lunes, 18 de abril de 2016

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 4 YA PASAKA

JUMANNE WIKI YA 4 YA PASAKA
Somo: Mdo 11:19-26
Zab: 87:1b-3, 4-5, 6-7
Injili: Yoh 10:22-30
Nukuu:
Basi wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hata Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao,” Mdo 11:19

Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana,” Mdo 11:21

Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa Kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia,” Mdo 11:22

“Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia,” Mdo 11:26b

Basi Wayahudi walimzunguka, wakamwambia, Hata lini utatuhangaisha nafsi zetu? Kama wewe ndiwe Kristo, utuambie waziwazi,” Yoh 10:24

Yesu akawajibu, Naliwaambia, lakini ninyi hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia,” Yoh 10:25.

Lakini ninyi hamsadiki, kwa sababu hammo miongoni mwa kondoo wangu,” Yoh 10:26

Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata,” Yoh 10:27. 

Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu,” Yoh 10:28

TAFAKARI: “Matendo mema ndani ya Kristo na katika Kristo, umtambulisha Kristo pale tulipo; wote tumeitwa kuwa wamisionari.”

Wapendwa wana wa Mungu, kutawanyika kwa jumuiya ya kwanza ya Wakristo, kulitokana na kuhujumiwa kwa jumuiya hiyo, na hasa kile kifo cha Shahidi Stefano. Kwa upande mwingine, kupitia mateso haya, habari njema zinafika kila kona na wengi wanamwamini Mungu. Basi wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hata Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao,” Mdo 11:19. Kutawanyika huku kwa jumuiya hizi za Wakristo tukienda mbali zaidi tunaona ni kutokana na sadaka ile ya pekee aliyoitoa Yesu pale msalabani. Ni kwa kupitia sadaka hiyo hiyo-kwa kila mmoja wetu, Kanisa linakua na kuenea popote duniani.

Wapendwa, tunapokuwa na Kristo katika nia na matendo yetu tunabarikiwa kwa sababu tuyafanyayo ni mwendelezo wa kazi yake ya kuikomboa dunia. Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana,” Mdo 11:21. Hapa tunaona safari ya uinjilishaji ndiyo inaanza, na Kanisa katika maana ya kila Mbatizwa linakuwa Kanisa la Kimisionari. Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia,” Mdo 11:22. Kazi hizi za kimisionari ndizo zinazolifanya Kanisa likue na kuenea kila mahali. Kazi hizi pia ndizo zinazo watambulisha wale wazifanyazo. Ni hapa Antiokia kwa mara ya kwanza wanafunzi wa Yesu wanaitwa Wakristo. “Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia,” Mdo 11:26b. Kuitwa kwao huku ni kutokana na matendo yao kuendana na kile walichokuwa wakikiamini na kukihubiri-Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai, kufanya toba ya kweli, na kukaribia kwa Ufalme wa Mungu.

Wapendwa katika Kristo, mtindo huu wa kimisionari unaitajika sana nyakati zetu. Matendo mema ndani ya Kristo na katika Kristo, umtambulisha Kristo pale tulipo; na kwa namna hiyo wote tumeitwa kuwa wamisionari. Umisionari wa kutembea na vipasa sauti kwa sasa hauna nafasi sana. Tunaitaji umisionari wa matendo mema kwa watu wote. Kristo alishaanza kulifanya hili pale ambapo Wayahudi walitaka kupata uhakika kama kweli yeye ndiye Kristo mwenyewe. Yesu akawajibu, Naliwaambia, lakini ninyi hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia,” Yoh 10:25. Kazi azifanyazo Yesu ndizo zinazomthibitisha. Ni kwa namna hiyo hiyo kwamba kazi tuzifanyazo kama Wabatizwa na Kanisa kwa ujumla wake zitamtambulisha Kristo pale tulipo.

Wapendwa, asiyesadiki matendo hayo mema ni wazi hamsadiki hata Kristo pia. Je, tuache kutenda mema? Jibu ni HAPANA. Tusiache kutenda mema kwa vile tu wapo watu ambao hawayaoni mema tuyatendayo, na wala hawamsadiki Kristo. Yesu anasema, Lakini ninyi hamsadiki, kwa sababu hammo miongoni mwa kondoo wangu,” Yoh 10:26. Ni Kristo mwenyewe anayejua hatma ya wale wasiomsadiki. Kazi yetu ni kusambaza upendo wa Kristo kila kona. Ni Kristo mwenyewe atakaye wabadilisha mioyo yao wasiomsadiki kadiri atakavyoona yeye na wakati ufaao. Naye anasema, Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata,” Yoh 10:27. Kondoo walio mbali na sauti ya Kristo ipo siku watavutwa karibu kwa matendo yetu mema kama wafuasi wake Kristo. Ni Kristo mwenyewe atawapa uzima na kuwahifadhi katika mikono yake.Yesu anasema, Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu,” Yoh 10:28. Mimi na wewe kama wabatizwa tutimize vyema ahadi zetu za ubatizo.

Tumsifu Yesu Kristo.

Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana,” Mdo 11:21


Tusali:-Ee Yesu Kristo na Mchungaji wetu Mwema, tujalie neema ya kutenda matendo mema kila wakati. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario