IJUMAA
WIKI YA 5 YA PASAKA
Somo:
Mdo 15:22-31
Zab:
57:8-9, 10, 12
Injili:
Yoh 15:12-17
Nukuu:
“sisi
tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwapeleka
kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo,” Mdo 15:25
“watu
waliohatirisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo,” Mdo
15:26
“Basi
tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa
vyao,” Mdo 15:27
“Kwa
maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo
lazima,” Mdo 15:28
“yaani,
mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama
zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu,” Mdo
15:29
“Amri
yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi,” Yoh 15:12
“Hakuna
aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki,”
Yoh 15:13
“Si
ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka
mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote
mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Mdo 15:16
TAFAKARI:
Maamuzi na wakaraka wa Mtaguso wa Yerusalemu: “Sisi sote tuna mastahili sawa
mbele ya Kristo, yeye ndiye aliyetuchagua bila mastahili yetu ili tuzae matunda
ya kudumu.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, “sisi sote tuna mastahili sawa mbele ya Kristo, yeye ndiye
aliyetuchagua bila mastahili yetu ili tuzae matunda ya kudumu.” Yakiwa haya
ndiyo majumuisho ya Mtaguso wa Yerusalemu, Kristo anatupenda kama tulivyo na
kutuhesabia haki mbele zake na mbele ya Mungu Baba bila kujali familia
tulizozaliwa, koo tulizotoka, kabila tulizotoka, na hata mataifa tuliyotoka.
Hakika, ingekuwa haya niliyoyataja kuwa gizezo cha kuwa Mkristo na hata kuwa
Mtumishi katika Kanisa lake KRISTO, bila shaka ingekuwa ndoto leo mimi kuwa
kama nilivyo. Ni katika msingi huu nilioutaja (Kristo ametuchagua bila ya
mastahili yetu), Mtaguso wa Yerusalema wanaafikiana vyema kuhusu swala la watu
wa mataifa waliolipokea neno na kuunda ujumuiya ya Kikristo. Ukristo wetu
hautokani na hayo matabaka niliyoyasema hapo juu. Ukristo wetu unatokana na
kuhesabiwa haki na Kristo mwenyewe, kulikotokana na kutupenda upeo. Hivyo
Mtaguso wa Yerusalemu unatoka tamko lifuatalo, “sisi
tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwapeleka
kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo,” Mdo 15:25. Mtume Paulo na Barnaba wanachaguliwa
kwa vigezo vya maisha yao kupeleka ujume huu kwa wale waliolipokea neno. Ni “watu
waliohatirisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo,” Mdo
15:26.
Hata
hivyo Yuda na Sila ndio watakaosema kwa vinywa vyao juu ya ujembe huo. “Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia
wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao,” Mdo 15:27. Yuda na Sila bila shaka
ni watu waliokuwa karibu sana na jumuiya hiyo mpya ya Antiokia. Uwakilishi huu
ni njia mojawapo ya kuboresha ukaribu wao na jumuiya ya Yerusalemu, na kuanza
kuishirikisha jumuiya hii mpya ya Antiokia yale yote yamuhusuyo Kristo. Ukaribu na umoja huu si wakubebeshana mizigo,
bali ni fursa ya kuyatafakari makuu ya Mungu na upendo wake kwa kila mmoja
aliyeridhia upendo na umoja huo wa Kristo. Roho Mtakatifu ndiye mleta umoja
huo. “Kwa maana ilimpendeza Roho
Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima,” Mdo 15:28.
Hivyo
basi, ili kuendelea na umoja huu na upendo huu ndani na katika Kristo,
iliwapasa kujitengana na yale ambayo hayakuwa na mwelekeo wa Kimungu. Ni ukweli
kwamba kama tunataka kuishi katika Kristo, yatupasa kujikana wenyewe na
kumfuata. Yatupasa kuacha yale ya zamani na kuyachuchumilia yale yampendezayo
Kristo. Hivyo basi, jumuiya hii mpya ya Antiokia, inapaswa kufanya haya
yafuatayo; “yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu,
na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya
vema. Wasalamu,” Mdo 15:29. Tunapoachana na makandokando haya ya maisha ndipo
tunapokuwa karibu na upendo wa Kristo na kutimiza mapenzi yake. Huu ndio upendo
anaotutaka Kristo tuuishi kama familia yenye hofu ya Mungu na kuwajibika. “Amri yangu ndiyo hii,
Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi,” Yoh 15:12. Ndugu yangu, jambo hili si
rahisi! Mimi na wewe leo tupo hiki tulicho kama tokeo la historia yetu tangu
kuzaliwa, makuzi yetu ambayo yameathiriwa na mila na desturi zetu, ufahamu wetu
ambao umeathiriwa pia na mfumo mzima wa elimu tuliokuwa nao. Katika mazingira
hayo ya makuzi, lengo ni kuuona ukweli kama ulivyo, na siyo kuuona ukweli kama
tulivyo. Hapa ndipo penye tofauti kubwa ya kusoma na kuelimika. Wote
walioelimika wamesoma, ila siyo wote waliosoma wameelimika. Hapa kusoma
simaanishi kwenda darasani kama ilivyo ada, bali kuyaelewa vizuri mazingira
yanayokuzunguka, ambayo kwa kiasi kukubwa si lazima kwenda darasani kadiri ya
mfumo unavyotutaka. Hivyo kwa mazingira ya Kanisa la mwanzo, na changamoto
iliyowakabili, Mtaguso ule uliwalazimu kuyaona yote katika upendo wa Kristo na
hatma ya upendo huo ambao ni kifo kile cha Msalaba.
Upendo huu miongoni
mwetu wenye taswira ya Kristo mwenyewe, ni upendo unaoitaji kujitoa sadaka kwa
wengine. Kupenda kama Kristo alivyotupenda kunatudai kujitoa sadaka kwa wale
tunaoishi nao kila siku. Upendo usiojitoa sadaka bado hujafikia ukomavu wake.
Yanipasa kujisikia furaha tena na tena ninapojitoa sadaka kwenye familia yangu,
jumuiya yangu ya kitawa, jumuiya yangu ndogo ndogo ya Kikristo, na hata Kanisa
langu ninaposali na kumsifu Mungu. Yesu anatuambia, “Hakuna
aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya
rafiki,” Yoh 15:13. Hili Yesu kalifanya kwa vitendo. Hatua hii ya upendo ni
ukomavu katika maisha ya Kiroho. Mimi na wewe iwe changamoto yetu ya kudumu.
Ndugu yangu,
tunayafanya haya yote si kwa vile sisi ni mashujaa wa kufanya hivyo. La hasha!
Tunafanya hayo yote kwa sababu yupo
ambaye kabla ya sisi kuyafanya hayo kesha yafanya na anaendela kuyafanya ndani
mwetu kwa nguvu na neema zake. Mtu huyu
ni Kristo mwenyewe. Unapoona unatenda jambo jema na watu wakaliitikia kwa moyo
wa upendo, elewa jambo hilo linamkono wa Kristo ndani yake. Wewe na mimi katika
tendo hili tutakuwa tumetumika vizuri kama watumishi waliofanya vyema yale
waliopaswa kuyafanya. Hivyo katika kweli hii, Yesu natuambia, “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi
niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu
yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Mdo
15:16. Hakika matunda yanayotokana na kutumika vyema kwa nguvu na neema za Mungu,
hudumu daima hata kama kwa wakati ule sisi hatutakuwepo kushuhudia ukweli huo.
Hivyo mara zote tujione hivi: “Vivyo hivyo
nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio
na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk 17:10
Ndugu yangu usiache
kutenda mema hata kama kwa hali ya ubinadamu wako unakatishwa tamaa kufanya
hivyo. Uhalisi wa wema huo ni Mungu mwenyewe.
Tumsifu Yesu Kristo.
“Si
ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende
mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba
kwa jina langu awapeni,” Mdo 15:16
Tusali:-
Ee Yesu wangu na yote kwangu, nitumie vyema kama chombo chako kisicho na faida.
Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario