristo leo wameumizwa vya kutosha kwa UPENDO kiasi kwamba wanaweza kuwaponya walioumizwa? Je, ni kweli wakristo leo wamefufuka kutoka kifo cha kujijali wenyewe, na ubinafsi, kwamba wanaweza kuwa matumaini na kielelezo cha kuwarudisha waliopotea kwenye kundi kwa kuumizwa kwao?

Ndugu yangu, kuurithi ufalme wa Mungu, ni kuishi vyema wito wako na vipaji alivyo kupa Mungu. Vipaji hivyo siyo mali yako bali viwafaidie wengine, na hasa katika kuyaponyesha majeraha na maumivu waliyokuwa nayo. Hiki ndicho kielelezo cha maisha yetu kama Wakriso na wafuasi wa Kristo Mfufuka. Jambo hili si katika kuangamizana, bali katika ufaidiana na kuongozana katika umilele ambao ndiyo makusudi ya Ufalme wa Mungu.

Wapendwa ulimwengu wa leo unamwitaji sana Kristo. Kama ulimwengu usipomwona Kristo kwa Wakristo wa leo, waliojerehiwa watajitoa kwa Mungu, na kubeba mioyo yao inayovuja damu na vidondo visivyoponyeka kwingine kusipo Mungu. Na wanavyojitoa huku ufikia mahali na kuinamisha vichwa vyao na kufikiri katika akili zao: “Mungu amekufa!”

Ndugu wana wa Mungu, baada ya miaka mingi ya kufanya biashara bila mafanikio, Mungu alitaka kumwezesha mfanyabiasha mmoja alijulikana kwa jina la Songambele.

Alimwendea katika ndoto na kumwambia, “omba jambo lolote nalo nitakupatia. Na utakachokiomba nitampa mfanyabiashara wa jirani yako aliyeko upande wako wa kulia mara mbili zaidi. Kwa mfano, ukiomba uwe na mtaji wa milioni 20, nitakupa na mwenzako nitampa mara mbili yako yaani milioni 40.”

Mungu alimpa wiki moja Bwana Songambele kufikiria na kisha kumpatia jibu. Baada ya wiki moja, Mungu alimjia tena na kumwuliza, “je tayari umeshapata jibu? Songambeli alimjibu hivi, “baada ya kufikiria kwa undani na umakini mkubwa mimi naomba niwe chongo.”

Je, kama Songambele ameomba awe chongo yaani jicho moja tu lake liwe na uwezo wa kuona, mwenzake atakuwa nani?

Tumsifu Yesu Kristo!

Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu!” Yoh 20:28


Ee Yesu Mwema, tuponye majeraha na maumivu yetu ya ndani kwani ni wewe tu unayejua ukweli wake kwa majereha na maumivu yako. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario