JUMANNE
WIKI YA 3 YA PASAKA
Somo: Mdo 7:51-59
Zab: 31:3cd-4, 6, 7b,
8ª, 17, 21ab
Injili: Yoh 6:30-35
Nukuu:
“Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio,
siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni
vivyo hivyo,” Mdo 7:51
“Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu
amesimama mkono wa kuume wa Mungu,” Mdo 7:56
“Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao,
wakamrukia kwa nia moja,” Mdo 7:57
“Wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi
wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli,” Mdo 7:58
“Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana
Yesu, pokea roho yangu,” Mdo 7:59
“Wakamwambia,
Unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda kazi gani?” Yoh 6:30
“Yesu
akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha
mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni,”
Yoh 6:32
“Yesu
akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa
kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe,” Yoh 6:35
TAFAKARI:
“Kifo Chema ni kuishi katika Kristo na ndani ya Kristo, yeye ndiye chakula cha
uzima.”
Wapendwa wana wa Mungu,
hakuna shaka kabisa wote tuliozaliwa ipo siku wote tutakufa kila mmoja kwa
wakati wake. Kifo kwa Mkristo ni daraja ya kuvuka kwenda upande mwingine wenye
mazingira tofauti na haya tuliyonayo: wenye uzima na uhai. Kifo kwa
anayemwamini Kristo ni mlango ambao watupitisha kwenye maisha mengine ya
umilele. Kifo kinamaana ndani na katika Kristo kwa sababu kupitia mateso yake,
na kifo chake msalabani laana ya kifo imefutwa. Kwa Mkristo kwenye imani, kifo
si kitu cha kuogopa bali ni tukio la kujiandaa.
Maandalizi ya kifo
Chema ni kuishi kweli ya Kristo kila siku. Ni kumshuhudia Kristo kwa yale
yaliyomema na anayotuwasa kuyafanya kama watoto wa Mungu. Ni kutokumwonea aibu
Kristo mbele za watu hata kama yatupasa kufa kwa ajili ya kweli. Ukweli huu
ndiyo anaouishi Shahidi Stefano na kuhushuhudia. Stefano Shahidi anawaaambia
Wayahudi, “Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala
masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na
ninyi ni vivyo hivyo,” Mdo 7:51. Jambo la kuelewa hapa katika maisha yetu ya
Kiroho, hatuwezi kupingana na mpango wa Roho Mtakatifu. Sifa na kazi mojawapo wa Roho Mtakatifu ni kuleta umoja wa
kweli na wakimungu kwa wote walioumbewa kwa sura na mfano wa Mungu, Mwa 1:26.
Palipo
na Roho Mtakatifu kuna umoja wa kweli na hapo Roho Mtakatifu utenda mambo yake
kwa wale aliwaridhia. Shihidi Stefano, “akijaa
Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa
Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu,” Mdo 7:55. Stefano
Shahidi anapewa hakikisho la kile anachokisimamia na kukishuhudia. Pamoja na
ukweli huu, watesi wake “wakapiga kelele kwa
sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja,” Mdo 7:57
Ndugu yangu, ni mara
ngapi katika mazingira yetu tunakutana na hali kama hii na wala hatufanyi
chochote? Yawezekana hali isiwe kama ya Shahidi Stefano ya kupondwa mawe. Ila
wote ni mashahidi na labda tumeshaona jinsi watoto wadogo wanavyotendwa kwenye
usafiri wetu wa daladala. Mzazi ambaye naye anamtoto kama huyo anayeteswa na
kunyanyapaliwa na kondakta, asemi wala akemei chochote. Je, tunatofauti gani na
walimrarua Shahidi Stefano? “Wakamtoa
nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa
kijana mmoja aliyeitwa Sauli,” Mdo 7:58. Sauli, ambaye leo anajulikana sana
kama Mtume Paulo, anashiriki katika kosa hili. Mtume Paulo analifanya kosa hili
kwa kutetea mila na desturi za mababu zake, ambaye baada ya kuongoka kwake
anakuwa mtetezi mashuhuri wa Kristo na mkosoaji wa mila na desturi hizo. Huku
ndiko maana halisi ya kuongoka
Katika
kipigo hiki cha kikatili, Stefano anaikabidhi roho yake kwa Mungu, kama Bwana
wetu Yesu Kristo alivyofanya. “Wakampiga
kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu,” Mdo
7:59. Hata katika hali hii ya kutisha, Stefano Shahidi habadili msimamo wake,
wala hakatishwi tamaa kwa kujitoa kwake muhanga. Mungu anabakia kuwa tumaini
lake hadi mwisho. Wengi wetu katika hali kama hii na mara nyingine tunapo ugua
kwa muda mrefu bila kujua sawasawa sababu ya magonjwa yetu, huwa tuna kata
tamaa na kusaliti Imani yetu na Mungu wetu. Ni mara ngapi tunawaona Wakristo
waliokuwa mstari wa mbele wanakwenda kupiga ramli na hata wengine wanakutwa na
umauti kwa waganga?
Mpendwa,
haijalishi wewe ni nani ila kuwa Mkristo bila kuwa na imani thabiti ni hatari
sana. Ni sawa na mkate usioiva vizuri kwani ni hatari kwa tumbo. Yesu Kristo
katika Injili ya leo anawashangaa wale wasio mwamini pamoja na yote anayoyaishi
na kuyatenda. Nao wanataka kuona ishara ili wamsadiki kwamba yeye ndiye kweli
wanayemtumainia. “Wakamwambia,
Unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda kazi gani?” Yoh 6:30. Kwa Wayahudi, Musa alikuwa na nafasi ya
pekee sana hata kuweza kuvuka uelewa wa Mungu. Kwa mantiki hiyo, yeyote
aliyekwenda kinyume na kile alichosema au fanya Musa alionekana kama mhaini
hivi. Yesu kabla ya yote anawapa uelewa wa Mungu ni nani na Musa ni nani. “Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye
Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula
cha kweli kitokacho mbinguni,” Yoh 6:32. Musa aliweza kuyafanya hayo yote kwa
mkono wa Mungu, ila Kristo ni zaidi ya Musa kwani kwake upo uzima. Kiu na
mahangaiko yetu yote yanamajibu tunapoishi katika yeye na ndani yake. “Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima;
yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe,” Yoh
6:35. Je, unamwamini Kristo? Hakuna sababu ya kutafuta ulizi kwa njia ya giza
kama tunaye Kristo. Hakuna sababu ya kuzindika majumba yetu na kutembea na
mahirizi kama tunaye Kristo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Yesu
akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa
kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe,” Yoh 6:35
Ee Yesu wangu, nami nasadiki wewe ndiye chakula na
uzima wangu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario