domingo, 24 de abril de 2016

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 5 YA PASAKA

JUMANNE WIKI YA 5 YA PASAKA
Somo: Mdo 14:18-27
Zab: 145: 10-11, 12-13ab, 21
Injili: Yoh 14:27-31a
Nukuu:
Lakini Wayahudi wakafika toka Antiokia na Ikonio, wakawashawishi makutano hata wakampiga kwa mawe Paulo, wakamburuta nje ya mji, wakidhania ya kuwa amekwisha kufa,” Mdo 14:19

wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi,” Mdo 14:22

Hata walipofika wakalikutanisha Kanisa, wakawaeleza mambo yote aliyoyafanya Mungu pamoja nao, na ya kwamba amewafungulia Mataifa mlango wa imani,” Mdo 14:27

Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga,” Yoh 14:27

Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu,” Yoh 14:30

TAFAKARI: “Kanisa la Mwanzo, umisionari na changamoto zake.”

Wapendwa wana wa Mungu, tunaendelea kutafakari umisionari wa Kanisa la Mwanzo, na changamoto zake. Mtume Paulo na mwenzake Barnaba wanakuwa mstari wa mbele kuhakikisha neno la Bwana linafika hata kwa wale walikuwa mbali na Yerusalemu. Kazi hii haikuwa rahisi hata kidogo. Mtume Paulo katika safari yake huko Ikonia na Antiokia, anakutana na kikundi cha Wayahudi ambao wanawashawishi watu wa miji hii kumpiga kwa mawe Mtume Paulo, ili kuzuia uinjilishaji huu. Hivyo, Wayahudi wakafika toka Antiokia na Ikonio, wakawashawishi makutano hata wakampiga kwa mawe Paulo, wakamburuta nje ya mji, wakidhania ya kuwa amekwisha kufa,” Mdo 14:19. Hata hivyo kunusurika huku katika kifo hakukwamishi kazi hii ya kitume.

Mtume Paulo na wenzake walikuwa kweli majitu ya sifa. Majitu ya sifa hapa inamaanisha kwamba hawakuwa na woga wote kulinena neno hata pale walipokatishwa tamaa. Hawakuogopa kusafiri na kumuhubiri yule waliyekuwa wanamwamini na kumwishi kila siku ya maisha yao. Walisafiri kila mji wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi,” Mdo 14:22. Yesu Kristo hasa katika fumbo zima la mateso, kifo na kufufuka kwake, ndiyo sababu ya nguvu na msimamo wa Mitume katika safari hii ya kulihubiri na kuliishi neno la Mungu. Walitambua wazi ni katika dhiki nyingi wataupata ufalme huo wa Mungu. Maisha na sadaka yao ya kila siku ndio msingi wa Kanisa letu hadi leo. Je, mimi natoa sakaka gani kuimairisha msingi huu wa Imani katika Kanisa langu?

Wapendwa wana wa Mungu, tusianze sasa kufikiri namna ya kusafiri na kufanya umisionari wa mbali. Sinodi ya Afrika imeweka wazi namna na mtazamo wa Kanisa letu la Afrika. Kanisa letu la Afrika kiini chake ni familia. Kwa mtazamo huu, umisionari wetu uuanze kwenye familia zetu. Familia zikiimarika, jumuiya zetu ndogondgo za Kikristo nazo zitaimarika. Jumuiya hizi zikiwa imara hakika Kanisa mahalia usitawi na hofu ya Mungu utawala ndani ya mioyo ya watu. Hivyo umisionari wetu leo kama wabatizwa ujikite katika kuimarisha familia zetu. Hapo ndipo kwenye uhai wa Kanisa.

Uinjilishaji huu utafanikiwa kama kweli tutakuwa na AMANI ya kweli ndani yetu. Tunaposema amani hatumaanishi tu amani ya kiroho, bali pia amani ya kijamii. Popote duniani leo swala la amani limeanza kuwa kama kitendaliwi kisichoteguka. Kumekuwepo na misuguano ya chini kwa chini na wakati mwingine misuguano ya wazi kati ya imani moja na nyingine. Yesu Kristo anatupa angalizo juu la swala hili anaposema, Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga,” Yoh 14:27. Ni wazi amani tuipatayo leo huku duniani haina uhakika. Hata hivyo Yesu anatuambia tusiogope. Katika hali ya sintofahamu anatuhaidia Roho wake Mtakatifu ambaye kupitia yeye Roho huyo atatupa viangalizo vyote. Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu,” Yoh 14:30. Katika mashaka na kutoweka kwa Amani katika ulimwengu huu, kwa wezwa rudishwa tu  kwa kukubali kuongozwa na Roho Mtakatifu na kuacha ubinafsi na maslahi binafsi.

Wapendwa katika Kristo, kwa sasa tupo katika kipindi cha kuelekea Sikukuu ya Pentekoste. Tuwekeze nguvu zetu zote kumwomba huyu Roho Mtakatifu atuongoze vyema katika kipindi cha sintofaumu nyingi katika Taifa letu. Tukiikosa hiyo amani, hata uinjilishaji  wetu na umisionari wetu kifamilia hautawezekana. Tuwaombee pia viongozi wetu wajue dhamana waliyonayo juu ya maisha ya watu na mali zao. Tuliombee pia Kanisa liendelee kuishi katika umoja na upendo kama Kristo mwenyewe alivyotaka liwe.

Tumsifu Yesu Kristo!

Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga,” Yoh 14:27


Tusali:-Ee Yesu, mtume Roho wako Mtakatifu atuangazie yaliyo haki na matakatifu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario