miércoles, 6 de abril de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 2 YA PASAKA

IJUMAA WIKI YA 2 YA PASAKA

Somo: Mdo 5:34-42
Zab: 27:, 4, 13-14
Injili: Yoh 6:1-15
Nukuu:
Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akawaambia, Enyi waume wa Israeli, jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa,” Mdo 5:34a-35.

Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa, lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu,” Mdo 5:38-39 

“Nao walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao,” Mdo 5:40b

Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo,” Mdo 5:41 

Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo,” Mdo 5:42

Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa,” Yoh 6:2

Yesu akasema, Waketisheni watu. Basi watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao,” Yoh 6: 10a-10c

Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka,” Yoh 6:11

“Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote,” Yoh 6:12b

“Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni,” Yoh 6:14b 

“Akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake,” Yoh 6:15b

TAFAKARI: “Nguvu ya Maadili na Unyenyekevu hutuhesabia haki na kweli kama wafuasi wa Kristo. Mwono huu wa maisha utuweka karibu na Kristo nyakati zote.”

            Wapendwa wana Mungu, kwa pamoja tutafakari masomo ya leo na hasa nini maana ya nguvu ya kimaadili na unyenyekevu kwa kile tunachoishi kama wafuasi wa Kristo. Matokeo ya ukweli huu ndiyo ushuhuda wa kweli kwa jamii inayotuzunguka. Hapana shaka yoyote kwamba, jumuiya ya kwanza ya Wakristo walipata nguvu ya kulinena jina la Kristo, na hivyo kugeuka kuwa mwiba mkali kwa watesi wao, kutokana na nguvu yao kimaadili na unyenyekevu waliokuwa nao.

Mamlaka haya ya kimaadili hujijenga kwanza kabisa kwa KUJITAMBUA. Kujitambua huku ni pamoja na kujua nini shabaha ya kile unachokiishi, na malengo yake. Kwa upande mwingine ni kujua malengo ya maisha yako. Maisha ya aina yoyote ile huongozwa na malengo. Maisha yanapokuwa na malengo, maisha hayo huwa na mwono tofauti kabisa, kwani rasilimali muda hutumika vizuri. Maisha yasipoongozwa na malengo ni sawa na wingi wa miaka usio na maana.

Haina maana yoyote kujitapa kwa kuwa na miaka 50 au 90-(yaani kuishi kwa ‘bonus’), bila kutafakari umaana wa miaka hiyo na uhusiano wako na Mungu. Ni ukweli pia idadi ya miaka kwa Mungu haina maana. Umaana wa idadi ya miaka huja pale tu, unapoanza kujiuliza na kufanya tafiti moyo ya “ulichofanya na idadi hiyo ya miaka uliyopewa kama zawadi.”

Ndugu yangu tunaye safiri wote katika tafakari hii, ukishajitambua katika maana niliyokwisha isema hapo juu, hatua ya pili itakuvuta KUJISHUSHA. Na hii ndiyo maana halisi ya kujinyenyekesha kwa kile ulichodhani mwanzoni ulikuwa kumbe sivyo, ili uwe kile ulicho katika uhalisia wako na yale unayotaka kuyafanya ili ufikie malengo halisi ya maisha yako. Jambo hili kulifikia si hatua ya mara moja kama kulala na kuamka. Kinachotukwamisha mara nyingi ni pale tunapovaa kinyago “mask” kwa kuficha ukweli wetu halisi ambao mara nyingi hatupendi kuugusa wala kuuzungumzia popote pale. Hakuna filamu nzuri ya maisha zaidi ya maisha yako mwenyewe. Kuitazama filamu hii ni kujinyenyekesha kuliko kwa ndani kabisa. Ukiweza fanya hivyo, ni mwanzo wa safari ya maisha yenye malengo.

Mambo haya mawili muhimu; kujitambua na kujishusha ambayo matokeo yake ni kuwa na nguvu kimaadili na unyenyekevu. Hii ndiyo silaha pekee ya kumjua Kristo na maagizo yake kadiri ya mafundisho yake. Jambo hili ndiyo sababu ya kuogopwa kwa jumuiya ya kwanza ya wakristo na kuwafanya tofauti na waliowatangulia kama akina Theuda na Yuda Mgalilaya ambao walipata umaarufu na mara wakatoweka, Mdo 5:37-37.

Jambo hili kwa Kanisa la Mwanzo lilikuwa na faida kuu tatu; kwanza kabisa waliumega mkate-kwa kutambua mahitaji yao ya kila siku “basic needs.” Pili waliumega Mkate kama adhimisho la Ekaristi Takatifu-ikiwa ndicho kiungo pekee cha umoja wao kijumuiya. Yesu Kristo hapa alikuwa kiunganishi cha umoja huo hadi leo. Jumuiya yeyote ile ya Kikristo kwa mfumo wowote ule wa maisha bila Yesu wa Ekaristi kuwa kiungo cha maisha hayo, jumuiya hiyo hubakia kuwa kama kikundi cha waigizaji wasicho kijua wakiigizacho, Yoh 15:5. Na tatu waliumega mkate kwa kulisikiliza, kulifundisha, na kulinena neno la uzima, yaani Maandiko Matakatifu.

Wapendwa, ni katika maana hii tunaona mtu maarufu kama Gamalieli akisimama na kutoa angalizo kwa mafarisayo wenzake kuhusu dhuluma wanayoifanya dhidi ya wafuasi hawa wa Kristo. Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akawaambia, Enyi waume wa Israeli, jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa,” Mdo 5:34a-35. Mambo wayafanyayo Wakristo hawa msingi wake ni Kristo, na utendaji wake ni nguvu ya Kimaadili na Unyenyekevu.

Wakati mwingine tusipo lijua jambo hili, hubaki kupingana na nguvu tusiyoijua. Gamalieli anawakumbusha uwepo wa Mungu na uweza wake juu ya lililo haki. Kamwe hatuwezi kushinda dhidi ya haki ya Mungu. Vita hii na msuguano huu dhidi ya Mungu ni angamizo kubwa kwetu binafsi. Gamalieli anasema, basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa, lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu,” Mdo 5:38-39. Leo mimi binafsi najiuliza ‘nini sababu ya mfululizo wa ajili za magari katika Taifa letu, na majanga mengine ambayo kwa kiasi kikubwa ni huzini na majonzi katika jamii.’

Wapendwa, nina Imani pasipo shaka kwamba, yawezekana wakati fulani mahali fulani, na watu fulani hatukutenda iliyo haki. Ni ukweli pia katika jamii yetu, licha ya maovu mengi tunayotenda mbele za Mungu, jambo hili ni wazi kabisa hatujachukua hatua za utosha. Kumekuwepo na dhuluma za muda mrefu katika jamii yetu, na kubwa zaidi ni dhulumu dhidi ya uhai. Ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi-Maalbino wamekuwa wakiwindwa na kuuwa kama vile si binadamu na hawana haki ya kuishi. Vyombo vya usalama ikiwa ndala yenyewe, haijafanya vya kutosha kunusuru maisha haya ambayo ni zawadi ya Mungu kwa kila mwenye pumzi. Uhai ukiwa ndiyo uwepo wa Mungu mwenyewe, kuukatiza au kuuchukua bila mamlaka yake Mungu ni kupingana na Mungu mwenyewe. Je katika jambo hili tupo na tutakuwa salama?

Jambo lingine ambalo ni laana pia kwa taifa hili, ni kufumbia macho haki za wanyonge, na kuzipora haki hizo bila woga wowote. Leo usipojulikana na mbaya zaidi kama huna fedha, huwezi patiwa haki yako. Jambo hili limeshakuwa la kawaida kabisa hata pale unapotakiwa kupata haki zako za kijamii kadiri ya katiba, kama vile matibabu, elimu na mengineyo. Rushwa na Ufisadi ndiyo virusi hatari kabisa katika jamii yetu leo. Je, na hili tupo na bado tutakuwa salama? Ni Mungu gani amabaye hatajitokeza na kusimama katika uovu huu?

Wakristo wetu wa kwanza wanahesabiwa haki kwa nguvu yao ya kimaadili na unyenyekevu pale wapoishi yale wayasemayo na kuyashuhudia dhidi ya dhuluma ya watesi wao, na uovu wao juu ya mwenye haki Yesu Kristo waliomwondosha katika ulimwengu huu kwa ukatili mkubwa kushuhudiwa na binadamu. Wanapopigwa na kuteswa Wafuasi wa Yesu hawaachi kusimama katika kweli na haki. Wanapokatazwa kulisema jina hili lenye nguvu ya ajabu-Yesu Kristo hawaachi kuwa na furaha. Baada ya kipigo na mateso, nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo,” Mdo 5:41.

Ndugu yangu, ni mara ngapi wafurahi kwa kuaibishwa kwa ajili ya Jina hili kuu ya Yesu Kristo Mnazareti? Ni mara ngapi twataka kusafishwa majina yetu kwa vile tu hayakutendewa haki? Ni mara ngapi tunapenda kutambulika tulivyo zaidi ya kumtambulisha Kristo aliye mfalme wa amani, haki, upendo na unyenyekevu? Ni ukweli usiotia shaka kwamba Kristo anapoinuliwa kwa yale tuyafanyayo ni kwa namna hiyo hiyo nasi tunanyanyuliwa. Kinyume chake ni balaa kubwa, na maanguko yake hayana mfano. Kristo asipokuwa kielelezo cha maisha yetu, hatutaweza kumshuhudia hata majumbani mwetu, majirani zetu na jamii inayotuzunguka. Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo,” Mdo 5:42. Bila nguvu ya kimaadili na unyenyekevu bado hatutaweza kufikia hatua hii ya Kanisa la mwanzo.

Bila shaka kila mmoja wetu anayo sababu kubwa kabisa ya kuwa hapo alipo sasa. Jambo la kujiuliza ni hili; Je, sababu hiyo imebeba ukweli wa kile ninachokichuchumilia kila siku ya maisha yangu? Injili ya leo inatupa angalizo kuhusu changamoto hii muhimu ya maisha. Ni kweli kila aliyemwona Yesu na kumfuata alikuwa na sababu yake. Injili ya leo inatupa mbili ya sababu za kumfuata Kristo kadiri ya kundi lile siku ile na wakati ule. Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa,” Yoh 6:2. Je, kutakuwa na sababu yeyote ya kumfuata Yesu Kristo kama akiwaponya wangonjwa wote tulikuwa nao leo? Ndugu yangu ishara tu ya kitu fulani katika ufuasi wa Kristo hauakisi Imani ya kwetu juu ya Kristo licha kwamba ni moja ya kutupa uhakika wa nguvu na uwezo wa Kristo.

Tunachopaswa kufanya kama wafuasi wa kweli wa Kristo ni kufundisha ukweli juu ya Kristo na nafasi yake katika maisha yetu ya kila siku. Huku ni kuwaketisha chini wanaotaka kumjua. Yesu akasema, Waketisheni watu. Basi watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao,” Yoh 6: 10a-10c. Kuwaketisha watu chini wenye shahuku ya kumjua Kristo ni kutoa mafundisho ya kweli, ili kuziponya mwili, nafsi na roho zao kutoka katika mahangaiko ya kila siku. Leo katika tukio hili, Kristo anawaponya hangaiko hilo la mwili kwa kuwalisha mikate na samaki. Tendo hili ni moja ya yale mambo makuu matatu waliyoyafanya mitume na wafuasi wengine wa Kristo baada ya ufufuko wake.

Tendo hilo la kuwalisha kimwili katika mahitaji yao, linatanguliwa na shukrani kwa yale aliyowashirikisha, ambayo leo tunapata taswira halisi ya adhimisho la Ekaristi Takatifu. Adhimisho hili ni karamu ya Kristo na shukrani kwa Mungu. Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka,” Yoh 6:11. Ndugu yangu, moyo usio na shukrani hukausha mema yote machoni mwa Mungu. Ni kwa moyo huu wa shukrani wanakula na kusaza na kukusanya mabaki yaliyoyajaza makapu kumi na mbili. Makapu haya kumi na mbili ni idadi ya makabila kumi na mbili ya Israeli. Kwa maana nyingine kilichobaki likiweza kuwalisha taifa zima. Kwa maana hii, muujiza huu wa Yesu siyo tu kwa watu wale elfu tano waliokula na kusaza. Kristo katika jambo hili la shukrani anatukumbusha wajibu muhimu sana. Kwa vile yote tulivyonavyo tumepewa kwa upendo wa huruma ya Mungu. Hivyo ili tuendelee kupata neema hizo, yatupasa kuhifadhi yale yaliyobaki kwa sababu hatuna uhakika wa kesho. Yesu anasema, “Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote,” Yoh 6:12b. Ni mara ngapi unatumia hovyo aliyokukirimia Mungu kwa upendo ili hali jirani yako analala na njaa kila siku? Je na baada ya kula na kushiba, bado unaona sababu ya kumfuata Kristo kwa karibu?

Ndugu yangu, kula na kunywa vikiongozwa na ishara mbalimbali, siyo sababu msingi wa imani yetu kumfuata Kristo, na imani yetu haijajengwa katika mambo hayo. Tunaona baada ya watu hawa kula na kushiba  walitaka kumfanya Yesu kuwa mfalme wa Mikate. Kwa maana nyingine tunamgeuza Kristo kama “Supermarket” ambayo tunauhakika wa kupata kila kitu, na pale tu tunapokuwa na hitaji hilo. Tunapokuwa na mwono huu, Kristo ujitenga nasi kwa sababu bado hatujamjua vizuri, na hatujui nafasi na lengo lake katika maisha yetu ya kila siku. “Akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake,” Yoh 6:15b. Kwa mantiki hii, inawezekana sala zetu hazijibiwa kadiri tuombavyo kwa sababu tunamchukulia Kristo kama sehemu ya kuyapata tu yale tuyamataniyo hata kama siyo ya muhimu katika maisha yetu. Na ndiyo maana Mtume Yakobo anatupa angalizo kwa kutuwasa, “Hata mwomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.” Yak 4:3

Tumsifu Yesu Kristo!

Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo,” Mdo 5:41


Ee Yesu na Mchungaji wetu Mwema, lisimamie Kanisa lako leo katika nguvu ya kimaadili na Unyenyekevu kwa Viongozi wako na Wakristo wote kwa ujumla wao. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario