JUMAMOSI YA OCTAVA YA PASAKA
Somo: Mdo 4:13-21
Zab: 118:1, 14-15ab, 16-18, 19-21
Injili: Mk 16:9-15
Nukuu:
“Basi
walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na
elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja
na Yesu,” Mdo 4:13
“Petro
na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza
ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; maana
sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia,” Mdo 4:19-20
“Nao walipokwisha
kuwatisha tena wakawafungua, wasione njia ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu;
kwa kuwa watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa hayo yaliyotendeka,” Mdo 4:21
“Walakini
hao waliposikia kama yu hai, naye amemwona, hawakusadiki,” Mk 16:13
“Baadaye
akaonekana na wale kumi na mmoja walipokuwa wakila, akawakemea kwa kutokuamini
kwao na ugumu wa mioyo yao, kwa kuwa hawakuwasadiki wale waliomwona alipofufuka
katika wafu,” Mk 16:14
“Akawaambia,
Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe,” Mk 16:15
TAFAKARI: “Mungu hutenda
mambo makuu kwa wanyenyekevu wa moyo; msingi wa yote ni kuamini na
kujisalimisha kwake.”
Wapendwa
wana wa Mungu, jumuiya ya kwanza ya Wakristo haikujengwa na mijitu yenye upeo
mkubwa sana wa akili na maarifa. Jumuiya hii ilijengwa na MAJITU YA SIFA,
nikimaanisha; wanyenyekevu wa moyo na wenye imani ya kweli kwa yale waliyokuwa
wanaamini juu ya Yesu Kristo. Jambo hili lilikuwa mshangao mkubwa kwa watesi
wao, yaani Wayahudi walikuwa na msimamo mkali, hasa lile baraza lao la
Kiyahudi.
Watesi
wao wanatoa ushuhuda wa jumuiya hii ya Wakristo. “Basi
walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na
elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja
na Yesu,” Mdo 4:13. Ingawa hawakuwa na Yesu katika hali ya kushikika/kimwili,
Kristo mwenyewe ndiye aliyekuwa Kiongozi wa jumuiya hii. Jina lake lilikuwa
tishio kubwa sana. Ni kupitia jina lake hili wengi waliponywa na wanazidi
kuponywa hadi sasa.
Ili
kuondokana na karaha hii, na kushindwa kwao kuwazuiya, Baraza la Kiyahudi
linatoa amri ya wao kutokusema tena juu ya Jina hili Tukufu la Bwana wetu Yesu
Kristo. Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia, “Kwamba ni haki mbele za Mungu
kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena
mambo tuliyoyaona na kuyasikia,” Mdo 4:19-20. Ujasiri huu wa Petro na Yohana
unathibitisha uthabiti wa Imani ya kweli juu ya kile walichoona na kuamini.
Wapendwa
wana wa Mungu, kunamsemo unaosema kwamba ‘mara zote historia hujirudia.’ Leo
tunaona Wakristo kusongwa sana na kuuwawa kwa sababu tu ya Jina hili Kuu kupita
majina yote. Mitume walichapwa viboko hadharani na wengine kuuwawa kama Bwana
wao Yesu Kristo, ila hawakusita kutoa ushuhuda wa kweli. Damu zao ndiyo msingi
wa Kanisa letu leo. Leo Wakristo wenzetu wanapatwa na msukosuko na mateso hayo
kwa njia tofauti tofauti. Wapo wanochinjwa kama kuku, kuchomwa kwa moto,
kupigwa risasi, na vifo vya ukatili ambavyo havijawahi tokea. Mfano kule Irak
wapo walioingiziwa misalaba kinywani hadi kufa. Leo twapaswa kusimama Imara
katika Imani yetu.
Nyakati
zile, Mitume walitishwa kwa kufungwa magerezani, kuchapwa na kulazimishwa
kutolitaja tena Jina hili. “Nao
walipokwisha kuwatisha tena wakawafungua, wasione njia ya kuwaadhibu, kwa
sababu ya watu; kwa kuwa watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa hayo
yaliyotendeka,” Mdo 4:21. Tunaposimama katika jina hili, yote yanawezekana kwa
sababu mwenye kuliongoza Kanisa hili ni Kristo mwenyewe.
Imani
ni msingi wa yote yale tunayoyasema na kuyasimamia. Tusipokuwa na Imani ya
kweli na thabiti, ni vigumu kuitetea na wala kuwa Mashahidi wa Imani hiyo. Leo
tunalazimishwa kulikana hili Jina badala yake kusilimishwa. Watu wengi kati
yetu kutokana na ugumu wa maisha wameshajisilimisha ingawa wamebaki na majina
yao Kikristo kama makapi. Tukio la ufufuko wa Bwana yetu Yesu Kristo kadiri ya
Injili ya leo halikuwa jambo la kuaminika kwa urahisi hata kwa mitume wenyewe. “Walakini hao waliposikia kama yu hai, naye
amemwona, hawakusadiki,” Mk 16:13. Mariamu Magdalena anapopeleka habari za
ufufuko wa Yesu kwa Mitume, hawakuamini. Ni kweli isiyo shaka kwamba namna na
kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo kilivyokuwa kiliwatia hofu kubwa sana wafuasi
wake na hasa Mitume hata kufikiri wenyewe kupoteza maisha yao kwa kuuwawa
kikatili kama Mwalimu wao.
Katika
hofu hii, Yesu Kristo Mfufuka anawatokea. “Baadaye
akaonekana na wale kumi na mmoja walipokuwa wakila, akawakemea kwa kutokuamini
kwao na ugumu wa mioyo yao, kwa kuwa hawakuwasadiki wale waliomwona alipofufuka
katika wafu,” Mk 16:14. Baada ya Yesu
kuwakeamea anawapa majukumu ya kufanya. “Akawaambia, Enendeni
ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe,” Mk 16:15. Majukumu haya
ya kuihubiri Injili ulimwenguni mwote na kwa kila kiumbe ndicho kitambulisha
cha Kristo Mfufuka na aliye hai. Jukumu hili ni kwa kila mbatizwa na yule
mwenye kuamini kwa kushika ahadi zake za ubatizo.
Leo
ndugu zangu tunachangamoto nyingi sana katika jumuiya yetu na Kanisa letu.
Ikiwa tunaona aibu kufanya ishara ya msalaba hadharani, na hasa sehemu za kula
kama mahotelini, itakuwaje sasa kusimama wazi na kusema mimi ni Mkristo, na
ninamwamini Kristo, na nipo tayari kufa kwa anjili ya Jina hili? Vile vile
natoa angalizo kwa wale wanaopenda kuwa na uraia pacha wa Imani. Watu hawa ni
wale mara wanapokuwa kwenye alaiki ya watu na kwenye masherehe upoteza uhalisia
wao kwa kutoa salamu za kuwapendezesha kila kundi la watu.
Utamsikia
Mkristu anaanza utambulisho wake kwa mbwembwe; Wasalam Maleku, Bwana asifiwa,
Kristo mshinda, Bwana ni jibu, Tumsifu Yesu Kristo, nk. Hatuna upacha katika
IMANI. Ni vigumu sana kumsikia Muislamu akijitambulisha mbele ya alaiki ya watu
kama sisi. Ni aheri kukaa kimya kuliko kuonyesha ujinga wako katika swala hili
la Imani. Hivyo ni heri kuwa baridi au joto kiimani, kuliko kuwa vuguvugu.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Petro
na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza
ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; maana
sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia,” Mdo 4:19-20
Ee Yesu,
lisimamie Kanisa lako, na utupe ujasiri wa kutosha kuisimamia Imani yetu na
kuiishi pasipo woga. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario