JUMAPILI
YA 3 YA PASAKA YA MWAKA-C
Somo
I: Mdo 5:27b-32, 40b-41
Zab: 30:1, 3, 5, 10-12
Somo
II: Ufu 5:11-14
Injili: Yoh 21:1-19
Nukuu:
“Petro na mitume
wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu,
ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti,” Mdo 5:29-30
“Nao wakatoka
katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa
kwa ajili ya Jina hilo,” Mdo 5:41
“Baraka na heshima na utukufu na uweza una
yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-Kondoo, hata milele na
milele,” Ufu 5:13b
“Akawaambia,
Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata.Basi wakatupa; wala
sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki,” Yoh 21:6
“Basi
walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa?
Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha
wana-kondoo wangu,” Yoh 21:15
“Akamwambia
tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe
wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu,” Yoh 21:16
“Akamwambia
mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile
alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe
umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.” Yoh 21:17
“Akasema,
Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na
kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine
atakufunga na kukuchukua usikotaka,” Yoh 21:18
“Akasema
neno hilo kwa kuonyesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu. Naye akiisha
kusema hayo akamwambia, Nifuate,” Yoh 21:19
TAFAKARI:
“Ndani na katika Yesu kuna Mwanga na Amani ya kweli. Kwa kumtii Yesu Kristo na
kuishi ndani ya Neno lake kwa kuyafanya mapenzi yake, huyajenga upya maisha
yako yaliyobomolewa na dhambi. Kwa Yesu kuna Njia ya kweli, Kweli halisi, na
Uzima wa Milele.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya ‘3’ya Pasaka ya Mwaka ‘C’ wa Kanisa.
Leo Mama Kanisa kwa namna ya pekee anatualika tutafakari kwa undani kiini cha
Imani na Msingi kwa Kanisa-jumuiya ya kwanza ya Wakristo. Tunapotazama Kiini
cha Imani na Msingi huu wa Jumuiya hii ya kwanza ya Wakristo, mambo matatu ni
dhahiri; Uwepo na kazi ya Nguvu ya Roho Mtakatifu, Moyo wa kupokeana
{kushirikishana na kutabikiana katika hali zote bila kujibakiza}, na Nguvu ya
Kimaadili. Kristo mfufuka akiwa ndiye kielelezo na sababu ya kuishi na kutenda
kwao, Jumuiya hii ya kwanza ya Wakristo walisimama imara kwa kila jambo hasa
pale kulipotokea hujuma juu ya kweli na haki iliyolenga fumbo zima la wokovu
wetu.
Hivyo kwa nguvu ya ROHO
MTAKATIFU licha ya uduni wao ‘kiufahamu’ hawakusita kusema lililo kweli kwa
wale walionekana kupindisha ukweli kwa manufaa yao binafsi. Tuelewe jumuiya
hii ya kwanza na hasa Mitume, hawakuwa
watu wa elimu ya pekee sana. Wengi wao walikuwa na taaluma ya uvuvi tu ambayo
kwa kiasi kikubwa waliipata kutokana na mazingira na makuzi yao. Roho huyu
Mtakatifu aliwapa ujasiri wa ajabu na kusimama imara katika kweli na haki.
Mitume wanaponyamazishwa kulinena Neno la uzima, na hasa maswahibu yaliyompata
Yesu Kristo, Mtume Petro anakemea jambo hilo kwa ujasiri mkubwa na kusema, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu,
ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti,” Mdo 5:29-30. Huyu siye Petro yule
aliyekuwa na woga hata kumkana Yesu mara tatu. Huyu ni Petro aliyevuviwa na
Roho Mtakatifu na aliyezaliwa upya kwa Roho Mtakatifu. Kuhusu Roho Mtakatifu
Petro Mtume anasema, “sisi tu mashahidi wa
mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio,” Mdo
5:32. Roho Mtakatifu ni zawadi ya pekee kwa
kila mmoja wetu na Kanisa kwa ujumla wake. Uwepo wa Roho Mtakatifu Katika
Kanisa-Sakramenti ya wokovu, ni ukamilifu ya haya aliyoyahaidi Yesu Kristo
angali na wanafunzi wake kwamba, “Nami
nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa
kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui;
bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. Sitawaacha ninyi
yatima; naja kwenu,” Yoh 14:16-18. Ndugu yangu, Kanisa nikimaanisha yeyote yule
aliyebatizwa si mayatima. Tunaye Roho Mtakatifu atakaye tuongoza katika hali
zote. Ni mimi na wewe kumpa nafasi tu.
Umoja na nguvu ya
jumuiya hii ya Wakristo wa kwanza uliimarika kwa utayari wao katika KUPOKEANA,
KUCHUKULIANA, NA KUTAABIKIANA katika hali zote bila kujibakiza. Siyo kwamba
matatizo hayakuwepo, bali yalipotokea yalipatiwa ufumbuzi wa haraka ili ukweli
kuhusu Kristo Yesu usikwamishwe. Hapa tunaona namna ambavyo
walivyolishughulikia tatizo lile la wajane katika jumuiya yao kwa kuwateua watu
saba ‘mashemasi’ kutoa huduma ili neno la uzima lisikwame, Mdo 6:1-7. Hivyo, “Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi,
wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani,” Mdo 6:2.
Moyo huu wa undugu uliounganishwa na kufungamanishwa na neno la uzima ulikuwa
kiungo muhumu sana katika kuishika Imani, kuikuza Imani, na kushirikishana
tunda ya Imani ya kweli, ambayo ndio Upendo na Matumaini ndani na katika Kristo
Yesu Mfufuka kwa kila amuaminiye. Jumuiya hii ilipokuwa pamoja mateso yao na
kutaabika kwao kulibadilika kuwa furaha kwa sababu walijua sababu ya mateso na
mahangaiko yao. “Nao wakatoka katika ile
baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa
ajili ya Jina hilo,” Mdo 5:41.
Wapendwa katika Kristo,
furaha ya kweli katika maisha ya mtindo wowote ule, iwe maisha ya wakfu au
ndoa, msingi wake si mali au utajiri kama wengi wetu tunavyofikiri na kutaabika
kuyatafuta hayo usiku na mchana. Furaha ya kweli kabla ya yote hujengwa katika
maana na sababu ya maisha yale unayoyaishi. Utawezaje basi kupata furaha ya
kweli kama unachokiishi huoni umaana wake na sababu yake? Maana na sababu ya
kile unachokiishi hukupa fursa ya kuona kesho ya kile unachokiishi. Kesho ya
kile unachokiishi umulika umilele wake hata kama umilele huo kwa kiasi fulani
bado umefichwa kwako.
Jumuiya hii ya kwanza
ya Wakristo pamoja na kuongozwa na Nguvu ya Roho Mtakatifu, na umoja na
mshikamano wao katika kila hali bila kujibakiza, ilikuwa imara na hasa kwa
viongozi wao ambao ni Mitume kutokana na NGUVU YA KIMAADILI. Nguvu hii ya
kimaadili ilikuwa mwiba kwa watesi wao na wahujumu Kanisa kwa sababu Mitume na
Wakristo kwa ujumla wao waliyaishi kwa uaminifu mkubwa yale yote waliyoyasema
na kuyaamini. Maisha ya hapa duniani baada ya Ufufua wa Kristo waliyaona kama
jaribu, dhamana na jukumu la muda mfupi tu. Hivyo tenda yao, fikiri yao, na
hata ona yao ilikuwa na mwelekeo wa mwisho wa nyakati na kwenye uzima wa
milele. Hivyo kwa maono jumuiya hii iliweza kuliona Kanisa la Watakatifu
waliopo mbinguni baada ya kuishinda vita hii ya imani hapa duniani. Tunaona
ukweli huu kutoka somo letu la pili leo, kwamba watu wale huko mbinguni
walionekana “wakisema kwa sauti kuu,
Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na
nguvu na heshima na utukufu na baraka,” Ufu 5:12. Mwana-kondoo huyu ambaye ndiye Yesu Kristo ni
sababu na kielelezo cha maisha na furaha ya kweli ya jumuiya hii ya kwanza ya
Wakristo na hata sasa kwa Kanisa kama Sakramenti ya wokovu kwa wale wote
waliomridhia. “Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye
juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-Kondoo, hata milele na milele,” Ufu 5:13b.
Hakika tuwapo hapa duniani tusisahau wosia huu wa Yesu juu ya maisha ya kila
siku, kwamba, “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na
hayo yote mtazidishiwa,” Mt 6:33
Tunapojaribu kuchenga ukweli huu {kuutafuta Ufalme wake na
haki yake}, tunakuwa nje ya kweli mzima ya mafundisho ya Kristo na lengo zima
la umilele wa maisha haya tunayoyaishi. Mara kwa mara kunakuwa na vishawisha
vya kurudi nyuma na kufanya yale tuliyoyazoea. Hata Mitume hawakuweza kukwepa
hali hiyo, kwani maisha yao na ukuuaji wao wa Imani ulilandana sana na maisha
na mazingira yao. Hivyo Mtume Simoni Petro anawaambia wenzake, “Naenda kuvua samaki. Nao wakamwambia, Sisi nasi tutakwenda nawe.
Basi wakaondoka, wakapanda chomboni; ila usiku ule hawakupata kitu,” Yoh 21:3.
Wapendwa
wana wa Mungu, tunapokuwa nje ya mpango mzima wa Mungu, na hasa kwa wale
tuliopewa thamana hiyo {Wazazi, Wahudumu wa Kiroho, Viongozi wa Serikali, na
ak}, mafanikio ya yale tuyatamaniyo huwa hewa na kutoweka kabisa. Kumhubiri
Kristo na kumshuhudia kwa maneno na matendo ni kazi ya kila aliyebatizwa na kuimarishwa. Hivyo basi,
yatupasa kulifanya tendo hilo pasipo shaka. Kristo hachoki tukumbusha
tunapokengeuka kuhusu ukweli huu. Kristo aweza kutumia njia mbalimbali
kuwakilisha ujumbe wa kweli hii. Kwa upendo wake, Kristo mara zote anapenda
kujua mahangaiko yetu, na kuturudisha katika mstari. Katika hali ya kuchoka na
uchovu mwingi kwa kupigika usiku kucha bila kupata samaki, anawaambia wanafunzi
wake, “Wanangu, mna kitoweo? Wakamjibu, La,” Yoh 21:5. Kwa maana
nyingine Yesu anataka kutuambia, Je, mnapozifuata njia zenu na kuacha maagizo
yangu mnapata mafanikio?
Kuonyesha
ukweli wa jambo hili, Yesu Kristo, anawafundisha njia na maagizo yake yaliyo
kweli na sahihi kwa uzima wa mwili na roho. “Akawaambia, Litupeni
jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa
hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki,” Yoh 21:6.
Wapendwa
katika Kristo, yawezekana ushapigana sana na maisha kiasi kwamba kila siku ni
aheri ya jana. Jambo la kwanza usitafuta mchawi wala kwenda kwa waganga, au
kusafisha nyota kama tunavyosikia wengi wakidanganywa. Jambo la kwanza chunguza
uhusiano wako na Mungu. Je, umelitupa jarife hilo upande wa kuume wa chombo
chako, yaani, maisha yake? Je, unaisha kadiri ya matakwa ya Mungu? Kama hapana,
Je, unaridhika na hali hiyo? Kama siyo, Je, ni kitu gani kinachokukwamisha
kurejesha uhusiano huo? Kama uhusiano wako na Mungu ni mzuri na bado unapigika
sana na maisha, jambo hilo unalichukuliaje? Je, walichukulia kama kusahauliwa
na Mungu, au kutokutendewa haki na Mungu? Je, unaelewaje subura ya Mungu kwa
yale uyaombayo na kuyatamani?
Ndugu yangu,
hakuna jambo lolote tuombalo Mungu aache kutupatia. Kama itatokea kwa hapa
duniani hatukulipata basi jua umeandaliwa jambo hilo kwa umilele wake, mara
baada ya maisha haya ya hapa duniani. Kamwe Mungu hamtupi mja wake. Kwa wale
ambao Mungu ametukirimia zaidi na hata kupita mahitaji yetu, tunachukuliaje
jambo hilo? Je, tunamtambua Mungu katika mali na utajiri wetu? Ukweli ni kwamba
kamwe hatutaweza mtambua Mungu kwa yale tuliyonayo, kama hatuna upendo na
Mungu. Yohane Mtume anamtambua Kristo kwa sababu alikuwa na upendo wa dhati kwa
Kristo na Kristo alikuwa anampenda kwa namna ya pekee. Na hivi ndiyo Injili
inavyotuambia, “Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro,
Ndiye Bwana,” Yoh 21:7.
Kumtambua
huku Kristo, Yohani habaki na hali hiyo mwenyewe. Anamwambia na Petro pia. Je,
tunapoguswa na upendo wa Kristo na Mungu tupo tayari kuushirikisha kwa wenzetu
nao wapate wokovu huo? Rejea maisha ya jumuiya ya kwanza ya Wakristo. Tunaona
baada ya Petro Mtume, kusikia habari hiyo, anajitosa kwenye maji maana alikuwa
uchi. “Naye Simoni Petro, aliposikia ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake,
(maana alikuwa uchi), akajitupa baharini,” Yoh 21:7b. Mpendwa tunayesafari wote
katika tafakari hii, Petro kuwa uchi hapa kunamaanisha kwa upande mwingine
kwamba anatambua kujikwaa kwake kunakotokana na kutokuyafanya yale aliyopaswa
kufanywa kama kiongozi, kama niliyoeleza hapo mwanzo.
Mara
baada ya Petro kujitambua, anaingia chomboni na hapa tunaona maajabu haya. “Basi Simoni Petro akapanda chomboni, akalivuta jarife pwani,
limejaa samaki wakubwa, mia hamsini na watatu; na ijapokuwa ni wengi namna
hiyo, jarife halikupasuka,” Yoh 21:11. Ndugu yangu, jarife hili halina tofauti
na Kanisa kama chombo na Sakramenti ya wokovu wetu, ambacho kazi yake kubwa ni
kuwavuta watu kwa Kristo na kuwapeleka kwake wakiwa salama. Usalamu huu ni
idadi inayotolewa ya samaki hawa. Tutajulikana kwa idadi yetu mbele za
Mwanakondoo. Nasi tukifika mbele ya uso wa Mungu tutajulikana kwa idadi, na
wale tuliopewa kazi hiyo yatupasa tutoe hesaba ya idadi tulioifikisha mbele ya
Mungu na Mwanakondo.
Hata
hivyo tunasikia jarife hili-Mtego huu, haukupasuka licha ya wingi wa samaki
wale. Jibu ni kwamba mtego haukupasuka kwa sababu u imara. Mtego, yaani Jarife
kama Kanisa, na Sakramenti ya wokovu wetu, uimara wake unatokana na uwepo wa
nguvu ya Roho Mtakatifu, ambaye uyaratibisha yote kadiri ya mahitaji ya Kanisa
lake kwa nyakati zote. Tumruhusu Roho Mtakatifu huyu afanye kazi yake, na siyo
Roho Mtakavitu. Roho Mtakavitu atalipasua JARIFE-KANISA. Roho Mtakavitu huyu
ni: SIFA, CHEO, KUJULIKANA KULIKO BINAFSI, MAMLAKA MBELE ZA WATU, NA MBAYA
ZAIDI KWA VIONGOZI WALA RUSHWA. Na kama tulivyoona katika Jumuiya ya kwanza ya
Wakristo, uimara wa Kanisa leo unategemea pia kupokeana kwetu, kuchukuliana kwetu,
na kutaabikiana kwetu katika hali zote bila kujibakiza. Na mwisho uimara wa
Kanisa leo unategemea Nguvu ya Kimaadili kwa kila Mbatizwa na hasa kwa njia ya
peke wale wote waliohesabiwa haki na Mama Kanisa kama viongozi wetu wa Kiroho.
Hivyo, tusichoke kuhubiri na kuishi kwa vitendo Huruma ya Mungu kwa sababu hata
hawa viongozi wala rushwa, wote wasio na
hofu ya Mungu ndani yao, na sisi sote kwa ujumla wetu kama Kanisa na wabatizwa
tunahitaji huruma hiyo na wokovu wa Mungu.
Wapendwa
wana wa Taifa la Mungu, sehemu ya mwisho ya Injili yetu ya leo, tunaona
kukamilishwa kwa yale Kristo aliyoyaanzisha ndani ya Mtume Petro hasa ule ukiri wake, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai,” Mt 16:16, ndiyo hayo leo Yesu anataka kujua ukweli wake. Tukumbuke
pia kuwa baada ya ukiri ule wa Petro Yesu alihaidi hii kwa Petro, “Nami
nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu;
wala milango ya kuzimu haitalishinda,” Mt 16:18. Ni wazi, uwepo wa Petro kati
ya Mitume wenzake na jumuiya ile ya kwanza ya Wakristo kunampatia nafasi ya
pekee katika kutimiza wajibu wake na kutumika kwake. Ni wazi pia nafasi hii ya
pekee kwa Petro siyo tokeo la umahiri wake, bali ni neema ya Mungu. Naye Yesu
anathibitisha ukweli huu kwa kusema, “Heri
wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba
yangu aliye mbinguni,” Mt 16:17. Mamlaka haya ya Petro kama Halifa wake Kristo
ni Neema ya Mungu mwenyewe. Mbadiliko wa jina Simoni na kuwa Petro, yaani
Mwamba, unathibitisha Mtu mpya mwenye jukumu Jipya. Hii ndiyo sababu pia ya
Mababa watakatifu kuchagua majina mapya mara baada ya kuhesabiwa haki na Mama
Kanisa.
Ni
Petro huyu pamoja na ujasiri huu aliounyesha katika ukiri wake juu ya Kristo
aliweza kumkana mara tatu Yesu kutokana na hofu ya kuuwawa pamoja na Kristo
kifo kile cha aibu cha MSALABA. Leo Yesu anamuuliza mara tatu kama kweli
anampenda kama alivyomkana mara tatu. Yesu anamuuliza, “Je!
Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe
wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu,” Yoh 21:15. Neno
‘kuliko hawa’ linabeba ujumbe mzito sana. Kwa ufupi twaweza kutafsiri hivi, ‘je
wanipenda kuliko ulimwengu huu na fahari yake yote?’ Analoulizwa Petro
unaulizwa wewe na mimi tuliobatizwa kwa jina lake. Huku pia ni kumkataa shetani
na fahari zake zote na mambo yake yote. Msisitizo wa Yesu ni huu; ‘lisha
wana-kondoo wangu,’ ‘chunga kondoo zangu,’ na ‘lisha kondoo zangu.’ Msisitizo
wa kwanza ni kuwalisha wote walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, Mwa 1:27,
bila kutazama utofauti wao kifamili, koo, kabila, utaifa, zangi zao, imani zao,
na itikadi zao. Kwa kulitenda hili Petro ndiko kunakomrudishia nguvu yake ile
ya kimaadili na kuendelea kusimama kama alama halisi ya Kristo-Upendo, Haki,
Amani, Huruma, Msamaha na Unyenyekevu wa kweli. Huu ndio mwaliko wa Mahalifa
wote wa Yesu Kristo toka Mtume Petro hadi leo Baba Mtakatifu wetu Fransisco.
Pia huu ni wito wa kila Mbatizwa kufanana na Kristo katika kufikiri, kuona,
kutenda, kusema, na kuamua. Mtume Petro
kama alama halisi ya Kristo ambayo huakisi kwa wote waliomfuata baadaye, na
wale wote waliohesabiwa haki katika Kanisa-Makleri, kunawataka kufanana na
Kristo kwa mambo makuu matatu kama hatma ya kufika pale alipofika Kristo Yesu:
Moja, ni mwitikio wa kufanana na Kristo
kama mchungaji mwema wa kondoo wote mbele ya Mungu na Kristo Mtukuka. Pili,
kufanana na Kristo kama sadaka hai na yenye kupendeza katika maana ya sadaka na
mtoa sadaka bila kujibakiza. Na tatu, kufanana na Kristo kulipojionyesha wazi kwa
upendo wake wa kukubali kufa kifo cha aibu pale Msalabani kwa kukubali kuwa
upendo wa wakosefu na wadhambi ili wawe huru. Hili la mwisho ndilo kwa
msisitizo Yesu anamkumbusha Mtume Petro na kusema,
“Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na
kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine
atakufunga na kukuchukua usikotaka,” Yoh 21:18. Kama Kristo alivyojitoa sadaka pale Msalabani, ni
kwa namna hiyo hiyo anavyomkumbusha Petro itakavyokuwa kwake. “Akasema neno hilo kwa kuonyesha ni kwa mauti
gani atakayomtukuza Mungu. Naye akiisha kusema hayo akamwambia, Nifuate,” Yoh
21:19
Wapendwa
wana wa Mungu, Ukulu huu wa Mtakatifu Petro unakipa uzito Kiti hicho katika
mamlaka yake kama Yesu mwenyewe asemavyo, “Nami
nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani,
litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa
limefunguliwa mbinguni,” Mt 16:19. Haya ndiyo mamlaka ya kiti hiki na hasa kwa
swala hizi la Huruma ya Mungu kwa ondoleo la dhambi. Hii ndiyo sababu pia ya
Baba Mtakatifu kuwa na uwezo na mamlaka ya kuutangaza mwaka huu wa Kanisa kuwa
mwaka wa HURUMA YA MUNGU.
Wapendwa wana wa Mungu,
maswali mawili ya mwisho ya Yesu na msisitizo alioutoa Yesu {chunga
kondoo zangu, na lisha kondoo zangu}, unalenga katika majukumu na mwonekano wa Ukulu huu
ambao ni ule wa kutumika badala ya kutumikiwa. Na Yesu anasema, “na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na
awe mtumwa wenu; kama vile Mwana
wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya
wengi,” Mt 20:27-28. Kiongozi yeyote yule aliyepewa dhamana na kuhesabiwa haki
na Kanisa, yampasa kutumika na siyo kutumikiwa. Mtume Petro anasema, “lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na
kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa
kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo,” I Pet 5:2. Ndugu yangu, wewe na mimi
tuliye hesabiwa haki na kupewa dhamana na Mama Kanisa, hatupo hapo tulipo kwa
maslahi yetu binafsi. Mimi na wewe tupo hapo tulipo kumwakilisha Kristo Yesu
aliyetumika badala ya kutumikiwa. “Vivyo
hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu,
mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa
wanyenyekevu neema,” 1Pet 5:5. Huduma yo yote ile isiyokuwa na taswira ya
unyenyekevu kamwe haimwakilishi Kristo. Na kwa namna hiyo hakuna utukufu. Kristo kamwe hajidhihirishi pasipo
unyenyekevu. “Na Mchungaji mkuu
atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka,” 1Pet 5:4.
Unyenyekevu katika huduma tuzitoazo utawashangaza wengi na hasa wale ambao mawazo yao hutanguliza nafsi zao.
Bwana na Bibi Fikiri
walibahatika kupata zawadi ya watoto wanne-wawili wa kike na wawili wa mwisho
wakiume. Wakiwa wanarejea nyumbani baada ya wiki moja kutokuwepo kutokana na
kuwa kwenye Msiba wa Baba Mkwe wake, ambaye ndiye Baba Mzazi wa Bibi Fikiri,
kila mmoja alijinunulia tunda alipendalo baada ya kupata chakula cha mchana
katika hoteli ile ambapo Mabus husimama
na abiri hupata huduma hiyo.
Bibi Fikiri alinunua
machungwa matatu, na Bwana Fikiri alinunua Peasi moja. Wakiwa ndani ya Bus na
safari ikiendelea, Bwana Fikiria alichukua Peasi lake na kuanza kulitafuna
taratibu. Baada ya masaa manne walifika nyumbani na kwa furaha watoto
waliwapokea vizuri kwa sababu waliwakosa kwa muda wa wiki moja.
Basi Bibi Fikiri
alimwambia mmoja wa binti yake alete sahani. Bibi Fikiri aliyachukua yale
machungwa matatu aliyoyanunu na kuwagawia watoto wake wale wanne kila mmoja
nusu kipande. Hivyo likabaki chungwa moja. Mama Fikiri akaagiza binti yake
alete maji kwa ajili ya kumnawisha Baba yao. Hivyo Bibi Fikiri alimnawisha
mikono mumewe na kulimenya chungwa lile na kumpatia.
Baada ya kula chungwa
lile, Bwana Fikiri aliwaza moyoni kwa kutokujali kwake na hasa kuonyesha upendo
wa kweli kwa familia na watoto wake. Yeye kama Baba alikula Peasi lake njiani
na hakuwa na wazo lolote juu ya Mke wake wala watoto wake.
Bwana Fikiri alimtazama
mke wake na kumwambia, “hakika tangu kuzaliwa kwangu, na miaka hii 22 ya ndoa
yetu sijawahi kupata somo na fundisho zuri kama ulilonifundisha leo. Nimejiona
jinsi nilivyo mtupu. Asante sana Mke wangu.” Basi kwa tabasamu, Mama Fikira
alijibu, “Baba Monica nawe umeshaanza! Asante kwa kuliona hilo Mme wangu.”
-Mama Fikiri anatupa
mfano mzuri wa kujali na kuwajibika kila mmoja pale alipo na nafasi aliyokuwa
nayo kila mmoja kadiri ya wito wake. Huu ndio wajibu wa kila mwenye hofu ya
Mungu. Amina
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi
walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa?
Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha
wana-kondoo wangu,” Yoh 21:15
Ee
Yesu Mwema na Mchungaji wetu, tukumbushe mara zote kuyaona mahitaji ya wengine
na kuwa tayari kufanya chochote kadiri ya hali na nafasi tulizokuwa nazo katika
jamii. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario